NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, September 3, 2009

ASKOFU KAKOBE "AONYA" KUHUSU UPOLE WA JK NA HATARI ZAKE

Madhehebu ya dini (mf. Wakatoliki na Waislamu) kuibuka na kutoa "nyaraka/miongozo" ya kisiasa kwa waumini wao ni sawa? Je, hali hii ikiachiwa haiwezi kweli siku moja 'kufufua" hisia za udini miongoni mwa Watanzania na kuweza kuleta shari? Mbona kiongozi wa nchi amekaa kimya kuhusu suala hili muhimu? Askofu Kakobe anasema kwamba JK ni mpole mno na upole wake unaweza kuwa hatari kwa taifa. Sijui kama hii ni kweli. Unaweza pia kutazama hapa na hapa kuhusu masuala yanayohusiana na hili.

Kakobe: Upole wa JK hatari
Asema viongozi wa dini ndio chanzo cha ufisadi
Chanzo: Tanzania Daima, 3/9/2009

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zacharia Kakobe, amesema ameshtushwa na ukimya wa Rais Jakaya Kikwete kushindwa kukemea nyaraka zinazotolewa na madhehebu ya dini, hali ambayo inaweza kusababisha machafuko kama haitadhibitiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Askofu Kakobe alisema tamko la Rais Kikwete lina uzito kuliko kiongozi yeyote nchini.

Alimtaka Rais Kikwete asikae kimya, kwani kufanya hivyo kutaonekana kama ni kutaka kumfurahisha kila mtu.

Alisema kama hali hiyo ikiendelea, inaweza kuligawa taifa ambalo limekuwa na misingi ya amani, umoja na utulivu tangu wakati wa Mwalimu Nyerere.

“Rais Kikwete anapaswa kutoa tamko juu ya viongozi wa dini, ambao sasa wanatoa nyaraka mbalimbali… tunaamini kauli yake itakuwa nzito kuliko kiongozi yeyote,” alisema Askofu Kakobe.

Alisema Rais Kikwete ni mpole, lakini anapaswa kuonyesha ujasiri wake ili taifa lisipoteze amani iliyojengeka muda mrefu isitoweke.

Akionekana dhahiri kutoridhishwa na nyaraka hizo za kidini, alisema umefika wakati uhuru wa kutoa maoni utumiwe kwa mipaka, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa maoni yanayotolewa hayasababishi kwa namna yoyote ile taifa kugawanyika.

Alisema moja ya jukumu kubwa la viongozi wa dini, ni kuilinda serikali kwa manufaa ya Watanzania wote na si kwa manufaa ya dini fulani.

“Mtu kama anataka kutoa maoni yake atoe kama yeye na si kushirikisha dhehebu zima, na aangalie kitu gani anachozungumza si kama walivyofanya Wakatoliki na Waislamu kwa kusema kuwa ‘huu ni waraka wa Wakirsto’ na ‘huu ni muongozo wa Waislamu’,” alisema Askofu Kakobe.

Sababu kubwa ya viongozi wa madhehebu ya dini kutoa waraka na mwongozo, ni kuwataka wafuasi wa dini hizo na Watanzania kwa ujumla kuchagua viongozi wanaofaa.

Alisema viongozi wa dini hawatakiwi kutoa waraka unaohusu siasa na kuwahimiza waumini wao kuchagua viongozi wa dini zao kwani katika uchaguzi mkuu wa mwakani watatakiwa kuchagua viongozi wa serikali na wala si wa dini.

“Kiongozi akienda kuomba kura, haendi kama muumini wa dhehebu fulani, bali anaenda kama mfuasi wa chama fulani. Sijawahi kusikia mbunge wa dini fulani, ila ni mbunge wa Watanzania wote. Kinachotuunganisha ni Utanzania si dini wala ukabila,” alisema Askofu Kakobe.

Alisema nyaraka zilizotolewa na Wakristu na Waislamu, zimejaa maneno ya kichochezi ambayo yanatumika kama miongozo kwa waumini wa dini hizo na Watanzania kwa ujumla.

“Waislamu walipozindua waraka wao, walisema; ‘Wakatoliki wamemwaga ugali na sisi tunamwaga mboga. Kama Wakatoliki wangezingatia ushauri huenda tusingefika huku sisi Waislamu’. Kauli hizi ni za hatari, zinaweza kuleta vita,” alisema Kakobe.

Kuhusu waraka uliotolewa na Kanisa Katoliki, Askofu Kakobe alisema hali hii inaonyesha mpasuko kwani kila dhehebu linataka mfuasi achague kiongozi kutoka kwenye dini husika.

Akitoa mfano wa maneno yanayoashiria mpasuko katika waraka wa Kanisa Katoliki, Kakobe alinukuu kifungu kinachosema; “wagombea wanavyotawaliwa na dini yao ni muhimu kuwadhibiti kwa lengo la kuwasaidia kuanzia ngazi za vijiji hadi taifa kwa jumuia za kanisa ili tunu za Kikirsto zionekane katika sera na uongozi.”

Katika hatua nyingine, Kakobe alikemea kauli iliyotolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wakati wa mazishi ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza, Antony Mayalla, kwamba wanasiasa hawana haki ya kuwafundisha viongozi wa dini kama walivyofanya mara baada ya kanisa hilo kutoa waraka wake.

Alisema, Pengo alionyesha jeuri na utovu mkubwa wa nidhamu kwa kiongozi wa nchi, kwa kutoa kauli hiyo mbele ya Rais Jakaya Kikwete.

“Nikemee vikali tamko la kiongozi mmoja wa dini aliyesema ‘wanasiasa wasitufundishe’. Kauli ile aliitoa mbele ya rais, ule ulikuwa ni utovu wa nidhamu. Ilionyesha jinsi alivyo jeuri na asivyotaka kushaurika. Sisi kama viongozi wa dini, tunapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda amani na utulivu,” alisema Kakobe huku akiepuka kutaja jina la Pengo ingawa baadaye alijisahau na kumtaja.

Alisema kawaida waraka hutolewa na viongozi wa vyama vya siasa wakati wa kampeni kwa ajili ya kujinadi mbele ya wananchi.

“Dini inapotoa waraka, inamaanisha inataka kushika madaraka kama vyama vya siasa… wote tunaamini kwamba dini inafanya kazi kama ilivyosajiliwa,” alisema Askofu Kakobe.

“Unajua kama DECI ilisajiliwa na kufanya shughuli zake, lakini ilivyogundulika kwenda kinyume cha sheria, ilifungiwa na kushuhudia inafikishwa mahakamani. Hivyo dini hizi zinapaswa kufunguliwa mashitaka kwa kwenda kunyume na usajili,” alisema Askofu Kakobe.

Alisema anawashangaa viongozi wa dini na watu wanaoshabikia waraka huo wa Kanisa Katoliki, kwamba unapinga viongozi mafisadi wasichaguliwe, ilhali chanzo kikuu cha kuwepo kwa mafisadi ni viongozi wa dini kushindwa kuwajibika na kuwaelimisha waumini wao hadi wakajiingiza kwenye ufisadi.

“Mafisadi wana dini na wamelelewa katika dini hizi hizi, sasa iweje wao wawasemee mafisadi? Ina maana wamekuwa wazembe katika kukemea na kujenga maadili. Kwa hiyo wao ndio wanaotengeneza mafisadi,” alisema Askofu Kakobe.

Aliwataka wananchi kutoshabikia nyaraka zinazotolewa na viongozi wa dini na waziogope kama ukoma kwani vita ikitokea, hakuna fidia watakayopata wananchi kama walivyopata wahanga wa matukio ya milipuko ya mabomu Mbagala.

Alishauri viongozi wa madhehebu ya dini, wanasiasa na viongozi wa kiserikali wakutane na kujadili mustakabali wa umoja na amani ya taifa, ikiwa ni pamoja na athari za dini au dhehebu kutoa waraka unaowaandaa wananchi kwa ajili ya chaguzi za kisiasa.

5 comments:

 1. huko kwa kakobe hakuna mafisadi? wanaokwenda na mabenzi na kuacha funguo na vito vya thamani nk wamezitoa wapi kama siyo ufisadi.

  na yeye mbona anapokea dinari toka kwao na ana-insist watoe mapesa mengi?

  to be honest, dini zetu zimeshindwa kupigana na ufisadi kwani waamini ni walewale wanaotoa mamichango makubwa makubwa ya shughuli za kanisa na misikiti?

  hakuna atakayekemea ufisadi kwa ukweli toka moyoni mwake...mimi tu sithubutu kwani wakati wa uchaguzi huwa nakula chakula ambacho chumvi ilotumika imetoka kwenye kampeni pia natumia kanga kwenda bafuni ilotolewa na mh. fulaniiii!!!

  ReplyDelete
 2. Kakobe naye Bwana. Huyu jamaa ameshafilisi watu wengi sana. Watu wanauza nyumba, magari na kila kitu halafu wanampelekea yeye. Ametajirika kupindukia huyu sawa na akina Yona, Mramba na Mgonja. Huu siyo ufisadi kwa jina jingine tu? Ufisadi ni ufisadi tu hata uuvike sura ya Yesu bado ni ufisadi! Inashangaza kuona kuwa anawakemea mafisadi wenzake. Hoovyo!!!

  ReplyDelete
  Replies
  1. Kila unachikinena utakitolea hesabu je una uhakika na unayoyasema?

   Delete
 3. Ukitazama hiyo picha ya Kakobe utaona naye amezungukwa na utukufu kama vile picha za Yesu zinavyochorwa. Kazi ipo!!!

  ReplyDelete
 4. Anony, pamoja na utakatifu/utukufu unaoonekana katika hiyo picha pia kuna asilimia kubwa saaaaana ya UTAKAVITU!!!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU