NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, January 29, 2009

TUZUNGUMZIE KIFO

 • Watu wengi huwa hawapendi kuzungumzia kifo. Mimi pia ni mmoja wao. Hata hivyo nimeamua kuandika kidogo kuhusu kifo baada ya kusoma makala ndefu juu ya kifo kutoka katika blogu ya Kamala (bofya hapa). 
 • Niliposoma makala hiyo nilianza kufikiria mitazamo mbalimbali na hasa kutoka kwa wanafalsafa na jinsi wanavyokitazama kifo. Hapa chini basi ni mawazo machache tu yenye kufikirisha kutoka kwa wanafalsafa mbalimbali kuhusu kitu hiki kiitwacho kifo. Mbali na mambo mengine mkazo hasa wa wanafalsafa hawa ni kujaribu kutuondolea hofu ya kifo na kutufanya tusikiogope, kuomboleza na kutetemeka wakati tunapokabiliana nacho.
(I) Seneca (Mwanafalsa wa Roma ya kale aliyeishi kati ya mwaka 4 K.K na 65 B.K.) anaonekana kuwa ni mmoja kati ya wanafalsafa ambao walihangaishwa sana na kifo. Katika makala yake ya “On Asthma and Death”, kwa mfano, anasema hivi kuhusu kifo.

“Kufa ni kutokuwako na ninajua hii inamaanisha nini. Ambacho kilikuwako kabla yangu kitakuwako tena baada yangu. Kama kuna maumivu au mateso katika hali hii ya kutokuwako basi ni lazima pia kulikuwa na mateso au maumivu kabla ya kuzaliwa kwetu. Kusema kweli, hata hivyo, hatukusikia maumivu yo yote kabla ya kuweko kwetu. Na ninawauliza, ati usingemwona kuwa ni kingunge wa wapumbavu yule anayeamini kwamba taa iko katika hali mbaya zaidi baada ya kuzimwa kuliko kabla ya kuwashwa? Sisi tufao, kama vile taa, huwashwa na kuzimwa na kipindi cha maumivu na mateso hutokea katikati – yaani baada ya kuwashwa na kabla ya kuzimwa. Lakini katika pande zote mbili -kabla ya kuwashwa na baada ya kuzimwa - kuna amani isiyo na kikomo”

Katika makala yake nyingine iitwayo “On Taking One’s Own Life” Seneca ana haya ya kusema kuhusu kifo:

“Hakuna mtu ambaye ni mpumbavu kiasi cha kutojua kwamba siku moja tutakufa. Pamoja na ufahamu huu, wakati wa kufa unapokaribia watu wengi huogopa, wakitetemeka na kuomboleza. Usingemwona kuwa ni mpumbavu kabisa mtu ambaye anaomboleza kwa sababu ati hakuwako miaka elfu moja iliyopita? Na usingemwona kuwa ni mpumbavu kabisa pia mtu ambaye anaomboleza kwa sababu hatakuwako miaka elfu moja ijayo kutoka sasa? Yote ni sawa: hutakuwako na hukuwako. Vipindi vyote hivi viwili si vyako”

(II) Marcus Aurelius (a.k.a Mwenye hekima) alikuwa mtawala wa himaya ya Roma ya kale kutoka mwaka 161 mpaka kifo chake mwaka 180 B.K. Mawazo yake kuhusu kifo yanapatikana katika kitabu chake cha Meditations alichokiandika kati ya mwaka 170 na 180 B.K. Anasema hivi kuhusu kifo:

“Hebu tazama kipindi kirefu kilichopita nyuma yako, na muda mrefu usio na kikomo ambao haujaja bado. Katika ombwe hili la muda kuna tofauti gani kati ya yule anayeishi siku tatu na yule anayeishi vizazi vitatu?”
(III) Epictetus – mwanafalsa wa Ugiriki aliyefundisha kwamba falsafa ilikuwa si somo tu bali jinsi ya kuishi. Alifundisha kwamba matukio ya nje yanatawaliwa na majaliwa (fate) na hatuwezi kuyadhibiti, na kwa hivyo tunaweza kukabiliana na jambo lolote bila papara wala kulalamika. Mateso na maumivu hutokea wakati binadamu anapojaribu kudhibiti mambo yasiyodhibitika, au kwa kupuuza mambo ambayo yako chini ya uwezo wake. Alifundisha kwamba binadamu wote walikuwa memba wa jamii moja ya kilimwengu na kwamba kila binadamu alikuwa na wajibu wa kuwatunza na kuwajali binadamu wenzake. Mtu ambaye angefuata mambo haya basi angepata furaha. Kutokana na mtazamo wake huu, mwanafalsafa huyu anasema hivi kuhusu kifo.

“Kifo – tukio ovu linaloogopwa kuliko matukio yote, si tukio linalopaswa kutuumiza kichwa kwa sababu tunapokuwapo kifo hakipo na kifo kinapokuwapo sisi hatupo”

(IV) Bembelezo bora kabisa la kutoogopa kifo linatoka kwa Epicurus – mwanafalsafa wa Kigiriki aliyeishi kati ya mwaka 341 na 270 K.K. na ambaye alitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sayansi kutokana na mafundisho yake ya kutoamini vitu hovyo hovyo hata kabla ya kuvipima na kuvichunguza sawasawa. Kulingana na mwanafalsafa huyu lengo kuu la falsafa lilikuwa kuleta furaha na maisha ya utangamano – maisha yasiyo na maumivu wala hofu ambayo aliyaita maisha yenye aponia. Kuhusu kifo alifundisha kwamba kifo kilikuwa ndiyo mwisho wa mwili na roho na kwa hivyo hakipaswi kuogopwa. Hebu fuatilia hoja kuu za Epicurus kuhusu kutoogopa kifo hapa chini.

(1) Unapokuwapo kifo chako hakipo; na kisichokuwepo hakiwezi kukudhuru

(2) Kifo chako kinapokuwepo wewe haupo; na kisichokuwepo hakiwezi kudhuriwa

(3) Ni upumbavu kuogopa ambacho hakiwezi kukudhuru

(4) Ni upumbavu pia kuogopa ambacho hakiwezi kudhuriwa

(5) Katika wakati wo wote ule ama wewe unakuwepo au kifo chako kinakuwepo

(6) Kwa hivyo katika wakati wo wote ama kifo hakiwezi kukudhuru, au huwezi kudhuriwa na kifo

KWA HIVYO (anahitimisha Epicurus);

(7) Ni upumbavu katika wakati wo wote ule kuogopa kifo!
 • Unakubaliana na hoja na uchambuzi wa Epicurus? Baada ya kuzisikia hoja hizi za wanafalsafa wa Kimagharibi, sasa unakionaje kifo? Bado unakiogopa? Au tumaini lako liko katika kufufuka baadaye na kwenda kuishi milele peponi/ahera/paradiso?
 • Hebu tuwasindikize wanafalsafa hawa kwa wimbo huu wa "Kifo" wa Remmy Ongala ambaye yeye mwenyewe baada ya kuugua sana na kuzushiwa mara nyingi kwamba kafariki alipona na kuamua kuokoka na kuanza kumtumikia Mungu kwa kuimba nyimbo za injili.

4 comments:

 1. Asante sana Profesa. Uchambuzi na utambuzi unatoa changamoto mbalimbali ambazo twahitaji katika jamii. Nashukuru kwa kusindikiza kwa wimbo ambao unaongeza ladha katika kile tusomacho. Sina la ziada zaidi ya shukrani kwa kazi nzuri na ngumu kusaaka habari na mutujulisha.
  Baraka kwako

  ReplyDelete
 2. Nimekupata mzee wa changamoto na asante kwa kunikaribisha vizuri namna ile. Tuendeleeni kuelimishana na kuimarishana kifikra

  ReplyDelete
 3. Ni vizuri kufahamu wengine wanafikiriaje kuhusu kifo.Je wewe Prof. kwako kifo kinamaanisha nini?

  ReplyDelete
 4. prof. umeniongezea ufahamu juu ya kifo kwa kuwarejea hawa wanafalsafa wa enzi zile. sijui kama unaweza kupata pia hoja za watu wa kale walioogopa kifo kama akina alexander the great nk.

  karibu uwanja wa blogu mzee. kasinge

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU