NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, June 30, 2009

JE, WAGOGO WATAFAIDIKA NA UBUYU WAO?

Baada ya utajiri wake kunyonywa na wageni kwa muda mrefu, Afrika sasa inakabiliwa na ukoloni mpya - ukoloni wa kibayolojia na kiikolojia. Makampuni ya madawa na vyakula ya nchi za Kimagharibi sasa yanakimbilia kujimilikisha (kwa kuchukua hati miliki) mimea ya Kiafrika ambayo ina manufaa ya kitiba na kilishe. Mfano ni Hoodia - mmea kutoka jangwa la Kalahari na ambao unasaidia kuzima hamu ya kujisikia njaa. Inavyoonekana mbuyu (Adansonia Digitata kwa jina la kisayansi) nao utachukuliwa hivi karibuni. Nasi Waafrika kama kawaida yetu tumekaa tu tunaangalia. Katika makala haya ninauliza: kama ubuyu utaanza kuuzwa kama zao la Kibiashara kimataifa, Wagogo ambao ni wenyeji wa Dodoma ambako mibuyu mingi inapatikana (na Waafrika kwa ujumla) wataambulia cho chote? Inabidi wataalamu wa biashara na sheria za Kimataifa waliangalie suala hili la makampuni ya Kimagharibi kujimilikisha mimea yetu na kuhakikisha kwamba Waafrika hawaachwi kwenye mataa tena kama ilivyotokea katika madini na rasilimali nyinginezo za bara lao tajiri. (Makala imechapishwa katika gazeti la Kwanza Jamii la Leo nami naitundika hapa kama ilivyo)
====================================================
Wagogo Watafaidikaje na Biashara ya Ubuyu?
Na Dkt. Masangu Matondo Nzuzullima

Afrika kwa hakika ni bara la ajabu. Kwa upande mmoja, ni bara tajiri pengine kuliko mabara mengine yote ulimwenguni. Kwa upande wa pili, Afrika pia ni bara masikini pengine kuliko mabara mengine yote. Hali hii kanganyifu wazungu huwa wanaiita “paradox” Ati, inawezekanaje uwe tajiri nambari wani na wakati huo huo uwe masikini nambari wani? Hili linawezekana tu kama umewaachia watu wengine wakunyonye na wautumie utajiri wao kwa faida yao; na kukuacha wewe ukiwa huna kitu. Ndivyo Afrika inavyofanya, au tuseme inavyokubali ifanyiwe.

Pamoja na utajiri wake wa maliasili (madini, mapori, wanyama wa kila aina, watu, bahari, maziwa, mito, ardhi n.k.) Afrika bado ni masikini kwa sababu utajiri wake hauusaidii umma wake wa wakulima na wafanyakazi katika kuleta maendeleo ya kweli. Kwa mtazamo mmoja utajiri huu umegeuka kuwa kama “laana” kwa bara la Afrika kwani ndiyo hasa ulikuwa chanzo cha Afrika kutawaliwa. Wakati wa biashara ya utumwa Waafrika wenyewe waligeuzwa bidhaa wakauzwa mnadani kwenda kuzalisha malighafi zilizohitajika Ulaya. Malighafi hizi ndizo zilizochochea mapinduzi ya viwanda na hatimaye ukingunge wa nchi za Ulaya katika sayansi, teknolojia, uchumi na utamaduni. Wakati wa ukoloni, Afrika iliingizwa rasmi katika mfumo wa uchumi tegemezi ambamo ilijikuta (kama asemavyo Walter Rodney katika kitabu chake cha How Europe Underdeveloped Africa) ikizalisha isichokifaidi na ikifaidi isichokizalisha. Kuanzia hapo Afrika ilipoteza rasmi umiliki wa malighafi zake ambazo uzalishaji wake sasa ulidhibitiwa na mabwana kutoka Ulaya. Hata bei za malighafi za Afrika zikawa zinapangiwa Ulaya bila kujali hali halisi ilivyo Afrika kwenyewe. Malighafi hizo zilizalishwa na kuuzwa kwa bei ya chini sana lakini zilipofikishwa Ulaya na kubadilishwa kuwa bidhaa, bidhaa hizo hizo zilirudishwa Afrika na kuuzwa kwa bei ya juu sana. Kwa hali hiyo mabepari wa Ulaya waliweza kujitajirisha huku Waafrika ambao hasa ndiyo wenye mali ghafi wakiendelea kusikinika.

Baada ya uhuru mabepari wa Kimagharibi walihakikisha kwamba wanaweka tabaka lao la vibwanyenye kushika hatamu katika nchi nyingi za Kiafrika, tabaka ambalo lilihakikisha kwamba mfumo huu tegemezi wa kiuchumi waliouanzisha unadumishwa na kuimarishwa. Viongozi “vichwangumu” ambao walisitasita kufuata mfumo wa kibepari na hivyo kugoma kuwa vibwanyenye wa wakubwa wa Ulaya ama walipinduliwa au waliuawa. Hiki ndicho kilichowapata akina Kwame Nkrumah wa Ghana, Patrice Lumumba wa Kongo na wengineo. Mfumo huu wa “aliyenacho ataongezewa na yule ambaye hana hata kile kidogo alichonacho atanyang’anywa” ndiyo umetawala duniani na baada ya miaka 60 ya uhuru, hali haijabadilika na utajiri wa Afrika bado unazinufaisha nchi za Kimagharibi (pamoja na tabaka dogo la watawala “viranja” katika nchi nyingi za Kiafrika). Kama unabisha nenda pale mgodi wa almasi wa Mwadui ukaangalie almasi zinazozalishwa pale. Halafu ukitoka nje ya geti la mgodi angalia maisha ya Wasukuma katika vijiji vinavyouzunguka mgodi huo wanavyoishi. Utabakia kujiuliza, almasi yote ile inayochimbwa pale inamsaidia nani? Nilipata bahati ya kutembelea mgodi huo mwaka 1995 na nilipotoka nje ya mgodi ule machozi yalinidondoka baada ya kuona hali za wenyeji ambao almasi zile zinafukuliwa kutoka katika ardhi yao wenyewe – ardhi ya mababu zao! Haya ni makala ya siku nyingine. Sasa tuendelee na mada yetu ya wagogo na ubuyu wao.

Baada ya kupora utajiri wa Afrika kwa muda mrefu, makampuni ya Kimagharibi na hasa yale yanayotengeneza madawa na hata vyakula sasa yanakimbilia kujimilikisha mimea yenye asili ya Afrika ambayo ina manufaa kitiba na kilishe. Ukoloni huu mpya wa kibayolojia na kiikolojia umeyafanya makampuni haya kuanza kuchukua hati miliki za mimea hii ambayo Waafrika wamekuwa wakiitumia kama tiba ya maradhi mbalimbali na chakula kwa muda mrefu. Mfano mzuri ni huu mmea wa Hoodia ambao Wasan - wenyeji wa jangwa la Kalahari kule Namibia wamekuwa wakiutumia kwa muda mrefu kama kizuia njaa. Kampuni moja la Uingereza liitwalo Phytopharm ndilo limejimilikisha hati miliki ya mmea huu na sasa mmea wa Hoodia umegeuzwa zao la kibiashara na mashamba makubwa yamefunguliwa kule Afrika Kusini na jangwani katika jimbo la Arizona kule Marekani. Vidonge vya kupunguza hamu ya chakula (na hivyo kusaidia kupunguza uzito) vinavyotokana na mmea huu (Hoodia diet pills) sasa vinauzwa na kununuliwa sana hapa Marekani. Chupa moja ndogo inauzwa kwa dola 39.95 za Kimarekani. Mwafrika hapa, kama kawaida yake, amepigwa chenga ya mwili na utajiri wake unafaidiwa na watu wengine. Japo Wasan walikwenda mahakamani kudai haki yao, walifikia makubaliano ya muda mwaka 2002 ambapo iliamriwa kwamba walitakiwa walipwe asilimia 8 ya faida yote ambayo kampuni la Phytopharm lilikuwa limepata mpaka wakati ule; na kuanzia hapo wangeendelea kupata asilimia sita (6%) ya mapato yote yanayotokana na mmea wa Hoodia. Hata hapa mtu unaweza kujiuliza: ni nani anayehakikisha kwamba kweli hata hiyo asilimia 6% waliyotengewa wanaipata?

Mmea wa Mbuyu (Adansonia Digitata kwa jina la Kisayansi) inaonekana nao utakumbwa na mkasa kama wa Hoodia (yaani kumilikiwa na makampuni ya Kimagharibi) muda si mrefu ujao. Kwa karne nyingi mmea huu umekuwa ukitumiwa katika sehemu nyingi za Afrika kwa matibabu na shughuli nyingine mbalimbali. Karibu kila sehemu ya mmea huu ina faida – sehemu ya mti hutumiwa kutengenezea kamba na nyavu za kuvulia samaki, majani hutumiwa kulishia wanyama kama mbuzi, kondoo na ng’ombe; shina lake kubwa linaweza kutumiwa kama makazi kwa binadamu, matunda yake ni chakula na tiba. Kule Gambia kwa mfano, inaaminika kwamba mbuyu unatibu malaria, ugumba, pumu, maumivu ya kichwa, meno na magonjwa mengine.

Makampuni ya madawa pamoja na vyakula ya nchi za Kimagharibi yanaunyemelea mmea huu wa mbuyu na kuna imani kwamba siku moja pengine unaweza kuwa ndiyo chanzo kimoja kikuu cha madawa na chakula. Imeshathibitishwa kisayansi kwamba ule unga mweupe katika matunda ya mbuyu una faida lukuki: Una antioksidanti (antioxidants), potasi (potassium) na fosforasi kwa wingi, vitamini C mara sita zaidi ya juisi ya machungwa na kalisi (calcium) mara mbili zaidi ya ile inayopatikana katika maziwa ya ng’ombe. Majani yake yana madini ya chuma, potasi, maginesi (magnesium), manganizi (manganese), fosforasi na molybdenum kwa wingi sana. Mbegu zake pia zina protini ya kutosha. Kwa uchambuzi wa kisayansi kuhusu madini yaliyomo katika mbuyu pamoja na bidhaa mbalimbali zinazotokana na mbuyu soma makala ifuatayo (pdf)

Kutokana na faida zake hizi, (linaripoti gazeti la New York Times la tarehe 26/5/2009) bidhaa zinazotokana na mbuyu zimeruhusiwa kuingizwa sokoni katika nchi za Jumuia ya Ulaya kuanzia mwaka jana na shirika la viwango la madawa na vyakula la Marekani (Food and Drug Administration) linategemewa kutoa ruhusa mwaka huu kwa bidhaa hizo kuingizwa na kuanza kutumiwa hapa Marekani. Sehemu ya ndani ya tunda la mbuyu itauzwa kama kiungo muhimu katika “smoothies” na “cereal bars”. Tayari kikopo kidogo cha jamu iliyotengenezwa kutokana na mbuyu kinauzwa kwa dola 11 za Kimarekani kule Uingereza. Kulingana na tathmini ya Natural Resources Institute ya Uingereza, biashara ya kimataifa ya ubuyu inaweza kuzalisha dola za Kimarekani zaidi ya bilioni moja (sawa na shilingi za Kitanzania 1,300,000,000,000) kwa mwaka pamoja na kutoa ajira kwa familia za Kiafrika zipatazo milioni mbili na nusu.

Niliposoma makala haya kutoka gazeti la New York Times na kuona faida na mategemeo makubwa ya kibiashara ya mmea huu wa mbuyu niliwakumbuka marafiki zangu Wagogo kutoka Dodoma ambako kama sikosei ndiko kuna mibuyu mingi kuliko sehemu nyingine hapa Tanzania. Kama mmea huu utaanza kuzalishwa kibiashara natumaini kwamba Tanzania haitabaki nyuma na kwamba wazalishaji wa zao hili watawezeshwa ili hatimaye waweze kufaidika na kuuona uhalisi wa sera ya maisha bora kwa kila Mtanzania. Kama Kahawa ilivyoweza kuwanufaisha wenyeji wa mikoa ya Kilimanjaro, Kagera na Mbeya, bila shaka zao hili la Ubuyu pia litaweza kuwanufaisha wenyeji wa mkoa wa Dodoma na kwingineko linakopatikana. Nchi za Kiafrika ni lazima ziamke na kupambana na ukoloni huu mpya wa kibayolojia na kiikolojia; na kuhakikisha kwamba mimea hii yenye faida kubwa (kama hoodia na mbuyu) ambayo ni mali ya watu wake ambao wamekuwa wakiitumia kwa muda mrefu kama tiba (ambazo wazungu hao hao waliziita sehemu ya utamaduni wa kishenzi) inalindwa na kubakia mali ya Waafrika. Hata kama ikianza kutumiwa kibiashara kama ilivyotokea kwa Hoodia na pengine mbuyu (Adanjsonia Digitata), basi uandaliwe utaratibu ambao utahakikisha kwamba marafiki zangu Wagogo wanafaidika na ubuyu wao. Vinginevyo, baada ya kumiliki almasi, dhahabu, tanzanite na utajiri mwingine wa bara letu, walafi hawa wa Kimagharibi kamwe hawatosheki na kama wakiweza wataweza kumiliki kila kitu kilicho chetu. Ni lazima tuwaambie kwamba Hoodia, Mbuyu na Mwarobaini ni vyetu na sisi ndiyo tunastahili hiyo hati miliki.

1 comment:

  1. Ikianyika jitihada ya ziada bila ufisadi inawezekana

    ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU