NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, May 8, 2009

KIDOGO NIPIGWE FAINI (TIKETI) YA DOLA 350!!!

Basi la wanafunzi lilikuwa limesimama likipakia wanafunzi - na ile alama ya STOP ikiwa imeinuliwa. Lilikuwa ni eneo karibu na shule na tayari nilikuwa naendesha maili 20/saa. Nilipoliona hilo gari nilisimama mara moja ingawa jamaa aliyekuwa nyuma yangu alianza kunipigia honi. Kumbe kwenye kona tu mbele yetu kulikuwa na polisi mwenye pikipiki amejibanza. Basi alikuja na kuanza kuniambia kwamba japo nilikuwa nimesimama, nilikuwa nimesimama karibu sana na hilo basi. Jamaa akaanza kupima umbali kati ya basi na gari langu, akakuta nilikuwa nimezidi kama futi moja hivi. Basi akanipa onyo kwamba mara nyingine nisimame mbali zaidi vinginevyo dola 350 zitanitoka. Aliponiuliza ni nani alikuwa anapiga honi nilimwambia ni huyo jamaa wa nyuma yangu. Basi alimwendea huyo jamaa na sijui kama alimpa tiketi au la.

Tukio hili linaonyesha vizuri kabisa jinsi wenzetu walivyojiwekea utaratibu mzuri wa usafiri kwa wanafunzi wao. Katika maeneo ya shule spidi ni maili 20/saa na kama basi la wanafunzi linapakia au kushusha wanafunzi, magari yote ni lazima yasimame. Halafu nikakumbuka mshikemshike wanaokumbana nao wanafunzi wetu kule nyumbani kama hizi picha zinavyoonyesha. Ni kweli hatuwezi kuwa na utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba wanafunzi hawa wanapata usafiri unaoaminika (na salama) wa kwenda shuleni na kurudi majumbani mwao? Au tunasubiri mpaka wafadhili waje watusaidie?

10 comments:

 1. Prof: Matondo hili swali linabidi lipelekwe panapohusika ili lifanyiwe kazi. Kwani kweli nyumbani hali ni mbaya sana kuhusu usafiri wa wanafunzi. Na sasa wameanza ktowachukua wanafunzi yaani hizi daladala wanakataa sababu wanasema wanafunzi hawalipi kwa hiyo wanaacha. Binafsi sioni saababu ya kutokuwa na mabasi ya wanafunzi.

  ReplyDelete
 2. yaani dunia hii kuna matabaka!wewe uliyeko marekani unashangaa kuona huruhusiwi kakaribia basi lao na kushangaa walioko bongo wanapanda maroli na daladala kwa kusimama.

  basi nilipofika dar kwa mara ya kwanza niliwaonea wiu wanafunzi wa dar kwa kupanda daladala angalau kwa kusimama na maroli ya mchanga nk huku wakiwa na viatu.

  nilizoea kule kwa kutembe kilomita kadhaa bila viatu au unabahatisha kimkweche cha baisikeli kwa shida sana harafu milima kibao. yaani ukiwa unaenda shule mvua inyesha mpaka inakatika na jua linatoka bado unaenda tu na sijui kurudi lini na ukirudi lazima ukachaje kuni na kuteka maji huku ukifuata mifugo.

  yaani kwangu mimi ninayemlinganisha mwanafunzi anayesome dar na yule wa tweyambe nilikosomea, natamani kuwa mwanafunzi wa dar ili nipande mabasi kwa kusimama au roli la mchanga. Dar rahaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa

  ReplyDelete
 3. Mara nyingi nimekuwa nikiwabeba wanafunzi mara ninapotoka shamba sehemu za kisarawe, wanafunzi wengi wanakuwa kuanzia njia panda ya chanika, kuna siku niliwajaza mpaka defender la polisi likanisimamisha, lakini walipoona ni wanafunzi wakaniruhusu, gari langu ni la wastani (station wagon) linabeba watu 12 pamoja na dereva kama sisi tuko wawili ina maana wanafunzi 10 tu ndio nitakao wabeba, lakini wao huingia zaidi maana hupakatana, tena hufurahia sana maana wakipanda wanakuta na matunda basi huanza kula.
  Mamlaka husika huwa hazioni tatizo hili, ndio maana hata magari ya serekali yanatembea matupu na kuwaacha wanafunzi barabarani, nafikiri pia wanafunzi wachaguliwe karibu na makazi yao itasaidia kupunguza adha hii kwa wanafunzi

  ReplyDelete
 4. Dada Yasinta;
  Hili ni tatizo na ni lazima lishughulikiwe. Kuna kipindi walijaribu programu ya mabasi ya wanafunzi. Sijui yaliishia wapi au pengine wajanja waliyageuza miradi binafsi.

  Kamala;
  Ukitaka kupima ubora wa afya yako kamwe usijilinganishe na mgonjwa!

  Bennet - kwanza asante na hongera kwa moyo wako wa kuwasaidia wanafunzi. Kama kila mtu mwenye gari angejitolea kubeba wanafunzi wachache kila anapoweza naamini ingesaidia. Na hilo wazo la kuchagua wanafunzi karibu na makazi yao ni wazo zuri sana hasa ukizingatia kwamba karibu kila kata sasa ina shule yake ya sekondari - ingawa wengi wana wasiwasi sana na ubora wa elimu inayotolewa katika shule hizi za kata.

  ReplyDelete
 5. Hivi tunamuelewa Kamala ama twamuona anayefurahisha? Well! Namuelewa saana. Nadhani asemalo ndilo tatizo la wengi. Na yeye nadhani anafunua kile ambacho viongozi wetu wanafanya na ndicho ambacho Kaka Matondo umemwambia. Viongozi wetu WANAFANANISHA HALI YA MGONJWA NA MAITI. Yaani kwao ukipumua japo kwa mashine una hali njema kuliko aliyekufa na hawana la kukufanyia zaidi ya hapo. Viongozi wetu "wanatembea na maiti" mawazoni mwao na wanapoulizwa swali wanachofanya ni kutulinganishia hali yetu na ya wengine walio na hali mbaya zaidi yetu, kisha wanaturidhisha kuwa licha ya hali mbaya tuliyonayo, bado tuna afadhali kuli fulani (hata kama fulani huyo hana rasilimali kama zetu)
  Kibaya zaidi ni kuwa na sisi tunachukulia hivyohivyo. Tunakubali na kudanganywa kisha twadhulumiwa. Tunachguuzwa, tunapuuzwa na kujidharaulisha.
  Tunahitaji ku RISE UP, WISE UP, WAKE UP nad SHAKE UP

  ReplyDelete
 6. aisee, kuna wakat hujui nani mgonjwa mpaka upimwe

  ReplyDelete
 7. Mzee wa Changamoto - shughuli zinaendeleaje huko uliko? Ulituaga kwamba unajichimbia mahali kwa wiki mbili nasi tukakutakia kila lililo jema. Natumaini kwamba kilichokufanya ujichimbie huko uliko kinaendelea vyema na ndiyo maana unapata muda hata wa kutembelea vijiwe kama hiki changu. Kama nilivyosema awali - jamii inasubiri kufurahi pamoja nawe!

  Kama wewe, mimi pia huwa namwelewa sana Kamala na kusema kweli huwa nafurahia maoni yake na ni mojawapo ya sababu ambayo hunifanya nitembelee vijiwe vingine na kusoma maoni mbalimbali nikitegemea kuona Kamala atakuwa amesema nini. Kwangu mimi maisha daima ni kujifunza na katika vijiwe hivi kuna watu makini wenye mawazo pevu kabisa na yaliyokomaa. Kamala ni mmojawao ingawa wakati mwingine hasa kwa mtu mgeni anaweza kutishwa na jinsi anavyoweza kukushambulia kama hukubaliani na nadharia na mtazamo wake wa KIUTAMBUZI. Asante kwa kufafanua nilichotaka kukisema kwa ufasaha vile.

  ReplyDelete
 8. Wasalam wote!
  Je lini nasi tutafika huko? au kuna mkakati wowote wa kuonja japo kaustaarabu kiduchu wa wenzetu? hapa bongo mbali na wanafunzi au umbali kati ya gari na gari lakini kwa madereva wetu kuheshimu watumiaji wemgine wa barabara haupo kabisa,

  kwenye zebra dereva na si wa daladala bali karibia wote upita spidi mia na kuwapigia honi wavukao kwa miguu pasi kujali kuwa hapo ndo wanapopaswa kuvukia.

  ReplyDelete
 9. Bwana Rwebangira;
  Tulioko huku tunataka kurudi huko nanyi mlioko huko mnataka kuja huku. Mambo duara ati! Mambo mazuri kwa hawa jamaa yapo (elimu yao, huduma za afya (kama una bima), miundo mbinu na utaratibu mzima wa kujiendeshea mambo yao kama hili la wanafunzi na madereva)).

  Mambo yanayokera pengine ndiyo mengi zaidi na kinachoshangaza ni kwamba na sisi huko nyumbani tunajaribu kweli kuyaiga. Wabeba maboksi wengi tulioko hapa tupo kwa sababu za kiuchumi (au elimu za watoto na sababu zingine za kifamilia) na si vinginevyo. Nyumbani ni nyumbani ati!

  Kuhusu madereva wa Bongo wala usiseme. Niliazima Prado kipindi fulani na jamaa kidogo wanimalize pale Morocco. Hakuna cha taa, right of way wala nini, ni akili yako kichwani tu. Vinginevyo utaporomoshewa matusi mpaka ushangae. Nilishindwa kuendelea na safari, nikarudisha Prado ya watu na kuanza kupanda daladala. Mfumo mzima umekaa shaghalabaghala kuanzia mamlaka zinazosimamia leseni za madereva (wengi hata leseni hawana au wanazo za bandia, na hawajui cho chote kuhusu alama au sheria za barabarani), wakikamatwa wanahonga na duara inaendelea. Ni kazi kweli kweli!

  ReplyDelete
 10. nilipokwenda nyumbani dom baada ya miaka 19 ughaibuni, niliona wanafunzi wamebebwa na tiper la serekali, nilifurahi sana kuona, wakati wetu 1970s wanafunzi wanatembea toka kikuyu mpaka central sekondari au dodoma seko.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU