NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, August 31, 2009

KWA NINI NI LAZIMA TUULIZE "KWA NINI?" - FUNZO KUTOKA KWA SIR ISAAC NEWTONBado unazikumbuka Newton's Laws of Motion? Inasemekana chimbuko lake ni utundu wa Sir Isaac Newton wa kuuliza "kwa nini?" Inasimuliwa kwamba siku moja alikuwa amejipumzisha karibu na bustani alipoona tunda likidondoka kutoka mtini. Jambo hili lilimtatanisha na alianza kujiuliza: kwa nini tunda limedondoka chini badala ya kwenda juu au wimawima na kuangukia sehemu nyingine? Kwa nini chini?

Inasemekana pia kwamba leo hii mambo mengi yanakwenda mbagombago kwa sababu badala ya kuuliza "kwa nini?" tumebadilika na kuwa watu wa "ndiyo". Hata mfumo wetu wa elimu kwa kiasi kikubwa hauwapi nafasi ya kuuliza "kwa nini" akina Isaac Newton wetu. Matokeo yake vyuo vyetu vimegeuka kuwa viwanda vya kufyatua watu wasiohoji mambo - mabingwa wa kukariri na kusema "ndiyo" tena kwa HERUFI KUBWA ZENYE MSISITIZO uliojaa mwangwi wenye ombwe.

Matokeo ya jumla ya mtindo huu tindifu ni jamii ya kikondoo, jamii isiyosaili mambo, jamii isiyouliza "kwa nini?", jamii ambayo (kama kondoo) iko tayari kuifuata sauti tamu ya mchungaji laghai kuelekea machinjioni. Lini tutaanza kuwauliza "wachungaji" wetu "kwa nini?". Kwa nini hawajatufikisha kwenye nchi ya ahadi waliyotuahidi, nchi inayotiririka maziwa na asali? Kwa nini bado tunazunguka jangwani - bila maji, bila malisho, bila kivuli, bila matumaini? Kwa nini inaonekana kama vile wanakotupeleka ndiko siko? Kwa nini?

1 comment:

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU