NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, August 12, 2009

NIMETUMIWA HOMEWORK YANGU YA PHYSICS YA KIDATO CHA NNE (KAHORORO SEC, MWAKA 1988)

Mdau Ephraim amenitumia homework yangu ya Fizikia niliyofanya nikiwa kidato cha nne katika shule ya Sekondari ya Kahororo. Yeye alisoma Kahororo baadaye kidogo na aliikuta homework hiyo ikiwa bado ingaliko. Mwalimu wangu wa Fizikia - Christian Agricola - alikuwa anapenda sana mwandiko wangu kiasi kwamba alikuwa ananipa madaftari ya bure mara kwa mara kama zawadi ingawa uwezo wangu katika somo hilo ulikuwa ni wa hivi hivi tu!

Kama unavyoweza kudhani, homework hii imenikumbusha mambo mengi sana, kwani baadhi ya misimamo yangu kuhusu maisha ilifinyangwa katika kipindi hiki - uvumilivu, kutokata tamaa, kufanya kazi kwa bidii, kusamehe, kujizuia na mengineyo.

Ijapokuwa nilikuwa napenda masomo ya sayansi (hasa Bayolojia kiasi cha kushika namba moja katika mtihani wa Mock mkoa wa Kagera), kusema kweli nilikuwa sipendi kukariri tu vitu nisivyovijua katika Fizikia na Kemia. Na japo mpaka leo ninaweza kukutajia Newton's Laws of Motion, elementi 21 za mwanzo katika Jedwali Radidi la Elementi (Periodic Table of the Elements) na mengineyo, mambo mengi kwangu yalikuwa kama usiku wa giza na tulikariri tu kwa lengo la kufaulu mitihani. Ndiyo maana ulipofika wakati wa kuchagua "combination" nilimwasi mwalimu wangu wa Bayolojia (Mwl. Kabyemela) aliyenisisitiza sana kuchagua PCB (Physics, Chemistry na Biology) kama combination yangu ya kwanza. Alipoondoka nilirudi kwa mwalimu wa taaluma na kujaza fomu zile upya safari hii nikichagua HGK (History, Geography na Kiswahili) kama chaguo langu la kwanza. Nilitaka kusoma vitu ambavyo nilikuwa navifahamu - vitu ambavyo sikuhitaji kujifunza kipurure (rote learning) na Historia, Jiografia na Kiswahili yalikuwa ni masomo ambayo yalinipatia nafasi hiyo, kwanza Sengerema High School na baadaye Mlimani.

Mpaka leo siujutii uamuzi huu ambao niliufanya wakati ule nikiwa bado kijana mdogo ninayejitafuta mimi mwenyewe na nafasi yangu hapa duniani. Maisha yetu ni mafupi sana hapa duniani na hakuna jambo la muhimu kama kufanya kile ukipendacho na ambacho kinakupa ridhiko moyoni mwako ali mradi hakiwadhuru wengine na wewe mwenyewe.

Katika jitihada zangu za kuipa "uhai" sayansi machoni mwa vijana wetu, nimeamua kuanzisha mfululizo uitwao "Wajue Vingunge wa Sayansi". Hizi zitakuwa ni makala zilizoandikwa kwa lugha ya kawaida na mimi mwenyewe katika blogu hii juu ya maisha ya wanasayansi mashuhuri na mchango wao katika sayansi. Makala hizo zitakuwa zinatoka hapa kila siku ya Jumatatu. Lengo langu la baadaye ni kuzikusanya makala hizi, kuzihariri na kisha kuzichapicha kama kitabu - kitabu ambacho naamini kitawasaidia vijana wetu kuwasona mabingwa wa sayansi wanaowasoma mashuleni (akina Pythagoras, Archimedes, Isack Newton, Ivan Pavlov, Ohm, Faraday, Hertz, Galileo Galilei na wengineo) na kuwaona kama watu wa kawaida tu ambao, pamoja na kuwa na vipaji, mafanikio yao hasa yalitokana na kufanya kazi kwa bidii na kutokata tamaa. Nitafurahi sana mkiniunga mkono kwa kuwafikishia habari vijana wetu walioko mashuleni kule nyumbani!

9 comments:

 1. Nimeuona mwandiko baba. Bado unaandika hivyo hata leo au kompyuta zimeshakuharibu. Watoto siku hizi hawawezi kuandika kwani kila kitu ni email, kompyuta na text messaging. Kukaa down na kutype hawawezi tena.

  ReplyDelete
 2. interesting mzeee. sikupenda phyisics wala Chemistry nilipokuwa shule kwani kwanza mwalimu wa physics alikuwa mchapaji viboko hatari na matusi na maneno ya kejeli mpaka nikalichukia somo hilo. alikuwa pia mvuta sigara na mimi nilichukia moshi wa sigra na kwa kuwa alikaa kwenye maabara ya physics kama ofisi yake, niliichukia hata Chemistry kwani maabara zilikuwa jengo moja na Moshi wa sigara haukufutika. nikayachukia masomo hayo.

  niliipenda biology (hasa reproduction) japo nilipata F katika mtihani wa mwisho. hiyo ni miaka karibia kumi tu iliyopita pale Tweyambe Secondary

  ReplyDelete
 3. Umenikumbusha wakati tuko Mlimani nawe!!Daftari lako na la Kakoko ndo yalikuwa yakitafutwa sana na sie tuliokuwa tukisoma masomo kujifunza kipurure (Physics and Maths(Computing))ili tupige copy kama unakumbuka walimu wetu PWD(Borer),PAK(CONSCIETIZER),JOYCE,KALAFUNJA OSAKI(FUKUFUKU),MARY WANGAI(MBOYA),SIXTUS,HERME MOSHA.......

  ReplyDelete
 4. Lakini mzee naona ulifanya kosa kutokuichagua sayansi. it seems it is still blinking in your head indicating that you went in the wrong direction.

  ReplyDelete
 5. Anony. wa mwisho. Kwa nini unasema hivyo? Hapana, naamini kabisa kabisa kwamba sikufanya kosa kutokuichagua sayansi. Au wewe ni mmoja kati ya wale wanaoamini kwamba sayansi ni bora kuliko masomo ya sanaa? Sikwenda kwenye wrong direction na naamini kwamba kama ningechagua sayansi pengine nisingefika hapa nilipofikia. Nimebarikiwa mno na sina aina yo yote ya majuto!!! Maisha ni nini kama siyo kufanya kile ukipendacho?

  ReplyDelete
 6. Nimesoma hapa huku nikijikuta nikitikisa kichwa kwa mwendo wa pole kwenda mbele na nyuma. Huu ni mfano mzuri wa namna ambavyo mtu anaweza kuwa determined na akasimamia anachokitaka maishani na akakipata. Ni mfano wa mtu ambaye haangukii kwenye taaluma fulani kwa sababu tu ‘mazingira’ yamemlazimisha kuwa asivyotaka.
  Wanafunzi wengi wanaharibikiwa kwa sababu ya kukosa ulichokuwa nacho Profesa Matondo.
  Wanasoma wasichokipenda. Wanatamani wasichokiweza.
  Angalia. Watu wengi wanadhani kusoma masomo ya sayansi ndiyo kuwa na akili na eti wanaosoma masomo ya sanaa ni vilaza. Na hii haiishii hapo. Kuna wanaodhani wale wanaosoma fani za uanasheria na udaktari ndio vipanga kuliko wengine. Wengine wanadhani dili ni kusoma masomo ya kushika shika hela. Jambo hili lina mizizi yake katika kutokujifahamu.
  Tunaishi maisha ya wengine. Tunaishi maisha yanayoongozwa kuanzia nje, na si ndani. Tunaishi maisha yasiyo yetu, tukitafuta kuwapendeza/kujipatia sifa za bure kuanzia nje. Hili ni kosa. Na kwa kweli tusipoharibu utaratibu huu na kujenga upya, hatutaweza kupata maendeleo ya maana kama nchi.
  Ni wanafunzi wangapi wanasoma HGL kwa sababu tu sayansi imegomba? Ni wanafunzi wangapi wanasoma sayansi si kwa sababu ndicho wanachokitaka kuanzia ndani, bali kukidhi matakwa ya wengine (ulevi wa sifa)? Ni wanafunzi wangapi wanapoteza miaka mingi kusoma kitu ambacho hawakipendi, na wanajua kabisa sicho watakachokifanya maishani mwao? Wangapi wanabadili badili fani kwa kila kiwango cha elimu kwa sababu tu hawana hakika na walichokisoma awali?
  Nadhani sababu ni kwamba shule zetu zina walimu wasiowasaidia wanafunzi kujua wanataka nini na kwa nini. (wao wenyewe hawajijui, wako frustrated na hawajuji wanafanya nini kwenye ualimu, sembuse kumsaidia mwanafunzi). Sababu ni kwamba mitaala yetu inakosa somo la kumfundisha mwanafunzi maarifa ya kujitambua yeye binafsi.
  Kwa hiyo utakuta mwanafunzi anaweza lugha vizuri, anaamua kuchepukia kwenye PCM kwa sababu tu ya shinikizo la marafiki rika na mategemeo ya walimu, mwisho wa siku pamoja na kuingia na daraja la kwanza kidato cha tano, wanamaliza na daraja la nne kama sio sifuri kabisa.

  ReplyDelete
 7. Namshukuru Mungu alinisaidia kuvuka kizingiti cha shinikizo la nje wakati huo mgumu wa maamuzi unaofanana na huu unaouzungumzia. Nilimaliza kidato cha nne kwa ufaulu mzuri tu katika masomo yote. Pamoja na kwamba nilikuwa na nafasi ya kaumua wapi pa kwenda kwa nafasi, lakini kwa kweli isngekuwa sababu hii ama ile, ingeniwia vigumu sana.
  Walionizunguka hawakunisaidia kunielewa. Pengine ni kwa sababu nilikuwa na vingi vya kufanya kwa wakati mmoja. Maana pamoja na kuwa katika madarasa ya sayansi, bado nilikuwa ‘Mhariri’ wa gazeti la shule na mzungumzaji (nadhani mzuri) kwenye debates. Nilikuwa mwizi wa vitabu maktaba kwa sababu ya kupenda kusoma vitabu visivyo vya kimasomo pamoja na magazeti. (Nakumbuka wakati wakufunga shule, ilikuwa ni lazima niwe na boksi la kusafirisha nakala za magazeti ya Rai –ya kipindi cha akina Jenerali –kwenda nyumbani). Sikumbuki idadi ya walimu wangu wa sayansi ya jamii ambao walinioshauri nisome sanaa wakiamini nitafika mbali sana. Lakini pamoja na hayo, moyo wangu ulipenda sana sayansi. Na sikuwa natumia nguvu nyingi sana maana niliipenda sana. Sayansi ilionekana kujibu maswali yangu mengi ‘ya kwa nini ni hivi na kwa nini ni vile’. Sanaa haikujibu maswali yangu mengi ila pia niliipenda (nakumbuka nilikuwa-ga na dili la kuwaandikia poem rafiki zangu kwa wapenzi wao.) Lakini juu ya hayo yooote nilisisimuka sana kujifunza nadharia za kanuni za kimaumbile. Namshukuru Mungu kuwa sikusoma PCB kwa bahati mbaya japo (tangu awali) zikupanga kabisa kuwa daktari. Na mpaka sasa, najiona nikiwa katika mwelekeo sahihi, kwa sababu tu sikufuata maelekezo kutoka nje. Nilifanya maamuzi yanayokidhi haiba yangu.

  Kama ningepata nafsi ya kuwashauri wazazi, ningewaambia kwamba chaguo la nini akisome mtoto si lao wazazi na si lazima kiendane na performance ya mtoto. Chaguo la mtoto aliyeelimishwa(informed child) likifanyika kwa kuzingatia anachotaka kukifanya maishani, hiyo itakuwa poa sana.
  Ningemshauri mzazi atumie muda mwingi kugundua mission na vision ya mtoto, badala ya kutumia nguvu nyingi kumlazimisha kusoma vitu ambavyo mtoto mwenyewe havipendi. Namaanisha amfundishe mtoto kufanya informed decisions kuanzia kwenye nfasi yake kwanza.
  Vinginevyo, soma yote itakuwa ni ya kipurure (nimelipenda sana neno hili) na mwisho wa siku ni lazima akimbilie siasa maana hajui anachotaka kukifanya kwenye jamii. Hapo inakuwa bila bila. Tamathilia inakatikia njiani.

  ReplyDelete
 8. Bwaya - asante sana kwa maelezo haya ya kina. Mimi kwa upande wangu kwa kweli Fizikia ilikuwa inanipa shida kidogo. Japo nilikuwa naweza kukariri na kupata A au B nikitaka, kulikuwa na kitu fulani kilichokuwa kinaniambia kwamba kamwe sayansi haikuwa wito wangu. Walimu wangu wao hawakuona hivyo. Mwalimu wangu wa Bayolojia baada ya kuona kuwa nimeshika namba moja katika mtihani wa Mock kwa mkoa mzima wa Kagera alikuja juu vibaya sana na kunilazimisha kuchagua PCB kama chaguo la kwanza. Naamini ningefuata ushauri huu nisingefika mbali na pengine ningegonga mwamba kidato cha sita. Ndiyo maana nikaamua kuitii sauti iliyokuwa ikiniambia kwamba masomo ya sanaa yangenifaa zaidi. Na kweli mpaka leo silalamiki kwa uamuzi huu. Wapo jamaa wazuri sana tulikuwa nao O'level lakini sijui kilitokea nini form 6 wakaishia kupata divisheni 3 na 4 na PCB zao.

  "Presha" ya wazazi na jamii kwa watoto wao kuwa madaktari/wanasheria pengine ni kubwa mno kwa watoto - na hii, kama vile kokoro, inawasomba hata wale ambao kusema kweli hawana mvuto na sayansi na matokeo yake tunayaona. Miaka michache tunayoishi hapa dunia haipaswi kupotezwa katika kujaribu kuwafurahisha watu wengine na kuishia kufanya kile tusichokipenda!

  ReplyDelete
 9. Kaka Matondo.. tumekuwa wote sengerema wakati uko a-level nasi tuko o-level... unamkumbuka buga, balbu, Aigosh

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU