NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Sunday, August 30, 2009

MATUMIZI YA KISUKUMA KATIKA NYIMBO ZA MTOTO WA DANDU (COOL JAMES)

Ulimwengu unakumbuka miaka saba (na siku tatu) tangu James Maligisa Dandu a.k.a Mtoto wa Dandu a.k.a Cool James a.k.a Ng'wanamalia a.k.a CJ Massive a.k.a Ng'wanawapelana a.k.a Nzokaihenge aage dunia kwa ajali ya gari tarehe 27/8/2002 (tazama hapa). Sikupata bahati ya kumwona lakini yeye pamoja na Saida Kalori na Mr Ebbo pengine ndiyo waimbaji wa kizazi kipya ambao kwa kiasi kikubwa wameweza kuzitukuza lugha zao za mama katika nyimbo zao - na hivyo kutupilia mbali ile dhana kwamba kizazi cha dot.com hakiwezi kuguswa na nyimbo zenye ladha ya kikabila. Mtoto wa Dandu japo hakuimba katika Kisukuma moja kwa moja, hapa na pale hakuisahau lugha yake ya mama iliyomkuza na kumlea kule Mwanza (Kisukuma). Hapa ni baadhi ya mifano tu ya matumizi ya Kisukuma katika nyimbo za mwanamuziki huyu mashuhuri aliyeondoka akiwa bado mchanga.

Jina lake mara nyingi alipenda kujiita Nzokaihenge yaani nyoka mwenye makengeza (nyoka makengeza). Alikuwa akijiita pia Ng'wanawapelana yaani Mtoto mwenye hasira. Alipenda pia kujiita Ng'wanamalia - mtoto wa Maria. Hii inaonyesha kwamba pengine jina la mama yake ni Maria (Wasukuma hawana sauti " r" na hivyo mara nyingi huitamka kama "l" - kinyume na Wakurya)

Korasi mashuhuri inayosikika katika nyimbo zake nyingi inasema hivi:

Ng'wanamalia
Kolobelaga lukumo lwane.
Jaga Ng'wigulya.
Jaga Ubagisha shikamoo abakolobela ng'weli...

Tafsiri

Mtoto wa Maria
Umashuhuri wangu acha uenee sehemu zote
Uende juu zaidi
Uende ukiwasalimia shikamoo waliokwishasonga mbele

Kwingineko mara kwa mara anasikika akisema:

Nabiza wa galama.
Nulunagaja gubugeni nadiko gwigashiji gogo mpagi sumbi lya nghana

Nimeshakuwa mtu wa thamani (heshima)
Hata nikienda ugenini siwezi kukalia gogo
Inabidi nipewe kiti kizuri cha kukalia

Inavyoonekana pia alikuwa ni mtu wa kutoa shukrani. Katika baadhi ya nyimbo zake anaonekana akimsifia na kumshukuru Jumanne Kishimba - tajiri mkubwa kule Mwanza na mmiliki wa duka kubwa la Imalaseko Supamaketi jijini Dar es salaam. Anasema hivi:

Jumanne Kishimba
Mlinamoyo gwape giti buluba

Tafsiri

Jumanne Kishimba
Mna roho nyeupe mithili ya pamba

Huu ni mfano wa kuigwa. Hebu fikiria kama wanamuziki wengi wa kizazi kipya wangeiga mfano wa Saida Karoli, Mr Ebbo na Mtoto wa Dandu, wakaimba nyimbo katika lugha zao za mama (Saida Karoli - Kihaya) au kuingiza vipengele vya lugha zao za mama katika nyimbo zao kama Mtoto wa Dandu (Kisukuma) na Mr Ebbo (Kimasai). Hatua hii ingesaidia sana kukikumbusha kizazi hiki cha dot com kwamba lugha zao za mama zipo, zina hadhi kama lugha nyingine yo yote na zina manufaa ya kimatumizi hata katika ulimwengu huu wa kisasa. Kwa hivyo dhana ya kwamba lugha hizi ni za kizamani, zimeshapitwa na wakati na hakuna sababu ya kujifunza au kuzizungumza tena haina ukweli wo wote. Ingefurahisha kama nini kama wanamuziki hawa wangetimiza wajibu huu wa kitamaduni na kuziunga mkono lugha zetu za asili katika wakati huu zinapopita katika mikikimikiki ya kudharauliwa na kuonwa kwamba hazifai tena.

Mungu aendelee kumpumzisha salama Mtoto wa Dandu/Cool James/Ng'wanamalia/Ng'wanawapelana/Nzokaihenge/CJ Massive.

Muziki wake kwa hakika utadumu!

Nyimbo zake mbili hizi hapa:

(1) MPENZI


(2) SINA MAKOSA

4 comments:

 1. nyimbo zake nazikubali pia kwa kiasi japo sikumjua kwa karibu wala nini

  ReplyDelete
 2. Du! haya maneno yake ya huu wimbo wa pili hapo chini utazani alikuwa anajua,nini kitamtokea muda sio mrefu,nilikuwa simfahamu lakini alikuwa na kipaji,hakika maisha ni kama ua.

  RIP Ng'wana wa DANDU.

  ReplyDelete
 3. Kamala, una nyimbo mpya za Saida Karoli unitumie? Nazipenda sana nyimbo zake. Hali kadhalika Mr Ebbo. Napenda sana wanapoimba/wanapoingiza ladha za kikabila katika nyimbo zao watu hawa.

  Wakati mwingine binadamu wengine huweza kuhisi nini kinakuja, na ni kweli ni kama vile alijua. Apumzike kwa amani.

  ReplyDelete
 4. sina nyimbo mpya sidhani kama saida anaimba tena kihaya. labda zipo kwani mimi sio mpenzzi saana wa miziki

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU