NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, February 9, 2009

WAMAREKANI WANAPOMIMINIKA KWA "WAGANGA WA KIENYEJI"

 • Hali ya uchumi hapa Marekani ni mbaya. Watu wengi wamepoteza kazi zao, kazi hazipatikani na karibu kila jimbo lina matatizo ya fedha. Shule na vyuo vikuu vya umma vinapunguza wafanyakazi na kwa ujumla hali si ya kutia moyo. Katika msukosuko huu wa kiuchumi, watu hawawaamini tena wataalamu na washauri wao wa mambo ya fedha na badala yake wanamiminika kwa waganga wa kienyeji (a.k.a. watabiri au wapiga ramli) kuangalia bahati zao na mwelekeo wa mambo yao ya kifedha. Bei ya waganga hawa wa kienyeji wa Marekani ni ghali na inaweza kuwa kati ya dola 75 na dola 1,000 kwa saa moja – shilingi za Tanzania 75,000/ mpaka 1,000,000 kwa saa moja! Lakini watu hawajali bei hizi ghali na wanamiminika huko na biashara ya utabiri na upiga ramli ni kati ya biashara chache zinazotia fora katika kipindi hiki kigumu cha kiuchumi. Kinachoshangaza ni kwamba wengi wa watu wanaokimbilia kwa hawa waganga wa kienyeji ni wasomi na wenye (au waliokuwa na) kazi nzuri. Soma makala kutoka katika gazeti la New York Times hapa.
 • Niliposoma makala haya kutoka gazeti la New York times na kutazama habari na maoni ya wanasaikolojia katika televisheni jana kuhusu jambo hili, nilijaribu kulinganisha na suala la waganga wa kienyeji huko nyumbani ambao wameshapigwa marufuku kufanya kazi zao kutokana na sakata la mauaji ya maalbino. Tunajua kwamba Marekani ni taifa lililoendelea na lenye watu wengi ambao wamesoma. Kupamba moto kwa biashara ya utabiri na upigaji ramli katika kipindi hiki cha shida za kiuchumi kunatufundisha au kunatuambia nini? Pengine tunapaswa kujiuliza maswali ya msingi: Nani wanakwenda kwa waganga wa kienyeji? Kwa nini wanafanya hivyo? Ni kwa nini watu hawa wanakuwa tayari kutoa cho chote wanachoambiwa (mf. viungo vya maalbino, ngozi za binadamu, shilingi 1,000,000 kwa saa moja n.k.) na waganga hawa? Nini kifanyike? Japo inaweza kuwa ni hatua muhimu, mimi siamini kama kuamka tu siku moja na kupiga marufuku shughuli za waganga wa kienyeji kama serikali ilivyofanya bila kujibu baadhi ya maswali hapo juu ni suluhisho la kudumu la tatizo hili. Tukumbuke kwamba kitu kinapokatazwa huwa adimu na mara nyingi hadhi yake hupanda. Tusije kushangaa kuona kwamba hatua hii ya kuwapiga marufuku waganga wa kienyeji inawanufaisha na kuwaongezea hadhi zaidi badala ya kuwatokomeza (au lengo lolote ambalo marufuku ya serikali inakusudia kulitimiza).
 • Pata mtazamo mwingine wa suala hili kutoka katika gazeti la KIU (Februari 9-12). Hili ni gazeti la udaku na usitegemee kupata uchambuzi wa kina.
 

4 comments:

 1. Mheshimiwa mwandishi hapa nadhani unakosea. Jinsi ulivyoandika hapa kuhusu hawa ya wasoma viganja, mtu anayesoma hii habari na akawa nje ya hapa Marekani anaweza kuamini kabisa kwamba watu "wanamiminika" kwa hawa "wataalam".

  japo lengo lako linaweza kuwa zuri, kumbuka kwamba hawa watu huwa wana wateja wao fulani ambao "regulars'. Wana hata washabiki wao na naamini mara nyingi sio kwa sababu za kiganga kama sisi nyumbani tunavyokwenda kupiga ramli sababu ya hali ngumu kama ulivyosema. Mfano raper Snoop Dogg anasema huwa ana kama ki-addiction fulani na hawa watu na hivyo ni moja ya "mashabiki" kwa maana inawezekana huwa analipa pesa nyingi kutumia huduma huduma yao. Pia nadhani kwa sababu Larry King wa CNN huwa anawakaribisha kwenye show yake mara kwa mara naye unaweza kusema ana fascination fulani nao. Hawa si mifano ya watu wenye shida kwa vyovyote vile

  Naamini kuna wamarekani wa kawaida ambao wanawatumia psychics kwa sababu mahsusi ila sababu na wewe unaishi hapa Marekani bila shaka hutegemei kuna ulinganisho wa "matumizi" ya hawa watu ndani ya Marekani hii na sehemu nyingi za nyumbani.

  Point yangu haiko wazi sana ila nachotaka kusema ni kwamba, unapoweka post kama hii, ujue kuna watu nadhani unawapotosha kwa jinsi fulani - hasa ukizingatia kwamba kuna waswahili wengi wanaoamini -- tena kwa usahihi -- kwamba kama na wazungu wanafanya kitu fulani, na wao hawana budi kukifanya. Wamarekani hawaui Maalbino na ushenzi kama huo!

  ReplyDelete
 2. Hili jambo la kwenda kwa waganga limeanza miaka mingi sana huko Marikani. Tazama na chunguza hata seal na nimbo za wamarekani hata kwenye note – pesa zao.

  Wamarekani wana mambo ya kienyeji sana. Mimi nilizaliwa huko na kukulia huko hivyo ninajua ninachosema. Sema tuu hawa wenzetu wamaendelea hivyo si-kwamba ataenda kwa mganga kwenye nyumba ya makuti. Wanauza mafuta ya mapenzi, bahati, kuumiza wato na mengineyo. Pia wana conference na mikutano mikubwa sana ya white magic, black magic na mambo mengine mengi ya nguvu za giza.


  Marekani wanafanya the following:

  When I cast a spell on your behalf, you can change the following areas of your life - for the better:
  • Love
  • Money
  • Career
  • Friendships
  • Family
  • Sex
  • Well Being
  • Happiness
  These are the kinds of Magic in USA and Mexico
  Kinds of "Magic":
  A- Personal:
  1- White Magic, Black Magic, Ghosts.
  2- Witchcraft, Witch Doctors - Wicca
  3- Satanism, Black Mass.
  One "difference", between the kinds of Magic, is that "regular Magic" has a clientele, works at home, or in an apartment; the "Witches" have a Coven; "Satanism" a temple...
  B- Impersonal:
  4- Magic Prayers, Spells, Fetishes.
  5- Amulets, Talismans, Superstitions.
  6- Spoils (in Spanish: Despojos, Riegos... ).
  Haya ngoja ni acha haya maana mie ninaamini Mungu. Mungu ni mkubwa kuliko haya yote na Mungu ni more powerful than anyone of these darkness’s.

  ReplyDelete
 3. Anonymous hapo juu. Nimekupata sawia. Umesoma hiyo article kutoka katika gazeti la New York Times? Discovery Channel pia walikuwa na programu ya saa nzima kuhusu jambo hili. Hata History Channel waligusia jambo hili siku ya Wapendanao. Lengo langu hasa lilikuwa siyo kupotosha bali kuonyesha kwamba imani za "uchawi" na nguvu za kimiujiza ziko popote pale na pengine swali la muhimu zaidi tunalopaswa kujiuliza ni hili: ni kwa nini watu wanakwenda kwa waganga? Makala ya gazeti la New York Times inaonyesha kwamba Wamarekani wengi wanakwenda kwa hawa wasoma viganja kwa wingi hasa wakati huu wa hali mbaya ya uchumi. Je, inawezekana pia kwamba hata sisi huko nyumbani watu wengi wanawategemea waganga kwa sababu ya umasikini na hali ngumu ya uchumi? Na kwamba hata wale wachache waliofanikiwa wanadhani kwamba wataweza kunyang'anywa kile walichonacho na hawa watu wanaowaendea kwa waganga? Kwa nini watu wako tayari hata kuua watu wengine mfano maalbino ili waweze kutimiza masharti wanayopewa na hawa waganga ambao wengi wao ni masikini pia? Nilitaka tujadili jambo hili kwa upana na wala sikuwa na lengo la kupotosha wala kusifia. Kama "mama" alivyosema hapo juu, mambo haya yapo sana hapa Marekani na History Channel walifikia hata kusema kwamba Wamarekani wengi wanakimbilia Haiti kutafuta madawa makali zaidi ya uchawi. Swali linabakia pale pale, kwa nini watu wanakwenda kwa waganga wa kienyeji na wako tayari kutimiza masharti yo yote wanayopewa? Tufanye nini ili kupambana na tatizo hili hasa huko nyumbani? Kama alivyosema Ndimara Tigambwage -leo ni maalbino na kesho wanaweza kuja na sharti jingine. Tufanye nini?????

  ReplyDelete
 4. Suala la imani za kishirikina linanigusa sana mimi binafsi na linanipa uchungu na hasira SANA kwani limeleta kutoelewana ndani ya familia yangu mimi mwenyewe huko kijijini Muleba ninapotokea. Ni mpaka watu kama mimi tukiwa wazi kueleza yanayotusibu ndo labda tunaweza kuwa na mafanikio japo kuiweka jamii kwa jumla kuanza kuwa wazi kujiuliza maswali ambayo tunajiuliza sisi na hatimaye jamii kubadilika labda.

  Mheshimiwa Prof, mimi ndo nilipost kama anon hapo juu. Nitajaribu kufupisha mawazo yangu ila ningeweza hata kuandika kijitabu kuelezea mawazo yangu na upinzani wangu kuhusu suala zima la hizi imani zetu za ushirikina na za dini - katika jamii zetu za Kitanzania naamini imani hizi zina kufanana kwingi ukiziangalia kwa jicho la “madhara” yake.

  Nakuhakikishia kuwa, sina kumbukumbu ya rafiki yangu yeyote ambaye naongea naye kwa uwazi ambaye hajanambia masimulizi ambayo yanaendana na hali ilivyo ndani ya familia yangu mwenyewe. Kifupi ni kwamba kuna watu ndani ya familia yangu, wanasali vizuri tu na wakati huo huo wanaenda kwa waganga wa kienyeji kwa sababu mbali mbali kitu ambacho binafsi nisingekuwa na upinzani nacho iwapo maelekezo ya hao waganga wao yasingeingilia uhuru wangu mimi wa kwenda kijijini bila kupewa masharti ya kipumbavu kama vile naweza kumtembelea nani, kuongea na nani, kwenda wapi kwa kuaga au bila kuaga majirani fulani fulani au na kuhoji iwapo safari yangu ya kuelekea huko ni kweli ilikuwa ni mipango yangu au “nimeitwa” kwa madawa na hivyo nastahili ulinzi wa ziada nisidhurike. Bado hao waganga walipwe pesa zaidi kuhakikisha nafika salama nitakaporudi (kama wengine wanavyoamni ukiombewa sala na ibada ndo ndege haitalipuka angani) au kuhakikisha kwamba siamui kubaki Tanzania bali nirudi Texas. Ujinga mtupu!!

  Ni rahisi kwangu mimi au kwa mtu mwenye uelewa kama wewe Prof, kutambua na kuwaacha watu fulani vile walivyo na imani zao (japo kwa sasa) kwa kutambua kwamba sisi tuna utambuzi tulio nao kwa sehemu kubwa sababu ya shule - na mimi sio msomi kivile - walio gizani ni vigumu zaidi kuwabadili kwani minyororo iliyowafunga ni mikubwa mno - hasa kwa wale wasio na control ya aina yoyote ile na hatima ya maisha yao. Ila wanapotokea watu walioenda shule, waliotembea, waliofanikiwa kimaisha, wenye kila dalili ya utambuzi na ustaarabu lakini wenye hizi imani za mambo yasiyoweza kuhakikishwa hapo ndipo mtihani unapokuja. Wewe msomaji wangu hapa hauko nje sana na uzio wa huu ujinga ninaoulezea iwapo unaamini kabisa kwamba hivi vita vinavyopiganwa sehemu mbali mbali za dunia ni moja ya dalili za mwisho wa dunia - hii ni kwa wakristo - nilikuwa mtu wa dini pia, mfuasi wa Kristo huko nyuma.

  Ni wazazi wachache sana, ambao kwa makusudi huwadhuru watoto wao. Sababu wengi wa wazazi huwatakia watoto wao mambo mema na mafanikio, ndio maana sisi kama watoto huwasikiliza na huwaamini wazazi wetu. Kama wengi wetu wa kizazi hiki tulivyoingia ukiristo au uisilam sababu wazazi wetu tuliwakuta humo, vile vile, wazazi walio wazi na imani zao za kienyeji na ushirikina wao huwaelekeza na kuwarithisha watoto wao. Na ndio sababu kubwa nadhani ya ugumu wa sisi kama watu baki kubadili imani za watu wasioutujua - imani hizo wanatoa kwa watu wanaowaamini na wenye mamlaka halisi juu yao.

  Nambie: Iwapo mama yako mzazi, hii leo anataka upigwe chale kwa sababu “nzuri” anazojua yeye na hawezi kukwambia ukweli ni kwa nini, au hata akikwambia hukubaliani naye. Unakataaje iwapo huna historia ya kumkatalia chochote anachosema kama mama yako? Iliyonitokea mimi, ni kwamba, kwa sababu najulikana “ni mbishi” alipewa mtu dawa fulani ‘waliyeamini” ana ushawishi juu yangu ili anipige chale nikiwa Dar - nikakataa. Sijui lengo halisi lilikuwa lipi, ila sababu nilikataa hizo dawa na hiyo ilikuwa mwaka 2006, naamini nimekuwa nikifanyiwa “remote monitoring” tangu kukataa kwangu mpaka leo. Nikipata ajali leo nikafa hapa hapa Marekani au chochote “kibaya” kikanitokea, huyo mganga atajua tu na atasema hili limempata huyu kijana sababu alikataa dawa miaka mitatu iliyopita!! Hebu fikiria mama yangu mbinu atakazotumia kumpa dawa kama hizo ndugu mwingine ambaye “atadhihirika” kuhitaji “kinga” zitakazosemekana kutakiwa -- si ana “ushahidi” sasa wa athari za kukataa?. Usisome hapa ukadhani mzazi wangu ni mtu mbaya, au mwanga au namna gani. Ni mtu safi sana tu, ila ana udhaifu wa kuamini mambo haya yasiyoweza kuhakikishwa, kama ambavyo wewe mkristo unavyoamini biblia neno kwa neno (binadamu aliyedai kuwa Mwana wa Muumba kutembea juu ya maji, mimba yake ilikuwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na si tendo la ndoa, alifufuka akapaa zake Mbinguni, etc).

  Naamini kabisa mfano wangu ni kioo cha hali halisi kwenye familia nyingi na ndo kushamiri kwenyewe kwa imani hizi nchini mwetu. Familia yangu si familia iliyochoka sana, bado kuna imani za namna hii. Naamini mzazi wangu yuko tayari kufanya chochote anachoweza kuhakikisha watoto wake wanakuwa salama - hata kama watoto wenyewe hawakubali na au hawaamini. Kwa upande wa familia ya kwangu, kinachoniudhi kuliko yate ni kwamba mzazi ana support ya baadhi ya ndugu zangu ambao wana uelewa wa kutosha tu - watu ambao ningetegemea wangempa mwanga mzazi mwenyewe. Mimi nilijaribu sana kwa mbinu mbali mbali bila mafanikio mpaka leo. Unajua tena na mila zetu, wazazi wanachosema ndo hicho. Hao wengine ambao tungeweka nguvu pamoja labda tungefanikiwa, ndo hao nao wako “knee deep in the game”. Bado najikusanya tena naendelea kuumiza kichwa nijaribu mbinu gani.


  Tatizo kwenye post kama hizi watu hawaelezei masimulizi halisi yanayowahusu wao kwa ukweli na uwazi unaokaribia na masimulizi yangu haya. Na hivyo hata ukitokea mtu au watu wakapata nafasi murua ya kufikia Watanzania wengi, si raia wengi wataguswa kihalisi - watoa mawazo, mapendekezo, maelekezo n.k watatoa mifano ya wa Wamarekani, Wagiriki, Wachina na kadhalika na kuacha mifano hai ambao walengwa wangeweza “ku-relate” nayo

  Inapotokea mtu akajitokeza kueleza simulizi kama nilizosema hapa, mara nyingi mtu anakuwa “ameokoka” na anatoa “ushuhuda” kwenye steiji fulani au anakuwa katika hali ya “kupandwa na roho mtakatifu”. Katika hali zote hizo, unapomsikiliza mtu akisema anayosema, ni kama kumsikiliza mtu aliyelewa saaaana akikuelezea kitu cha maana na cha ukweli -- ni vigumu kumfuatilia anasema nini, utakachomuuliza kama follow up, sicho atakachokujibu n.k. Na kwa case za walokole watoa ushuhuda, huwezi hata kuuliza chochote - si jukwaa sahihi la kubadilishana fikira.


  “Mama” hapo juu, mbona watu hapa Marekani wanaonekana kuishi maisha yao tu na hayo mambo uliyosema hapo juu hayaonekani katika maisha ya kila siku? Huwa hata mimi nayaona matangazo ya hao wasoma viganja mahala mahala na ni kweli wana wateja fulani fulani ila kwa sababu ya mfumo mzima wa maisha wa hapa Marekani, hata bila uchunguzi wa kitaalam, ni wazi matumizi ya hao “waganga” ni tofauti na vile wanavyotumika nyumbani. Kinachonisikitisha kwa kusoma post kama ya huyu “mama”, ni utambuzi wangu kuwa, kwa usahihi tunawaamini wazungu kila wanachofanya. Hivyo kama ‘hata wao” wana imani za namna hiyo sisi pia hatuna budi kuziamini. Hapa inaniwia vigumu kutoa point yangu ila nataka tu kusema kwamba kuna watu ambao kwao matumizi sahihi ya taarifa kama ya “mama” hapo juu ni kuimarisha imani zao. Nikiwazia hivyo tu INANIUMIZA MOYO WANGU KABISA. Na ndo maana Prof pale mwanzo akanilewa kwa usahihi kiasi fulani kwamba nilidhani hata yeye kwa hii post yake kuna uwezekano ikazidi kupoteza watu.

  Ningekuwa na muda, ningemwambia “mama” hapo juu kwamba, kumwambia mtu aachane na imani za kishirikina awe mcha Mungu -- kama Mungu wake yeye alivyosema -- ni kama kumshawishi mtu mpiganaji wa vita fulani anayoamini kwa dhati sababu ya kuipigana asitumie AK47, bali atumie M16 -- badala ya kumshawishi kuweka silaha chini na kutumia njia mbadala labda. Bluntly ni kwamba japo unaamini kabisa kabisa Mungu wako ndiye sahihi, washirikina wengi hawako ndani ya game juu juu tu - wanaamini wanayoyafanya yana mafanikio na wanaweza kukupa vidhibiti vingi sana kukuhakikishia imani zao zinawasaidia - watu wanakufa kwa ushenzi wa hizi imani: Bush kasababisha vifo vingi tu, ulokole wake ukiwa kiongozi chake kimojawapo, Osama kaua makafiri na mazayuni wengi tu sababu ya imani zake, watanzania wakristo wengi hii leo wanaposikia Wapalestina wakiuawa ovyo na kuonewa na Waisraeli hawaoni kosa kwani wanaamini hilo ni Taifa Teule linaloweza kufanya linavyotaka mpaka mwisho wa dunia. Ni mpaka Albino auawe toka kwenye familia yake ndo labda mtu aweze kutambua athari halisi za imani za ushirikina. Dini pia zina athari zisizo wazi moja kwa moja kama ushirikina japo huo ni mjadala tofauti ndo maana siamini kama ni pendekezo zuri la kumpa mtu mwenye imani za kishirikina kama imani mbadala - japo natambua katika short term bora imani za dini kuliko ushirikina.

  Nadhani kwa sababu ya uwezo mkubwa sana wa bongo zetu kama binadamu, uwezo wa kujiuliza tulianza vipi na nini hatima yetu kama binadamu na hii dunia yetu hii ndo chanzo kikubwa cha yote yaha: dini zote hizi kubwa na ndogo, imani za kienyeji na ushirikina wa kila aina. Kundi pekee la watu walio na uhuru halisi na uhalali wa kukemea matendo ya kishirikina na imani zote za mambo yasiyokuwa na uhakika, ni watu wasiomini miungu wowote wale - Kashasira, Yehova, Yesu, Muhammad, Papa wakiwa ndani la kundi la hiyo Miungu na wapambe wao. Samahani “Mama” hapo juu.

  Mimi ni muhanga wa hizi imani kama ulivyo wewe msomaji, uwe unatambua hili au la. Nitatoa maoni yangu kila nipatapo nafasi katika hili, kwani nina mengi, marefu na ya kina zaidi nikipata watu wa kunisikiliza.

  Toa maoni kidogo Prof au yeyote atakayesoma hii post yangu.

  Kwa uchungu, NAOMBA KUWAKILISHA

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU