NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, June 23, 2009

JESHI LA KUJENGA TAIFA (JKT) LINARUDI TENA RASMI !!!

Nimeyaona haya makala katika gazeti la Habari Leo la leo (Juni 23, 2009) na inavyoonekana Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linarudi tena rasmi. Lengo la uamuzi huu, kama alivyofafanua Waziri Mkuu, ni "kujenga jamii ya vijana watakaoshiriki katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali vijijini na mijini, ulinzi wa taifa, na kuonyesha mfano katika kujitegemea". Swali ni kwamba - jeshi hili ni kweli litatimiza lengo lake kuu sawasawa? Je, lengo hili kuu linaendana na mazingira ya sasa ambayo yanamzunguka kijana wa Kitanzania? Tunaposema vijana wetu wawe "mfano katika kujitegemea" tunamaanisha nini? Ati, siasa yetu ya Ujamaa na kujitegemea bado iko hai?

Mimi sina ugomvi na JKT. Nilikata mwaka mzima pale Makutupora JKT, Dodoma (Operesheni Miaka 30 ya Uhuru); na kusema kweli nilipenda uzoefu na mafunzo niliyoyapata pale. Hata kama ningekuwa na mtoto wa kiume ningehakikisha kwamba anakwenda JKT - na hasa hawa vijana wa kizazi cha dot.com. Kupiga kwata, kumwagilia maji nusu eka ya bustani, kupalilia mizabibu, kuchunga ng'ombe, kukata kuni, kufyatua matofali na kuyachoma, kujenga nyumba, kukesha usiku katika lindo na mengineyo pengine yatawarudisha kidogo katika mambo halisi katika jamii yetu na kuwakumbusha kwamba haya ndiyo maisha halisi wanayoishi Watanzania wengi kule vijijini.

Ni lazima niseme pia kwamba sikupenda waliyokuwa wakitendewa mabinti - hasa katika ile miezi mitatu ya mwanzo wakati mambo bado yako moto moto; na ningekuwa na wasiwasi sana kama ningekuwa na binti ambaye angetakiwa aende JKT. Kutokana na uwazi uliosababishwa na vyombo vya habari, pamoja na mwamko mzima katika jamii naamini pengine mambo sasa yameshabadilika - na kwamba sasa hii itakuwa ni JKT mpya na ya kizazi kipya - itakayoendeshwa kwa uwazi, kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya!

Makala ya gazeti ni kutoka blogu ya Kennedy

8 comments:

 1. Matondo,

  Je waweza kutukumbusha ilikuwa ni operation gani? bila kurejea kwenye cheti chenyewe!

  ReplyDelete
 2. Bwana Malkiory - sijui kama nimeliewa swali lako. Kama nilivyosema hapo juu, ilikuwa ni Operesheni Miaka 30 ya Uhuru (1990 - 1991). Cheti chenyewe wala sijui kiko wapi. Tena umenikumbusha nije nianze kukitafuta!

  ReplyDelete
 3. Safi sana, swali langu umelijibu vizuri, ilikuwa ni kosa langu niliisoma article kwa haraka mno bila kupitia yalimo kwa umakini.

  Chakufurahisha ni kwamba tulisote JKT pamoja, ila mimi nilikuwa Mlale Songea. Ila operation hiyo hiyo ya miaka 30 ya uhuru.

  ReplyDelete
 4. Mlale ilikuwa ni moja ya kambi tulizokuwa tunaambiwa kwamba ilikuwa "hatari" zaidi. Sijui kama ni kweli. Maoni yako juu ya JKT ni yapi Bwana Malkiory? Unafikiri "ilikuonyesha mfano katika kujitegemea" kweli? Unaunga mkono kurudishwa kwake?

  ReplyDelete
 5. Matondo,
  Dhana nzima ya uwepo wa JKT nadhani ni nzuri tu,mfano nilikuwa kwenye kombania ya HQ kama wanavyoitaga kwa ajili ya kujenga nyumba za maafande na za shule za jirani, hapo tuseme nilijifunza ufundi ujenzi pamoja na kutokuwa na taaluma hiyo awali, jambo jingine ni suala la nidhamu,nakumbuka maafande walikuwa wakituchemsha saa zingine kwa kukutukana, mf. we kuruta unavuta bangi wewe lakini jibu ni ndiyo afande, jambo jingine la nililojifunza ni zoezi la uvimilivu ambapo mtu hukabiliana na kazi ngumu za mikono. kusema kweli nisingependa JKT irudishwe hasa ukizingatia kuwa uchumi wa nchi yetu bado ni tegemezi.

  Hapa Finland vijana hasa wa kiume ni lazima baada ya kutimiza miaka 18 lazima waende Jeshi kwa muda wa mwaka mmoja, nadhani wao wanalenga zaidi kwenye mbinu za kijeshi tofauti na JKT ambayo msingi wake mkubwa ulikuwa uzalishaji.

  ReplyDelete
 6. Hapo nimeponea kwenye tundu la sindano. bIla shaka haitanihusu! ha ha ahaaa

  ReplyDelete
 7. Bwaya usiogope. Ikibidi kwenda nenda ukajifunze kujenga nyumba, kufyatua na kuchoma matofali na kazi zinginezo....

  ReplyDelete
 8. Nimekumbuka ulikuwa D au C lakini siyo A wala E wala HQ na hukuwa ujenzi au Jikoni au Dispensary au manpower!!Utakuwa ulikuwa Bustani mtaalam wa kupiga ndoo.Hukuwa kwa CO karibu na nyumba ya Salim Ahmed Salim enzi zile za utawala wa Mwinyi akiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi na JKT vyeo vya Mzee Mwinyihavijajirudia tena!Nimekumbuka mengi ya wizi wa nyanya,matikiti,nyama kwa Quarter Master,Kichele cha kufanya part DODEP, kubadilisha maharage,unga na digidigi,kwa mbuzi,mzakwe,disco,tofali,Mayamaya, Afande Kingu,Bandiaji,Rajabu,PEO,Singira,Matondo Mapengo,Shija Makelele,Mwiba,LB,Masikio,Mzee Mambo!!!Hadisi ndefu tamu.Napenda JKT irudi kwa vijana wa kiume. Ntisi

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU