NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, August 21, 2009

UTAFITI: TALAKA INAWEZA KUKULETEA MATATIZO SUGU YA KIAFYA

Ingawa tafiti mbalimbali tayari zimeshaonyesha kwamba watu waliooa au kuolewa (wanandoa) wanaishi maisha yenye afya nzuri zaidi kuliko makapera (Mzee wa Changamoto na Dada Koero mnasikia?), wanasayansi walikuwa bado hawajajua kinachotokea kiafya ndoa inapovunjika.

Utafiti mpya unaonyesha kwamba wanandoa wanapokuwa makapera tena ama kupitia talaka au kifo, mbali na kupata misukosuko ya kimihemko (emotions), mara nyingi afya zao pia huporomoka. Mporomoko huu wa afya huwa ni wa kudumu hata kama wakioa/wakiolewa tena baadaye. Ili nisirudie kila kitu katika utafiti huu, hapa chini ni baadhi tu ya mambo muhimu yaliyotajwa.

 • Kiafya inaonekana ni bora kutooa kabisa kuliko kuoa na kuacha ama kuachika. Watu wa makamo ambao hawakuwahi kuoa wana matatizo sugu ya kiafya machache kuliko wale waliooa na baadaye kutalikiana au kufiwa na wapenzi wao.
 • Kwa ujumla wanandoa waliotalikiana au waliofiwa na wapenzi wao wana matatizo sugu ya kiafya (mf. kisukari na saratani/kansa) mengi zaidi kwa asilimia 20 kuliko wenzao ambao hawajatalikiana au kufiwa na wenzi wao.
 • Japo kuoa/kuolewa tena kulionekana kuboresha afya, utafiti umeonyesha kwamba wanandoa waliorudia ukapela ama kupitia talaka au ujane, kamwe hawarudii afya walizokuwa nazo kabla ya ndoa zao kuvunjika. Watu ambao ndoa zao zilivunjika halafu wakaoa/wakaolewa tena walikuwa na matatizo sugu ya kiafya mengi zaidi kwa asilimia 12 kuliko wenzao ambao ndoa zao hazikuwahi kuvunjika. Kwa habari zaidi juu ya utafiti huu soma hapa.

Kama kawaida utafiti huu umefanyika kwa wazungu ambako kiutamaduni ni tofauti sana na nyumbani. Kwa mfano, ningependa kujua kama talaka ina madhara yo yote kiafya kwa mwanaume mwenye wake zaidi ya mmoja au mwenye nyumba ndogo. Nyumbani pia nadhani kwamba wanawake ndiyo wanaathirika zaidi na talaka kwani wao ndiyo hutakiwa kubeba visulupwete vyao na kuondoka. Huku Marekani mara nyingi mwanaume ndiye anafungasha virago vyake na kuwaachia mama (na watoto) nyumba.

 • Mwathirika mkuu wa talaka, kwa maoni yangu, ni watoto!
 • Inasemekana India ndiyo ina idadi ndogo kabisa ya talaka wakati Sweden ndiyo inaongoza (Dada Yasinta upo?) ikifuatiwa na Marekani. Tazama hapa.

6 comments:

 1. Kwanza nasema ahsante kwa kuliweka hili jambo kwa mara nyingine. Ni kweli hapa Swweden inatisha sana leo "kuoana" kesho kuachana yaani imekuwa kama kubadili nguo. Na ni kweli ni watoto ndio wanaothirika szaidi maana kila wiki inabidi aende kwa baba au mama na akienda kwa baba anakuta mke (mama) mwingine akienda kwa mama anakuta "babb" mwingine. Na mbaya zaidikuna wengine waachanapo wanakuwa maadui kabisa. Halafu pia inawezekana ni jambo ndogo sana ambalo linawaachanisha.

  Kama nilivyoandika makala moja ya kuwa wanawake wa ughaibuni wanapenda sana kuwaamri waume zao. kwa hiyo asiposikilizwa basi hawezi kuongea kwa upole na wenzake isipokuwa anachukua uamiuzi wa kutaka talaka. Kwa mimi hii inaonyesha hawa watu hawakupenda kwa dhati:

  ReplyDelete
 2. tatizo ni kwamba watu wamejiingiza kwenye ndo bila kufahamu maana ya ndoa na bila kufuata misingi ya ndoa, ambapo kati ya hiyo ni HESHIMA, UVUMILIVU na UPENDO. Kwakweli watoto huathirika sana. Hata hapa nyumbani(Tanzania)Mara nyingi watoto hubaki na mama zao ambao kimsingi huwa kiuchumi hawajiwezi kabisa. Hii hupelekea watoto wazururaji,wizi,umalaya, kubakwa na madhila yoyote ambayo unaweza kuyataja. Kwakweli watu wanatakiwa wamrudie Mungu. Na wanawake pia wanatakiwa kupata elimu ya kutosha ili waweze kulea watoto pindi nyumba zinapovunjika kulikoni kwenda kuwatupa watoto kwa baba zao ambao huko wanakutana na mama wa kambo. Nimeipenda mada hii

  ReplyDelete
 3. Lo, hii hatari. Niliwahi kusikia usemi kuwa ndoa ni mtego: walio ndani wanahangaika kujitoa, na walio nje wanahangaika kutumbukia. Makubwa haya :-)

  ReplyDelete
 4. Profesa Mbele. Ni kweli ndoa ni mtego - walio ndani wanahangaika kujitoa na walio nje wanahangaika kutumbukia.

  Nilimsoma mtafiti mmoja gazetini (simkumbuki jina lake vizuri) ambaye aliwahoji wanandoa kwa nini waliamua kuoa/kuolewa. Nilishangaa kuona kwamba wengi wao hawakuwa na sababu ya maana. Wengine waliishia kusema "I thought I would be happy", "I loved him before he changed" na "I don't know" Wakristo wengi walisema kwamba "I wanted to raise a family as God wants us to do". Ni kazi kwelikweli. Pengine vijana inabidi wafikirie vizuri kabla hawajatumbukia katika "mtego" huu. Anony. na Yasinta - asanteni kwa maoni mazuri. Kama nilivyosema hapo juu, waathirika hasa wa talaka ni watoto.

  ReplyDelete
 5. Nakumbuka kuna prof mama mmoja tukiwa chuo alitufundisha topic ya gender. alisema moja kati ya viashirio kuwa kuna usawa wa gender ni talaka nyingi. akatoa mfano nchi ya sweden. Ila nakumbuka sikukubaliana nae kwa kutoa mfano wa zanzibar ambapo napo talaka ni kitu cha kawaida na sidhani kama kuna gender equity.
  HIYO NAHISI HAITUHUSU WAAFRIKA. TOFAUTI KWETU WATOTO NDIO WANA ATHIRIKA ZAIDI.

  ReplyDelete
 6. Godwin, prof pengine alikuwa sahihi kwa mtazamo wa nchi za Kimagharibi. Lakini kama ulivyosema, kwa nchi zetu si kweli. Sikujua kama Zanzibar talaka ni jambo la kawaida. Nilichokuwa nafahamu ni kwamba nchi nyingi zenye idadi kubwa ya waumini wa dini ya Kiislamu zina idadi ndogo ya talaka. Sijui ni kwa nini Zanzibar haifuati ruwaza (pattern) hii.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU