NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, July 31, 2009

RAIS BUSH NA BASTOLA YA SADDAM HUSSEIN

Hapa duniani kweli hakuna haki. Ile bastola ambayo Saddam Hussein alikamatwa nayo shimoni alikokuwa amejichimbia imeinukia kuwa mojawapo ya vitu vya thamani sana kwa rais Bush na amekuwa akiwaonyesha wageni wake mara kwa mara. Bastola hiyo pengine ndiyo itakuwa kivutio kikubwa katika maktaba ya Rais huyo inayojengwa katika chuo kikuu cha Southern Methodist kilichoko Dallas (Kwa habari zaidi soma hapa)

Pamoja na kwamba Saddam alikuwa dikteta lakini alikuwa kiongozi wa nchi huru; na Marekani hawakuwa na haki yo yote ya kuvamia nchi huru na kumuua kiongozi wake na maelfu ya raia wasio na hatia. Kuna madikteta wangapi ambao Marekani hiyo hiyo inayohubiri "demokrasia" inawalea na kuwaenzi? Ni nani aliyemlea Saddam katika miaka ya sabini? Ni nani aliyempa silaha na pesa Osama Bin Laden wakati ule akipambana na Warusi Afghanistan? Ni nani aliyemuua Patrick Lumumba na kumuweka dikteta Mobutu Sésé Seko Nkuku Ngbendu wa Za Banga mahali pake? Ni nani aliyempindua Kwame Nkrumah? Ni nani...? Kilichomuua Saddam ni jeuri yake ya kukataa kuwamilikisha Wamarekani mafuta ya Iraq. Na sasa bastola yake itakuwa mojawapo ya vipimo vya "mafanikio" kwa rais aliyeshindwa, rais aliyeiingiza nchi yake katika vita visivyo na maana na kuharibu kabisa uchumi wake. Aibu, ulimbukeni na uzezeta wa mwaka!

Huyu hapa Saddam katika vipindi tofauti vya maisha yake. Onyo na funzo kwa viongozi wa dunia: Ipe Marekani inachotaka vinginevyo utaishia kwenye "gallows". Je, Marekani yenyewe itakuwepo milele?

3 comments:

 1. Niliwahi kuuliza "tunazidi kujipoteza katika harakati za kujitafuta" (http://changamotoyetu.blogspot.com/2009/03/tunazidi-kujipoteza-katika-harakati-za.html) na nakumbuka mwishoni niliandika "Watu kutenda yasiyotendeka ili mradi tu wanataka kujidhihirisha kuwa nao wana uwezo. Nchi zinavamia nchi nyingine ili "kutuma ujumbe" kwa wengine kuwa wasithubutu kuwa kama wenzao. Viongozi wanasitisha huduma kwa baadhi ya sehemu kwa kuwa tu hawakupigiwa kura sehemu hizo. Watu wanaotoa utu na kutenda mauaji kwa albino ili tu kutafuta nafasi ya maendeleo maishani mwao. Madereva ambao kwa kutaka kudhihirisha kuwa nao wamo kwenye kuendesha wanakwenda zaidi ya mwend kasi wa kawaida na kuishia kuua wasio na hatia."
  Ndipo ninapokuwa na tatizo na siasa. Siasa hutafsiri mambo kulingana na MASLAHI., Mtu atakuwa SHUJAA sasa lakini akibadili maslahi atakuwa GAIDI. Watakwambia Demokrasia ni ile ambayo inawapa wananchi nafasi ya kuchagua kiongozi wao (chini ya uangalizi wao) lakini wakihisi hufai watakuletea "version" mpya ya demokrasia kwa kukuingilia, kukutoa madarakani (kama hawatakuua) kisha kumuweka wampendaye mpaka akatakapokuwa na uwezo wa kuwarubuni wananchi na "kuchaguliwa" na hapo wataona "mwanzo mpya wa demokrasia) katika nchi yako.
  Watapinga utoaji mimba wakisema ni dhambi na ukatili kwa mtoto (naamini wako sahihi) lakini watoto hao hao wanaweza kukua na kuuawa na wao wapingao mauaji ya watoto kwa kuwa tu MTAWALA wao ameshindwa kukukubaliana na MAHITAJI yao.
  Hapa Marekani wanasema mtu wa chini ya miaka 21 hana uwezo wa kufanya maamuzi makubwa saana kwa hiyo haruhusiwi kunywa pombe, lakini ukia na miaka 19 unaweza kupelekwa vitani na kukabidhiwa BUNDUKI kisha ufanye maamuzi ya kumfyatulia mtu risasi ama la.
  Ndio maana pia niliandika kuhusu CRY FO JUSTICE na ukisoma kwa makini utaona aliyoyasema Luciano. http://changamotoyetu.blogspot.com/2009/05/them-i-themlucianocry-for-justice.html
  Naacha.
  Asante kwa CHANGAMOTO MOTOMOTO

  ReplyDelete
 2. Mzee wa Changamoto, nimekupata sawasawa. Nimesoma hizo post zako mbili ulizozirejelea na zote zinachangamsha na kufikirisha sana. Asante.

  ReplyDelete
 3. Suala la mashindano ya urembo ni kama kasumba ambayo imetukaa vilivyo watanzania kwa sasa. Si viongozi wa ngazi za juu serikali wala si watoto wanaoanza kutembea nao huwa wapozi mbele ya wenzao na kutembea ki-miss. Kikubwa pia ni umasikini. Kama miss anashinda gari nyumba na zawadi nyingine kama UKIMWI MIMBA (ambazo huporomoshwa bila huruma)na magonjwa mengine ya zinaa. Lakini hii yote hutokana na uvivu wetu wa kufikiri na kuwa wa bunifu. Tunapenda vya mkato vingi.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU