NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, July 3, 2009

NIMEULIZWA SWALI, NIKAJIPIGAPIGA - NA SASA NAOMBA MSAADA!!!

Mwanafunzi wa shahada ya uzamifu (PhD) anayeandika tasnifu yake juu ya Historia ya ukoloni Afrika leo alinizukia ofisini kwangu na kuniuliza swali lifuatalo:

"Ukilinganisha na sehemu nyingine duniani, Afrika haikutawaliwa kwa muda mrefu sana (takriban miaka 100 tu). Sehemu nyingine duniani kama India na sehemu nyingine za bara la Asia zilitawaliwa kwa muda mrefu zaidi (zaidi ya miaka 300).

Swali: Kwa kiasi kikubwa, ni kwa nini ukoloni wa muda mrefu zaidi India na bara la Asia ulishindwa kuziangamiza mila, tamaduni na desturi za wenyeji wa sehemu hizo wakati ilikuwa rahisi sana kwa wakoloni wa Kimagharibi kuziangamiza tamaduni, lugha na mila za Waafrika?

Nilikuwa sijawahi kufikiria kuhusu suala hili na jibu langu la haraka haraka (impromptu answer) lilikuwa kama ifuatavyo:

....Kwa bahati nzuri, tamaduni za India na Asia tayari zilikuwa na falsafa kongwe jumuishi kama vile Ubudha kule India, Uisilamu kule Uarabuni na Uconfucianism kule Uchina. Kutokana na kujikita mizizi kwa falsafa hizi, propaganda za wakoloni za "ustaarabishaji" hazikufua dafu na baada ya miaka zaidi ya miaka 300 ya kutawaliwa, tamaduni za India na Asia zilifanikiwa kutoingiliwa sana na falsafa za Kimagharibi (Ukristo, ustaarabishaji n.k.)

Afrika, kwa upande mwingine, haikuwa na falsafa jumuishi zilizoongoza maisha ya kila Mwafrika. Badala yake kila kabila lilikuwa na falsafa yake kuhusu maisha na mtazamo wao kuhusu ulimwengu na mazingira yanayowazunguka; pamoja na nafasi yao duniani. Kwa hali hiyo, ilikuwa rahisi zaidi kwa wakoloni (wakitumia mkakati wao wa "divide and rule") kuvuruga utamaduni wa Kiafrika kiasi kwamba leo Waafrika wamepoteza kabisa utambulisho wao. Kuthibitisha dai hili, nilimwambia mwanafunzi huyu, katika sehemu chache za Afrika ambazo tayari zilikuwa na falsafa jumuishi, athari za kisaikolojia na kitamaduni za ukoloni zimeshindwa kujidhihirisha sana; mf. Afrika Kaskazini ambako Uislamu tayari ulikuwa umejikita mizizi wakati wakoloni walipoingia.

Wasiwasi wangu ni kwamba, sina uhakika kama jibu langu lilikuwa na usahihi (au uzito) wo wote. Mwanafunzi huyu nilimwambia kwamba nitajaribu kutafuta maoni zaidi kuhusu suala hili. Ati, jamani, ni kwa nini ilikuwa rahisi sana kwa Waingereza, Wajerumani, Wafaransa, Wareno, Wahispania na Waitalia kuvuruga tamaduni zetu kwa muda mfupi tu wakati, kwa kiasi kikubwa, walishindwa kufanya hivyo katika sehemu zingine duniani? Nitashukuru sana kwa maoni yenu...

25 comments:

 1. hilo jibu ulilompa huyo jamaa ni sahihi. kwa mfano nchi za ethiopia, eritrea, sudan kusini, na somalia na djibouti zilikuwa chini ya sabean empire lakini nchi za rwanda burundi uganda tanzania hadi sofala msumbiji zilikuwa chini ya bahima empire. nchi ya afrika ya kusini, swaziland botswana zilikuwa chini ya zulu empire. hali hii pia ya tawala taofauti zilikuwa huko afrika ya magharibi. hivyo jawabu yako kwa maoni yangu ni sahihi.

  ReplyDelete
 2. Kwa mawazo yangu naona Asia walikuwa na utamaduni uliokomaa zaidi yetu na ulisambaa zaidi yetu, pia jamii zao zilikuwa zimepiga hatua fulani za maendeleo zaidi yetu.
  Ukiangalia hata muingiliano wa mambo mengine kama kuoana huku kwetu ilikuwa ni zaidi kuliko huko Asia, nahisi pia kwa sababu ya kuwa na moyo wa kuwakubali wageni na kuwathamini zaidi ndio kukafanya hata ustaarabu wetu tukaweza kuuchanganya na utamaduni wao

  ReplyDelete
 3. Prof naomba muda na mie nichangie mada.Nataraji kuwasilisha baada ya siku 2-3.

  ReplyDelete
 4. Bwana Evarist, hakuna neno. Naamini pengine unakwenda kubukua kwanza. Ninausubiri mchango wako kwa hamu. Asante sana Bennet kwa nyongeza yako pamoja na anony. hapo juu. Mjadala huu bado uko wazi na natumaini kwamba tutaendelea kubadilishana mawazo kuhusu suala hili.

  ReplyDelete
 5. Naaaaam!! Kwa hakika sina jibu la haraka haraka kwa hili lakini ntauliza na kufikiria na naamini siku moja ntarejea kuweka maoni

  ReplyDelete
 6. Asante kwa vitu vya kuchangamsha akili, ngoja na miye nikajifue kwanza kama Evarist.

  ReplyDelete
 7. Ninakiri sikuwai kufikiria hili, na sikuwa na hiyo historia.Ila kwa haraka nimeona huo ukweli wa huyo muuliza swali, Imenipa changamoto ya kufuatilia ili niweze kujua sababu ni nini haswa. NA TATIZO LA KUIGA UMAGHARIBI UMEKUWA KWA KASI ZAIDI MIONGO MICHACHE BAADA YA WAKOLONI KUONDOKA. Na tunaendelea zaidi kupoteza mila na desturi zetu jinsi muda unavyokwenda. INABIDI NIFANYE KWANZA UTAFITI KABLA YA KULIJIBU HILI. Nategemea zaidi kusoma kwa Chachali, najua hili pia lipo kwenye eneo lake...

  ReplyDelete
 8. Kuna maswali ambayo aulizaye anahisi anajibu na hili nni moja wapo.


  Waafrika kwa mtazamo wangu huwezi kuwauliza swali kama misingi ya swali imebobea kwa ujuaji wa kimagharibi wakati siri ya Muafrika haiko vitabuni na wasomao vitabu bado wanasononeka.

  Kuna mambo ukitaka kujichanganya muulize daktari wa moyo na sayansi zake maumivu ya moyo wako ki-FILINGI:-(

  ReplyDelete
 9. Mwanafalsafa Kitururu; Sina jibu na sihisi kama nina jibu. Vinginevyo nisingeuliza. Nilipoulizwa swali hili niliduwaa na kidogo niliona aibu ni kwa nini nilikuwa sijalifikiria swali kama hili kwa kina kwani kidogo linaonekana ni swali la msingi ambalo kusema kweli mimi binafsi (kutokana na kuvutiwa na masuala ya kitamaduni zikiwemo lugha za asili) ningependa kupata jibu lake, kama lipo. Jana nimeongea na Profesa mmoja wa Historia na amenipa nadharia tete ambayo pengine inatoa fununu kuhusu swala hili. Lakini kama ulivyodokeza hapo juu ni nadharia iliyoegemea katika ujuaji wa Kimagharibi (ambao pengine hausaidii sana). Siku nikienda kijijini nitawauliza wazee kuhusu suala hili na naamini nitapata jibu la uhakika zaidi. Ngoja tusubiri wachambuzi (Evarist, Mzee wa Changamoto, Da Mija na Godwin) waliokwenda kujifua watasema nini.

  Halafu hapa umeniacha patupu na hasa neno ki-FILINGI. Wakati mwingine Wanafalsafa nyie huwa hamueleweki kirahisi..."Kuna mambo ukitaka kujichanganya muulize daktari wa moyo na sayansi zake maumivu ya moyo wako ki-FILINGI:-(

  ReplyDelete
 10. kwa mtizamo wangu ni kwamba kwa upande wa afrika wakoloni walifanya hima kuhakikisha wanaharibu kila aina ya utamaduni wetu na teknolojia zetu zote na kuhakikisha tunaishi hovyo hovyo. hujawahi kusoma pale wanaposema kuwa baadhi ya wafua vyuma na watengenezaji wa nguo walikatwa mikono?

  kazi kubwa ilikuwa ni kuahakikisha waafrika wanasahau mambo yao yoote na kufuata ya wazungu kama ilivyo leo katika utandawazi wetu. pia waliharibu mifumo yetu ya kufikiri na vyakula vyetu vizuri vijangavyo akili. jiulize ni kwa nini kuna baadhi ya makabila yanaonekana kuwa na akili nyingi linganisha na yale yasiyokuwa na akili nyingi, isho ni chakula. walihakikisha tunakula kujaza tumbo badala ya kujenga mwili. mnaokula ugali wa Sembe mnadhani mnakula au mnajaza tumbo na vyakula vingine vya kujenga akili na afya, waafrika wakabaki na hafya hatarishi (risk) na kulazimika kutegemea huruma za misaada ya utabibu wa kizungu zaidi huku akili zikishidwa kuchangamka.
  ikawa rahisi kufananisha tamaduni zetu na ushenzi na sisi tukakubali. zikaja dini zinazo mchora Yesu na wenzie wakiwa wazungu huku shetani akiwa mwafrika mwenzetu! eti hata kwenye biblia tumelaaniwa! na sisi tukakubali. ilikuwa ni rahisi sana kwao kufanya walivyotaka

  lakini pia yawezekana saana walijifunza huko walikotoka (Asia) kuwa bila kumbaka mtu kimwili, kiutamaduni na kiroho, huwezi fanikiwa kumwongoza vyema kwa hiyo ikawa njia rahisi kwao. hili linajidhibitisha kama hapa tanzania wajermani walivyoingia kwa vita na kupambana vikali na akina mkwawa, walipoenda maeno ya Kagera wakawa wapole, wakaingia kwa kutoa huduma za kijamii nk ili wakubalike na kuabudiwa.

  ndo mtizamo wangu kwa leo! GINEHE faza

  ReplyDelete
 11. Ukoloni waliongia nao wakoloni Afrika ni tofauti na ukoloni waliongia nao Asia na China. Afrika wanaume wenye nguvu walichukuliwa kama bidhaa (commodities),kumbuka katika mila zetu za Afrika za wakati ule, mfumo dume ndiyo ulikuwa unaongoza jamii, kwa kitendo cha kuwaondoa wanaume wenye nguvu katika jamii kilitosha kuyumbisha jamii.
  Ukoloni ulioendeshwa india (inslaving) kuwatawala katika nchi yao, lakini still walikuwa katika jamii yao na hii ilisaidi kulinda tamaduni zao.
  Lucy

  ReplyDelete
 12. Kwanza,kwa mtizamo wangu,nadhani itakuwa si sahihi kuhitimisha kwamba “Wakoloni walifanikiwa kuziangamiza mila,tamaduni na desturi za Waafrika” kwa vile mambo hayo matatu bado yapo katika kila jamii ya Kiafrika.Pili,ni vigumu kuzungumzia mila, desturi na tamaduni za Afrika kwa umoja kana kwamba Afrika ni bara lenye kabila au jamii moja pekee.
  Tuanzie hoja yangu ya kwanza. Kwa ujumla wao, mila, desturi na tamaduni zinajumuisha vitu kama lugha; imani za asili, kwa mfano katika mizimu, dini za asili, nk; taratibu za misiba,harusi,jando na unyago, mavuno, miiko, nk; kusherehekea maisha ikiwa ni pamoja na kutoa majina kwa watoto; matambiko, miiko, tiba na kinga dhidi ya maradhi, na vitu kama hivyo. Tukikubaliana kwamba hayo niliyotaja (na mengineyo) basi ni dhahiri tutakubaliana pia kwamba jamii za Kiafrika zimeendelea si tu kuwa na utajiri wa mila, desturi na tamaduni bali pia zimejaliwa kuwa na utajiri wa mambo hayo matatu. Kusini mwa Afrika tunaona namna wenzetu wa Swaziland, kwa mfano wanavyoendekeza mila, desturi na utamaduni wao chini ya utawala wa Kifalme.Na kama kuna jambo linawatambulisha vema wenzetu wa Kusini mwa Afrika ni majina yao: Sikhotwe, Phumi, Nsikholele, nk.Kuthibitisha kuwa “Wamagharibi” hawakufanikiwa “kihivyo”, kila mwaka tunasikia “malalamiko” kuhusu mila ya Mfalme Mswati kuoa mke mpya kila mwaka na visichana vigori kufanya maandamano huku wakiwa “nusu-utupu” kumvutia mtawala wao. Mara nyingi malamiko hayo ni kutoka kwa “watetezi wa haki za wanawake”, jambo jingine lenye asili ya u-Magharibi.
  Magharibi mwa Afrika tunashuhudia wenzetu wa Nigeria wanavyoendekeza utamaduni wao kwa kuenzi majina yao ya asili. Kama ilivyo kwa wenzetu wa Kusini,Wanigeria hutambulika zaidi kwa majina yao yenye sifa ya ugumu wa kutamkika: Ikwechuku,Ifekema,nk.Wanigeria wamefanikiwa pia kuwa katika kuutangaza utamaduni wao (au wa Kiafrika?) kwa njia ya sanaa ya filamu.Yayumkinika kusema kwamba moja ya vipengere muhimu katika filamu hizo ni mambo mbalimbali ya kitamaduni.
  Kaskazini mwa Afrika tuna Waafrika wenye asili ya Uarabu, au tuwaite Waarabu kabisa.Ni vigumu kuzihukumu jamii kama hizi kwamba mila, tamaduni na desturi zao zilimezwa na wageni kwavile nyingi ya jamii hizo ni za Kiislam pengine kabla ya ujio wa Wakoloni. Kilicho dhahiri, hata hivyo, ni ukweli kwamba ukoloni uliacha madhara flani hususan kwenye lugha, ambapo tunashuhudia uimara wa Kifaransa katika nchi kama Tunisia na Morocco. Hilo ni dhahiri pia hata kwa nchi kama India, ambapo Kiingereza si tu lugha muhimu bali pia hata katiba ya India ina chembechembe za sheria za Kiingereza.Ni majuzi tu Mahakama moja ya juu nchini humo imeharamisha zuio dhidi ya mahusiano ya jinsia moja ambalo ni matokeo ya sheria iliyowekwa na Waingereza nyakati za ukoloni.

  INAENDELEA

  ReplyDelete
 13. Afrika ya Mashariki, Kati na Pembe ya Afrika imeendelea kuwa na jamii zinazoenzi mila, desturi na tamaduni zao.Wamasai wa Tanzania na Kenya ni moja ya mifano hai, kama ilivyo kwa Mbilikimo wa misitu ya kitropiki ya Kongo.Licha ya kuwa chini ya tawala za wakoloni wa aina mbili tofauti,Wamakonde wa kusini mwa Tanzania na Wamakonde wa Msumbiji wameendelea na tamaduni zao za ngoma za unyago na “urembo” wa kuchora nyuso zao.Si Mjerumani na hatimaye Mwingereza (kwa upande wa Tanzania) au Mreno aliyeweza kufuta utamaduni huo.Wanyasa wa Malawi na Watanzania, kama ilivyo kwa Wamanda,wameendelea na kuenzi mila,tamaduni na desturi zao licha ya mipaka iliyowekwa na tawala za Wakoloni.
  Tuangalie hoja yangu ya pili.Ni vigumu kuzungumzia “mila, tamaduni na desturi za Waafrika” kana kwamba tunazungumzia jamii moja pekee. Licha ya kuwa na nchi zaidi ya 50,bara la Afrika lina utitiri wa makabila huko mengi yao makabila hayo yakiwa na mila, desturi na tamaduni zinazotofautiana na wenzao.Jaribio lolote la kutengeneza u-moja wa aina hiyo kwa minajili ya uchambuzi linaweza kuharibu matokeo ya uchambuzi huo.Tuchukulie Tanzania, kama mfano mwepesi. Tuna makabila zaidi ya 120 japo mengi ya makabila hayo yana asili ya Wabantu.Marehemu mama yangu alikuwa M-bena wa Malinyi.Lakini kuna Wabena wengine wako Iringa, japo ni makabila mawili tofauti. Kuna kabila huko Kilombero linaitwa Wambunga.Inaelezwa kuwa hawa wana ukaribu na Wangoni wa Songea na kabila jingine (jina limenitoka) lililopo Tabora.
  Lakini hata tukiachana na suala la viwango (kwa maana ya idadi) naamini tunaweza kukubaliana kuwa sio Wandamba (kabila langu) tunaoendelea kuamini nguvu za mizimu licha ya ukweli kuwa miongoni wa Wandamba kuna akina Evarist (Mkristo) na Hamisi (Muislam).
  Pengine hapa ni mahala mwafaka pa kugusia namna dini za kimapokeo, yaani ukristo na uislam zilivyoshindwa kuzimeza dini za asili za kiafrika ambazo kimsingi ndizo zilizosheheni mila, desturi na tamaduni mablimbali za Waafrika.Ni muhimu pia kupigia mstari uelewa kwamba “dini ZA Kiafrika” si moja kama ilivyo Ukristo au Uislam bali ni wingi. Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kwamba 2/3 ya Watanzania ni waumini wa dini hizo za mapokeo,ilhali sehemu iliyobaki ni waumini wa dini za asili za Kiafrika.Lakini,katika 2/3 hiyo kuna idadi ya msingi tu ya waumini wa dini hizo za mapokeo ambao bado wanathamini,kuenzi na kuendeleza mila, desturi na tamaduni zao za asili.

  INAENDELEA

  ReplyDelete
 14. Moja ya mambo yaliyousambaza Uislam kwa kasi katika sehemu mbalimbali za Tanzania ni uwepesi wake wa kukubali mila, tamaduni na desturi za “wenyeji”. Hapa napigia mkazo u-Sufi-“aina” ya Uislam unaoweza kuitwa pia Uislam wa Kiafrika (Kitabu cha Westerlund na Evers cha Uislam wa Kiafrika na Uislam katika Afrika kinaelezea vizuri kuhusu hilo).Kwa upande wake, Ukristo, ulikumbana na vikwazo mwanzoni kwa vile licha ya kuziona mila, desturi na tamaduni za Kiafrika kuwa za “KISHENZI” na kishetani, ulidhamiria kuziangamiza pia (kama hitimisho la mwanafunzi wako linavyoamini).
  Binafsi, hitimisho langu ni kwamba japo Uislam na Ukristo ulifanikiwa kuteka waumini wa dini za asili za Kiafrika haukufanikiwa na haujafanikiwa kufuta mila, desturi na tamaduni zilizotawala dini hizo za asili.Na baada ya dini hizo za kimapokeo kubaini kwamba suala hilo haliwezekani,zilichukua mwelekeo wa kuzijumuisha mila hizo.Hudhuria sherehe za kusimikwa upadre au uaskofu na utaelewa vizuri nachozungumzia.Kwa bahati nzuri kwa Waislam,u-Sufi una vipengere vinavyoshabihiana na baadhi ya matendo ya dini za asili za kiafrika kama vile nafasi ya mizimu kwa dini za asili na mysticism (samahani sina tafsiri yake kwa Kiswahili) kwenye u-Sufi,au dhikr na ngoma za asili,japokuwa kimsingi mambo hayo yana tofauti zake pia.
  Mhadhiri mmoja wa Sosholojia ya Dini, na mtajwa muhimu kwenye chambuzi za mahusiano ya dini Tanzania,anaeleza kwanini kanisa Katoliki pale Chang’ombe “linaangalia” eneo la “Machinjioni” .Anabashiri kuwa mwelekeo wa kanisa hilo ni sehemu ya kujumuisha mila za dini za asili za kiafrika kuhusu uhai na kifo. Katika dini za asili za Kiafrika, kuna “wafu-hai” na “wafu-wafu” (the living dead and the dead dead).Wafu hai ni roho za marehemu zinazokumbukwa baada ya vifo vyao, ikiwa ni pamoja na kuyaenzi majina yao kwa vizazi vipya (jina la marehemu babu au bibi, kwa mfano) ilhali wafu-wafu ni roho za marehemu waliokufa na kisha “kutelekezwa” (kwa mfano wanaokufa ajalini na kutotambuliwa na ndugu zao).Katika sosholojia ya dini, wafu-hai wanachukua nafasi ya umungu wa namna flani kwa kuleta baraka kutokana na kukumbukwa na walio hai ilhali wafu-wafu ni sehemu ya vyanzo vya mabalaa kutokana na “kutelekezwa” huko. Mfano mzuri ni maeneo ambapo ajali nyingi hutokea (kama hapo Machinjioni) ambapo wafu-wafu wanahusishwa na maeneo hayo kuwa vivutio vya ajali zaidi.

  inaendelea

  ReplyDelete
 15. Pengine tunaweza kujiuliza swali hili jepesi: ni kabila gani nchini Tanzania, kwa mfano, ambalo hivi sasa, au baada ya ukoloni limebaki halina mila, desturi na tamaduni? Yaani kabila ambalo habari za jando au unyago, matambiko, miiko, lugha za asili, nk viliangamizwa na mkoloni? Tukifanikiwa kuiangalia Tanzania kama eneo letu la uchambuzi wa awali, itatuwia rahisi “kuvamia” maeneo mengine ya Afrika, na hatimaye kupata hitimisho lenye kuepuka hitimisho wa mambo yenye tofauti.
  Swali hilo linaweza pia kugeuzwa kuwa hivi: je ni mila, desturi na tamaduni gani zilizoangamwizwa na mkoloni-iwe Tanzania au popote pale Afrika? Tunaweza kwenda mbali zaidi na kujiuliza iwapo baadhi ya jamii za Kiafrika “ziliamua kuachana na mila, tamaduni na desturi zao kwa hiari yao zenyewe” (kama ilishawahi kuwa hivyo) pasipo shinikizo kutoka kwa wakoloni. Nasema hivyo kwa maana kwamba si kila aliyeingia Ukristo au Uislam alilazimishwa kufanya hivyo. Kuna watumwa waliojiunga na ukristo kama njia ya kuepuka utumwa, kama ambavyo kuna waliojiunga na uislam kwa vile walichukizwa na “dini ya mkoloni”-ukristo.Tukumbuke kuwa kabla, wakati na baada ya ukoloni, Waafrika walikuwa na wameendelea kuwa na utashi wao, na baadhi ya maamuzi yao yalitokana na utashi huo.
  Hitimisho langu ni kwamba si kweli kwamba wakoloni walifanikiwa KUANGAMIZA mila, desturi na tamaduni za Waafrika kwani bado zipo na zinaendelea kuenziwa.Kilicho bayana ni kwamba ukoloni ULIFANIKIWA KUHARIBU NA KUACHA ATHARI KWENYE mila, desturi na tamaduni hizo. Kuna tofauti kati ya KUANGAMIZA na KUHARIBU. Wakati inatarajiwa kuwa kilichoangamizwa hutoweka, kinachoharibiwa kinaendelea kuwepo japokuwa si katika hali yake ya awali lakini kinaweza kukarabatiwa pia.
  Angalizo jingine muhimu ni nafasi ya mifano hai katika kuthibitisha hoja. Ingekuwa muhimu kwa muuliza swali kutoa mifano hai ya mila, desturi na tamaduni za Kiafrika zilizoangamizwa na Wakoloni sambamba za hizo za Wachina, Wahindi, nk zilizosimama kidete dhidi ya nguvu za Wakoloni. Sambamba na hilo ni muhimu kuangalia nafasi ya watawala wa asili kabla ya ujio wa wakoloni (u-mungu mtu wao na madhara ya kuanguka kwa tawala zao), mahusiano ya jamii mbalimbali kabla ya ujio wa wageni kutoka nje (vitu kama Mfekane na biashara ya utumwa) na mbinu mbalimbali zilizotumiwa na mawakala wa ukoloni, na baadaye wakoloni wenyewe katika kuwazitawala jamii mbalimbali za Afrika, na hatimaye kuangalia madhara ya ukoloni baada ya kuondoka kwake.
  Na pengine cha mwisho ni kwa muuliza swali kuangalia upya nafasi ya utandawazi-ambapo tunaambiwa kuwa dunia inakuwa kama kijiji-katika hizo jamii anazoamini kuwa “hazikuangamizwa na miaka takriban 300 ya tawala za kigeni”.Pamoja na utandawazi ni mfumo wa kisiasa na kiuchumi ulimwenguni ambapo maamuzi yanayofanyikwa Washington yanamgusa hadi mkulima anayetegemea uchumi haramu wa “poppy” huko Kandahar au tamaa za kibepari zilivyoishia kuwagawanya “Wahindi” wa Kashmir,au-lililo relevant zaidi-athari za kutengemaa kwa uchumi wa dunia zinavyovoka historia,jigrafia,siasa,uchumi na tamaduni za jamii mbalimbali.

  ReplyDelete
 16. Evarist! Duh!! umechambua haswa.
  Mimi nafikiri bado tuna mila zetu, na wala hazijaangamia kama mwana PhD alivyouliza. Achukulie mfano wa wamasai na warbaig, mabadiliko ni kama zero. Ukienda kwa wagogo, wamakonde nk, bado wanfuata mambo ya jadi. Mijini na maborn town tu ndio wanaiga mambo ya wakoloni kwa sana. Nchi za bara Asia, zina utitiri wa watu, kama asilimia 10 tu ndio imeathirika kwa kuiga tamaduni na 90% imebaki kama ilivyo, basi ujue hapo unaongelea mabilioni ya watu, wakati Afrika kama ni 5% tu ndio iliyoathirika, na 95% ILIYOBAKI BADO, BASI UJUE UNAONGELEA TUMILIONI TWA WATU. Fanya utafiti ili upate evidence based results. Utashangaa bado waafrika tuna msimamo na jadi. Mfano mzuri ni mwanablog hii, fuatlia majina yake ndio utajua kuwa mila bado zipo.
  Kinehe!

  ReplyDelete
 17. Swala bado linanizingua kichwa hili.

  Halafu Profesa katika Comment yangu ya juu niliyezungumzia aulizaye ambaye nahisi anahisi ana jibu ni yule aliyekuuliza swali hilo na sikumaanisha wewe. Ki-FILINGI nili maanisha kwa kutumia FEELINGS.

  Ngojea niendelee kukuna kichwa na Mkuu Evarist umeniongezea maswali Duh!:-(

  Bado najiuliza pia kama ni kweli WAAFRIKA wamepoteza TAMADUNI, lugha na mila zao!

  ReplyDelete
 18. Mwanafalsafa Simon; nimekupata. Ngoja kwanza nisome comments za Evarist halafu nitachangia kwa kina baadaye kidogo. Asanteni sana!

  ReplyDelete
 19. Evarist amefanya kazi kubwa kutupa mtazamo mpana kuhusu hoja hii. Nimesoma kwa makini hoja zake, na kusema kweli zinasisimua sana na kupanua mawazo.

  Kimsingi, kwa nilivyomwelewa mimi, Evarist amegoma kukubaliana na muuliza swali kwa hoja.

  Mimi nina mtazamo tofauti. Kwamba nakubaliana na swali la msingi kuwa Afrika imeweza kutokomeza mila na desturi zake kuliko Asia.

  Ushahidi rahisi huu hapa wakati tunasubiri wenye data za kitarakimu watupe:

  Dini. Katika Afrika, imekuwa rahisi zaidi kwa zile dini za kimapokeo kukubaliwana kuchukuliwa kama sehemu ya utamaduni wa mahali. Idadi kubwa ya wenyeji wa Afrika, ni waamini wa dini za kimapokeo. Hili liko wazi. Leo hii ni asilimia ndogo sana ya Waafrika wanaamini katika dini za asili. Ndio inawezekana kuwa yapo maeneo ambako dini za jadi bado zinatawala. Chukulia mifano kama wamasai kwa sisi waafrika Mashariki. Lakini asilimia kubwa, wamekubali kwa hiari yao kuachana na dini zao, na kuzipokea dini za watu wa magharibi ama Asia na kuwaita wenzao wasioamini dini hizo kuwa ni wapagani. Hali ni tofauti kwa Asia kwa mfano. Dini zenye nguvu India leo hii ni zile zenye asili ya kule kule mathalani Ubudha, Uhindu na kadhalika. Japani na China wanaamini katika dini zao (Shinto, Tao na kadhalika). Kwa hiyo utaona wenzetu pamoja na kutawaliwa, bado wameendelea kuamini dini zao, na dini zao zimeweza kusambaa hata na maeneo mengine kama Afrika Mashariki na kadhalika.

  Naendelea...

  ReplyDelete
 20. Majina. Asilimia kubwa ya wenyeji wa Afrika wamepuuza majina yao. Leo hii tunaamini kuwa yapo majina ya kidini –kwa mfano, ambayo kimsingi yanatukuza utamaduni wa wageni. Chukulia mfano wa jamii ya Kitanzania (ambayo kama anavyosema Evarist ina diversity ya watu), asilimia kubwa hawana majina ya jadi. Uchunguzi rahisi: Angalia orodha yoyote yenye majina zaidi ya mia moja (mfano ya wanaoitwa kwenye usaili, ama hata orodha ya Wabunge) asilimia tisini na, wana majina ya kigeni (ukiacha yale ya Ubini ama ukoo). Na hiyo haina maana kwamba hatuna majina hayo. Tunayo. Ila tunayaita ya utoto, ama ya kinyumbani. Na wengine wetu hatuyapendi. Wamasai wengi wanaitwa majina ya “Kikristo” hata kama wanaonekana kuamini katika dini zao. Kasi ya wamasai kuzigeukia dini za kigeni hivi sasa tunapojadili suala hili, ni kubwa vya kutosha. Hao wachache ambao wanaenzi majina yao, ni asilimia ndogo sana ukilinganisha na sisi tuliobaki.
  Ukija Asia, wenyeji wanatumia majina yao wenyewe. Na hata wanapobadili dini, jambo ambalo ni la nadra sana, bado wanabaki na majina yao wenyewe. Hili liko wazi.

  Lugha. Afrika imepoteza kwa urahisi sana lugha ya asili. Hili liko pote. Naijeria ambayo ina nafuu katika maeneo mengine ya kiutamaduni, leo hii inatumia Kiingereza kama lugha ya taifa. Hatujazungumzia Afrika Kusini na Kwingineko. Lugha zote zinazoheshimiwa na Waafrika wote ni zile za Kigeni. Asilimia kubwa ya mataifa ya Afrika, wanapuuza lugha za mahali. Tunaona fahari kujua Kiingereza, Kifaransa, Kireno na kadhalika ana sio kujua Kimasai, Kisukuma ama Kinyaturu.

  Mfano wa karibu, mpaka leo inasikitisha kuwa watu wazima wasomi bado wanahoji ikiwa ni lazima kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia sekondari (acha Chuo Kikuu). Tatizo hilo halipo kwetu tu, ni maeneo yote barani Afrika kwa ujumla wake.

  Lakini tukiangalia nchi za Asia, kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa. China, Korea, Japani na India, lugha zinazopendwa ni za wenyeji. Huu ni ushahidi wa wazi.

  Mtandao unadai naandika sana ngojea kidogo....

  ReplyDelete
 21. Ushahidi mwingine, ni mfumo wa maisha ya sisi Waafrika. Tizama mavazi. Ukiacha nchi za Afrika Magharibi, tuliobaki kwa asilimia kubwa tunavaa kimagharibi. Mashati na suti za Kiitaliano. Kama si kizungu, basi tunavaa Kiarabu. Hijabu. Kanzu. Tunafuga madevu. Hayo yote si sehemu kamili ya utamaduni wetu. Na kwa bahati mbaya hili limeenea kwa karibu Afrika nzima ukiacha execeptions ndogo ndogo zisizoleta tofauti sana.

  Na mifano mingine mingi kama namna tunavyoiga utamaduni wengine katika masuala kama harusi na kadhalika.

  Njoo Asia. Watu wale wamefanikiwa kuwa na namna yao ya maisha inayowatofautisha na wamagharibi. Angalia wanavyovaa. Samani wanazotumia katika nyumba zao (wengine wanakaa chini kabisa. Haya yote yana sura ya kienyeji zaidi kuliko kigeni. Naamini huu ni ushahidi mwingine wa wazi wa namna tunavyotofautiana na hawa.

  Kwa hiyo, nadhani kaka Evarist tukukubaliane na ukweli wa swali lenyewe kama nilivyojaribu kuliwekea mifano iliyonijia kwa haraka hapo juu.

  Hata hivyo, nakubalianana wewe kwamba jamii ya kiafrika iko divestified kwa maana ya kuwepo tofauti ndogo ndogo nyingi kati ya jamii moja na nyingine kuliko kule Asia. Lakini asilimia kubwa, inaonekana wazi kwamba mila na desturi zimepewa kisogo.

  Sasa kwa kusema hivi, nadhani tunahitaji kujikita katika kutafuta majibu ya kina ya kipi hasa kilichosababisha “uzembe” huu wa kiutamaduni, ambao kimsingi upo.

  Nisamehewe kwa mcharazo, nimejaribu kuandika kwa kasi kidogo.

  ReplyDelete
 22. Kwanza niombe msamaha kwa kupotea kwangu. Ni mahangaiko ya maisha tu.

  Kamala, nakubaliana nawe karibu kwa kila kitu, isipokuwa hilo la ugali wa sembe. Kwa msukuma ugali ndiyo maisha na ukisukumizia na maziwa ya mgando (protini kibao) na kesho yake ukakimbizana na ndama, sidhani kama kuna tatizo. Watu wa mambo ya lishe wanajua zaidi.

  “…lakini pia yawezekana saana walijifunza huko walikotoka (Asia) kuwa bila kumbaka mtu kimwili, kiutamaduni na kiroho, huwezi fanikiwa kumwongoza vyema kwa hiyo ikawa njia rahisi kwao. hili linajidhibitisha kama hapa tanzania wajermani walivyoingia kwa vita na kupambana vikali na akina mkwawa, walipoenda maeno ya Kagera wakawa wapole, wakaingia kwa kutoa huduma za kijamii nk ili wakubalike na kuabudiwa…”

  Hapa umegonga pointi – bila kumtawala mtu kifikra huwezi kumtawala kimwili na kumnyonya sawasawa. Wamarekani, kama taifa, hawakutawala mtu kimwili (physically) na pengine somo hili muhimu hawakulijua ama walikuwa wamelisahau. Kama wangelijua/kulikumbuka kamwe wangeacha tabia yao ya kukimbilia vitani bila kwanza kukaa chini na kupanga mikakati ya kuitawala akili ya hao wanaoenda kuwapiga (wawe ni Wavietnam, Wasomali, Wairaq au Waafghanistani) kabla ya “ukombozi” na “demokrasia” yao wanayodai wameipeleka huko haijaota mizizi. Sasa naamini wanajuta. Wakiwa kama Goliati mwenye majivuno, maringo, na silaha kali, wametatanishwa sana na Daudi mwenye kombeo tu. Ni aibu kwa taifa lenye kila aina ya silaha kuhangaishwa na watu ambao bado wanatumia ngamia! Walitakiwa kutambua mapema kwamba hakuna silaha hapa duniani ambayo inaweza kushinda utashi wa mtu. Ndiyo maana wenzao waliingia na Biblia kwanza na kuwafundisha Waafrika kugeuza shavu la kushoto wanapotandikwa lile la kulia, na kuheshimu mamlaka kwani mamlaka zote zimetoka kwa Mungu. Na walifanikiwa sana…. Naendelea na Evarist hapa chini.

  ReplyDelete
 23. Bwana Evarist, ni kweli ulikwenda kubukua kwani uchambuzi wako ni wa kina kabisa, tena uliosheheni mifano mingi. Huyu jamaa naona tayari umeshampa PhD kabisa. Nimemnakilishia maoni yako yote na nimemuomba atafute mtu anayefahamu Kiswahili vizuri amtafsrie. Asante sana kwa mchango wako. Mimi nina maneno machache tu hapa chini.

  “…Hitimisho langu ni kwamba si kweli kwamba wakoloni walifanikiwa KUANGAMIZA mila, desturi na tamaduni za Waafrika kwani bado zipo na zinaendelea kuenziwa. Kilicho bayana ni kwamba ukoloni ULIFANIKIWA KUHARIBU NA KUACHA ATHARI KWENYE mila, desturi na tamaduni hizo. Kuna tofauti kati ya KUANGAMIZA na KUHARIBU. Wakati inatarajiwa kuwa kilichoangamizwa hutoweka, kinachoharibiwa kinaendelea kuwepo japokuwa si katika hali yake ya awali lakini kinaweza kukarabatiwa pia…”

  Kwanza napenda niseme kwamba nakubaliana na hitimisho lako hapo juu. Ni kweli kwamba mila na utamaduni wa Mwafrika bado havijafa kama ulivyoonyesha kwa kina bali vimejeruhiwa tu. Swali ambalo tunapaswa kujiuliza ni hili: majeraha haya ni hatarishi au ni mikwaruzo tu na pengine yatapona? Nitatoa mifano kuhusu suala la lugha zetu za Kiafrika kwani, kama asemavyo Ngugi wa Thiong’o, lugha hasa ndiyo mlezi na mbeleko inayobeba utamaduni wa watu.

  Wanaisimu jamii wengi wana wasiwasi sana na hali duni ya lugha asili za Afrika kiasi kwamba wanazungumzia kuhusu kifo cha hadhara (nataka kusema mass extinction) kama ilivyotokea kwa “dinosaurs” Na kama hili litatokea basi Afrika itakuwa imepoteza utajiri mkubwa wa kitamaduni. Na lugha karibu nane hivi tayari zimeshakufa na nyingine nyingi ziko hoi bin taabani.

  Mwaka 2003, shirika la UNESCO lilikusanya vingunge wa isimu na kuwaomba wapendekeze “dalili” au vigezo vitakavyosaidia kuonyesha “afya” ya lugha. Wataalamu hawa walipendekeza vigezo kadhaa vikiwemo urithishwaji wa lugha mama kutoka kizazi kimoja hadi kingine, mtazamo wa wazungumzaji kuelekea lugha yao, idadi ya wazungumzaji wa lugha hiyo, idadi ya wazungumzaji ikilinganishwa na jumla ya idadi ya watu wote katika nchi husika, nyanja ambamo lugha hiyo inatumika (mf. matumizi rasmi au ni lugha ya nyumbani tu), mtazamo wa serikali na mashirika mengine kuelekea lugha, upatikanaji wa machapisho (mf. vitabu, kamusi) katika lugha husika, lugha inavyojishabihisha na mabadiliko ya kimatumizi kulingana na mabadiliko (mf. ya kisayansi na kiteknolojia kama vile mtandao n.k) - naendelea

  ReplyDelete
 24. Kwa kutumia vigezo hivi wataalamu wengi wanakiri kwamba lugha za Afrika hasa ndiyo ziko katika hatari kubwa ya kupungua kimatumizi na kama jitihada hazitafanyika basi zinaweza kutokomea kabisa. Ni wazi kwamba watoto wa kizazi cha dot com hawajifunzi lugha za mama kama inavyotakikana na wana sababu nyingi nzuri za kufanya hivyo. Uchumi na sera tulizorithi zinatilia mkazo matumizi ya Kiingereza (na kwa kiwango cha chini Kiswahili) na vijana hawaoni hasa sababu wala faida ya kujifunza na kufahamu Kisukuma sawasawa. Hali hii imeshaanza kufika hadi vijijini. Unafikiri kitatokea nini kwa watoto wa watoto wa vilembwe wa kizazi hiki cha dot com? Wataweza kweli kuzungumza Kindamba? Kindamba kitakuwepo? Unaweza kungalia hivyo vigezo vya UNESCO kimoja baada ya kingine na unaweza kuona kwamba pengine wasiwasi unaoonyeshwa na wanaisimu jamii wengi kuhusu lugha za Afrika ni wa kweli. Na kinachoshangaza ni kwamba japo kuna lugha chache kwingineko duniani zinazokabiliwa na hatari hii ya kutoweka, Afrika hasa ndiko kwenye uwanja wa mapambano kwani, karibu katika bara zima lugha za kiasili zimedumazwa na hazina nguvu za kiuchumi – zipo tu kama hazipo; Bara zima limekazania kujifunza lugha za mabwana wa kikoloni. Swali linakuja – kwa nini Afrika na si kwingineko duniani? Mbona hali hii ya kutisha hatuioni katika mabara mengine? Ndipo hapo uhalali wa swali la muuliza swali unapokuja.

  Leo hii kuna mikakati mingi ya kujaribu kuziokoa lugha za Afrika zisije zikafa. Kuna harakati kali kujaribu kuziandika na kuzirekodi lugha hizi ili hatimaye kuzihifadhi kabla hazijatoweka, na mashirika mengi yanatoa pesa kwa wanaisimu mbalimbali kufanya hivyo mapema. Sijui Kindamba kina hali gani? Unajua kina wazungumzaji wangapi? Watoto bado wana ari ya kujifunza? Unafikiri kwamba kitakuwepo baada ya vizazi vinne au sita hivi? Pengine tunaweza kukiandikia sarufi na kukirekodi (nyimbo, mashairi, matambiko n.k.) kama zinavyofanyiwa lugha nyingine ambazo vigezo vya UNESCO vinaonyesha kwamba zimo katika hatihati zaidi.

  Japo ni kweli kwamba utamaduni wa Mwafrika bado haujafa, utamaduni huo hata hivyo umejeruhiwa mno na majeraha mengine ni hatarishi kabisa ambayo kama yakiachwa bila kushughulikiwa yanaweza siku moja kuuangamiza kabisa utamaduni huo kama suala la lugha linavyoonyesha. Swali linabakia palepale, kwa nini Afrika?

  Kwa nini leo hii mtu unaenda kwa mganga wa kienyeji kwa kujifichaficha – hata kama lengo lako ni kutafuta tiba ya ugonjwa unaokusumbua na ambao pengine hospitali za kisasa zimeshindwa kukusaidia?

  Kwa nini inaonekana kuwa ni ustaarabu kwenda kanisani na siyo kwenda kutambika katika jiwe kubwa lililo karibu na ile njia panda ya mtoni – ingawa ni sawa kwa mamilioni ya Wahindu kwenda kutambika katika mto Ganges?

  Kwa nini leo ni bora kujiita Joseph au Hassan kuliko Kamala au Masangu, wakati ni sawa kwa Mthailand kujiita Kriengsak Niratpattanasai? Ni kweli kwamba Afrika iliathiriwa zaidi na ukoloni pengine kuliko sehemu zingine na hasa zile za Asia kama muuliza swali alivyodai? Sehemu ya mwisho inakuja...

  ReplyDelete
 25. Bwaya ametoa mifano mingi mizuri kuhusu suala hili.

  Mwisho napenda nimalizie na maoni ambayo nilipewa na Profesa mmoja wa Historia. Yeye pia alikiri kwamba Afrika pengine iliathirika zaidi na Ukoloni na alisema kwamba hili si jambo la kushangaza ukizingatia “tofauti za kimaendeleo” zilizokuwepo kati ya Ulaya (ambayo ilikuwa imeingia katika mfumo wa kibepari) na Afrika (ambayo kusema kweli sehemu zake nyingi zilikuwa bado katika mfumo wa ujima na chache katika ukabaila). Profesa huyu alifafanua kwamba inapotokea jamii mbili zikagongana ama kwa sababu za kibiashara, kiutawala au kiuchumi, kwa kawaida jamii ambayo inaonekana kuwa “imeendelea”, utamaduni wake ndiyo huigwa na ile jamii nyingine ambayo inajiona/inaonwa kwamba iko chini kimaendeleo. Alinitolea mfano wa lugha za Kibantu – kwamba pengine ziliweza kusambaa kutokea Cameroon, misitu ya Kongo, Afrika Kusini na hatimaye Afrika ya Mashariki kwa sababu wazungumzaji wake walikuwa (au walionwa kuwa) ‘wameendelea” na ilikuwa rahisi kuzimeza lugha zingine na utamaduni wa wazungumzaji wake. Kwa upande wa Asia, ama hakukuwa na tofauti kubwa za kimaendeleo kati yake na wavamizi wa Ulaya au tayari kulikuwa na falsafa zilizokuwa zimejikita mizizi ambazo zilifanya kazi kama gundi ya kuwaunganisha watu na kuupambanua utamaduni wao. Ndiyo, kama alivyotaja Bwaya, Profesa huyu alitaja Uhindu, Ubudha, Ushinto n.k. Alisema kwamba hizi siyo dini tu bali ni mifumo inayotawala maisha ya watu na wakoloni wa Kimagharibi hawakuweza kabisa kuzipenya ngome hizi za kiitikadi.

  Hitimisho: Japo pengine ni kweli kwamba utamaduni wa Mwafrika haukutokomezwa kabisa, kusema kweli uko katika hali mbaya mno na kama mojawapo ya vipengele muhimu kabisa (lugha) vinavyoonyesha, utamaduni huo unaweza kutokomea kabisa hatimaye kama tusipofanya jitihada za makusudi kuuokoa. Shirika la UNESCO pamoja na wanaisimu jamii wengi wametoa mapendekezo kadhaa kuhusu nini cha kufanya. Ajabu ni kwamba hakuna anayejali!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU