NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, September 28, 2009

HIKI CHOO KIMENIKUMBUSHA MBALI SANA - FUNZO KWA WATUNGA SERA

Kwa wale ambao mmekulia mijini pengine hamjawahi kutumia choo kama hiki. Lakini kwa wale waliokulia mijini, choo kama hiki ni cha kawaida sana na mpaka leo ukienda vijijini vyoo vya aina hii bado utaviona!

Nakumbuka katikati ya miaka ya 80 kulikuwa na kipindupindu kijijini kwetu na serikali iliamru kila familia kuchimba choo pamoja na kuchemsha maji ya kunywa. Kila siku ungewaona vijana wa mgambo wakizunguka kila kaya kukagua kama kulikuwa na choo na kama maji ya kunywa yalikuwa yanachemshwa.

Ambacho wanamgambo hawa hawakukijua ni kwamba watu walitii amri ya serikali na kuchimba vyoo lakini walikuwa hawavitumii, na walikuwa wanachemsha maji ya kunywa na kuyaweka katika mtungi mkubwa sana kwa ajili ya kuwaonyesha wanamgambo hawa wakija lakini maji haya walikuwa hawayanywi. Wakati ule sikuelewa ni kwa nini wakati kweli kipindupindu kilikuwepo na kilikuwa kinaua watu.

Baadaye niligundua kwamba kulikuwa na tatizo: watu walikuwa hawaamini kwamba kipindupindu kilikuwa kinasababishwa na kunywa maji machafu bali ushirikina. Eti watu walikuwa wanarogana na kusingizia kipindupindu. Kwa mantiki hii, watu hawakuona sababu ya kunywa maji yaliyochemshwa (ambayo walidai hayana ladha nzuri kama yale ambayo hayakuchemshwa) na kutumia vyoo (ambavyo walidai vinanuka sana) wakati wanajua kwamba haisaidii cho chote katika kuzuia kipindupindu.

Serikali nayo kwa upande wake haikuchukua hatua yo yote kuwaelewesha watu kwa kina kuhusu visababishi, kinga na tiba ya kipindupindu. Yenyewe iliweka amri tu ya kuchimba vyoo na kuchemsha maji ya kunywa ikidhani kwamba watu hawa wa kijijini "wasiofahamu" cho chote wangetenda kama walivyoambiwa. Mpaka leo, sera nyingi (hata ziwe nzuri namna gani) zinashindwa kwa sababu zimepandikizwa tu kwa walengwa wake - hasa walengwa hao wakiwa ni watu wa kijijini ambao inasadikiwa na kuaminika kwamba ni watu ambao wanastahili kuambiwa na kuelekezwa nini cha kufanya. Sera nyingi za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali zingepata mafanikio mno kama zingejipa muda wa kuwaelewa walengwa wake - zikajibidisha sana kujumuisha maoni, maarifa na uzoefu wao katika uandaaji na upangaji wa sera hizo. Bila kufanya hivi, tutaendelea kucheza katika mduara usio na fundo huku tukiwalaumu watu wa kijijini kuwa ni "wajinga", wasio na elimu, wasiostaarabika, wasiosaidika wakati ukiangalia na kuchunguza vyema - pengine watunga sera, "wasomi" na mabingwa wa kuelekeza ndiyo wajinga!

Picha ni kutoka kwa Mjengwa

6 comments:

 1. Umenikumbusha mbali kweli. Maana si muda mrefu nimekuwa natumia choo kama hiyo pia bafu maisha bwana tumetoka mbali. Asante sana

  ReplyDelete
 2. Hapo umenena saaana mkubwa...hali kama hiyo ilipatikana Mbeya ambapo walichimba kisima katikati ya kijiji ili kusaidia wadada na wamama wasitembee muda mrefu kufuata maji. Lakini baada ya mwezi kile kisima kiling'olewa pampu kisha kusokomeza changa na mawe na matokeo yake hakukuwa na maji.

  Wafazili wakaleta mutu ya Gender kutafuta sababu na akaambiwa kuwa hicho kisima hakikuharibiwa na wababa bali na wamama ambao walikuwa wanabanwa saaaana kuchota maji hapo kwa kuwa wamepunguziwa muda wa umbeya, udaku, kusutana, kuzodoana, mishemishe n.k. wanapokwenda kuteka maji....lol!

  social work ni ngumu? zavali hata kuwa daktari kama nanihiiino...lol!

  ReplyDelete
 3. nakuunga mkono profesa huwezi kuwahubiri wamaasai kama hujui kimasai, huwezi kuyajua maandiko kama huyasomi kwa undani, vivyo hivyo huwezi kuujua umaskini wa mtanzania mpaka uje alipo, sera ni kihamasisho cha mkakati, kutunga sera bila kuwa na uelewa wa watungiwa sera ni ubabaishaji wa makusudi unaotakiwa kupingwa kwa nguvu zote, kwani ndio zao la kushindwa kwa sera nyingi . asante sana profesa.

  ReplyDelete
 4. Heshima kwako Kaka.
  Kuna mengi saana ya kunukuu hapa. Ni kama umeandika SUMMARY tu hapa kwani kila kitu ni kwa ufupi na kwa uhakika. Lakini kwa wajua napenda nukuu, ntakwenda na hii kwa leo. "Serikali nayo kwa upande wake haikuchukua hatua yo yote kuwaelewesha watu kwa kina kuhusu visababishi, kinga na tiba ya kipindupindu."
  Basi hapa naona KIPINDUPINDU chawakilisha karibu kila maamuzi yafanywayo na serikali kwetu.
  Yaani hawatuchanganulii kuhusu ZIARA za Rais Kikwete japo tunaweza kuhisi kuwa zina mamufaa. Lakini manufaa ni ya nani na ni kwanini mwenye kunufaika asiambiwe anavyonufaika? Serikali imesahau mwajiri wake ni nani na inampuuza. Inarejea kwenye HESABU ZA KISIASA na kuwadharau wale ambao ndio wengi. Serikali inaonekana kuwajali asilimia chache wenye kipato na kama ulivyosema kuwa "Mpaka leo, sera nyingi (hata ziwe nzuri namna gani) zinashindwa kwa sababu zimepandikizwa tu kwa walengwa wake - hasa walengwa hao wakiwa ni watu wa kijijini ambao inasadikiwa na kuaminika kwamba ni watu ambao wanastahili kuambiwa na kuelekezwa nini cha kufanya."
  Nadhani kama kuna kitu ambacho SERIKALI YA RAIS KIKWETE IMESHINDWA, basi ni kujiweka karibu na wananchi
  Tanzania yangu, yenye watawala wajiitao viongozi

  ReplyDelete
 5. nikienda kijijini ntatumia choo kama hiki, no water bills here

  ReplyDelete
 6. Yasinta - ni kweli. Lakini mimi sioni ubaya wo wote kutumia choo cha aina hii kwani kama alivyosema Kamala kusema kweli hakina usumbufu wo wote. Hakuna cha ati leo maji hakuna, sinki limeharibika...Hivi ndivyo vyoo hasa vya Mtanzania wa kawaida kule vijijini na hiki nimekipenda zaidi kwa sababu hakijafunikwa na hewa inazunguka bila wasiwasi na hivyo hakina harufu sana. Mzee wa Changamoto - asante kwa kupanua mawanda.

  Chacha - huo mfano wa akina mama wa Mbeya umenifurahisha. Na kama mtu huna akili pana basi unaweza kuondoka ukisema kwamba watu hawa ni wapumbavu na hawajastaarabika kama walivyofanya Wazungu. Kumbe kama ungekaa na kuongea na akina mama hawa na kujua hasa maoni yao kuhusu kisima hicho pengine usingeishia kupoteza pesa zako kukichimba - au ungekichimba sehemu ambayo wanataka wao. Bwana Tandasi - kama nilivyosema - hata uwe na sera nzuri namna gani bila kuwashirikisha walengwa - ni kazi bure. Sijui serikali na hawa watu wa NGO watautambua lini ukweli huu.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU