NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, April 16, 2009

KUSTAWI NA KUANGAMIA KWA JAMII

Umeshawahi kujiuliza ni kwa nini jamii zingine hustawi na zingine huangamia? Ni kwa nini kwa mfano dola kubwa kama Mayan liliweza kuangamia na kupotea kabisa? Alhamisi iliyopita (tarehe 9 April, 2009) nilihudhuria mhadhara ambao ulitolewa na Jared Diamond - mwandishi wa vitabu viwili mashuhuri kuhusu masuala ya kustawi na kuangamia kwa jamii (Collapse na Guns, Germs and Steel).

Mwandishi huyo anatumia vigezo vinne kuweza kubashiri ni jamii au dola gani ambazo zinayo nafasi ya kustawi na zipi zinaweza kuangamia (kama Historia inavyotufundisha). Vigezo hivi ni: hali ya mazingira, serikali, matumizi ya maliasili, marafiki na maadui. Alisema kwamba jamii ya binadamu na dunia nzima kwa jumla ni kama yai linaloengwaengwa huku na huko kwani katika jina la sayansi binadamu ameweza kujitengenezea na kujirundikia silaha ambazo zinaweza kumtokomeza asionekane kabisa katika uso wa dunia. Kama ataibuka kiongozi mwingine "mwehu" kama Adolf Hitler na kuamuru kutumia silaha za kinuklia basi jamii karibu zote hapa duniani zitaangamia. Hata hivyo alitupoza wasikilizaji wake kwa kutuambia kwamba kulingana na protokali zinazolinda silaha hizi, maangamizi yetu kutokana nazo pengine si jambo rahisi sana kutokea.

Kilichonivutia katika mhadhara huu - na ambacho hakitiliwi maanani sana katika vitabu vya Kihistoria, ni ukinzani wa kimatabaka ambao alisema ndiyo umeangamiza jamii na madola mengi pengine kuliko sababu nyingine yo yote. Alisema kwamba unapokuwa na jamii yenye watu wachache ambao ni matajiri kupindukia na umma ulio mwingi ukawa katika umasikini mkali, basi hizi ni dalili za mwanzo wa mwanzo wa kuangamia kwa jamii. Hawa masikini watavumilia lakini mwishowe uvumilivu wao utafika kikomo na hapo ama watagoma kuzalisha mali (ambayo ndiyo tegemeo kuu la dola) ama wataamua kupambana. Alisema na hapa nanukuu "Eventually, a gated community cannot keep the people outside the gates" Hatua hii inapofikiwa basi mwanzo wa mwisho wa jamii hiyo unakuwa umefikiwa. Mwandishi huyu anaamini kwamba dola kubwa la Maya lilianguka kwa sababu ya mapinduzi ya tabaka zalishi yaliyosababishwa na ubwete wa tabaka tawala ambalo kamwe halikuweza kushughulikia matatizo ya wananchi yakiwemo shida za kimazingira.

Niliondoka katika mhadhara huu nikiifikiria nchi yangu Tanzania na historia yake fupi. Je, tabaka la mabilionea wachache (wenye "vijisenti vyao") na tabaka la masikini wasio na kitu yatasimamiana na kukodoleana macho kwa amani mpaka lini? Je, utafika wakati ambapo tabaka zalishi litasema "sasa yatosha liwalo na liwe?" Nina matumaini kwamba hatutafikia hatua hii kwani ninaamini kwamba tunao viongozi makini ambao, kama kweli wanaitakia mema Tanzania a.k.a Kisiwa cha Amani, a.k.a Bongo, a.k.a. Nchi ya Vijisenti basi watahakikisha kwamba tabaka zalishi kamwe haligoti katika mwisho wa mwisho na kubwaga manyanga chini. Watahakikisha kwamba tabaka zalishi linaweza kupata elimu, afya pamoja na uhakika wa kujipatia mlo na mahitaji mengine ya lazima, hali ambayo italiwezesha kuendelea kuwa na matumaini ya kuishi na kuiona kesho. Kwa hali hiyo naamini na kutumaini kwamba Tanzania YENYE AMANI itaendelea kuwepo kesho na kesho kutwa. Mungu ibariki Tanzania!

2 comments:

  1. nipo karibu tu hapa kaka nakusoma na kutafakari haya mambo. nawaza zaidi ya kasi ya upepo huku nikihifandhi kumbukumbu kwa mwendo wa kobe kwani najua uvumapo upepo hutulia kwa hiari.

    kunaguka ni lazima na hii ipo kwa miaka michahce ijayo, ingawa jitihada kubwa za kuangamiza kizazi cha waafrika lakini nachelea kusema kwamba hakitaanguka,kitadumu na wale wanaotazama mbali wataona ukweli. historia ni mwalimu mkuu wetu

    ReplyDelete
  2. Karibu bwana Mpangala. Usiwe unapotea hivyo!

    Ni kweli kizazi cha Kiafrika kimepita katika misukosuko mikuu kikashinda. Nakubaliana nawe kwamba hakitaanguka!

    ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU