NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, August 11, 2009

UTAFITI: KUNYONYESHA HUZUIA KANSA YA MATITI KWA ASILIMIA 25 - 60

Mbali na ukweli kwamba kunyonyesha ndiyo chanzo cha lishe bora kabisa kwa mtoto, wanasayansi sasa wanadai kwamba kunyonyesha pia kunaweza kupunguza uwezekano wa mama kupata kansa ya matiti kwa asilimia 25 hadi 60.

Hizi ni habari njema kwa akina mama wa Afrika ambao kimsingi huchukulia kunyonyesha kama mojawapo ya wajibu wao baada ya kupata mtoto. Pengine hii inaweza kuwa ndiyo sababu iliyofanya saratani ya matiti isijidhihirishe sana Afrika.

Wasiwasi wangu ni juu ya kizazi kipya ambacho kinaiga mambo ya Kimagharibi kwa pupa. Nimeshasikia kwamba mabinti wengi sasa hawana hamu tena ya kunyonyesha vichanga vyao wakichelea kuharibu matiti na miili yao. Ukijumlisha na vitu vingine vinavyoingia Afrika vikiwemo vyakula vilivyolimwa "kisayansi", madawa na mabadiliko mazima ya mfumo wetu wa maisha, sitashangaa kama kansa itafumuka na kuwa ugonjwa wa kawaida tu muda si mrefu ujao. Hili likitokea, atakayefaidika bila shaka ni makampuni ya madawa ya nchi za Kimagharibi - na naamini kwamba hiki ndicho wanachotaka. Tuweni waangalifu na tuache mambo ya kuiga vitu kiholela bila kuelewa hasa kiini chake.

Kwa habari zaidi soma hapa. Kwa faida zingine za kunyonyesha soma hii makala ya Kiswahili.


6 comments:

 1. Nitanukuu "Hizi ni habari njema kwa akina mama wa Afrika ambao kimsingi huchukulia kunyonyesha kama mojawapo ya wajibu wao baada ya kupata mtoto. Pengine hii inaweza kuwa ndiyo sababu iliyofanya saratani ya matiti isijidhihirishe sana Afrika."mwisho wa kunuuu.

  Ni kweli kabisa na habari njema kwana huku Ugahaibuni kwa kweli ni aibu sana kwani utakuta akina mama waliopata watoto wanaanza mara moja kuwapa watoto wao maziwa kwa kutumia chuchu na kuwapa vidudu visivyoeleweka yaani kitu kinafanana na chuchu za mama. Kwote huko ni kumdanganya mtoto.
  Huwa wanashangaa sana nikiwaambia sisi Afrika tunanyonyesha watoto pengine hadi umri wa miaka mitatu. Wanashangaa sana, wao ikifika miezi mitatu ni mingi sana. Nimefurahi sana.

  ReplyDelete
 2. Ni kweli kuwa ni habari njema Kakangu. Ila la kusikitisha watu wanaanza kuamini kuwa kunyonyesha "hudondosha" matiti na kama nilivyoandika leo, wanajitahidi "kuukimbia ukweli wa umri wao". Kwa hiyo wanaamua kufanya "kizungu" kwa kutowanyonyesha.
  Bahati mbaya saaana "hatujakazia" mstari mwembamba uliopo kati ya uelimikaji na ustaarabikaji., Kati ya Maisha halisi kulingana na mazingira na maisha ya kimagharibi. Kutambua baya na zuri kwa mazingira na taifa letu.
  TUNAJIPOTEZA KATIKA HARAKATI ZA KUJITAFUTA. Lakini kwa makala kama hizi, tunaweza kuirejesha jamii katika KUJITAMBUA na kutambua umuhimu wa kuheshimu njia halisi za maisha ambazo hatustahili kuziacha kwa kuwa zina manufaa kwetu.
  Asante kwa hili

  ReplyDelete
 3. Yasinta - nawafahamu watoto kule nyumbani ambao walinyonya kwa miaka sita mizima kitu ambacho leo sidhani kama inawezekana. Hili suala la kutonyonyesha kwetu sijui kama linawezekana kwani sidhani kama tunazo raslimali hasa zinazotakiwa (mf. huduma nzuri za afya kuhakikisha kwamba mtoto hadhuriki kwa kutonyonyeshwa) Nimeshaona watoto ambao badala ya maziwa ya mama wananyonyeshwa eti wananyonyeswa maziwa ya ng'ombe kwa sababu mama hataki kunyonyesha na uwezo wa mzazi haumruhusu kununua maziwa ya makopo ambayo ni ghali. Matokeo yake kitoto kinakondeana sana na kuandamwa na magonjwa kila leo. Shida tupu.

  Mzee wa Changamoto - ngoja tuone kuiga kwetu huku kwa pupa kunakotupeleka lakini haipendezi tunapotupiia mbali jambo la msingi kabisa kama kunyonyesha mtoto kwa vile tu eti tumeona katika TV na kuaminishwa kuwa binti mrembo wa kizungu ni yule mwembamba kama kijiti na mwenye matiti makubwa (japo ya bandia) yaliyosimama. Makala tunaandika na kuonya lakini je, nani anazisoma? Ukitaka blogu yako isomwe sana na kuwa maarufu basi jaribu kuandika udaku - zusha mambo, singizia watu, wafurahishe watu kama Ze Utamu alivyofanya. Hapo utapata wasomaji kwelikweli. Lakini tusikate tamaa, juhudi zetu si bure!

  ReplyDelete
 4. Ni kweli kabisa Kaka Masangu. Ili uwe maarufu anza kuweka picha nu nusu-ukamilifu ama nusu-mavazi na kama ulivyosema kuzusha. Yaani utamaarufika. Lakini haya yanapita kwani baada ya muda, UKWELI UTADHIHIRIKA.
  Blessings

  ReplyDelete
 5. safi sana, my wife ni kunyonyosha mpaka kieleweke

  ReplyDelete
 6. Kunyonyesha kuna raha yake. Sisi tuliobahatika kupata watoto na kuwanyonyesha inapendeza pale kamalaika kanapokutumbulia macho na kujaribu kukariri sura yako. kwaweli huwa ni wakati (moment)nzuri sana na inaleta muunganiko fulani kati ya mama na hako kamalaika. Mtoto yake nyonyo angalau kwa kipindi cha mwaka na miezi sita. Siku hizi watu si kwamba hawataki kunyonyesha tu bali watoto pia huwekwa kwenye majeneza ya bei rahisi tu (Tsh. 100) na kuzikwa wangali wazima. Cha ajabu ni kwamba wapo wanaoiba watoto wa wenzao lakini pia wapo watoa mimba na watupa watoto. Natamani wangekuta sehemu fulani ili akitupwa tu aokotwe. Wito kwetu sote kujenga vituo ili wasiohitaji hivyo vimalaika badala ya kuvitupa na kuviua viwe na sehemu ya kuokolewa maisha yao

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU