NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Sunday, March 22, 2009

TAMADUNI ZINAPOGONGANA

 • Nilishangazwa na mshtuko walioupata wanafunzi wa Kimarekani baada ya kuwaonyesha picha hii ya keki ya arusi ya Kichaga. Wengine mpaka ilibidi watoke nje ya darasa kwenda "kujikusanya" na wengine walisema huu ulikuwa ni unyama wa kupindukia. Niliwaambia kwamba hata wao walikuwa na vipengele vingi tu katika utamaduni wao ambavyo vingeweza kuwatia kichefuchefu Waafrika. Niliwakumbusha kwamba kumbe hata wao hawakuwa na tofauti na babu zao wa Ulaya waliokuja katika bara letu na kuita karibu kila kitu kuwa kilikuwa cha kishenzi. Sijui mshenzi alikuwa nani - yule mgeni mjinga asiyeelewa utamaduni wa mwenyeji na hataki kujifunza au mwenyeji anayeyajua vizuri mazingira yake na kujivunia utamaduni wake uliomkuza na kumlea? Niliwaambia hawa wanafunzi kwamba tabia yao hii ya kutotaka kujifunza na kutokuwa na uvumilivu na tamaduni zingine ndiyo imewaletea matatizo katika vita vyao vya Iraq na Afghanistan - ambako walidhani kwamba silaha zao kali za kutisha na mabilioni ya dola yangeweza kushinda utashi na utaifa wa watu. Mwisho wa darasa walikuwa wamesuuzika na wale wenye mtazamo mpana waliahidi kuziangalia tamaduni zingine kwa heshima na jicho jumuishi.
 • Hata hivyo ni lazima nikiri hapa kwamba hawa jamaa waliokuja "kutustaarabisha" walifanya kazi nzuri mno ya "kutustaarabisha" kifikra na kutushenzisha; na kutufanya tuamini kwamba utamaduni wetu ulikuwa wa kishenzi. Ndiyo maana leo hii tunaiga kila kitu cha kigeni na kudharau vya kwetu. Ndiyo maana baada ya miaka zaidi ya hamsini ya uhuru bado tunafundishana "mlima Kilimanjaro uligunduliwa na ...." Chanzo cha mto Nile kiligunduliwa na..." Nitaandika kwa kirefu juu ya mada hii katika makala itakayotoka katika gazeti jipya la Jamii Kwanza. Tumalizie na maneno ya Steve Biko - yule mwanaharakati shujaa wa Afrika Kusini asiyetetereka aliyeuawa kikatili na makaburu..."the most potent weapon of the oppressor is the mind of the oppressed"

8 comments:

 1. Kusema kweli inasikitisha sana sisi waafrika tunavyoiga tamaduni za kigeni na kuaacha tamaduni zetu za asili ambazo ni nzuri kabisa.Kwa sababu sasa imefikia mahali mpaka waafrika hawataki rangi zao, hawataki nywele zao jamani vipi?

  ReplyDelete
 2. Profesa umenena. Unajua kitu kizuri ukiwa vitani ama kwenye mapambano yoyote ni kujua kuwa adui yako mkuu ni adui yake mwenyewe. Yaani ukishaweza kumgawa na kumtawala akili kisha ukamfanya asijithamini basi hapo "unaye".
  Na ndio kilichotokea. Sasa hivi watu wanadhani kuelimika na kustaarabika ni kukana mambo yetu ya asili (na hapa nazungumzia yale yasiyoathiri maisha yetu) na kutumikia yale ambayo yamegeuzwa kufanywa ya kimagharibi. Yaani modification ndogo tu yasomba umati. Na mbaya zaidi ikiwekewa kigezo cha "kuiona mbingu" basi watu wanakana kwao, wanakana majina na njia zao za kuishi. Wanadiriki hata kuita yale ya kwao ni upuuzi. Eti kwa kuwa si ya kimagharibi. Sasa hao wanafunzi nao wana issue. Wanatakiwa kutambua kuwa namna waonavyo tatizo ndio tatizo. Nakumbuka kama wiki mbili zilizopita tulipokuwa darasani tulikuwa tukizungumza / kujadili kuhusu mashujaa wetu na swali la kwanza kwa Professor wangu likawa SHUJAA NI NANI naye bila kusita wala kumeza mate akasema kuwa ni yule ambaye yuko tayari kufa kwa ajili ya jamii yake, nami bila kumeza mate nikamuuliza kama anaweza kusema kuwa Yassir Arafat ni shujaa na akaishia kujimwayamwaya. Nikamuuliza kama ushujaa na ugaidi unatokana na mazingira na jamii na kama anaamini kuwa hawa wanaowaita magaidi sasa waliwahi kuwa mashujaa wao na hata mashujaa wa sasa kina Mandela waliwahi kuwa magaidi kwa mtazamo wao. Akasema ndio. Nikamwambia kuwa kuna mambo ambayo huwezi kutafuta upande mmoja ulimwenguni. Na hao "wapendwa" wanafunzi walistahili kuelewa kuwa kwa tofauti ya mazingira, mifumo ya maisha, maendeleo na hata mila na tamaduni, si kila kitu (ama niseme vingi ya vile wajuavyo) vitakuwa tofauti.
  Hawa ndio wale ambao hawajawahi kula nje ya nyumbani kwao na katika akili zao wanaamini kuwa HAKUNA MPISHI BORA ZAIDI YA MAMA YAO.
  Wanahitaji maombi hao

  ReplyDelete
 3. Topic yako kwa kweli is so fun! and important! Naipenda kweli. Natarajia kusikia mengi ihusuyo kwani nimekuwa nikifikiria pia. Nilikuwa nawauliza rafiki zangu wanafikiria nini kuhusu picha hii, mmoja alionesha kushangaa sana, hata kusikitika.

  ReplyDelete
 4. aisee, unajua hata watu wanaofanya huo ushenzi wanashangaa na kukusaidia kusikitika unapousema hadharani. mammbo mengine bwana, tumefungwa akili mpaka hatuoni tatizo letu lilipo.

  basi tukutane katika hoja nzito kupitia kwanza jamii, juma nne

  ReplyDelete
 5. Yasinta na Mzee wa Changamoto. Nimewasikia vyema. Kinachonipa wasiwasi mimi ni nini kitatokea huko mbele. Tutaendelea kuwa Wasukuma, Wahaya, Wangoni n.k? Tumefikia sasa mahali ambapo tunaziona hata lugha zetu na makabila yetu - kama kinavyosema kizazi cha dot com - kuwa ya "kirugaruga" - yaani ya kishamba. Swali ni hili: Je, waweza kuwa Mhaya hata kama hujui Kihaya na utamaduni wa Kihaya? Je, ni kweli Mfaransa anaweza kusema kwamba yeye ni Mfaransa hata kama hajui Kifaransa na utamaduni wa Kifaransa. Je, kama tunakikana Kihaya na Uhaya wetu, tutakuwa nani? Utumwa mbaya sana huu!!!

  Laiser, hao marafiki zako walioshangaa na kusikitika ni wazungu au Waafrika? Kama ni wazungu, ulijaribu kujitetea au?

  ReplyDelete
 6. wenzetu kutoka "Asia" hata awe ameishi ughaibuni, let say, for more that 20 years! ukimuuliza "where are you from?" atajibu " i am from India of Pakistan! wakati kuna waafrika au watanzania wako tayari kuukana uafrika au utanzania wao,ukimbana sana atajibu, "i am Tanzanian by parentage! halafu tunalalamika kuwa we are not respected! mtu atakuheshimu vipi wakati wewe mwenyewe unajidharau, kujiona duni na kutojiheshimu? kwa mfano kwa sisi tulioko ughaibuni wakati mwingine tunakuwa na hamu na mambo ya nyumbani hivyo kwa wakati mwingine ni kawaida wikiendi mtu kwenda kwenye club za kiafrika, utashangaa nyimbo zinazopigwa huko ni za akina 50 cent, Beyonce, Usher na wengineo, ukiuliza kwa nini utaambiwa aah unajua walioko humu si waafrika peke yao wamo wazungu pia! na pengine hawa wazungu wanaoingia kwenye hizi african club ni wale wenye nia ya kujifunza mambo ya kiafrika ikiwa ni pamoja na muziki wetu. Kwa hiyo tunapoona wanzetu wanashaanga na kupuuza desturi zetu (mfano mila)za kiafrika tusiwe wakali kwani sisi wenyewe tumeshindwa kuutangaza na kuutetea uafrika wetu! tujirekebishe kwanza sisi kabla hatujawalaumu wageni.

  ReplyDelete
 7. Bwana Daudi;
  Umegonga pointi kabisa. Kama tunauonea haya Uafrika wetu ni nani ambaye atajivunia? Juzi juzi hapa nilikutana na jamaa kutoka Congo amejisiriba hereni katika masikio yote. Mimi nilijua kwamba ni Mwafrika kwani sisi Waafrika hata tujifanye vipi, tunajulikana tu. Basi miye nikamsalimia na nilipomwuliza anatoka nchi gani Afrika akasema yeye hatoki Afrika. Baadaye akabadilisha gea na kusema kwamba anatoka Congo lakini amekulia Paris na hajui kabisa mambo ya Congo na hajafika huko...Hakuna utumwa mbaya kama wa FIKRA na hawa wakoloni walituweza kweli!

  ReplyDelete
 8. Wazungu walifanikiwa kuuwa lugha za watumwa waliowapeleka Marekani Kabla ya hapo watumwa waliweza kuwasiliana bila mabwana wao kuelewa na hii waliona ni hatari kwao, walifikiria njia ya kuua lugha za asili watumwa walizokuwa wanazitumia na njia ilikuwa kuwapeleka watoto wote katika shule za boda na kule watoto walifundishwa lugha ya wazazi wao ilikuwa ya kishenzi. Si muda mrefu lugha zote za asili zilikufa marekani.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU