NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, August 25, 2009

UTAFITI: KUENDESHA GARI HUKU UKITUMA UJUMBE KWENYE SIMU (TEXTING) NI HATARI ZAIDI KULIKO KUENDESHA UKIWA UMELEWA POMBE AU BANGI

Utafiti uliofanywa na "The Transport Research Laboratory" nchini Uingereza umeonyesha kwamba madereva wanaotuma ujumbe huku wakiendesha wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata ajali kuliko wenzao waliokunywa pombe kiasi au kuvuta bangi. Madereva hawa ni wale wenye umri kati ya miaka 17-24 (matineja). Kwa mfano utafiti umeonyesha kwamba:

(1) Utayarifu wa madereva hawa kuepuka ajali ulipungua kwa asilimia 35 ikilinganishwa na asilimia 12 kwa waliokuwa wamekunywa pombe kiasi na asilimia 21 kwa wavuta bangi.

(2) Madereva waliokuwa wakituma au kusoma ujumbe katika simu zao walikuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kutangatanga kutoka sehemu moja ya barabara kwenda nyingine na uwezo wao wa kudhibiti usukani ulipungua kwa asilimia 91 ikilingalishwa na wenzao wanaoendesha bila kutumia simu. Wavuta bangi, kwa upande mwingine, uwezo wao wa kudhibiti usukani ulipungua kwa asilimia 35.

(3) Madereva hawa pia walikuwa na taabu ya kuacha nafasi inayotakiwa kati yao na magari yaliyo mbele yao. Kwa habari zaidi kuhusu utafiti huu soma hapa.

Tatizo hili ni kubwa hasa hapa ninapoishi kwani ni kamji kadogo na kuna wanafunzi wapatao 50,000 hivi na mara kwa mara utawaona wengine wakituma na kusoma ujumbe kwenye simu zao na wengine wamelala au wanasinzia huku wakiendesha.

Kama na wewe mdau una tabia hii ya kutuma na kusoma ujumbe kwenye simu yako wakati unaendesha, fikiria mara mbilimbili kabla ya kufanya hivyo. Ajali nyingi sana (za magari, treni, mabasi n.k.) zimetokea hapa Marekani na zimethibitishwa kwamba zilisababishwa na utumaji na usomaji wa ujumbe kwenye simu kwa madereva waliohusika. Kwa mfano tazama hapa (Onyo: Kuna picha za kutisha. Usitazame kama hujiwezi). Hiyo text message bila shaka inaweza kusubiri mpaka utakapofika nyumbani!

2 comments:

  1. Ni kweli ni hatari kubwa sana hii na asante kwa ujumbe ningependa hawa matineja wangesoma ujumbe huu. Kwani ni ajali nyingi sana zinatokea.

    ReplyDelete
  2. Si matineja tu - hata sisi na wao, inabidi tuache tabia hii kwani ni hatari sana. Na mara nyingi hata text message yenyewe unayohangaika kuituma au kuisoma na kuhatarisha maisha si ya muhimu. Hata kama ni mazoea inabidi tujibidishe tuyashinde!

    ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU