NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, February 5, 2009

NI KWELI WAAFRIKA HATUNA ROHO YA UDADISI, KUJITOA MUHANGA NA UGUNDUZI?

Majuzi juzi hapa nilikuwa naangalia Comedy Central na mwanakomedia/mkomedia/mchekeshaji? mmoja mweusi alinichekesha sana aliposema kwamba yeye anafikiri kwamba wazungu ni watu wa ajabu. Aliwauliza watazamaji wake kwamba mtu mzima na akili zako timamu unawezaje kuacha kazi yako nzuri na kujitolea kwenda kuishi katika misitu ya Indonesia eti kusaidia kuokoa jamii ya nyani inayokaribia kuangamia? Aliendelea kusimulia kwamba bosi wake (mzungu) ndiye alikuwa amefanya hivyo na kwake yeye jambo hili haliingii akilini kabisa.

Maneno ya huyu mwanakomedia yalinikumbusha swali ambalo mama yangu mzazi aliniuliza alipokuja kunitembelea hapa Marekani. "Hawa wazungu wana nchi nzuri namna hii, kuna simenti kila mahali, hakuna vumbi, maduka yamejaa, umeme haukatiki, kuna raha za kila aina, mahospitali mazuri, kwa nini wanaacha nchi kama hii na kuja kukaa vijijini"? Hapa alikuwa anamwongelea padri mmoja aliyekuja tangu zamani na kujenga kimisheni chake cha Kikatoliki katika kijiji kimojawapo kule Bariadi, Shinyanga.

Nilipofikiria vizuri nilianza kuwafikiria wasafiri, wafanyabiashara na "wagunduzi" wa Kizungu kutoka Ulaya waliomiminika Afrika enzi zile - akina Vasco da Gama, David Livingstone, Carl Peters, Mungo Park na wengineo. Japo wengi wao walikuwa wametumwa na nchi zao, wengi wao hawakujua walikokuwa wanakwenda na kama wangerudi salama lakini walikuwa tayari kujitoa mhanga. Kutokana na juhudi na "ugunduzi" wao, ndiyo maana Ulaya, na hasa Uingereza, iliweza kuitawala dunia nzima. Kwa wazungu, roho hii ya kukabili yasiyojulikana na kujaribu yasiyowezekana ndiyo mtaji wao mkubwa kabisa - mtaji ambao umewafanya waweze kuendelea - hata kama ni kwa kuwanyonya na kuwatumikisha watu wengine. Kwa mzungu kufa huku akijaribu kupanda mlima Everest, akipambana na mawimbi makubwa baharini au akijaribu kuruka kwa ndege yake aliyojitengenezea mwenyewe gerejini mwake si jambo la ajabu. Udadisi, udadisi, udadisi...Lakini sisi je?

Je, roho hii ya udadisi, kujitoa mhanga na ugunduzi sisi watu weusi hatuna? Kama jibu ni ndiyo, ni kwa nini? Nawaza tu. (By the way, sikuweza kumpa mama jibu la kuridhisha. Pengine nitapata jibu la maana katika mjadala huu.)

Hebu tujikumbushe jinsi hawa jamaa walivyotutawala hapa chini:Msikilize pia Noam Chomsky - mwanaisimu bingwa na mchambuzi makini wa mambo ya kisiasa akitoa maoni yake kuhusu ukoloni kupitia jicho la mgogoro wa Uganda.

9 comments:

 1. Nashukuru kwa kulileta jambo hili kwene mjadala. Nami nimekuwa nikikerwa na jambo hili. Baada ya kufikiria kwa muda mrefu juu ya swala hili, nimekuwa nikifikiria juu ya "utegemezi" waafrica tumekuwa wategemezi kwa wazungu kwa vitu vingi sana. Mwimba muziki utamwona anaimba na tisheti iniondikwa CHICAGO, yenye bendera ya marekani, tena yuko okay kabisa!!
  Kwa habari ya vitabu vinavyotumika mashuleni vingi sana hata vya shule za msingi vimeandikwa na wazungu. Jambo letu ni kuyakariri yalioandikwa hapo, hakuna kuijadili, kwene mtihani wa taifa unaulizwa taja sababu, characteristic, bila hata kujua kwanini Darwin alisema kuwa twiga wanakuwa na shingo ndefu. Kwani sisi waafrika ambao tuko na twiga kila wakati tusingeweza kusema hivyo.
  Lingine hata serikali zetu, ni tegemezi, kuchimba madini, kufanya research, everything, mzungu kahusika. Ugunduzi fossils, watu wanaishi katika mazingira yayo ila hatuna udadisi wa kusema kwanini lile jiwe linawaka, kwanini huyu mdudu amebadili rangi, mzungu akiona anasema evolution imetake place.
  Kwa kweli ni jambo linalotakiwa lifanyiwe kazi, kwani watu wengi wana PhDs ila wamefanya nini? kazi zao ziko wapi?
  Jambo la mwisho ni habari ya kutosaport kazi za waafrica wenzetu, yaweza kuwa kwa sababu ni duni au kwa sababu tunapeda tuonekane tumeendelea. Sijui kama huo ni kuendelea. Mtu kashona nguo, waafrica wengine watapenda kuvaa nguo zilizotengenezwa Uingereza tena yenye bendera au imeandikwa jina, kuliko kuinunua kilichotengenezwa africa. Pia watoto wetu ni wagunduzi lakini hawana mtu wa kuwasaport. Nakumbuka nilipokuwa nyumbani kijijini kwetu, watoto wanatengeneza vyombo vya ajabu, kitu ambacho akisaidiwa kinakuwa ni ugunduzi. Well, nipate majibu mengine toka kwenu. Mubarkiwe.

  ReplyDelete
 2. Nai, umegusia mambo mengi ya msingi. Elimu yetu kwa kweli hairidhishi kabisa na inahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa. La kupenda vya nje hilo ni zao la kutawaliwa na sasa linaendelezwa na utandawazi. Ndiyo maana matineja wetu hawataki kuzungumza lugha za makabila yao kwani ni ushamba, hawataki kufahamu cho chote kuhusu utamaduni wao n.k. Jambo jingine ni wivu na kutoungana mkono. Hata ukigundua kitu, basi utaishia tu kuchekwa na kupondwa. Wapo vijana wengi tu wenye vipaji ambao hatimaye wanaishia kukata tamaa. Hali hii inasikitisha sana. Hata uwe na akili vipi na ugundue nini, hakuna anayejali. Na usipokuwa makini waweza hata kuonekana adui. Ndiyo maana watu wetu wenye vipaji wamekimbilia nje. Hapa Marekani kama una kipaji mara moja wanakupa Green Card na kazi nzuri. Ndiyo maana wameweza kugundua vitu vingi (likiwemo bomu la Nyuklia) kwa kutegemea wataalamu kutoka nje. Tunahitaji mabadiliko ya msingi kuhusu mtazamo mzima.

  ReplyDelete
 3. Masangu, umesema mambo mazazuri hapo. Ila nataka kuongezea kidogo juu ya watoto wanaopenda kutozungumza their native languages. Nadhani wanakosea kidogo, kwani inaishia kuwa hawajui lugha yao na ya kigeni pia hawaijui vizuri. Unajua watu hawa weupe hawakiachii walichonacho. Kusudi kubwa lao ni kukiongeza walicho nacho kiwe kikubwa (Noble price anapewa mtu alieandika vitu ambavyo tumezaliwa tukivijua) kwanini tusiyaandike sisi?. Mfano, wakikuta lugha ya kispanish wanakijifunza, kiswahili wanakijifuna, wanakuwa wanayajua yote. Niliwashirisha watu fulani topic hii, nikakumbushwa jambo ambalo lilikuwa kama kicheko na huzuni pia. Huyo ndugu alisema "unajua hata kamusi za lugha za asili zimeandikwa na wazungu" That really sad. Kwa sababu tungeweza kufanya hivyo. Wako wapi wasomi wa Kitanzania, mbona wengi tunawasikia wanaitwa Dr. so and so?
  Kwa habari wa wivu, hiyo pia inasikitisha kwani wengi wanaoinuka na kutamani kutafit jambo, maybe wanakata tamaa au wanauawa. Watu wengi wanaweza kuongopa kifo kitu ambacho in someway it make sense kwani ni bora kuishi kuliko kuuwawa. Jambo linguine ambalo waafrikca tumefungwa macho nayo ni habari ya kuzipokea misaada kutoka nje. Hivi kwanini hatufumbui macho. Nadhani jambo hili liko wazi kwani watu wengi weupe wanafahamu kwanini viongozi wao, au kikundi fulani kinatoa msaada. Well, inasikitisha kama ulivyosema.

  ReplyDelete
 4. Wow! Shukrani kwa wandugu Nai na Laiser na kwako Kaka Matondo kwa mada na maelezo. Naamini mmemaliza nami nasema bila kujaribu kisichokuwepo hakutakuwa na kipya. Na ndio maana kwetu huwa tuko nyuma katika kutoka na vipya
  Baraka kwenu

  ReplyDelete
 5. tunapojadili masuala kama haya inabidi tuwe makini sana badala ya kujilaumu na kujiona wajinga, tuangalie uhalisia wa mambo. mimi sio msomi kama nyie na sijaenda ulaya japo sipatamani sana lakini tusiungane na wazungu kujionyesha kwamba hatuwezi lolote. kuna sehemu nimesoma kwamba chuo kikuu cha kwnza kilikuwa misri na mpaka sasa kuna vitu vya ajabu kwenye library za nchini mali. kijijini kwentu yamegundulika maandiko ya zaidi ya miaka 2000 kwenye miamba. inabidi mjue jinsi wakoloni walivyokata mikono na kuwauwa wanasayansi wetu aka wachonga vyuma.

  kule kwetu BKB kuna nguo za mabaka ya miti, viatu vya miti na migomba na kuna nyumba nzuri za asili. vibuyu vizuri vya kunyweo pombe maji nk na kuna nyumba zilizojengwa kwa nyansi, udongo, miti nk.

  pia tuna mitumbwi ya miti, pombe ya ndizi (lubisi) nk.

  haya na mengine mengi hatukufundishwa na mzungu yeyote. hata hivyo mkumbuke kwamba tuliishi tangu dunia kuumbwa bila mzungu kuja africa wala nini na maisha yalikuwa mazuri na tulikula vyakula vya asili na kutumia madawa ya asili bila kuwa na side-effects. hata vifaa vyetu havikuwa na side effects na hatakuleta matatizo kama global warming.

  mpaka sasa sisi bado tunaamini katika utu, umoja, undugu nk. ninyi milosoma na kwenda nje inabidi mjue kabisa kwamba mliyoyasoma na mnayoendelea kuyasoma ni mawazo, mitizamo nk vya wazungu ambao wanawajengea picha ya kujidharau ili muwatumikia bila swali!!

  kaeni ulaya na US sisi tunaishi pia. kama waafrica hatutamani sana mali kwani tunajua mali zinaachwa lakini "utu" tunaondoka nao. tofauti yako wewe msomi na mzee wa Bugandika au bugabo ni kwamba wewe unaishi maisha ya wasiwasi na hofu wakati yule wa kijijini katulia na ana amani ya kutosha!

  hata imani zetu ni nzuri ukilinganisha na za wazungu. soma makala ya padri kalugendo juu ya wamisionari wa ulaya na mungu wa watu weusi.

  kauli zenu za kisomi kama hizi, zaweza kunifukuza mahali hapa kwenye blogu hii kama mtaendelea kuangalia uafrika wetu kwa mkabala wa kizungu tu kwamba nyie mnajua upande mmoja tu.

  OKOKENI MUNGU WA WAISRAEL ANAKARIBIA KURUDI WAKATI WA WAAFRIKA YUPO NA HAKUWAHI KUONDOKA! ANATUPENDA!

  ReplyDelete
 6. Ndugu,Kamala J Lutatinisibwa, ninaomba radhi. Ila nadhani umetuelewa vibaya. Kwa kweli mimi binafsi napapenda Africa sana sana hata sijui namna ya kuelezea upendo wangu na jinsi tunapoishi Africa.
  Nadhani tulichokuwa tunazungumzia ni hali ya kuwa wazungu wanafaidi yakwetu. Tulikuwa tunajiuliza kwanini wazungu waviuze vitabu walivyovitafsiri juu ya lugha zetu za asili, na kuitwa madaktari. Kwanini sisi tusiyapate hayo. Kwa kweli naamini mwafrica atakayeidharau africa kwa sababu amesoma, au amekwenda Ulaya, hana akili timamu. Nadhani wengi tunayapenda nchi zetu. Ndio maana hatupendi kuona wazungu wakifaidi yaliyoyakwetu. Tungependa kuona kuwa ndugu "Kamala J Lutatinisibwa" amepewa tuzo kwa sababu ya yote yanapatikana katika nchi zetu.
  Jambo jingine ambalo umelizungumzia ni habari ya kuishi kama Africa yetu ya zamani. Kwa kweli ndugu yangu nadhani mambo yanabadilika. Kwani kama nilivyozungumzia habari ya wazungu kuyafaidi yaliyoyakwetu, mpaka habari ya serikali zetu wazungu wanayaingilia, nimesikia sasa hivi wanaanza kutoza kodi ya aridhi. Nakumbuka hayo yote hayakuwepo hapo kijijini kwetu. Mara nyingi inanihuzunisha, kwani nikifikiria kama baba atalipa kodi ya aridhi inamaana ng'ombe wetu wanafungiwa ndani. Pili, wazungu walikuwa wakiwahamisha wafugaji wanoishi ngorongoro. Nadhani wewe unafahamu kuwa hao ndungu wameishi kwa miaka mingi na hao wanyama, lakini sasa wazungu wanayatumia serikali zetu kuyaingiza mambo yoyote wanayotaka katika jamii zetu. NDIO MAANA MIMI NA WENZANGU TULIKUWA TUNASEMA KUWA TUNAPASWA KUFUMBUA MACHO. Kwani hatupendi wanachotufanyia wazungu kama enzi za ukoloni. Niombe tena radhi kama kwa mazungumzo yetu tumekukosea mpaka unataka kuacha block hii. ila ningekuomba uangalie mabadiliko yanayotokia hata hapo kijijini kwako, halafu fuatilia yametokeaje, nakuambia ukuta ni sheria zilizoingizwa na weupe kwenye serikali za nchi mpaka zimekufikia wewe au wale wanaoishi kijijini kama wazazi wangu. Mungu atusaidie.

  ReplyDelete
 7. Bwana Kamala;
  Sijui hata nianzie wapi kujibu "hoja" zako ulizoziibua hapo juu. Inavyoonekana, ulikuwa very emotional ulipoandika comments zako. Nilipokuwa naanzisha blogu hii nilikuwa naamini kwamba huu ungekuwa ni uwanja wa kujadili mambo kwa kina, bila woga na kwa kuzingatia pande zote tatu - ule unaounga mkono, unaopinga na ule usioegemea upande wowote. Na tena tungefanya hivyo kwa heshima. Ndiyo maana nikasema "Chakula kitamu na kichungu vyote vinaweza kumfanya mlaji akakunja uso". Nimeshtuka kidogo ulipofikia hata hatua ya kutoa tishio na hapa nanukuu..."kauli zenu za kisomi kama hizi, zaweza kunifukuza mahali hapa kwenye blogu hii kama mtaendelea kuangalia uafrika wetu kwa mkabala wa kizungu tu kwamba nyie mnajua upande mmoja tu" Mbona tusijadili mambo bila kutishiana? Mbona tunataka kuendeleza tabia zile zile tunazozilalamikia kwamba zimeidumaza jamii yetu kwa kutokuwajali watu wanaohoji mambo - hata kama wako upande hasi wa hoja? Yaelekea ulikuwa na siku mbaya ulipoandika maoni yako hayo na binafsi nashindwa kuamini kwamba eti huo ndio msimamo wako tisti. Kama hatuwezi kujadili mambo hapa kwa hoja bali jazba na mihemko tena bila kuheshimu hoja za upande kinzani kuna faida gani ya kuwa na hizi blogu???

  ReplyDelete
 8. ni vigumu kuelewana wakati mwingine ehe?
  sikumbuki mara ya mwisho ni lini nilpoongozwa na hisia.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU