NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, January 30, 2009

FALSAFA YA MLEVI (1)

Shairi hili la Falsafa ya Mlevi (1) nililiandika zamani kidogo na limo katika kitabu changu cha mashairi kiitwacho Mashing'weng'we kitakachotoka hivi karibuni. Nilipata msukumo wa kuliandika shairi hili baada ya kusoma shairi la Wimbo wa Mlevi ambalo limo katika katika kitabu mashuhuri cha mashairi cha Kichomi kilichoandikwa na Euphrase Kezilahabi. Katika shairi la Wimbo wa Mlevi Kezilahabi anasema hivi:


Kama Mungu angewauliza wanadamu

Wanataka kuwa nani kabla ya kuzaliwa

Hilo ndilo lingekuwa swali gumu maishani.

Mtawala na kabwela, mrefu na mfupi
Mweusi na maji ya kunde, mwembamba na mnene
Wote wangetamani kuwa kinyume cha walivyo.
Sijui nani angekuwa nani.


Lakini mimi mlevi ningependa kuwa ye yote
Mradi tu niruhusiwe kunywa pombe yangu.
Hapo nyumbani kwa baba Madaka hamjambo!
Ni usiku mi napita nakwenda zangu!

Katika Falsafa ya Mlevi (1), mimi ninasema hivi:

Walimwengu wanasema:

Kuna kujua

Na kujua kwamba unajua

Pia kuna kujua

Na kutojua kwamba unajua

Lakini pia kuna kutojua

Na kujua kwamba hujui

Pia kuna kutojua

Na kutojua kwamba hujui


Walimwengu pia wanasema:

Mtu anayejua

Na kujua kwamba anajua

Yeye ni mwerevu na msomi

Na mtu anayejua

Lakini hajui kwamba anajua

Yeye ni mdadisi na mgunduzi

Mtu asiyejua

Na anajua kwamba hajui

Yeye ni mwanafunzi

Lakini mtu asiyejua

Na hajui kwamba hajui

Yeye ni mpumbavu!


Mimi mlevi ninasema:
Yote haya ni uwongo na uzushi

Mtu anayejua

Na kujua kwamba anajua

Yeye ni mpumbavu!

Kwani wasomi, wanasayansi na wanasiasa

Hawakugeuka Mashing’weng’we,

Na kutufikisha Pagak?


Mimi mlevi nasisitiza

Mtu pekee mwerevu hapa duniani

Ni mtu asiyejua

Na hajui kwamba hajui!


Maneno Magumu:


Mashing’weng’we - mazimwi katika hadithi za Kisukuma

Pagak - kutoka katika kitabu cha Wimbo wa Lawino kilichoandikwa na Okot p'Bitek. Ni mahali ambako mtu akienda harudi yaani kuzimuni.

Je, unakubaliana na falsafa hii ya mlevi?


(c) Falsafa ya Mlevi (1) - Mashing'weng'we (uk. 11)
Na Dr. Masangu Matondo Nzuzullima

No comments:

Post a Comment

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU