NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, August 19, 2009

MWALIMU NYERERE ALIPOUNGURUMA CHIMWAGA (1995) NA KUTUPATIA BENJAMIN MKAPA. ALIKUWA SAHIHI?

Ni katika hotuba hii ambayo Mwalimu aliitoa kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM waliokuwa wamekutana katika ukumbi wa Chimwaga kule Dodoma mwaka 1995 kuchagua mgombea wa urais ambapo kimsingi alianza na hatimaye alifanikiwa kumtengenezea Mheshimiwa Benjamin Mkapa njia ya kuwa rais. Mwalimu alitaja sifa nne kuu za kiongozi aliyekuwa akimtaka: (1) Kiongozi ambaye angeweza kupambana na rushwa (2) Aliyekuwa anafahamu kwamba nchi ya Tanzania bado ni nchi ya wakulima na wafanyakazi ambao bado ni masikini, kiongozi ambaye angepambana na (3) Udini pamoja na (4) Ukabila (Sikiliza sifa hizi kuanzia dakika ya 9:06). Mwalimu aliamini kwamba kiongozi mwenye sifa hizi kamwe asingeweza kutoka nje ya CCM, ambamo pia aliamini kwamba kulikuwa na kansa ya uongozi mbovu. Tazama baadhi ya kauli zake hapa.

Baada ya kuisikiliza tena hotuba yake hii (ambayo nimeitoa kwa Dada Subi a.k.a Nukta 77) naamini kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa na nia njema kutuchagulia Mkapa; na aliamini kabisa kwamba Mkapa ndiye alikuwa kiongozi safi kati ya wagombea wote wa urais wa wakati ule. Kutokana na tunayojua (au tunayofikiri tunajua) sasa kuhusu baadhi ya wagombea wale, Mwalimu alikuwa sahihi kutuchagulia Mkapa? Mimi nadhani kwamba Mwalimu alikuwa sahihi kwani sioni mgombea mwingine wa wakati ule ambaye "angejaribu" kama alivyojaribu Mkapa.

9 comments:

 1. ndio alikuwa sahihi kwa mawazo yake na kwa fikra zake. mimi naona alikuwa sahihi kabisa.

  hiyo ndiyo hatari ya kumwona mtu kama Mungu mtu au mesiah pekee na kwamba akisema yeye basi au biila yeye kusema hakuna maendeleo au hakuna awezaye kusema akasikika.

  ujinga huo umetufunga badala ya kutafuta na kuchagua viongozi bora tunaendelea kumlilia mesiah nyerere 'kama sio juhud zao....' yaani itafika h atua watu wataaanzisha dini yake 'nyererians' au vip huku nchi ikitafunwa na michwa.

  mimi ni kati ya watu wachache tusioamini saana katika mazuri aliyoyafanya nyerere.

  mkapa alifanya alichotumwa kufanya.

  ReplyDelete
 2. Kamala, unajua kwa nini Nyerere anapendwa sana na Watanzania? Anapendwa si kwa sababu eti alikuwa mtakatifu au hakufanya makosa (ingawa nasikia Wakatoliki wanataka kumfanya Mtakatifu). Sote tunafahamu ile tabia yake ya "kidikteta" na kutovumilia mawazo kinzani. Ungempinga kidogo tu basi ungeitwa haini na vijana wake wa Usalama wa Taifa wangekula nawe sahani moja. Ndiyo maana tukawa na "Zidumu Fikra sahihi za Mwenyekiti" Unakumbuka enzi hizo? Pengine ulikuwa bado mdogo au hujazaliwa kabisa. Nyerere alikuwa "mungu!" Tunajua pia kwamba baadhi ya siasa zake zilikuwa ni za kiutopia mno na pengine zilikuwa hazitekelezeki.

  Pamoja na matatizo yake haya, Watanzania naamini wanavutiwa na ule ukweli kwamba sasa wakiangalia nyuma na kutafakati wanagundua kwamba karibu kila kitu alichofanya au alichojaribu kukifanya, kilichofanikiwa na kilichoshindwa, kilikuwa ni kwa maslahi ya Watanzania na siyo yake pekee na familia yake au na kikundi kidogo cha watu katika jamii. Hakuwa na zile siasa za kinafiki za "tendeni niwaambiavyo lakini kamwe msitende nitendavyo" Siyo kiongozi anakuwa na sera ya kupambana na rushwa halafu mwenyewe huyo huyo anaendelea kujilimbikizia mali kama tunavyoona kwa baadhi ya viongozi waliomfuata. Leo watu wakiangalia maisha aliyokuwa akiishi, na familia yake inavyoishi, wakilinganisha na viongozi wa sasa, wanamwona kama mtu aliyeweka maslahi yao mbele. Juhudi zake za kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu, juhudi zake za kupunguza tofauti za kitabaka kati ya matajiri na masikini, juhudi zake za kuhakikisha kwamba ukabila na udini vinathibitiwa, juhudi zake zilizoshindwa za kupambana na rushwa na mengineyo ni mambo ambayo watu wengi wanavutiwa nayo sana.

  Uchaguzi huo unakuja na Nyerere sasa hayupo, na tunayo nafasi nzuri sana ya kuchagua kiongozi bora anayetufaa. Ngoja tuone.

  ReplyDelete
 3. ndio mzee lakini sijui umuhimu wa elimu yake uliozuia watu kuwa na maoni na mitizamo huru uko wapi. ndio maana nasema alikuwa na mapungufu japo alionekana mwema. alihakikisha yeye anakuwa juu siku zote na ndiyo maana alipoondoka CCM wanaparaganyika na wanabakia kuwa kama kondoo wasio na mchunga kwa sababu wana CCM wenye mawazo mazuri labda kuliko ya kwake Nyerere alihakikisha anawapoteleza mbali kuleee.

  sasa alijenga chama kwa ubora na uzuri gani kwamba baada ya yeye kuondoka hakuna kiongozi wa maana anayesikirizwa au mwenye msimamo.

  aliyoyafanya yanageuka kuwa kazi bure na sasa tanzania inabaikia kuwa na watu waoga wasiojua ksema na waliobakia kuutukuza mzimu ule

  ReplyDelete
 4. Pengine ili kumwelewa Nyerere vizuri inabidi tusisahau muktadha (context) ambamo alitawala. Yeye ni mmmoja wa viongozi wa kwanza baada tu ya kupata uhuru kutoka kwa wakoloni. Viongozi hawa hawakujua nchi hizi zingeelekea wapi na naamini kwamba waliitumia nafasi hii ya upya wa nchi hizi huru kudhibiti mambo yalivyokwenda. Hakuna hata kiongozi mmoja wa kipindi hiki ambaye aliruhusu vyama vingi na karibu wote walikuwa na chembe za udikteta - walilolisema ndilo lililotendeka. Hata ukimwangalia Nyerere katika muktadha huu na kumlinganisha na wenzake waliotawala kipindi hiki bado utaona kwamba pamoja na "udikteta" wake (ambao tunaweza kumtetea kwamba pengine kulingana na mazingira ya wakati ule ulikuwa ni wa lazima ili kusimika falsafa na mwelekeo wa taifa), bado ni kiongozi ambaye aliweka maslahi ya nchi yake mbele. Aliipondelea mbali siasa ya divide and rule na kuamua kupambana na ukabila pamoja na udini (ingawa waisilamu wanaamini kwamba alipendelea wakristo wakati wa utawala wake), na matunda yake tunayaona mpaka leo ingawa mambo yanabadilika kwa kasi.

  Kuhusu elimu, mimi sijali kama elimu hiyo ilikuwa na malengo gani lakini ukweli tu kwamba kila mtoto wa Kitanzania aliweza kwenda shule kutoka darasa la kwanza mpaka chuo kikuu bila kujali tabaka la wazazi wake, ni uthibitisho tosha kwamba alikuwa na nia njema. Na kuhusiana na wanaCCM sasa kuwa na ombwe la uongozi sidhani kama ni kosa la Nyerere. Hawa ni watu wasomi ambao wana mawazo huru na wanaweza kuja na falsafa zao wanazoziona kama zina faida kwa taifa. Mbona wameweza kuja na dhana mpya nyingi tu (mf. takrima) ambazo zinapingana na Nyerere wao wanayemwabudu? Sidhani kama ni sawa kumsingizia Nyerere kwamba ndiyo amewadumaza kifikra ingawa kusema kweli inashangaza kidogo kuona kwamba mpaka leo eti falsafa ya kiitikadi ya Tanzania bado ni Ujamaa na Kujitegemea! Sijui wanaogopa nini kusema kwamba siasa ya Ujamaa na Kujitegemea imeshakufa na mambo ya binadamu wote ni sawa hayatekelezi - wakaja na itikadi nyingine itakayotoa msukuma mpya wa kimaendeleo. Kama ulivyosema pengine wanaogelea katika dimbwi la itikadi ya Nyerere ingawa dimbwi hilo halina maji bali matope. Hata kama hivi ndivyo, hili ni kosa la Nyerere?

  ReplyDelete
 5. Naomba tuwekee video nyingine za mwalimu nimefurahi sana kumsikia .

  Tukumbuke wakati tanzania inapata uhuru tulikuwa na gradutes hata kumi hawafiki, how can you run a country na huna watu wa kufanya kazi? ilibidi awe hivyo ili mambo yaende otherwise tungesha shikiana mapanga hapa. sasa tunawasomi kidogo , tufanye kazi Tanzania ni moja ya nchi ambayo inautulivu africa ....kila mtu anataka kuwekeza hapa watu inabidi waajibike instead of pointing fingers do something usisubiri mpaka kiongozi akufanyie tujitume na mambo yatakwenda tuu.

  ReplyDelete
 6. matondo, hao ndio wasomi aliowazarisha mwalimu na hapo ndipo lilipokuwa tatizo la elimu yake aliyiotupatia ya kufyatua mashine za uzalishaji na sio watu wanaofikiri na kusimamia mawazo yao!

  udini, ukabila, nk, ilibidi Nyerere atulete pamoja ili aweze kututawala. viongozi wa Mwanzo wa afrika karibia wote (ispokuwa Nkurumah na wengine wachache) walikuwa hovyo ndio maana akina Nyerere wakapinga Muungano wa Afrika huru kwa kuogopa kupoteza nafasi zao wakaunda li-OAU lisilo na meno!!! interesting ehe??

  ReplyDelete
 7. Kamala. Mimi nadhani tatizo siyo elimu ya Nyerere. Tatizo ni Unyerere kama mkondo wa mawazo na falsafa. Popote kunapokuwa na kiongozi ambaye mawazo na itikadi yake inavuka kiwango na kuwa mkondo (movement) basi ni kawaida watu kufumwa mumo kwa mumo katika mkondo huo na kuishia kuabudu mawazo hayo kwa muda mrefu - bila kujali kama ni sahihi ama la. Umao kule Uchina, Ucastro kule Cuba na kwingineko ni mifano mizuri. Kwa vile mawazo na itikadi hizi za kimkondo huwa zimejikita sawasawa katika akili za watu, viongozi wapya huogopa kujitenga nazo wakichelea kutibua mambo na kukosa kuchaguliwa tena. Ndiyo maana kumekuwa na kigugumizi kwa viongozi wa CCM kuamka na kusema kwamba wanaachana rasmi na siasa za Ujamaa na Kujitegemea. Wakati hata hivyo haushindwi na baada ya muda mawazo haya abudiwa mwishowe huanza kufifia na viongozi wapya huja na nadharia na falsafa zao mpya. Nyerere alikua zaidi na kuwa Unyerere na viongozi bado wamefumwa katika mkondo huo wa falsafa zake. Japo elimu ilikuwa nyenzo mojawapo ya kusambazia falsafa zake sidhani kama unaweza kulidogosha lengo zima la elimu ya wakati ule kuwa lilikuwa ni kuNyereresha watu. Elimu kamwe haiwezi kubanwa katika kona nyembamba namna hiyo. Tuwape muda viongozi wetu na polepole watatoka katika Unyerere na tutakuwa na itikadi mpya itakayoongoza taifa.

  Kuhusu suala la Afrika kuungana, kwa wakati ule mara tu baada ya uhuru sidhani kama ingewezekana. Nchi hizi ndiyo tu kwanza zilikuwa zimepata uhuru na huu ulikuwa ni wakati wa vita baridi. Hiyo serikali ya Afrika ingefuata itikadi gani ukitilia maanani kwamba viongozi wenyewe walikuwa wamegawanyika - wasoshalisti (Nyerere, Obotte, Kaunda na wengineo) na mabepari (Kenyatta na wenzake). Wakubwa wa Kimagharibi (waliomuua Patrick Lumumba, Samora Machel na kumwondoa madarakani Kwame Nkrumah) wasingekubali maslahi yao yapotee kwa kuwa na serikali moja ya Afrika. Japo lilikuwa ni wazo zuri sana mimi nadhani utekelezaji wake usingewezekana hasa katika kipindi kile cha Afrika changa.

  Historia pia imeonyesha kwamba miungano ya aina hii (ukiachilia mbali Marekani) haijafanya vyema sana, na mara nyingi imeishia kuparaganyika. Watazame Warusi - na hata sisi wenyewe jinsi Muungano wetu wa nchi mbili tu unavyokwenda kwa mwendo wa kusuasua. Afrika - ukizingatia historia yake ya kutawaliwa na mataifa tofauti ya Ulaya yenye maslahi tofauti tofauti, wingi wa makabila na hivyo tofauti za kitamaduni, tofauti za utajiri wa kiraslimali na mengineyo - kuwa na serikali moja imara ya Afrika nakwambia ingekuwa ngoma nzito. Ulaya kwenyewe pamoja na historia yao kuwa moja bado EU yao inakumbwa na misukosuko hii. Kuna wanaodhani kwamba watamezwa n.k. pamoja na kwamba kila nchi ina mamlaka yake kamili.

  OAU ilipaswa kuwa mwanzo wa hatua hii ya Muungano lakini kama nilivyotaja hapo juu - wakubwa wa Kimagharibi wasingeruhusu muungano wo wote wa maana. Ndiyo maana OAU ikawa haina meno - sawa na Umoja wa Mataifa tulionao!

  ReplyDelete
 8. Love love Mwalimu regardless to his selfshiness and power controll freak!!! But he never steal like.....!!!!

  ReplyDelete
 9. Mabishano kati ya msomi na mjinga mmoja (Kamala). Hata kusoma hajui, kuandika ndio kabisa. Masangu unajaribu kumfumbua macho huyu mbumbumbu ambaye sijui hata anachokilalamikia kwa Nyerere. Unategemea anaweza kuchekecha akili na kuyapima uyaongeayo?

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU