NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Sunday, January 25, 2009

BARUA YA OBAMA KWA MABINTI ZAKE NA WATOTO WOTE WA MAREKANI

BARUA YA OBAMA KWA MABINTI ZAKE NA WATOTO WOTE WA MAREKANI

(AHADI KWA KIZAZI KIPYA)

Baada ya kushinda uchaguzi wa uraisi wa Marekani na kabla ya kuapishwa, raisi wa Marekani Barack Obama aliwaandikia barua mabinti zake Malia (10) na Sasha (7) pamoja na watoto wote wa Marekani. Barua hiyo ilichapishwa katika gazeti la Parade la tarehe 18/1/2009. Katika barua hiyo (ambayo nimeitafsiri haraka haraka katika Kiswahili hapo chini) Obama anawaeleza mabinti zake na watoto wote wa Marekani sababu kubwa zilizomfanya agombee uraisi: kuwajengea ulimwengu ambao hautazikinza ndoto zao za kupata cho chote wakitakacho, kuwa na nafasi sawa za kujifunza, kuelimika na hatimaye kuweza kuiboresha dunia hii. Akisisitiza mambo aliyojifunza kutoka kwa bibi yake na historia, rais Obama anataka watoto wote wa Marekani wawe na nafasi sawa za kwenda shule zenye uwezo wa kuvichanuza vipaji vyao na kuwafanya wawe wadadisi. Anataka kila mtoto wa Marekani aweze kwenda chuo kikuu hata kama wazazi wake si matajiri kwani kazi nzuri na zenye marupurupu mazuri zinategemea sana elimu nzuri na ya kiwango cha juu. Isome tafsiri yangu ya haraka haraka ya barua hiyo yenye kugusa moyo na kuonyesha upendo halisi alio nao mzazi kwa mtoto wake ampendaye na kumtakia mema hapo chini. Ukitaka kuisoma barua hiyo kama ilivyoandikwa na raisi Obama katika lugha ya Kiingereza bofya hapa

Nilipoisoma barua hiyo ilinifanya nifikiri ni wazazi wangapi wa Tanzania ya leo ambao wanaweza kutoa ahadi kama hizi kwa watoto wao na kutegemea kuzitimiza. Wakati ninapoandika makala hii kuna watoto wengi wa Kitanzania ambao wamenyimwa nafasi ya kurudi chuo kikuu kuendelea na masomo yao kwa vile, mbali na vijisababu vingine, wazazi wao hawana uwezo wa kuchangia gharama za elimu yao. Inavyoonekana huu ndio mwisho kwa watoto wa masikini (ambao kwa bahati mbaya ndiyo wengi) kupata elimu ya juu katika nchi yetu. Wakati taifa kubwa lililoendelea na lenye nguvu kuliko yote duniani linajiwekea ahadi na mikakati ya kuhakikisha kwamba watoto wake wote wanapata nafasi ya kwenda chuo kikuu, sisi ndiyo kwanza tunajenga vizingiti kuzuia watoto kutoka familia masikini (nasisitiza tena – ambao ndiyo wengi) wasipate nafasi hiyo muhimu. Elimu ndiyo mkakati mama kabisa katika ukombozi wa jamii yo yote ile katika jitihada zake za kujikomboa na hatimaye kuondokana na ujinga, maradhi na dhuluma - jamii yenye watu waliokaramka na ambao wako tayari kupambana na vipingamizi vya kijamii, kisiasa, kijamii, kiuchumi na kimazingira. Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alilitambua jambo hili vyema na ndiyo maana alipigana sana kuhakikisha kwamba kila mtoto wa Kitanzania anapewa nafasi sawa ya kupata elimu bila kujali uwezo na nafasi ya mzazi wake. Ni ukweli ulio wazi kwamba bila mwalimu Nyerere kutupigania wengi wetu tusingeweza kusoma na kufika chuo kikuu. Ati, tunapowanyima watoto wa familia masikini (ambao ndiyo wengi) nafasi ya kupata elimu ya juu, tunataka wafanye nini? Hakuwezi kuandaliwa utaratibu mzuri wa mikopo utakaowaruhusu watoto kutoka familia zisizojiweza kupata elimu ya juu? Ni jamii gani ambayo tunajaribu kuijenga? Nini itakuwa athari ya matabaka haya kinzani ambayo tunajaribu kuyajenga na kuyaimarisha kwa utaifa, umoja na amani yetu? Jamii yetu inaelekea wapi?


Hii hapa chini ndiyo tafsiri yangu ya haraka haraka ya barua ya Raisi Obama kwa mabinti zake Malia (10) na Sasha (7) pamoja na watoto wote wa Marekani.

Wapendwa Malia na Sasha;

Ninajua kwamba nyote mmeifurahia sana miaka miwili iliyopita katika kampeni – kwenda kwenye pikiniki na paredi, maonyesho ya biashara na kula kila aina ya vyakula-nenepeshi, vyakula ambavyo pengine mimi na mama yenu tusingewaruhusu mvile. Ninajua pia kwamba wakati mwingine haikuwa rahisi kwenu na mama yenu na ingawa mna furaha sana kuhusu mbwa mpya mtakayempata hivi karibuni, yote haya hayafidii muda ambao hatukuwa pamoja. Ninajua ni kwa jinsi gani nilivyotamani kuwa nanyi katika miaka miwili iliyopita na leo ninataka kuwaambia ni kwa nini niliamua kuichukua familia yetu kwenda katika safari hii.

Nilipokuwa kijana nilifikiri kwamba maisha yalinihusu mimi pekee – jinsi ambavyo ningetafuta nafasi yangu katika dunia, kufanikiwa na kupata vitu ninavyovitaka. Halafu ninyi wawili mkaja katika maisha yangu mkiwa pamoja na udadisi, utundu na matabasamu yenu ambayo kamwe huwa hayashindwi kuujaza furaha moyo wangu na kuichangamsha siku yangu. Ghafla mipango yangu mikubwa ya maisha haikuonekana kuwa ya muhimu tena. Niligundua mara moja kwamba furaha kubwa katika maisha yangu ilihusiana moja kwa moja na furaha yenu. Niligundua pia kwamba maisha yangu hayangekuwa na maana sana kama nisingekuwa na uwezo wa kuhakikisha kwamba mnapata kila aina ya nafasi na ridhiko katika maisha yenu. Matokeo yake, mabinti, hii ndiyo sababu iliyonifanya nigombee uraisi: kwa sababu ya kile ninachowatakia ninyi na ninachomtakia kila mtoto katika taifa hili.

Ninataka watoto wote waende katika shule zenye uwezo wa kuvipevusha vipaji vyao - shule ambazo zitawachochea, kuwatia hamasa ya kujifunza na kuwafanya wawe wadadisi wa ulimwengu unaowazunguka. Ninawataka wawe na nafasi ya kwenda chuo kikuu hata kama wazazi wao si matajiri. Na ninawataka wapate kazi nzuri: kazi zenye mishahara mizuri na zitakazowapa marupurupu kama bima ya afya, kazi ambazo zitawapa muda wa kukaa na watoto wao na kustaafu kwa heshima wakiwa na uwezo wa kujikimu.

Ninataka tufanye mapinduzi makubwa katika ugunduzi ili katika maisha yenu muweze kushuhudia teknolojia na ugunduzi mpya ambao utayaboresha maisha yetu na kuifanya sayari yetu kuwa salama na safi zaidi. Ninataka sote tuzitumie ipasavyo karama zetu za kibinadamu bila kujali tofauti za rangi na kieneo, jinsia na dini – tofauti ambazo mara kwa mara hutufanya tusiyaone mambo mazuri ya kila mmoja wetu.

Wakati mwingine inatulazimu kutuma vijana wetu wa kike na kiume kwenda vitani na hali zingine za hatari ili kuilinda nchi yetu. Ninataka kuhakikisha kwamba tunapofanya hivyo ni lazima iwe ni kwa sababu nzuri kabisa na kwamba tujaribu kila tuwezalo kutatua tofauti zetu na wengine kwa njia za amani, na tufanye kila tuwezalo kuhakikisha kwamba wanajeshi wetu wako salama. Ninataka kila mtoto afahamu kwamba karama ambazo wamarekani hawa mashujaa wanazipigania siyo za bure na kwamba upendeleo mkubwa wa kuwa raia wa nchi hii unaambatana na wajibu mkubwa.

Hili ndilo jukumu kubwa ambalo bibi yenu alijaribu kunifundisha nilipokuwa na umri kama wenu, aliponisomea mistari ya mwanzo katika utangulizi wa Tangazo la Uhuru wa Marekani na kuniambia juu ya wanaume na wanawake ambao waliandamana kupigania uhuru kwa sababu waliamini kwamba maneno hayo katika utangulizi wa Tangazo la Uhuru wa Marekani yaliyoandikwa karne mbili zilizopita ni lazima yalimaanisha kitu fulani cha muhimu.

Alinisaidia kufahamu kwamba Amerika ni taifa lenye nguvu na lililoendelea si kwa sababu halina mapungufu yake bali ni kwa sababu linaweza kuboreshwa na kuimarishwa zaidi na kwamba kazi ambayo haijamalizika ya kuliimarisha na kuliboresha taifa letu ni yetu sote. Jukumu hili tunalirithisha kwa watoto wetu – kila kizazi kikiukaribia zaidi uhalisi wa Amerika kamili tunayoitamani.

Ninatumaini kwamba nyote mtajitwika jukumu hili, mkisahihisha makosa mnayoyaona na kuwapa wengine nafasi ambazo ninyi mmezipata. Inabidi mfanye hivyo si kwa sababu tu eti mna wajibu wa kuifanyia kitu nchi hii ambayo imeifanyia familia yetu mambo mengi- ingawa kusema kweli wajibu huo hauepukiki - bali ni kwa sababu mna wajibu kwenu wenyewe. Ni pale tu mtakapotamani mambo makubwa zaidi yenu ndipo mtakapoweza kukifikia kilele halisi cha uwezo na vipaji vyenu.

Hivi ndivyo vitu ninavyowatakia – kukulia katika ulimwengu ambao hautaziwekea mipaka ndoto zenu, kupata cho chote mkitakacho na hatimaye mkue na kuwa wanawake wenye huruma – wanawake makini watakaosaidia kujenga dunia njema. Na ninataka kila mtoto kupata nafasi za kujifunza, kuota ndoto na kuimarika kama mlizopata ninyi mabinti. Hii ndiyo sababu nimeichukua familia yetu katika safari hii. Ninyi ni mabinti ninaojivunia sana na upendo wangu kwenu hauna kikomo. Ninashukuru kila siku kwa ukarimu wenu, ushwari wenu, neema na ucheshi wenu hasa wakati huu tunapojitayarisha kuanza maisha yetu mapya pamoja katika ikulu ya Marekani.

Awapendaye;

Babenu.Imetafsiriwa na Dr. Masangu Matondo Nzuzullima
Chuo Kikuu cha Florida

Tazama pia tafsiri ya barua hiyo kutoka gazeti la KIU HAPA CHINI:

2 comments:

  1. Ananitamanisha nipate MTOTO!
    Asante kwa hugusia hili.

    ReplyDelete
  2. Bwana Simon, watoto wana mibaraka yake hasa kama ukiacha "ubabe" wa Kiafrika na kuwalea hasa inavyotakiwa. Nakumbuka nyakati zile watoto mkimsikia mzee anakuja mnakwenda kujificha. Nadhani sasa mambo yamebadilika kidogo. Suala kubwa hata hivyo ni jinsi ya kuwa na uwezo wa kuwapa nafasi zote wanazotaka na kuhakikisha kwamba wanapata maisha mema. Hiki ndicho kitu kilichonigusa katika barua hii ya Obama mpaka nikaaamua kuibandika hapa.

    ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU