NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, April 29, 2009

MWALIMU NYERERE - NABII ALIYEHUBIRI NA KUTENDA ALICHOKIHUBIRI

Makala hii imetoka katika gazeti la Jamii Kwanza la Jumanne (28/4/2009).
===========================================
Mwalimu Nyerere: Nabii Aliyehubiri na Kutenda Alichokihubiri
 Dkt. Masangu Matondo Nzuzullima
 
Mengi yameshasemwa kuhusu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika siku za hivi karibuni hasa kutokana na tamasha lililoandaliwa na wanazuoni wa Tanzania wakishirikiana na wenzao wa nje. Lengo langu katika makala hii siyo kurudia ambayo tayari yamekwishasemwa juu ya Mtanzania huyu hodari bali ni kumtazama Mwalimu Nyerere kutokana na maneno yake mwenyewe na kauli zake mbalimbali. Nimeamua kufanya hivyo baada ya kukipata na kukisoma kitabu chake cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania ambacho alikiandika mwaka 1993 na kuchapishwa na Zimbabwe Publishing House. Hiki kilikuwa ni kipindi ambacho nchi ilikuwa inapita katika misukosuko ya kiuongozi na Muungano wa Tanzania na Zanzibar ulionekana kuwa hatarini kutokana na kuibuka kwa kundi la wabunge waliokuwa wakidai serikali ya Tanganyika.

Mwalimu Nyerere alisimama kidete kuupigania Muungano na kuhakikisha kwamba nchi yetu inapita katika msukosuko huu kwa usalama. Akiamini kwamba "Tanzania ni lulu ya pekee kabisa katika historia ya Afrika huru" kwani "Nchi nyingine zote ni za kurithi kutoka katika Ukoloni" wakati "Tanzania ni ya kuundwa na sisi wenyewe, kwa hiari yetu wenyewe, baada ya kukomboa sehemu zake mbili kutoka ukoloni" (Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, uk. 57), Mwalimu hakuwa tayari kukaa pembeni na kushuhudia nchi ikiserereka kuelekea gema la hilaki . Hapa chini ni kauli zake mbalimbali kuhusu mambo mbalimbali ya muhimu yaliyokuwa yakilikumba taifa katika kipindi hiki. Katika kauli hizi unaweza kuuona uwezo wake wa kinabii, uwezo wa kuona mbali na kupima mustakabali wa nchi kwa darubini kali ya fikra na hali halisi ya wakati uliopo; ukweli usio na hofu pamoja na upendo wa kweli kabisa aliokuwa nao kwa Tanzania yake aliyoipenda. Kauli zote hizi zinatoka katika kitabu nilichokwishakirejerea hapo juu: Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, Zimbabwe Publishing House, 1993.
Aliposikia tetesi kwamba baadhi ya wakereketwa wa CCM walikuwa wameanza kampeni za kutaka rais Mwinyi aongezewe vipindi vya muda wa kuwa rais, Mwalimu Nyerere hakupendezwa na jambo hilo na mara moja alikwenda kwa Rais Mwinyi na kumsihi azizime kampeni hizo. Pia aliwatafuta viongozi wa kampeni hizo na kuwaomba wasilifuatilie jambo hilo. Aliposikia kwamba jambo hilo la rais Mwinyi kuongezewa vipindi vya kuwa rais lilikuwa bado linazungumzwa hata baada ya juhudi zake kulizima alikereka na kusema maneno yafuatayo:

"Plato, Myunani wa kale, alipendekeza kuwa mafilosofa ndio wanaofaa kuwa watawala wa nchi, maana wana sifa mbili muhimu: kwanza wana uwezo wa kutawala, na pili hawapendi kutawala. Kwa hiyo Jamhuri ya Plato itakuwa na sheria ya kuwalazimisha mafilosofa kutawala kwa zamu; na mtu zamu yake ya kutawala ikiisha, atafurahi sana kurudia shughuli zake za falsafa ambazo ndizo hasa anazozipenda. Lakini nchi zetu hazitawaliwi na mafilosofa wa Plato; watawala wetu ni wanasiasa wa kawaida ambao wanapenda sana kutawala, hata kama hawana uwezo wa kutawala; na ambao wako tayari hata kuhonga ili wachaguliwe kuwa watawala, na wakisha kuchaguliwa hawatoki bila kulazimishwa. Si busara kuwaachia wao wenyewe ndio wawe waamuzi wa lini waache kuwa watawala" (ukurasa wa 8)

Utabiri huu unaendelea kutimia. Chaguzi zetu sasa (hata zile za udiwani tu) zimegeuka kuwa miradi ya watu matajiri tena inayoghalimu mabilioni ya shilingi. Kule Bariadi Magharibi katika uchaguzi uliopita mgombea mmoja alikuwa anagawa pesa, chumvi, sukari, kanga,vitenge, mabati, baisikeli na hata pikipiki. Kwa vile, kama wasemavyo wazungu, "there is no free lunch:" "hakuna cha bure", mabilioni haya ni mradi wa mtu na ni lazima yarudishwe siku moja. Halafu wanasiasa hawa wakija kuibuka na "vijisenti" vyao, tunapiga makelele na kushangaa utadhani kwamba hatukujua. Rushwa katika chaguzi zetu ni tatizo kubwa linalofuta kabisa maana nzima ya demokrasia na kuzigeuza chaguzi hizi kuwa bidhaa tu zinazoweza kununuliwa na watu wenye mapesa yao.
 
Katika hoja ya kugombea serikali ya Tanganyika, hoja ambayo Mwalimu aliipinga kwa nguvu zake zote, aliyevishwa lawama ni waziri mkuu (pamoja na katibu mkuu wa CCM) wa wakati ule. Lakini pia alikerwa zaidi na kushindwa kwa raisi Mwinyi kumfukuza kazi waziri wake mkuu kutokana na kigeugeu alichokionyesha kwa kupinga hoja ya serikali ya Tanganyika bungeni na baadaye kubadili msimamo na kuunga mkono hoja hiyo. Alisema yafuatayo kuhusu jambo hili:

"Waziri Mkuu si mpishi wa Rais, hata tuseme kuwa maadamu Rais mwenyewe anayapenda mapishi yake, sisi wengine tusipoyapenda si kitu. Waziri Mkuu ni Mpishi Mkuu wa Tanzania nzima. Kama hatupendi mapishi yake, au kaanza kutupakulia vyenye sumu, au kachoka, au kashindwa kupika, ni wajibu wetu kumwambia Mwajiri wake ateue mpishi mwingine."(ukurasa wa 48).

Kwingineko anaendelea kusema hivi kuhusu jambo hili.

"Pengine inafaa niseme kwamba inashangaza na kutisha kidogo kuona kuwa kujiuzulu kwa Waziri ye yote kunafanywa kuwa ni jambo la kuvutana au la kubembelezana...lakini hata hivyo ni jambo la kushangaza kidogo kwamba Viongozi wetu wa Mageuzi, hata bado hatujafa, wanaona kuwa ni kosa kuwakumbusha kuwa vyeo walivyo navyo ni dhamana. Wanadhani kuwa uwaziri ni usultani: ukisha kuwa sultani utakufa sultani! Nadhani wanakosea. Nchi hii imewahi kung'oa masultani wa kila aina. Tukianza kuvumilia masultani wa kuchaguliwa tutapanda mbegu ya masultani wa kuzaliwa" (ukurasa wa 45)
Sote tunajua kwamba ukishakuwa waziri basi ni nadra sana kufukuzwa kazi. Hata uboronge vipi, hasa hasa utaambulia kubadilishwa wizara tu na au kupangiwa kazi nyingine. Hata hivyo jambo hili limeanza kuchukua sura mpya kutokana na kushuhudia kwetu mawaziri kadhaa wakiwajibika na kujiuzulu wenyewe. Hili, kwa maoni yangu, ni jambo jema linaloonyesha kwamba, japo safari yetu bado ni ndefu, demokrasia yetu changa inazidi kuimarika.
Mwalimu Nyerere pia hakuogopa kusema ukweli, hata kama ulikuwa ukweli mkali tatanishi. Hakukubali kukaa kimya huku akishuhudia nchi ikiyumbayumba. Kuhuhu uwezo wa Rais Mwinyi kutawala na utaratibu mzima wa marais kukabidhiana madaraka kwa usalama alisema yafuatayo:

"Rais Mwinyi ni mtu mwema na mpole, lakini ni kiongozi dhaifu; na upole wake na udhaifu wake unatumiwa na watu ambao wala si wema wala wapole kuhatarisha umoja na amani ya nchi yetu. Kipindi chake cha pili kinakaribia kwisha...Kwa sababu ya minong'ono-nong'ono ya watu wasioona mbali kuhusu Rais, na kubabaishwa anakobabaishwa na washauri wake wakuu, nililazimika kuiambia wazi wazi Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi kwamba najiona kuwa ninao wajibu wa kumsaidia Rais amalize kipindi chake salama. Kipindi cha mpito, cha kujaribu kujenga utaratibu wa kikatiba wa kubadili uongozi wa nchi yetu kwa heshima na amani hakitakamilika mpaka hapo Rais Mwinyi atakapomaliza kipindi chake kilichobaki kwa usalama, na kumkabidhi madaraka Rais mpya kwa utaratibu ule ule uliompa madaraka hayo" (uk. 50-51)

Katika kipindi hiki serikali ilionekana kuwa imeparaganyika na kukosa mwelekeo na Mwalimu Nyerere aliamini kuwa ubovu wa uongozi katika Chama cha Mapinduzi na serikali yake ulikuwa umefikia kileleni kabisa. Unaweza kuiona hasira yake katika maneno yake yafuatayo:

"Waingereza wana msemo: "Nature abhors a vacuum", "hulka huchukia ombwe". Hata siasa huchukia ombwe. Kama uongozi ni mbovu, upo kama haupo, au upo kwa maslahi ya wenyewe, watatokea watu waujaze uwazi uliopo; hauwezi kuachwa wazi hivi hivi. Lakini uongozi mbovu ni kama mzoga, una tabia ya kukaribisha mafisi na mainzi. Tusidhani kuwa hulka ya siasa yetu ni tofauti na hulka ya siasa ya watu wengine; kwamba sisi tunaweza kuvumilia uongozi mbovu na tusivune matunda ya hulka ya uongozi mbovu" (uk.52)

Katika suala hili anaendelea kusema yafuatayo:

"Kwa maana moja sasa hatuna serikali, tuna mawaziri tu. Serikali ni timu; na timu halisi ina dira na rubani. Mkusanyiko wa mawaziri bila mwelekeo, bila mwongozo, bila mshikamano na bila uongozi, kila Waziri na lwake, hauwezi ukaitwa serikali. Katika hali kama hiyo, hata bila ubovu mwingine wa nyongeza mambo muhimu ya Nchi hayawezi kujadiliwa wala kushughulikiwa" (uk.53)

Kwingineko aliwaonya wananchi kutowaogopa viongozi wao kwani viongozi wanapaswa kuheshimiwa na siyo kuogopwa. Na wanapotenda mambo ya haramu kama hili la kutaka kuunda serikali ya Tanganyika basi wananchi inabidi wakatae kwani kufanya hivyo ni haki yao.

"Kukubali kufanywa vikaragosi vya Viongozi ni dalili ya woga, si dalili ya heshima; na woga na heshima ni vitu viwili mbali mbali. Maadili mema yanatutaka tuwaheshimu Viongozi wetu, madhali wanajitahidi kutimiza wajibu wao. Maadili mema hayatudai tuwaogope Viongozi wetu. Na viongozi makini hupenda kupata heshima ya wananchi wenzao, lakini hawapendi kuogopwa. Kuogopwa ni sifa na ada ya madikteta, viongozi halisi hawapendi kuishiriki. Kujenga mazoea ya kutii viongozi hata katika mambo haramu ni dalili ya woga, ni kukaribisha udikteta." (uk.65)

Mwalimu Nyerere alikuwa amechoshwa na ubovu wa uongozi katika Chama cha Mapinduzi na hata mustakabali wa kisiasa na kiuongozi ndani ya vyama vya upinzani. Tazama kauli zake hizi zinavyobakia kuwa sahihi hata leo – miaka zaidi ya 15 tangu azitoe!

"Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi haiwezi kuepuka lawama. Lakini kuilaumu Kamati Kuu ni kukiri kwamba sasa Chama cha Mapinduzi kina kansa ya uongozi ambayo isipotibiwa itakiua Chama kizima. Pengine kwa Nchi yetu hili lisingekuwa jambo la kutisha kama tungekuwa tumeanza kuona Chama kizuri cha Upinzani ambacho kinaweza kuiongoza Nchi hii badala ya CCM. Hakijaonekana bado. Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuendelea kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ili mradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe" (uk.61)

Akisisitiza jambo hili hili la kansa ya uongozi ndani ya CCM na ubovu wa Vyama vya Upinzani, Mwalimu Nyerere anasema yafuatayo:

"Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona Chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi. Nilitumaini kwamba tunaweza kupata Chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona Chama makini cha upinzani; na wala dalili zo zote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila ya hofu na wasiwasi!" (uk.66)

Je, ni kipi ambacho kimeshabadilika hapa? Ati kansa ya uongozi ndani ya CCM ilishapatiwa tiba? Na vyama vya upinzani vimeshaboreka? Siwezi kuwasemea wanaCCM kwani wenyewe ndiyo wanajua kama wameshaitibu kansa ya uongozi ndani ya chama chao. Hata hivyo si lazima mtu uwe daktari kuweza kuona dalili wazi za mgonjwa anayetafunwa na kansa na dalili hizi bado zinaonekana ndani ya CCM. Misukosuko ya kashfa mbalimbali za ufisadi ni ushahidi tosha kwamba chama hiki kikongwe na chenye historia ya pekee katika nchi yetu bado kinaugua na mambo si salama ndanimwe kiasi kwamba kwa mara ya kwanza inasemekana kwamba makundi kinzani yamezuka mumo kwa mumo – makundi ambayo yanatishia kukidhoofisha. Kuhusu hali ya wapinzani hili si jambo la mjadala: Mwalimu Nyerere alikuwa sahihi. Kwa maoni yangu, bado hakuna Chama kizuri cha Upinzani ambacho kinaweza kuiongoza nchi badala ya CCM; na kwa vile wapinzani hawa wameshashindwa kabisa kuungana na kusimamisha mgombea mmoja, sidhani kama wanayo nafasi kubwa ya kushinda na kuongoza nchi katika uchaguzi wa mwakani. Lakini, jambo jingine linaweza kutokea: wananchi wanaweza kusema, "potelea mbali, liwalo na liwe" na wakachagua Chama cha Upinzani.

Sijui kama kitabu hiki cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania kinapatikana madukani. Ni kitabu kizuri ambacho kinafaa kisomwe na kila Mtanzania mpenda demokrasia, uhuru wa mawazo na anayeipenda na kuitakia mema nchi yake.

Napenda nimalizie kwa kusema kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa binadamu kama sisi na alitenda makosa. Kwa mfano sote tunajua kwamba siasa zake za Ujamaa na Kujitegemea zilishindwa. Lakini hata alipotenda makosa, nia yake ilikuwa njema na alitanguliza maslahi ya nchi. Mwalimu Nyerere aliamini na kutenda alichokihubiri. Ndiyo maana hakujilimbikizia mali na kujitajirisha yeye pamoja na familia yake kama tunavyoshuhudia leo kwa baadhi ya wanasiasa wetu walafi. Na huyu ndiye Mwalimu Nyerere ninayemfahamu mimi – mwanasiasa mwadilifu, msomi na mwanafalsafa makini aliyeipenda na kuipigania nchi yake, bara zima la Afrika na wanyonge popote walipo ulimwenguni. Nyerere aliyehakikisha kwamba hata sisi watoto wa wakulima kutoka vijijini tunapata elimu kwani aliamini kwa usahihi kwamba elimu ndiyo mkakati-mama katika ukombozi wa jamii yo yote ile. Nyerere aliyetuwekea misingi thabiti ya umoja, undugu na Utanzania – misingi ambayo imetuwezesha kuishi kwa amani kwa miongo kadhaa tangu tupate uhuru. Nyerere msema kweli na ambaye alijaribu sana kuionya, kuipigania na wakati mwingine kuionyesha njia kinabii nchi yake kila mara ilipoonekana kuwa katika hatihati. Huyu ndiye Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wangu – Mtanzania halisi na Nabii aliyehubiri na kutenda alichokihubiri!

3 comments:

 1. Profesa, Matondo haya mawaidha ya Mwl. Nyerere tunayahitaji sana hasa kipindi kama hiki ambapo naweza kusema serikali yetu inaelekea kukosa mwelekeo chanya.

  Inashangaza kuona mawaziri na wabunge kuanza kuwashambulia watu kama akina Slaa na Mengi ambao wamejitoa wahanga wa vita dhidi ya ufisadi na kutetea maslahi ya wanyonge.

  Nimeshangazwa sana pia na kauli za Prof. Lipumba kumpinga Mengi kwa kuwatuhumu wafanyibiashara wa kihindi ambao kwa namna moja au nyingine wamehusika kwa kiasi kibwa katika uhujumu uchumi wetu.

  ReplyDelete
 2. Mheshimiwa Malkiory. Tanzania Bwana mambo ni mchafukoge kwani huwezi kuelewa lipi ni lipi, na yupi ni yupi. Wapo wanaosema Mengi ana ajenda yake. Hao mawaziri, wabunge na akina Lipumba bila shaka pia wanajua wanachopigania. Pengine maslahi yao yameguswa. Ni kazi kwelikweli. Mwalimu Nyerere atabakia kuwa "malaika" kutokana na mtazamo wake na aliyoyatenda - yote mema na mabaya!

  ReplyDelete
 3. Mzee wa magaribeipoaJune 17, 2009 at 11:11 PM

  Great Profesa!nimekukubali

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU