Picha kwa hisani ya Wahakaroro Group (FB)
Kwa mliosoma Shule ya Sekondari ya Kahororo mjini Bukoba bila shaka mtakuwa mnamkumbuka mwalimu wa Fizikia Mr. Agricola. Pengine mtakuwa mnakumbuka ule mwandiko wake maridadi ubaoni. Au lile tabasamu pana usoni mwake. Au wema wake na kutopenda kuchapa wanafunzi hovyo hovyo hata enzi zile ambapo fimbo zilikuwa ndo mfalme mashuleni. Vipi kuhusu umaridadi na uhodari wake wa kufundisha Fizikia - somo gumu, lisilo na bashasha na lisilopendwa na wanafunzi wengi? Mnakumbuka alipoanguka na baisikeli katika kona za milima ya Rugambwa akaja kutupa mchapo kuhusu madhara na athari za centrifugal force? Mnakumbuka msisitizo wake kuhusu nidhamu, maadili na kuwa watu wema maishani?
Basi Mwalimu Agricola alifariki tarehe 7 Novemba 2012 jijini Dar es salaam kwa kansa ya koo. Watu waliopata bahati ya kuongea naye siku za mwisho mwisho kabisa wakati madaktari wakiwa wameshakata tamaa walisema kuwa walishangazwa na utulivu wake na imani kuu aliyokuwa nayo. Japo alikuwa katika maumivu makali, alikuwa akitabasamu na kuwaambia kuwa wasiwe na wasiwasi kwani alikuwa na imani kubwa kwamba atapona.
Binafsi namkumbuka sana Mwalimu Agricola kwani alikuwa anapenda sana mwandiko wangu. Wakati ule tukiwa kidato cha nne na akina Matungwa Lwamwasha, Samsoni Nkaitwabo, Ngulingwa Balele, Medadi Kalemani, Juma Ndekwa, Mihayo Msikela, Edwin Kalisa, Kulwa Kindija, Tindyebwa Nkunuzi, Marko Nyanda, Bundi Sida, Shega Nkingwa, Stanslaus Ephraimu .....aliwahi kunipa madaftari yenye kurasa nyingi kutokana na kuvutiwa na mwandiko wangu.
Pumzika salama mwalimu wetu mpendwa. Wanafunzi wako uliowajali na kuwapenda ndani na nje ya darasa lako la Fizikia wapo kila mahali. Na kupitia kwao, utaendelea kuishi !!!






















