NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, June 22, 2009

WATU WAPUNGUE MISAFARA YA VIONGOZI - JK

Baada ya mjadala mkali uliozuka baada ya makala ya Profesa Mbele kuhusu safari za nje za Rais Kikwete (bofya hapa), nimefurahi kuona kwamba Rais mwenyewe ameagiza idadi ya watu katika safari hizo ipunguzwe. Mimi nadhani hii ni hatua nzuri kwani itasaidia kupunguza gharama za safari hizo ambazo naamini zinafanyika kwa maslahi ya taifa na si vinginevyo. Soma makala hapa chini.

JK Aagiza Watu Wapungue Misafara ya Viongozi

Imeandikwa na Oscar Mbuza, Dodoma
(Gazeti la Habari Leo, Juni 19 2009)

Rais Jakaya Kikwete ameagiza kupunguzwa kwa idadi ya watu katika msafara wa Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu katika safari za nje ya nchi ili kupunguza gharama. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliliambia Bunge jana kuwa hatua hiyo imekuja baada ya kuonekana kuwa Sh bilioni nane zilizotengwa mwaka jana kwa kazi hiyo ya safari hazitoshi.

Alisema hatua hiyo inafanya mamlaka husika kuanza kuangalia namna nzuri ya kuandaa watendaji wanaopaswa kufuatana na Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. Alisema utaratibu unaotumika katika kuchagua nani afuatane na viongozi wa juu wanaposafiri unazingatia vigezo mbalimbali kama vile wapambe wa viongozi, maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambao hawana budi kufuatana na viongozi kwa mujibu wa itifaki.

Alisema pia wapo viongozi wanaoteuliwa kujiunga na misafara hiyo kutokana na kusudio na madhumuni ya safari ambapo uteuzi hufanywa na ofisi za viongozi hao kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa upande wa Zanzibar na Ofisi ya Spika kwa upande wa wabunge.

Alisema katika uteuzi huo, vigezo vya jinsia, uwakilishi kutoka pande zote mbili za Muungano na wa kambi ya Upinzani huzingatiwa. Alisema kila wakati viongozi wakuu wanaposafiri nje ya nchi, waandishi wa habari wamekuwa wakijumuishwa katika misafara hiyo na inapotokea kuwa viongozi wamekaribishwa kutembelea nchi jirani, basi wakuu wa mikoa inayopakana na nchi hizo huteuliwa kufuatana na viongozi.

Alisema kwa kuzingatia vigezo hivyo, makundi ya viongozi yanayofuatana na viongozi wakuu wa nchi ni mawaziri wa pande zote za Muungano, wabunge na watendaji wa idara mbalimbali za Serikali kutegemeana na madhumuni ya ziara. Waziri Membe alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Zulekha Yunus Haji (CCM), aliyetaka kujua ni utaratibu gani unaotumika kuchagua viongozi wanaofuatana na Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu katika ziara nje ya nchi.

8 comments:

 1. Ninachokipata kwenye taarifa hii ni kuwa safari hizo zitaendelea, kwa manufaa ya Taifa. Isipokuwa kinachosemwa ni idadi ya watu kwenye misafara.

  Katika yale mabishano yaliyofuatia makala yangu, madai ya watu wengi, na pia vile viumbe vinavyojiita "anonymous," ni kuwa Kikwete abaki nchini, kwa msingi kuwa safari hizo hazina manufaa. Hapo ndipo mgogoro utakapobaki.

  Nimewaalika watu wote na viumbe hivi "anonymous" kwenye warsha Tanga, tarehe 29 Agosti mwaka huu, kwa malumbano ya ana kwa ana. Natarajia mahudhurio yatakuwa makubwa, na hata kama itakuwa vigumu kwa baadhi kuhudhuria, wawashawishi watu wao walioko Tanga wahudhurie, na waandishi wa habari, na kadhalika. Tulumbane siku hiyo, ana kwa ana, hadi kieleweke.

  ReplyDelete
 2. We prof mbele ni prof wa siasa au kiswahili au mitishamba? Mada ulioiingia ni ya ki uchumi zaidi, inahitaji elimu ya uchumi sio mofimu, nahau au viima na virai..! Sikia baba, watu hawahitaji kulumbana kama walevi wa pombe vilabuni, au kwenye vijiwe vya kahawa. Watu wanahitaji data na maelezo yakinifu (kama aliyotoa Prof wa Uchumi Lipumba), sio utuimbie kwaya kama wana T.O.T (eti mpaka kieleweke)! We mzee kuwa prof wa vishazi na viambishi hakukufanyi uwe mtaalamu wa microbiology na anatomy, vile vile hakukufanyi uwe mtaalamu wa uchumi! Sikia mzee ni vyema ungerudi marekani ukafundishe wamarekani kiswahili au badala ya kupoteza muda kuongelea hilo jambo usilo na elimu nalo (lataka wachumi), ungeendelea kuandika vitabu vya kiswahili, kufunza lugha watoto wetu shule za msingi, kwani siku hizi kina commedy wanatuharibia watoto wetu kwa kuwafundisha misamiati ya ajabu..utaskia waambiwa" UMEFULIA prof Mbele"

  ReplyDelete
 3. Prof. Mbele umenifurahisha sana. Eti mpaka kieleweke. Naamini mtakuwa na mjadala mzuri huko Tanga. Tunategemea kusoma mjadala huo utakavyokwenda.

  Kwa anonymous uliyeona aibu hata kuweka jina lako, sidhani kama uliyoyasema yanastahili hata kuchambuliwa hapa; na sioni hata mahali pa kuanzia. Wengine wakianza nami nitachangia baadaye. Swali: kitaaluma wewe "umesomea" nini?

  ReplyDelete
 4. We Masangu si ndo wale wale...wataalam wa kiswahili mnaotaka kujifanya mnajuwa kila kitu! Fundisheni viima na viarifu, kitenzi kikuu na kiwakilishi mpumzike,hizi fani nyengine waachieni wenzenu! Mimi si mtaalamu wa uchumi na si thubutu kujifanya najuwa, wakati sijui..!

  Eti huoni pakuchambuwa...utaona wapi? Nawe unataka nikupe sentensi uchambuwe kitenzi kikuu, kiima, kiarifu, kiambishi, kielezi..ha ha ha! Hii haitaki kuchambuliwa ni "fact" Yangoswe muachie ngoswe baba!

  Wanasema "..bila utafiti wa jambo husika, hakuna kuliandika wala kuliongelea"

  Kitaaluma mimi fundi seremala, njoo kwa binyau kona ya mtogole, karibu na tandale kwa tumbo kabla ya kufika popobawa, hapo hapo upande wakushoto gereji kwa juu kidogo kabla ya nyumba nyekundu upande wa kulia kwenye mfenesi nyumba ya saba kutoka msikitini mwambie konda msaada karibu na makaburini kabla ya kufika kibanda cha voda, ukishuka ulizia kwa fundi Mangungo!

  ReplyDelete
 5. Kama wewe ndio fundi Mangungo, basi niko tayari kujibizana nawe.

  Umeongelea mambo mengi, na kila mojawapo linahitaji mjadala mrefu, kwa maoni yangu. Napenda kugusia jambo moja tu, la kufundisha watoto wa shule ya msingi.

  Mimi ningeona nimepiga hatua mbele iwapo ningekuwa na uwezo wa kufundisha shule ya msingi. Kuna waTanzania kadhaa nilishawahi kuwaeleza hivyo na hivi karibuni nimeandika makala hii hapa. Tafakari mwenyewe.

  ReplyDelete
 6. Mama Furaha (Mbeya)June 23, 2009 at 9:09 PM

  Huyu anony. ni mkorofi achaneni naye. Nimependa ujasiri wako mwenye blogu kuziacha comments zake chafu hapa. Ningekuwa mimi ningezi-delete mara moja kwani ni upumbavu mtupu. Ze Utamu imefungwa na sasa watu wenye chuki wanahaha kutafuta mahali pa kutua mizigo yao ya matusi, chuki, wivu na ujinga wanayotembea nayo. Tanzania is going down wallahi. Mijitu ina chuki sijui kwa nini. Siku hizi hata ndugu yako wa tumbo moja hakuna kuaminiana. Ni wivu, husuda na fitina mtindo mmoja. It is very sad!

  Kama kwa profesheni ya huyu anony ni fundi seremala na tukifuata lojiki yake basi naye asiruhusiwe kuongelea jambo lolote isipokuwa ufundi seremala pekee - na pengine aongee na wapiga randa wenzake tu kwani hao ndio watamwelewa. Ni lojiki ya kitoto, kijinga na kiwendawazimu. Huyu anatakiwa aende vijijini akaongee na wazee ambao "hawajasoma" na atagundua mara moja kwamba pengine wana elimu kuliko hao wachumi wenye "data" kama akina Profesa Lipumba.

  And I swear huyu ni mtu anayewafahamu vizuri na ndiyo maana anaficha jina lake. Anawachezea tu akili na please achaneni naye. Au akiweka comments zake just delete them. Blogu hizi zinazusha mijadala muhimu yenye kufikirisha kwa manufaa ya taifa letu na there is no place for myopic-minded people kama huyu anony mpuuzi! Nimekasirika sana sijui kwa nini. Mtanisamehe wadau.

  ReplyDelete
 7. Fundi Mangungo;
  Kumbe ni wewe? Za siku nyingi? NGO yako inaendeleaje? Nimeona nifute post yangu iliyotangulia baada ya kuambiwa kwamba ni wewe.

  Sina neno mzee. Viima na viarifu (na Isimu (Linguistics) kwa ujumla)) vipo kama kawaida tangu enzi zile za Sengerema, Mlimani na UCLA; na ndivyo vinanifanya niishi hapa kwa Obama. Na ni kweli, kama una sentensi ya lugha yo yote lete na nitakuchambulia virai bila wasiwasi.

  Mbali na hayo mimi sijifanyi/sijajifanya/sitajifanya kuwa mtaalamu wa jambo lolote kwani hata huko kwenye taaluma yangu mwenyewe (Isimu) mambo yanabadilikabadilika kila leo, na nadharia unayoiamini na kuitumikia leo kesho unakuta imeshapigwa dafrau. Ndiyo maarifa hayo - yanabadilikabadilika kwa kasi.

  Mbali na kutokuwa mtaalamu wa jambo lolote bado najihisi kwamba ninao welewa (japo wa juu juu tu kwa watu wazamifu kama nyie) wa kuanzisha na kushiriki katika mijadala na mada muhimu zinazohusu taifa letu. Nadhani hii ni haki yangu kama Mtanzania mwingine ye yote. Na sidhani kama nahitaji PhD ya uchumi kama Profesa Lipumba kuweza kuelewa kwamba raisi kuagiza watu wapungue katika misafara ya viongozi kutapunguza gharama katika safari hizo. Asante sana na karibu Florida siku utakapozungukia mitaa hii ya Obama!

  ReplyDelete
 8. mama furaha,ucoverreact,wala maoni ya m2 yacfutwe tuheshimu uhuru wa kuyatoa

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU