NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, September 30, 2009

ATI, WATOTO WA KIMAREKANI WANA AKILI KULIKO WATOTO WA KIAFRIKA?

Mwaka huu nimejitolea kufundisha wanafunzi wa darasa la tatu katika shule moja ya msingi (darasa la kwanza mpaka darasa la tano). Niliamua kufanya hivi ili niweze, mbali na mambo mengine, kujifunza na kuuelewa vizuri mfumo wa elimu wa hawa wenzetu "walioendelea" na kusema kweli nimeona, nimejifunza na kushangazwa na mengi.

(1) Shule zao nyingi zina karibu vitu vyote vya muhimu ambavyo vinawawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo. Kuna maabara nzuri, chumba cha kompyuta na vitu vingine muhimu.

(2) Elimu yao inamakinikia zaidi vitendo na wanafunzi wanasisitizwa sana kufanya majaribio yao wenyewe ama wakiwa shuleni au nyumbani wakisaidiwa na wazazi wao. Tafiti mbalimbali zimeonyesha kwamba wanafunzi hujifunza vizuri zaidi wanaposhirikishwa kivitendo katika kujifunza. Elimu ya kukariri kwa kweli imeshapitwa na wakati na haimsaidii mtoto kujifunza hadi kufikia upeo wake kiakili.

Nimeshangazwa na ukweli kwamba mtoto wa darasa la pili wa Kimarekani anaweza kukueleza vizuri kabisa na kwa kutumia maneno yake mwenyewe mfumo mzima wa maji (hydrological cycle) pamoja na dhana mbalimbali za msingi katika sayansi kama usumakishaji (magnetism), umeme, nguvu ya uvutano (gravity), mwendo (motion), ukinzani (friction), mfumo wa sayari (planetary system), sauti, sifa za mada (properties of matter), hali ya hewa na majira, nishati (energy) pamoja na dhana nyinginezo. Ni kutokana na ukweli huu kwamba nilianza kujiuliza kama wanafunzi hawa wana akili zaidi kuliko wanafunzi wa nyumbani. Nilikumbuka pia utafiti mmoja ambao ulilinganisha watoto wa Ulaya na wa Afrika. Utafiti huo ulionyesha kwamba watoto wa Afrika wako "slow" wakilinganishwa na wenzao wa Ulaya. Kwa nini?

Mbali na matatizo mengi yanayoukumba mfumo wetu wa elimu (ambayo mengi ni ya kujitakia tu), tatizo kubwa kabisa kwa maoni yangu ni lugha ya kufundishia. Ni ukweli wa kisayansi kwamba elimu ya kweli inawezekana tu pale mtoto anapofundishwa katika lugha anayoifahamu vizuri. Ili mtoto aweze kukomaa na kufikia kilele chake cha kiakili ni lazima afundishwe kwa lugha yake mwenyewe. Cha ajabu ni kwamba mtoto wa Kiafrika, kinyume na mtoto wa Kichina anayefundishwa kwa lugha yake ya mama, kinyume na mtoto wa Kijapani anayesomeshwa kwa lugha yake ya kwanza, kinyume na mtoto wa Kithailand anayefundishwa kwa lugha yake ya mama, kinyume na....mtoto wa Kiafrika yeye anafundishwa katika lugha ambayo HAIELEWI, lugha ambayo haifundishwi vizuri na hata wafundishaji wenyewe hawaimudu vizuri. Matokeo yake elimu inakosa maana na inageuka kuwa zoezi la kukariri tu - hata kwa dhana zilizoko katika mazingira yake mwenyewe kama hii ya "hydrological cycle", mmomonyoko wa udongo, mito n.k. Ati, kukariri "Newton's Laws of Motion" kikasuku kweli ni elimu?

Bila mabadiliko ya kweli katika mfumo mzima wa elimu mimi naamini kwamba Afrika tutaendelea kuwa washangiliaji tu katika mchezo wa kisiasa, kitamaduni na kiuchumi unaochezwa hapa duniani. Mbaya zaidi hata "wasomi" wachache tunaowapata kupitia mfumo wetu huu wa kukaririshana kikasuku hasa katika nyanja za utabibu na uhandisi wanakimbia kwenda nje na hakuna anayejali.

Watoto wote wako sawa na dai la kijumla kwamba eti watoto wa Ulaya/Kizungu/Kimarekani wana akili kuliko watoto wa Kiafrika halina ukweli wo wote wa kisayansi. Kama watoto wa Ulaya/Kizungu/Kimarekani wanaonekana kuwa "sharp" ni kwa sababu elimu yao iko makini zaidi na wanayo bahati ya kufundishwa katika lugha yao wenyewe. Kwa bahati mbaya sana mtoto wa Kiafrika hana bahati hiyo!

9 comments:

 1. Mimi nafikiri watoto wote weasio na mtindio wa ubongo ukiwaweka darasa moja na kuwapa kila kinachotakiwa kielimu na kiafya watafanya vizuri tu. Ninachojiuliza ni kwa nini watoto hao wa marekani wamekuwa na matukio ya kihuni na kuua wakati wamekuwa na msingi mzuri wa elimu, hapo, ndipo inapokuja dhana ya exposure kwenye matukio.

  ReplyDelete
 2. Chib,

  hao wamarekani ni matokeo ya kuwa na kila kitu. wanafika mahali hawaoni maana ya maisha wanaamua kulewa, bangi, ngono, mirungi n hata kujiua.

  ReplyDelete
 3. nimefikiri sana hata nimeumiza bichwa langu. nimeona kweli watoto wa kimarekani wana akili kuliko watoto wa kiafrika, hasa hasa kuliko watoto wa tanzania. ukitaka uthibitishe hilo tazama baba zao na mama zao je wana akili kuliko baba na mama wa watoto wa kiafrika. baba wa watoto wa kimarekani hawatumii madaraka vibaya kama baba wa wenzao wa afrika. wakipata madaraka wanakaa miaka mi4 au mi8 basi sio kama waina gadafi, mugabe na museveni.

  labda tuondoe mauozo kama haya tutaweza kuwawekea watoto wetu maabara, kompyuta, usafiri wa kwenda shuleni wa uhakika. watapata walimu ambao hawafundishi rasharasha darasani ili wapate darasa lingine la twisheni. pengine watapata msosi shuleni, japo mchana tu.

  ReplyDelete
 4. Najaribu kuwa makini kuchora mstari utenganishao akili na fikra kulingana na muda, mazingira na manufaa.
  Nadhani mtoto wa kimarekani ukimuweka na mtoto wa kiBarbaig kwenye msitu utagundua kuwa hana akili. Ila ukimuweka na mtu mzima wa Rubafu ama Nanjilinji ama pale kwa bibi yake Prof Matondo ataonekana ana akili.
  Najitahidi kufikiri kama akili ni kitu tunachowekewa ama tunachokichaji. Nadhani ni kama betri ya gari. Ukiichaji itaendelea kutoa umeme unaohitaji. Kama mfumo wa gari unavyotumia betri huku ukilichaji, ndivyo ilivyo hata kwa watoto wenye kila kitu. Wanapambana na maisha huku wakiwa na nyenzo za kuwasaidia kupambana nayo. Kwa hiyo naamini tunaweza kuwa na akili sawa ama zinazotofautiana kidogo kuliko tunavyoamini, lakini UWEZESHWAJI WA KUZICHAJI ndio unaotufanya tuonekane mazodobwa.
  Rejea maandishi yangu kuhusu ELIMU YETU YA UKARABATI hapa http://changamotoyetu.blogspot.com/2009/05/tanzania-yangu-na-elimu-ya-ukarabati.html

  ReplyDelete
 5. kijana wa Changamoto uko sawa kabisa.

  mtoto wa kihaya analima musiri wa bitakuli au biliibwa na kulisha familia na wakimarekani hawezi. huu ndio umuhimu wa blogu, kufundishana na kuelimishana mpaka baaasi

  hata mimi ninaakili kuliko mmarekani nikiwa bongo. akina matondo wanashangaa kwa sababu wako ugenini na wanabeba ya ugenini na kuyaleta yalivyo bongo. twaweza tusihitaji sana vya ugenini kwa sababu tumekamilika katika sisi

  ReplyDelete
 6. Huyo au hao waliofanya *utafiti* (nataka kujua variables na standards under equal conditions) na kuketi kitako na kukubaliana kuwa watoto wa Kiafrika hawana akili kama wengine, ni WAJINGA wa kwanza yaani STUPD and IDIOTS! That's all I can conclude, nina vigezo vya kuzingatia ambavyo ningekutana nao, ningewauliza walivitumiaje.
  Wende kwenye blogu za Mjengwa na Fransis na Gideon waone madarasa na vifaa vya shule kisha wafike na kuona hali halisi wanayofundishiwa watoto wa Tanzania ndipo walinganishe na kwao wanaochagua hata kitabu cha Raisi gani kisomwe shuleni na kingine kisisomwe.
  Ukicheza na haya majitu yenye fikra skewed yatakujaza maupumbavu kuwa, mwafika fulani na fulani na wewe na huyu na yule ni exception vile vile mmepata exposure, yanajikanganya yenyewe yanashindwa kujua kuwa hiyo exposure yanayozungumzia ndiyo inayotofautisha watoto wa kwetu na wa kwao, yananishangaza yanaposema you are unique wakati nimekua na kusoma na kujifunza na hao hao ambao wao wanawaona hawana akili, nakwambia wapo wenye akili hao wakipata nafasi wangewapita kama Buffallo inavyopita daladala ya Mlandizi.
  Ni wajinga kabisa kabisa kabisa hao, laiti huu utafiti ungeonesha kuwa akili zao ni ugali, wasingethubutu hata kutamka kuwa kuna utafiti umefanywa.
  Jinga kabisa kabisa hao natamani niyazabue vibao!

  ReplyDelete
 7. Asanteni sana kwa maoni haya ya kuchangamsha. Nilichokuwa nakizungumzia hapa hasa ni hii elimu ya Kimagharibi - hii tunayokaririshana mashuleni - Newton's Laws of motion, sijui dunia inazunguka kutoka huku kwenda huku, atomic number ya uranium ni, kokotoa kipeo cha ...na pointi yangu kubwa ilikuwa ni kuangazia baadhi ya vipingamizi tulivyonavyo katika mfumo wetu wa elimu hii hii ya Kimagharibi na hasa suala la lugha ya kufundishia. Ninajua kwamba kila mtu ni "msomi" katika mazingira yake na mimi naamini kwamba usomi huu ndiyo bora kabisa kuliko huu wa kukariri "Newton's Laws of Motion" kikasuku na hili nimeshalisema mara nyingi sana. Kwa hivyo haishangazi kwamba "mtoto wa Kihaya analima musiri wa bitakuli au biliibwa na kulisha familia na Wakimarekani hawezi" kwani mazingira na uzoefu wake unamwezesha kufanya hivyo. Je, vipi katika darasa la elimu ya Kimagharibi? Ni nini kinachomfanya mwanafunzi wa darasa la pili wa Kimarekani afafanue dhana zote hizi nilizozirejerea na Mwanafunzi wa darasa la pili na hata sekondari wa nyumbani asiweze? Maoni yangu kama mwanaisimu (Linguist) ni lugha ya kufundishia. Kwa hivyo lengo langu halikuwa kuonyesha kijumla kwamba eti vya wageni ndivyo bora zaidi kuliko vyetu, kuvileta vya nje kama vilivyo au kwamba eti wazungu ndiyo wana akili kuliko sisi. Nitamtazama kwa jicho la hatihati sana mtu atakayeleta dai kama hili.

  Tatizo lililopo ni kwamba watu wengine hawaheshimu "usomi" wa wenzao na hii ndiyo ilisababisha bara la Afrika kuitwa bara la giza wakati kama Wazungu wangemtazama Mwafrika kwa jicho pana basi wangegundua kwamba pengine alikuwa "msomi" na mwerevu mno katika mazingira yake kuliko wao.

  Mzee wa Changamoto - nimesoma makala yako na inagusa kiini kabisa cha tatizo lenyewe. Tuko pamoja. Dada Subi - naona umewapa vidonge vyao watafiti hawa. Nadhani utafiti huo ulifanywa na UNICEF na ulirejerewa na mwanaisimu mmoja wa Afrika Kusini ambaye alikuwa anadai kwamba kama kuna ukweli wo wote katika dai kwamba eti watoto wa Kiafrika ni "slow" linapokuja suala la kujifunza ELIMU YA KIMAGHARIBI madarasani basi ni kwa sababu ya tofauti ya lugha za kufundishia. Watoto karibu katika dunia nzima wanafundishwa kwa lugha yao wenyewe isipokuwa watoto wa Kiafrika ambao wanahangaika na lugha wasizozifahamu. Kwa hivyo siyo jambo la kushangaza kama wataonekana kushindwa kuelezea maana na faida za Newton's Laws of Motion kwa maneno yao wenyewe kwani lugha kwao ni kipingamizi. Nikiupata utafiti huu nitakutumia. Asanteni nyote na tuendeleeni kuelimishana!

  ReplyDelete
 8. Elimu muafaka kabisa. Mwaipopo umenichekesha sana. Subi hoja yako ni muhimu sana. Nakubaliana na wewe. Huwezi kuzungumzia utafiti ambazo vigezo linganishi havipo.

  Ndio maana mimi hupata shida kuamini hizi zinazoitwa tafiti za kisayansi ambazo mtu anaweza kuhitimisha ujinga wake kwa matumizi ya data na watu tukaogopa kuzihoji. Kumbe ni ujinga flani tu wenye jina la "utafiti".

  ReplyDelete
 9. Bwaya, ndiyo utafiti wo wote ulioandaliwa vyema ni tukio la kisayansi na ni lazima ufuate kanuni maalumu za uhakikifu, uangavu na uamilifu. Kwa mfano matokeo yake ni lazima yawe yale yale hata kama yakifanywa na mtafiti mwingine. Hata hivyo ni wazi kwamba tafiti nyingi hasa zinazohusu tabia za binadamu na maisha yao zinaweza kuathiriwa na mazingira kiasi kwamba athari hizi zinaweza kuonekana hata katika matokeo yake. Hii ndiyo sababu tafiti nyingi za aina hii zinazofanyika Ulaya zinaweza zisiwe na matokeo yale yale zinapoletwa katika mazingira ya Kiafrika. Kabla sijauita utafiti wo wote wa kijinga mimi ninayo tabia ya kuangalia kwanza taratibu zilizofuatwa kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa utafiti huo - na kama matokeo hayo (kama yanaweza kuwa jumuishi) yanaweza kuradidiwa katika tamaduni tofauti tofauti. Utafiti huu ninaouzungumzia hapa (kwa bahati mbaya sijaupata) nadhani ulikuwa ni utafiti rahisi tu uliohusu "reaction time" katika kujibu maswali mbalimbali kati ya watoto wa Ulaya na wale wa Afrika. Wanafunzi hawa waliulizwa maswali mbalimbali "ya kawaida" katika kiwango chao cha elimu na muda waliouchukua mpaka kutoa jibu ulipimwa - na kama majibu hayo yalikuwa sahihi ama la! Sijui yalikuwa ni maswali ya aina gani, yalichaguliwaje pamoja na wahusika walichaguliwaje lakini wanafunzi waliohusika ni wa Uingereza na Afrika Kusini - katika madarasa sawa. Nchi zote hizi zinatumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia. Hitimisho la watafiti lilionyesha kwamba wanafunzi wa Uingereza walikuwa "sharp" katika kujibu maswali, walijibu maswali mengi zaidi kwa usahihi na majibu yao yalikuwa ya kina zaidi. Watafiti walikuwa ni wanaisimu jamii na walisema kwamba matokeo kama haya hayashangazi kwani pengine matokeo haya yanaweza kuelezwa na ukweli kwamba wanafunzi wa Uingereza Kiingereza ni lugha yao ya kwanza na wanakifahamu vizuri kinyume na wenzao wa Afrika Kusini. Kwa vile wanafunzi hujifunza vizuri zaidi kwa lugha wanayoielewa vizuri basi matokeo ya utafiti huu yanategemewa kuwa kama yalivyo na kusema kweli yangeshangaza kama yangekuwa kinyume chake. Je, vipi kama tungefanya utafiti ule ule lakini safari hii tuchukue wanafunzi wa Uingereza ambao wanafahamu Kiswahili vizuri na wanafunzi wa Tanzania halafu tuwaulize maswali yale yale kwa Kiswahili. Nani angekuwa "sharp" safari hii? Ni nani angetoa majibu sahihi kwa wingi? Nani angetoa majibu ya kina zaidi?

  Hawa wanafunzi wa darasa la tatu niliojitolea kuwafundisha wanafahamu mambo mengi mno - mambo ambayo kule nyumbani hata wanafunzi wa shule za sekondari wanaweza wakatatanishwa nayo au wakashindwa kuyatolea majibu ya kina. Na pamoja na mazingira tofauti yaliyopo (hapa wakijifunza volkeno ni lazima watengeneze volkeno zao wenyewe kama mradi halafu waje waeleze darasani lava inakotoka na kwa nini ina joto) naamini pia suala la lugha ya kufundishia ni muhimu.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU