NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, April 13, 2009

TUTATUKUZA VYA WENGINE NA KUDHARAU VYA KWETU MPAKA LINI?

 
Makala haya yatatoka katika gazeti la Kwanza Jamii 
la Kesho Jumanne tarehe 14, 2009
 
Tutatukuza vya Wengine na Kudharau vya Kwetu Mpaka Lini?
Na Dkt. Masangu Matondo Nzuzullima  
  Marehemu Mariam Makeba katika wimbo wake mmoja analalamika kuhusu shujaa Shaka Zulu kuitwa Napoleoni Mweusi na Waingereza. Makeba anadai kwamba pengine Napoleoni alikuwa Shaka Zulu mweupe! Nimeshasikia pia Shaaban Robert – yule mwandishi bora kabisa katika fasihi ya Kiswahili – akilinganishwa na William Shakespeare, kingunge wa fasihi ya Kiingereza. Kwa mantiki hii nilianza pia kujiuliza: kwa nini William Shakespeare asiitwe Shaaban Robert mweupe?
Ulinganishaji wangu huu uliendelea kuimarishwa na kugunduliwa kwa mchoro asilia wa William Shakespeare mwezi jana kule Uingereza. Wapiga mnada walikuwa wanaamini kwamba kama mchoro huo ungepigwa mnada pengine ungeingiza mamilioni ya dola. Nilianza kujiuliza, mchoro asilia wa Shaaban Robert ukigunduliwa leo utauzwa kwa shilingi ngapi? Ni Watanzania wangapi wanafahamu Shaaban Robert alikuwa nani? Ni wangapi wanaoitambua sura yake wakiiona? Kuna anayejali?
Ninatumia mifano hii ya ulinganifu kuelezea jinsi utandawazi unavyoangamiza na kutokomeza tamaduni na historia zetu kwa kasi ya kutisha. Hili si jambo ambalo limetokea kwa kufumba na kufumbua. Hili ni tokeo la muda mrefu la mkakati maridadi wa watalawa wetu kuvuruga tamaduni zetu na hivyo kuharibu kujitambua kwetu na nafasi yetu katika dunia hii. Historia imeushuhudia utekelezaji wa mkakati huu huu katika hatua zake mbalimbali katika vipindi tofauti vya kihistoria.
Tunajua kwamba utumwa wetu wa fikra ulianzia katika matapo mbalimbali ya utandawazi yaliyotangulia, matapo ambayo yalitukutanisha na wageni kutoka Ulaya na kwingineko. Mahusiano yetu na ulimwengu wa wageni hawa kutoka nje daima yamekuwa ya kihasama, kiunyonyaji na dhuluma – kuanzia enzi za biashara ya utumwa mpaka wakati huu tulio nao. Uzalendo, utu na Uafrika wetu ulikunguwazwa na kufishwa wakati wa biashara ya utumwa “tulipokubali” kugeuzwa bidhaa na kuuzwa kama nyanya au vitunguu sokoni. Ni wakati huu ambapo tulipondwapondwa kisaikolojia na kuaminishwa kwamba tulikuwa binadamu wa tabaka la chini ambao kamwe tusingeweza kuwekwa katika daraja moja na “mabwana” kutoka Ulaya. Vita hivi vya kisaikolojia vilivyopiganwa kwa ujanja sana kupitia dini na sera za lugha dhidi yetu viliendelezwa na “mabwana” wakati wa ukoloni. Ni wakati huu ambapo bara letu liliitwa bara la giza na tamaduni zetu zilizotukuza, kutulea huku zikishabihiana vyema na mazingira yetu ya asili zilibatizwa kuwa za kishenzi na kinyama. Ukoloni ulitazamwa na hata kutambulishwa kama mkakati wa “kutustaarabisha” na kututoa katika giza nene la kuabudu dini za “kishenzi”, kuongea lugha za kishamba na kukumbatia tamaduni zetu za kiwango cha chini. Lugha zetu ambazo kupitia kwazo fikra zetu na mtazamo wetu pamoja na nafasi yetu katika dunia hii vimefinyangwa ziliitwa duni, zikadumazwa na kunyimwa nafasi za matumizi katika sekta rasmi. Matokeo yake lugha zetu ambazo ndizo zinaamua sisi ni nani na tunahusianaje na wengine katika mazingira yetu zilinyimwa “meno” na tangu hapo zimebakia kuwa lugha zisizo na mwelekeo wala matumaini. Kulingana na Ngugi wa Thiong’o, ukoloni na utumwa wetu wa kisaikolojia ulikamilika pale tulipokubali lugha zetu kuvishwa sanda na kutengwa na ulimwengu na mazingira yetu. Kuanzia hapo, tulikoma kuwa sisi na kuanzia wakati ule, sisi si sisi tena, hatujijui na hatujui kwamba hatujijui kuwa sisi ndisi. Tumekuwa watumwa wa fikra!
Kupatikana kwa uhuru (wa bendera) katika miaka ya sitini kulileta matumaini makubwa katika mioyo ya Waafrika. Iliaminika kwamba uhuru wa kisiasa ulikuwa ni hatua za mwanzo tu na ungefuatiwa na uhuru wa kiuchumi na kitamaduni. Ndiyo maana Kwame Nkrumah - raisi wa kwanza wa taifa huru la kwanza barani Afrika (Ghana) aliwatangazia Waafrika “kuutafuta kwanza uhuru wa kisiasa na uhuru mwingine ungefuata”. Baada ya miaka sitini ya uhuru, ni wazi kwamba tungali tunatawaliwa kiuchumi na uhuru uliotegemewa katika nyanja zingine za maisha yetu haujapatikana. Lakini utumwa mbaya kabisa ni ule utumwa wa kisaikolojia - utumwa wa kimawazo uliomdogosha Mwafrika na kumfanya ajione kuwa yeye ni binadamu wa daraja la pili na utamaduni wake kuwa wa kizamani, usioendana na wakati na wa kishenzi. Mkakati mama ulioanzishwa na watawala wetu wakati wa biashara ya utumwa na kuendelezwa (wakati mwingine kwa nguvu) wakati wa ukoloni bado unaimarika siku hadi siku na bado umejikita barabara katika fikra zetu. Na baada ya miaka sitini ya uhuru bado tunaamini kwamba lugha zetu ni za kishamba na hazifai kutumiwa katika sekta rasmi kama elimu na vyombo vya habari. Matokeo yake lugha zetu za jadi zimegeuka kuwa lugha za kuonewa haya na kizazi kipya hakitaki tena kuzizungumza. Sijui inamaanisha nini kuwa Msukuma wakati hujui Kisukuma na utamaduni wa Wasukuma. Ati, inamaanisha nini kuwa Mhehe wakati hujui Kihehe wala utamaduni wa Wahehe na mtazamo wao kuhusu maisha wala nafasi yao katika dunia hii? Je, Mfaransa anaweza kweli kudai kuwa yeye ni Mfaransa hata kama hajui lugha ya Kifaransa na utamaduni wa Wafaransa? Wanaisimu Sosholojia wengi wanaamini kwamba nyingi ya lugha zetu hizi ambazo sasa tunaziita eti za “kirugaruga” zitatokomea kati ya vizazi vitano hadi kumi vijavyo. Je, lugha zetu na utamaduni wetu utakapokufa, sisi tutakuwa nani katika dunia hii? Pengine sote tutakuwa “Waingereza!” 
Baada ya miaka sitini ya uhuru, bado hatuthamini akina Shaaban Robert wetu. Wakati Waingereza na Warusi wakiwatukuza na kuwaenzi akina William Shakespeare na Tolstoy wao, wakati Wachile wakimuenzi Pablo Neruda wao, sisi tunawaenzije akina Shaaban Robert wetu? Ati, tunawakumbuka na kuwaenzi akina Kinjeketile, Chifu Mkwawa na Mtemi Mirambo wetu kama akina David Livingstone na Karl Peters wanavyotukuzwa kule Ulaya? Tunao wasomi wazuri sana lakini kutokana na kutothaminiwa kwao wengi wao wanaishia kukimbilia nje ambako usomi na utaalamu wao unathaminiwa. Wasomi hawa wazawa hawalipwi mishahara kama wenzao kutoka Ulaya hata kama utaalamu wao unalingana, wamesoma katika vyuo vinavyolingana kwa hadhi na wanafanya kazi ile ile. Cha ajabu ni kwamba hakuna anayejali na inaonekana kama vile serikali zetu zinafurahia kuondoka kwao kwani kutokana na mwamko wao wa kisiasa hutazamwa na tabaka tawala kwa jicho la hati hati. Ni ndoto tu kufikiri kwamba tutaweza kuendelea bila kuwa na wataalamu wa kutosha katika nyanja zote muhimu kama vile elimu, afya, uhandisi n.k.
Ninapenda nimalizie makala hii na kisa hiki kilichonipata pale posta mpya jijini Dar es salaam. Nilikwenda pale kutafuta kadi mbalimbali za Valentine na Krismasi zilizoandikwa kwa Kiswahili kwa ajili ya kufundishia wanafunzi wageni. Cha ajabu ni kwamba kadi za Kiswahili zilikuwa hazipatikani. Niliambiwa kwamba kama nilikuwa nazihitaji ilikuwa lazima nifanye oda maalumu nikatengenezewe na hii ingechukua karibu wiki moja. Nilijaribu kuwauliza vijana mbalimbali ni kwa nini kadi za Kiswahili zilikuwa hazipatikani? Niliambiwa kwamba eti maneno “I Love you” hayatamkiki wala kusikika vizuri yakitamkwa kwa Kiswahili. Eti yanakosa “ladha” iliyokusudiwa na vijana wanapendelea kadi zilizoandikwa kwa Kiingereza hata kama hawafahamu Kiingereza. Lojiki hii kidogo ilinishangaza. Ninavyofahamu ni kwamba lugha zote hapa ulimwenguni zina msamiati wa kutosha kuelezea kila kitu kilichomo katika mazingira ya wazungumzaji wake. Lugha karibu zote zinayo namna ya kutamka “I love you”. Kwa mantiki hii hakuna sababu nyingine yenye mashiko inayoifanya “nakupenda” isiwe na “ladha” kama “I love you” mbali na utumwa wa fikra wa kudhani kwamba kwa vile Kiingereza ni lugha ya “mabwana” inayoshabihishwa na usasa na hadhi basi inaonekana kuwa bora kuliko lugha ya Kiswahili. Na kama Kiswahili kinaonekana duni na kukosa “ladha” mbele ya Kiingereza, je vipi kuhusu lugha zetu zingine zisizo na nguvu kama Kiswahili mf. Kisukuma, Kigogo na Kiha? 
Je, ni lini tutaendelea kutukuza vya wengine na kudharau vya kwetu? Ni kweli kwamba Ushaaban Robert wetu hauwezi kukamilika bila kulinganishwa na Shakespeare? Ni lazima Ushaka Zulu wetu ukamilishwe na Unapoleoni wao? Haya ni baadhi ya maswali ambayo inabidi tuanze kujiuliza tunapoanza kujitafuta na kujitambua upya sisi ni nani na nafasi yetu katika dunia hii ni ipi.
matondo.blogspot.com
profesamatondo@gmail.com

1 comment:

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU