NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, August 6, 2009

SIASA ZA (KIBAGUZI) MAREKANI: OBAMA HAKUZALIWA MAREKANI, URAIS WAKE NI BATILI

Vuguvugu na uvumi kwamba rais Barack Obama hakuzaliwa Marekani na hivyo, kulingana na katiba, hawezi kuwa rais wa Marekani vinazidi kupamba moto. Juzijuzi hapa mwanajeshi mmoja aitwaye Stefan Cook alikaidi amri ya kwenda vitani Afghanistan akidai kwamba hawezi kwenda kupigana chini ya Amiri Jeshi Mkuu haramu ambaye si Mmarekani kwa kuzaliwa. Wahafidhina wengine kutoka chama cha Republican wakiwemo Rush Limbaugh (mtangazaji mashuhuri wa redio ya Kihafidhina wa chama cha Republican) na Lou Dobbs (mtangazaji wa CNN) wameendelea kudai kwamba Obama alizaliwa Mombasa Kenya na hivyo si Mmarekani kwa kuzaliwa; na kuiweka nchi katika uongozi wa mtu ambaye si Mmarekani kwa kuzaliwa ni jambo la hatari. Pamoja na jimbo la Hawaii alikozaliwa Obama kutoa uthibitisho mara mbili kwamba ni kweli raisi huyo alizaliwa jimboni humo, vuguvugu hili linazidi kupamba moto. Cheti cha kuzaliwa kinachoonyesha kwamba Obama alizaliwa Mombasa Kenya kimethibitishwa kwamba kilikuwa kimeghushiwa (tazama hapa na hapa)

Wachambuzi wengine wanaliona vuguvugu hili kuwa ni juhudi za makundi ya kibaguzi ambayo mpaka leo hayajaamini kama kweli mtu mweusi ndiye rais na yanafanya kila liwezekanalo ili kumwondoa madarakani, au kumfanya ashindwe kama rais. Ni makundi haya haya ambayo yametajwa kuwa yanahusika na ule uvumi ulioenezwa sana kwamba Obama alikuwa/ni shoga (tazama hapa). Mabadiliko yatakuja polepole ingawa bado safari ni ndefu kwani fikra za ubwana za wazungu za karne nyingi za kumwona mtu mweusi kama mtumwa na binadamu wa daraja la pili hazitatokomea hivi hivi. Cha ajabu ni kwamba hata weusi wenyewe tumeaminishwa hivyo na tumeikubali hadhi yetu ya kitwana (mfano, tazama hapa).

2 comments:

  1. justsioni faida wala hasara ya mtu mweusi kuongoza marekani. kama ipo nipatie

    ReplyDelete
  2. Kamala, hakuna hasara yo yote kwa mtu mweusi kuongoza Marekani na nadhani huyu kijana anajitahidi pamoja na uoinzani wote anaopambana nao na watu kumtakia ashindwe. Tatizo ni hawa wahafidhina wa Republican na wazungu vichwa ngumu ambao bado hawaamini kama kweli wanaweza kuongozwa na mtu mweusi. Wameshajaribu kumharibia kwa kila njia wakimwita shoga, dikteta, mkomunisti, msoshalisti, gaidi na sasa si mzaliwa wa Marekani na hivyo uraisi wake ni batili. Wengi wanaamini kwamba kama angekuwa ni Mzungu yote haya yasingezushwa. Lakini pengine ni kama wasemavyo wenyewe - siasa ni mchezo mchafu.

    ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU