NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, July 30, 2009

KAMA NINGEKUWA MHESHIMIWA BENJAMIN W. MKAPA

Kama ningekuwa Mheshimiwa William Benjamin Mkapa ningefanya kama alivyofanya Ndugu Lee Myungbak - rais wa Korea ya Kusini.

Ndugu Lee Myungbak ametoa sehemu kubwa (asilimia themanini) ya utajiri wake (dola za Kimarekani milioni thelathini na tatu) na kuanzisha mfuko maalum (skolashipu) ambao utasaidia kupunguza tofauti za kitabaka kati ya walionacho na wasionacho katika nchi yake. Akitambua nafasi ya elimu kama mkakati mama katika ukombozi wa watu masikini , rais Lee Myungbak amesema kwamba mfuko aliouanzisha utajikita hasa katika kusaidia kulipia gharama za elimu ya juu kwa watoto wanaotoka katika familia masikini. Baada ya kutoa sehemu hiyo ya utajiri wake, amebakiwa na kama dola milioni nne (tu) za Kimarekani (Kwa habari zaidi soma hapa)


Ndugu Lee Myungbak pia aliwahi kuandamwa na kashfa za ufisadi alipokuwa rais wa makampuni ya Hyundai. Hata hivyo baada ya uchunguzi wa muda mrefu, ilibainika kwamba utajiri wake alikuwa ameupata kihalali na kwamba hakujihusisha na ufisadi. Akitangaza rasmi uamuzi wake huu, Ndugu Lee Myungbak alisema kwamba safari yake kutoka kwenye umasikini kijijini kwao mpaka kuwa Mkurugenzi wa makampuni ya Hyundai na hatimaye rais wa nchi isingewezekana bila kupata msaada kutoka kwa masikini wenzake hasa wakati ule akifanya kazi za kivujajasho ili kupata pesa za kujilipia ada za chuo.


Mimi pia, kama Ndugu Lee Myungbak, pamoja na kuandamwa na kashfa za ufisadi na kujilimbikizia mali kwa njia za mkato, serikali yetu tukufu tayari imeshanisafisha na kwa hivyo mimi ni mtu safi (kama unabisha soma hapa na hapa). Nimeshasema mara nyingi kwamba wote wanaonipigia makelele na kunisingizia kuwa nilitumia madaraka vibaya ni watu wenye wivu tu ambao niliwanyima ulaji nilipokuwa madarakani. Narudia tena, mimi ni mtu safi na tena siku hizi NIMEOKOKA.


Kutokana na mapinduzi yangu ya kiroho, na ili kukata mzizi wa fitina, huku nikifuata nyayo za Ndugu Lee Myungbak, nimeamua kutoa sehemu kubwa ya utajiri wangu (yakiwemo mabilioni nitakayopata kutokana na mauzo ya mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira) kuanzisha skolashipu ambayo itasaidia kulipia gharama za elimu ya juu kwa wanafunzi wa Kitanzania ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwasomesha. Nimetoa jumla ya dola za Kimarekani milioni sitini na tatu.


Mheshimiwa Andrew Chenge aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali katika utawala wangu, pamoja na aliyekuwa waziri wangu wa madini Mheshimiwa Daniel Yona wamekubali kuniunga mkono nao wamechangia dola za Kimarekani milioni hamsini na tano. Kwa hivyo mfuko huu unaanza na jumla ya dola za Kimarekani milioni mia moja kumi na nane. Naamini kwamba viongozi wengine wakereketwa wataniunga mkono na kuchangia katika mfuko huu muhimu.


Hakuna sababu sasa kwa mtoto wa Kitanzania kushindwa kwenda chuo kikuu kwa sababu eti wazazi wake ni masikini. Tutaandaa utaratibu mzuri ambao utahakikisha kwamba wanafunzi watakaopata msaada kutoka katika mfuko huu watakuwa ni watoto ambao kweli wazazi wao hawana uwezo wa kuwalipia.


Acheni siku njema ipambazuke!


Mungu aibariki Tanzania.


Ni mimi;


Aliyekuwa rais wenu mpendwa.

4 comments:

 1. Atoe pesa zake achekwe? Viongozi wetu hawa bomu sana. Mi ningekuwa JK ningewanyang'anya hao wanaoshtakiwa kwa ufisadi na kuanzisha scholarship kama ya huyu rais wa South Korea. Wazo zuri kabisa!

  ReplyDelete
 2. JK ni kiongozi makini lakini peke yake hataweza kitu. Alishindwa Nyerere sembuse JK. Tanzania hakuna matumaini kwani Uswahili na kuoneana haya vimetuzidi mno

  ReplyDelete
 3. Ni kazi kweli kweli!

  ReplyDelete
 4. Mimi sikubaliani hata kidogo na Nesta kuwa JK ni kiongozi makini. Ukweli kabisa uwezo wake wa uongozi nimegundua ni mdogo sana. na kila siku zinavyoenda ndio inakuwa balaa zaidi. Wewe unajua nchi sasa hivi ipo kwenye hali gani. haijawahi kutokea kwa kiongozi yeyoye wa nchi aliyepita. Watu wakazungumza na kuonyesha waziwazi tofauti zao za dini, ukabila, na sehemu walizotoka wazi wazi bila rais kuzungumza. Uongozi wa kutaka kila mtu akuone wewe ni bora, yaani kujipendekeza kwa kila mtu ni tatizo. wewe ndio rafiki wa mafisadi na pia ni mtetezi wa wanyonge. anyway haya ni mawzo yangu. ILA NCHI IPO PABAYA KUTOKANA NA KUKOSA UONGOZI IMARA,

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU