NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, July 31, 2009

TUTAFAKARI MANENO HAYA YA MWALIMU

Uchaguzi ndio huo unanukia. Nilifikiri kwamba si vibaya wikiendi hii tukijikumbusha maneno haya ya Mwalimu Nyerere. Ninawatakieni wikiendi njema!
========================================
"Plato, Myunani wa kale, alipendekeza kuwa mafilosofa ndio wanaofaa kuwa watawala wa nchi, maana wana sifa mbili muhimu: kwanza wana uwezo wa kutawala, na pili hawapendi kutawala. Kwa hiyo Jamhuri ya Plato itakuwa na sheria ya kuwalazimisha mafilosofa kutawala kwa zamu; na mtu zamu yake ya kutawala ikiisha, atafurahi sana kurudia shughuli zake za falsafa ambazo ndizo hasa anazozipenda. Lakini nchi zetu hazitawaliwi na mafilosofa wa Plato; watawala wetu ni wanasiasa wa kawaida ambao wanapenda sana kutawala, hata kama hawana uwezo wa kutawala; na ambao wako tayari hata kuhonga ili wachaguliwe kuwa watawala, na wakisha kuchaguliwa hawatoki bila kulazimishwa. " (Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania. Zimbabwe Publishing House, 1993: 8)

5 comments:

 1. Tukisema tulikuwa na kiona mbali, tunaambiwa tumelewa Siasa za marehemu Nyerere na ujinga wake, sawa, ujinga wake lakini werevu na uadilifu ndo sifa aliyokuwa nayo. Kwa kuwa hawamwelewi falsafa zake na misingi yake ya uongozi, na kwa kuwa walishindwa kuitekeleza kwa kuwa hawakuielewa, basi kilicho chepesi ni kwa wao kusema ulikuwa 'ujinga' hadii tutakapopata mtu mwenye akili, hekima na busara ya kuelezea huo wanaouita ni 'ujinga'. Hapa tulipo na jinsi tunavyoendeshwa sijui ndo akili na werevu? Mtu anielezee kinagaubaga ubaya wa misingi ya maendeleo ya Nyerere (sisemi kuwa yote ni mizuri) kisha alinganishe na sasa anifahamishe ipi kweli ingefanikiwa ingekuwa chimbuko letu la maendeleo enedelevu?
  Ni wivu tu umewajaa watu na umaamuma wa kupenda sifa za haraka haraka kwa kukosoa wengine.
  Asante Prof. Masangu kwa nukuu hii.
  Apumzike pema hayati J.K.Nyerere

  ReplyDelete
 2. Kwa kweli mwalimu alikuwa "kichwa". Ni kweli kabisa watawala wetu siku hizi hawatawali kwakuwa wana uwezo bali wana vigezo vingine vya kuwaweka madarakani.Mwalimu aliona mbali alipotoa maneno haya,laiti wanaogombea uongozi katika ngazi yoyote wangeongozwa nataswira hii.Asante Kaka kwa kuwasilisha

  ReplyDelete
 3. Mwalimu alikuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri kwa sababu daima alipenda kufikiri. Mtu anayefikiri kwa marefu na mapana (mwanafalsafa) daima huwa na mawazo yenye macho yaonayo mbali.

  Tatizo la wafanyasiasa wetu, hawaipendi kazi ya kufikiri kwa marefu na mapana. Hii hupelekea wafanye hovyo hovyo. Kisha wanaamini pesa ndiyo msingi wa kila kitu kwa sababu watazitumia kupata wanachokihitaji.

  Wafanyasiasa wameshindwa kuwa vile tunavyowatarajia.

  Uchaguzi unakuja. Wito wangu kwa jamii, tujizoweshe kufikiri kwa marefu na mapana. Tusihadaike na hadaa zao za vitu kama pesa na nguo ambavyo havidumu.

  Tuwe na msimamo thabiti wa kusema imetosha. Iwe dhamira ya dhati kusema hatuwachagui kwa hongo zenu mnazotoa ambao hutusaidia kwa siku mbili na kutufanya tuteseke muda mrefu. Tunawachagua kwa uimara wa sera zenu na uwezo wenu halisi wa kuongoza (siyo kutawala)

  Falsafa ya Mwalimu haikutaka tuchague viongozi kwa vijisenti vyao. Wakati ni huu. Hakuna wakati mwingine. Ni lazima wapiga kura tubadilike.

  Jumapili njema kwenu nyote.

  ReplyDelete
 4. nyerere pamoja na kwamba alikuwa chini ya ukatoliki wa kileo lakini alijitambua kwa kiasi kikubwa na nimegundua kumbe alikuwa anatahajudi sana (meditate)na hiyo ikamsaidia kujigundua yeye mkubwa (his higher self/God knowledge) na kkuona ukweli mpana. akajua kuwa ataishi muda mfupi na hivyo akaishi ili asife.

  meditation ni dili sana hebu jaribu kumeditate kila siku uone mabadiliko. utaijua kweli nayo itakuweka huru. huyo ndiye mwalimu nimjuaye

  ReplyDelete
 5. Dada Subi, japokuwa Mwalimu Nyerere alikuwa binadamu kama sisi na alitenda makosa (mf. tabia yake ya kutovumilia mawazo-kinzani) lakini alikuwa ni kiongozi anayeona mbali sana kama Nick alivyobainisha. Hawa viongozi wa sasa ni nani kati yao ambaye hata anaweza kumfikia japo robo tu ya uwezo na uadilifu wake?

  Fadhili, tatizo la wapiga kura kuhongwa ni umasikini unaowakabili na ukosefu wa mwamko wa kisiasa. Mwamko hata hivyo umeanza na naamini kwamba muda si mrefu wapiga kura watakubali kupokea vitenge, mabati, baisikeli na cherehani wanazohongwa na wakiingia katika kibanda cha kupigia kura watachagua mtu yule wanayemwona kuwa ni kiongozi makini atakayewasaidia na kuwaletea maendeleo, na si yule aliyewahonga. Polepole tu mambo yatabadilika.

  Kamala, sikujua kama Mwalimu alikuwa anafanya meditation. Sishangai kwani ni wazi alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kufikiri, na tunaambiwa na wataalamu kwamba kuweza kufikiri vizuri mtu unahitaji akili iliyotulia; na meditation inatajwa sana kama njia bora ya kutuliza akili na ku-fokasi fikra.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU