NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, August 26, 2009

HATA WEWE NI "CELEBRITY" TENA WA KWELI JAPO HUJUI

Binadamu sie, kwa vile hatujui tunachokijua kuhusu tukijuacho kwamba kinaweza kutupa furaha na ridhiko katika maisha yetu, watu wengi huvutiwa na watu wanaoitwa "ma-celebrity". Ndiyo maana udaku juu ya maisha ya watu hawa ni biashara ya mabilioni ya dola kila mwaka. Tunataka kujua "ma-celebrity" wetu jana walikula nini, walivaa nini, walikwenda wapi, walikuwa na nani, walionekanaje na kwa nini.

 • Tunafikiri kwamba maisha yao ya "u-celebrity" yameremetayo daima pengine ndiyo yanaakisi kiwango halisia cha mafanikio, ridhiko na furaha ya kweli ambayo tunaweza kuipata katika maisha yetu. Ndiyo maana tunashangaa sana tunaposikia kwamba wengi wa "ma-celebrity" hawa hawana furaha na ridhiko katika maisha yao na wengi wanaishi maisha ya ukaburi - kwa nje wanaonekana wamepambika na kumeremeta ajabu lakini kwa ndani wamejaa mafunza na uozo wa upweke, kutoridhika, madawa, ulevi na shida.
 • Orodha ya ma-celebrity waliojihitimishia maisha yao na kutuachia maswali lukuki juu ya maisha-mng'aro waliyoishi ni ndefu. Imethibitishwa, kwa mfano, kwamba Michael Jackson, pamoja na kumeremeta kwake kule, aliyahitimisha maisha yake katika lindi la madawa makali, upweke wa ajabu na maisha ya kukata tamaa (soma hapa).
 • Kwa vile hatujui tunachokijua kuhusu tukijuacho kwamba kinaweza kutupa furaha na ridhiko katika maisha yetu, "u-celebrity" wa kweli kwangu mimi ni kuwa na familia yenye furaha, familia inayopendana na kujaliana (kama hiyo katika picha)
 • Ninapotoka kazini nikiwa nimechoka na kuvikuta vibinti vyangu virembo vimalaika vya Mungu vikinisubiri kwa hamu tucheze, tukimbizane, tufanye "homework" pamoja, tusimuliane hadithi (zikiwemo za Kisukuma), tule ugali na kusali pamoja - kwangu mimi huu ndio "u-celebrity" wa kweli, "u-celebrity" unaozidi hata ule wa kuandamwa na mapaparazi barabarani wakiwa wamesheheni vimwekamweka. Huu ndio "u-celebrity" unipao ridhiko la kweli na furaha nono mno katika moyo wangu.
 • Naamini kwamba hata wewe ni "celebrity" wa kweli hapo nyumbani kwako japo hujui! Na kama bado hujawa, basi nakuomba sana uwe. Haigharimu cho chote!

8 comments:

 1. Nimeipenda hiyo picha kuliko chochote kile halafu ndo nikasoma maelezo, nimekubali kuwa kila mtu ana u-celebrity wake.
  Kaka Matondo kumbuka ucelebrity wako ulipoanza tangu unaumba herufi na kuunda mwandiko mzuri darasani? Kumbuka ile homework yako ya Fizikia uliyokuwa kinara hadi mtu akaihifadhi kisha akakutumia siku za hivi karibuni baada ya miaka kadhaa? Ni u-celebrity huo kakangu la sivyo wangeitupilia mbali!
  Mweh, hongera sana celebrity!

  ReplyDelete
 2. Wote Pro. Mtando na da Subi mko sawa kabisa nimependa jinsi ulivyoandika u-celebrity wako. Binafsi u-celebrity wangu ni kuwa na kuamka kila asubuhi na na kujua ni mzima wa afya pia kuwa na familia yangu ambayo inanijali na kunipenda mimi kama mimi. Kwa kweli huwa nawaonea sana huruma hao ma-celebrity wanaosakwa kama mbuzi.

  ReplyDelete
 3. Kaka yangu hapo! umenena, hakika kila mtu ni celebrity,tena wetu sisi tuna u-enjoy kulikoni hao wanaozungukwa na ma camera kila dakika.nice picture,nice couple and little angel, very cute. Wasalimie sana wifi na shangazi zangu wote!!

  ReplyDelete
 4. mke wangu anajivunia kuwa na mtu kama mimi wakati mimi pia najivunia kuwa naye.

  hata hivyo ukamilifu wetu, furaha ya kweli na ridhiko vimo ndani mwetu na sio nje yetu! kuna wakati tunakuwa hatuwezi kuwa na hiyo familia. tukisafiri na kwenda ndani mwetu zaidi ndiko mambo iliko

  ReplyDelete
 5. Ndugu Matondo ninakubaliana na hayo unayosema kabisa. Duh yaani mke wako kiboko ndungu yangu. Umebarikiwa na mie ngoja nichepuke kutafuta wangu.
  Poa!

  ReplyDelete
 6. U-celebrity kwangu mimi ni jinsi mke wangu na watoto wanavyonichulia,mathalan kama mke anani-consider kama mume bora na watoto wananichulia kama baba bora mwenye kujua majukumu yake basi nafaa kuitwa celebrity!

  ReplyDelete
 7. Dada Subi. Asante sana kwa maneno yako mazuri. Kumbe uliiona ile homework yangu ya Fizikia? We acha tu. Dada Yasinta - nimeupenda "ucelebrity" wako. Dadangu mwanamitindo (Passion4fasion) salamu zako zimeshafika nawe unasalimiwa sana. Kamala, nimezisikia busara zako za kiutambuzi. Kessy nadhani wewe mchokozi. Anyway, ukimpata tujulishe. Bwana Kaghembe - hicho hasa ndicho nilichokuwa nakiongelea. Kuwa na familia inayopendana kunaleta ridhiko zuri mno moyoni kuliko hata hii kasheshe wanayohangaika nayo hawa "macelebrity wetu" Nyote asanteni. Twendeni sasa tukaendeleze "ucelebrity" wetu!

  ReplyDelete
 8. Mzee nimekubali kuwa kila mtu ana nafasi yake na family yake.U-celebrity ni kupata ugali na maziwa na family yote wakifurahia na kuwa na raha japokuwa sisi kama binadamu tunataka kuwa na vitu vingi lakini wakati wetu unakuwa bado haujafika.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU