NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, March 5, 2009

WANAHISABATI WA KESHO...

Nakumbuka enzi zile nikisoma darasa la kwanza pale Shule ya Msingi Sima (Bariadi), tulikuwa tunatumia vijiti. Mimi nilikuwa na vijiti 100 nilivyokuwa nimevichonga kwa ustadi mkubwa sana. Ijapokuwa nilikwenda darasa la kwanza nikiwa tayari najua kusoma, kuandika na kuhesabu (kujumlisha, kugawa n.k.) ilikuwa bado lazima kuwa na vijiti. Japo mabinti zangu hapa wao wanajifunza haya mambo kwa kutumia picha na michezo ya kufurahisha katika kompyuta, vijiti na vifuniko vya soda hivi vinaonyesha ubunifu wetu wa kutumia kile tulichonacho katika mazingira yetu na kukifanya kile tunachojifunza kionekane chetu na chenye maana zaidi. Ubunifu huu hata hivyo hufifia mapema mtoto anapoanza kwenda madarasa ya juu ambako mkazo huwa katika kukariri zaidi na elimu huwa tena haihusiani kabisa na mazingira yanayomzunguka. Kwa mfano, kuna anayejua ni kwa nini tulikuwa tunakariri Jedwali Radidi la Elementi (Periodic Table of Elements)? Je, elementi hizo hazipo katika mazingira yetu? Elimu yetu masikini - mtu unakariri (au unadesa), unaandika ulichokariri katika mtihani, unapata A - unasonga mbele (hata kama hufahamu cho chote). Halafu kesho unapewa kazi unaboronga watu wanaanza kulalamika. Nani wa kulaumiwa?

5 comments:

 1. Nami pia umenipeleka mbali sana tena mimi ndo nilikuwa natumia matete. kazi kweli kweli

  ReplyDelete
 2. Jedwali Radidi la Viasili, nimekumbuka mbali sana. nilipokuwa shule ya msingi darsa la saba. tayari nilikuwa najua viasili ishiri vya mwanzo

  ReplyDelete
 3. Kweli kabisa kuwa tulikuwa tukijiweka karibu na mazingira. Ile elimu "isiyo rasmi" ambayo hutufunza kuwa tunavyostahili kuwa kulingana na mazingira na majukumu haipo tena. Tulikuwa tukifunzwa kuwa watu bora kwa familia. Wamasai kwa kazi zao, wasukuma kwa kilimo chao, wahaya kwa uvuvi na kilimo chao na mengine mengi. Kinadada nao wakilelewa na kuandaliwa kuwa wanavyotakiwa kuwa katika misingi ya kifamilia na kutimiza majukumu yao. Lakini kinachotokea sasa hivi ni kufuata yale yafunzwayo na waheshimiwa ambayo kwao yana maana nasi kwetu hayatufai hata kidogo. Dunia imegeuka yenye elimu lakini isiyi erevu. Ukisoma kwenye PARADOX OF OUR TIME ambayo ipo kwenye blog yangu chini ya "LABELS" na ambayo naipenda saana maana yaonesha uhalisia wa tulipo utaona mengi ambayo licha ya kujionesha, bado hakuna anayeshituka kujiuliza kulikoni. Ni kwa sababu hiyohiyo ya kukariri bila kujua ama kuangalia bila kuweka mkazo katika kuona ama kusikia bila kuhakikisha umeelewa, tunaona namna ambavyo mwandishi wa Paradox hiyo amesema "We have more Degrees but less common sense; more knowledge but less judgment. We have more experts but more problems; more medicine but less wellness.". Ni kwa kuwa hatufunzwi kukinga bali kutibu. Hatuyaangalii maisha yetu kuanzia kwetu bali kuelekea kwetu. Kwa hiyo twajitahidi kukimbilia kuliko na unafuu kulingana na tunavyokimbizwa na maisha. Ndio maana watu hawafanyi kazi watakazo, bali zitakazowapa kipato. Ni kwa maana hiyo tunapojikuta tunajikimbia wenyewe na hatutumii yaliyopo maana hatukuwa na nia ya kuwa nayo tulipoanza kuyatumia bali tumeyatumia ili msimu ama nyakati fulani zipite.
  Msome mwandishi wa hiyo Paradox alivyosema hapa kuwa "We build more computers to hold more info, to produce more copies but have less communications.
  .We’re long on quantity but short on Quality.
  .These are the time for Fast food and slow digestion"
  BLESSINGS

  ReplyDelete
 4. Nafikiri wa kulaumiwa ni sisi wenyewe. Kwa nini tunakubali kukariri mambo ambayo tukiisha "kuyameza" tunashindwa kabisa kuyahusisha na mazingira yetu halisi?

  Tunahitaji majadala mpana katika hili. Tukubaliane ni elimu gani tunaihitaji kwa manufaa yepi. Sioni kama ni lazima kuurithi mfumo uliopo wa kumezeshana nadharia zisizo na kazi ya maana katika kutuletea maendeleo. Elimu ya kweli itufunze mambo yanayotuhusu.

  ReplyDelete
 5. Nakubaliana nanyi. Mzee wa Changamoto - hiyo paradox yako ndiyo kitu cha kwanza ambacho niliiba kutoka katika blogu yako na ninayo hapa ofisini kwangu. Inaonekana tunakwenda mbele kwa kurudi nyuma. Bwaya - ni kweli. Hii elimu ya kukaririshana majedwali radidi ya viasili hata bila kujua hivyo viasili ni nini, viko wapi na vina faida gani kwako haitatufikisha po pote. Kama kweli tunataka kuendelea ni lazima tutafute mfumo mpya wa elimu - elimu ambayo itatukaramsha na kutufanya tuwe watu tunaofikiri kwa vitendo katika mazingira yetu wenyewe. Katika makala yangu ijayo nitazungumzia suala la mparaganyiko katika lugha yetu ya kufundishia kwani naamini kwamba sera hiyo kama ilivyo sasa inachangia kwa kiasi kikubwa sana katika kukariri kwetu.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU