NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, September 22, 2009

SERA YA ELIMU AU SERA YA LUGHA? - NA PROFESA CHARLES BWENGE

Hapa chini ni makala nzuri ya Profesa Charles Bwenge kuhusiana na sera mpya ya lugha ya kufundishia katika shule za Tanzania, sera ambayo imetilia mkazo Kiingereza kutumiwa kama lugha ya kufundishia kuanzia darasa la kwanza. Makala hii ilichapwa katika gazeti la Kwanza Jamii la tarehe 15/9/2009.

Sera ya Elimu au Sera ya Lugha?

Na Profesa Charles Bwenge

NI ukweli usiopingika kwamba lugha ndio nyenzo kuu ya kufundishia na kujifunzia. Walimu hutumia lugha kufundisha kile walichokusudia na wanafunzi hupata maarifa wanayotafuta kwa kusikiliza kinachosemwa na mwalimu au kusoma kilichoandikwa vitabuni au mitandaoni. Maktaba huhifadhi vitabu. Kitabu hakiwezi kuwa kitabu kama hakuna lugha. Kwa hivyo, huwa ni vigumu kuweka kando suala la elimu unapozungumzia au kuunda sera ya elimu. Pamoja na hayo, ukweli unabaki pale pale kuwa lugha sio elimu. Unaweza kuwa na sera ya lugha bila kuihusisha na elimu. Kwa mfano hapa kwetu tuna wizara ya elimu lakini si wizara ya lugha. Hii ina maana, elimu ni kitu kipana zaidi ya lugha. Lugha ni nyezo, bila shaka nyenzo muhimu katika mchakato wa kuelimisha na kujielimisha au kuelimishana.

Kwa bahati mbaya, uhusiano huu kati ya elimu na lugha haueleweki vizuri kwa watu wote. Kutoeleweka kwake vizuri katika jamii yetu kumepelekea watu wengi kujenga fikira potofu kwamba kiwango fulani cha ujuzi wa lugha fulani ni kielelezo cha kiwango fulani cha elimu. Kutokana na mtazamo na historia ya ukoloni ambapo kila kilichokuwa cha asili ya Ulaya ndicho kielelezo cha ‘ustaraabu’ na kila kilichokuwa cha asili ya Afrika ni kielelezo cha ‘ushenzi’, tulifanywa kujichukia na kuchukia vitu vyenye asili ya Afrika na kuenzi vitu vya wazungu. Lugha ilikuwa na inaendelea kuwa mojawapo ya ‘kasumba’ hii.

Waingereza walipotutawala walikuja na lugha yao ya Kiingereza na kuifanya kuwa lugha yenye hadhi ya juu kuliko lugha zote zilizokuwa zikizungumzwa hapa kwetu. Ilifanywa kuwa lugha ya kufundishia hususan katika elimu ya kati na ya juu. Na kwa vile lengo halikuwa kuwapatia watu wote elimu hiyo, wale wachache waliobahatika kuipata ndio wakawa pia wanaomudu Kiingereza. Zaidi ya hapo, elimu yenyewe ilikuwa ni kuwawezesha wakoloni kutawala na kuchuma bila shida.

Kuanzia wakati huo kiwango cha kumudu Kiingereza kikawa ndio kipimo cha kiwango cha elimu. Kwa Mtanzania, kila anayemudu Kiingereza , au ambaye mayai yanapanda chambilecho vijana wa mitaani, basi huyo ameelimika. Asiyejua Kiingereza huyo hana kitu! Sio tu kwamba tumefikia ambapo Mmarekani ambaye hajaenda hata shule lakini anazungumza Kiingereza kwa sababu ni lugha yake mama anaweza kuja hapa akapewa umeneja wa Tanesco kwa vile ‘amesoma sana’, bali pia kila tunapokuwa na mjadala wa kuhusu sera ya elimu tunaishia kujadili lugha tu kana kwamba lugha ni sawasawa na elimu.

Mjadala juu ya elimu na lugha nchini mwetu umekuwepo tokea tupate uhuru na unaendelea kuwepo. Lakini kila unapoibuka, tunajikuta tunajadili tu ni lugha ipi kati ya Kiswahili na Kiingereza inafaa kufundishia kiwango kipi cha elimu.

Mjadala wa lugha umekuwepo kwa sababu lugha hizi mbili ambazo ninaweza kuziita lugha dada zimekuwepo na sisi wenyewe kuendelea kuzishindanisha kwa sababu zisizokuwa za msingi. Wiki ya jana gazeti la The Guardian toleo la mtandaoni la tarehe 9 Septemba 2009 limeripoti kuwa katika pendekezo la sera mpya ya elimu serikali inasisitiza umuhimu wa kutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia katika elimu ya msingi. Na sababu za msisitizo huu ni kwamba matumizi ya Kiingereza yameongezeka kutokana na utandawazi. Kama habari hii ni kweli, basi utandawazi umegeuka kuwa utandumazi, yaani unatudumaza.

Tumerejea pale pale, kiwango cha elimu kinapimwa kwa kiwango cha Kiingereza. Wataalamu wa masuala ya elimu wa hapa kwetu na kwingineko walikwishaweka wazi suala la matumizi ya lugha na kiwango cha elimu. Wanafunzi wanapofundishwa au kujifunza kwa kutumia lugha ya ‘kienyeji ‘ ni rahisi kujenga ubunifu na ugunduzi kuliko wanapotumia lugha ya ‘kigeni’. Ushahidi juu ya hoja hii uko wazi. Nchi zote zinazoitwa ‘nchi zilizoendelea (kiviwanda na kiteknolojia)’ na hivyo ndio nchi tajiri zote zinatumia lugha zao za kienyeji katika elimu kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu. Kwa mfano, zile nchi za G8 na lugha zao za kienyeji katika mabano: Marekani, Uingereza na Canada(Kiingereza), Japan (Kijapani), Ufaransa (Kifaransa), Italia (Kiitaliano), Ujerumani (Kijerumani), na Urusi (Kirusi). Nchi zinazoibukia kwa kasi kama China inatumia Kichina. Kwao wanapofikiria kuboresha viwango vya elimu hawapotezi muda kujadili lugha ipi, bali wanajadili mbinu na mazingira ya kuongeza ubunifu na ugunduzi.

Hata hivyo, kwa zile nchi ambazo Kiingereza si lugha yao ya kienyeji zinatambua, kama nasi tunavyotambua, kuwa Kiingereza ni lugha iliyotokea kujipambanua kama lugha ya mawasiliano mapana duniani kote. Hili halipingiki. Na mintaarafu utambuzi huo, wamejumuisha mikakati mizuri katika sera ya elimu ya kufundisha Kiingereza katika viwango vya ubora kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu.

Kiingereza kinavundishwa kwa nguvu zote. Kwa mfano, ukiwakutanisha vijana wawili waliomaliza madarasa kumi na mawili mmoja kutoka Japan na mwingine kutoka Tanzania (tena ambaye amepitia akademi), Mjapani zaidi ya huo ‘uchawi ‘ wa koampyuta alio nao ambao aliupata kupitia Kijapani atakuwa anaongea Kiingereza safi tena chenye lafudhi kama ya wenyeji! Ni kwa nini? Kwa sababu sera yao ya elimu ni kuelimisha jamii na papo hapo bila kusahau kuwa hawaishi kisiwani – lugha ya dunia inafundishwa vizuri.

Sisi kwa sera zetu mbovu za elimu tunakosa vyote viwili – ubunifu na ugunduzi ni zero na hiyo lugha ya watu tunayong’ang’ania kiasi cha kutaka iwe ya kufundishia nayo ni zero. Wajibu wa Wizara ya elimu ni kupanga sera itakayowezesha wanajamii kupata elimu bora, elimu inayojenga ubunifu, utundu, na ugunduzi katika kila afanyacho binadamu. Si wajibu wa Wizara ya elimu kuwa wakala wa kupalilia kasumba ya kibeberu kwamba kufundishia kwa Kiingereza ndio kutafanya Watanzania wawe watandawazi. Mimi nilifikiri tumeishapita mitego hiyo ya kijinga. Lugha yetu ya kienyeji, Kiswahili, tunayo na inafaa kabisa kufundishia elimu ya kiwango cho chote kama tungeamua hata leo hii. Kwa kutumia Kiswahili tutawezesha vijana kuelimika. Katika sera yetu ya elimu bora hatutathubutu kuacha Kiingereza nje. Tutafanya kama Wajapani na Wachina wanavyofanya, yaani kuwa na mikakati mathubuti ya kufundisha Kiingereza kama lugha ya Kigeni.

Mtu anaposema tutumie Kiingereza kama lugha ya kufundishia, anataka kutwambia kwetu hapa Kiingereza ni kama lugha ya kienyeji ambavyo ukweli ni kwamba ni lugha ya kigeni na itaendelea kuwa lugha ya kigeni. Kamwe huwezi kutumia lugha ya kigeni kufundishia na ukatarajia kupata watu walioelimika. Hata kama ungekuwa na walimu wanaoimudu lugha hiyo ya kigeni wa kuweza kufundisha shule zote za msingi, kwa mfano, hutaishia kudumaza uwezo wa vijana wa kubuni na kugundua. Mathalani, watoto wa vijijini na hata wa mijini katika familia nyingi watakwenda darasani na kufundishwa kila kitu katika hicho kimombo, lakini wakiwa njiani kurejea majumbani na wakiisharejea dunia yote iliyowazunguka wanaiona, wanaisikia, wanainusa, na hata kuihisi katika Kiswahili.

Hali kama hii itawadumaza zaidi kuliko hata hiyo bora elimu inayotolewa kwa sasa kwa kutumia Kiswahili. Mwalimu Nyerere alipobuni ‘elimu ya kujitegemea’ kama nyenzo ya kujenga uchumi wa kijamaa na kujitegemea hili alikuwa ameliona na ndio maana ilikubaliwa kuwa Kiswahili ndio ilikuwa lugha muafaka ya kutolea elimu hiyo. Elimu ya kujitegemea ilikuwa na maana pana na ya ndani kuliko baadhi ya watendaji wake walivyoitafsiri. Kiini chake ilikuwa ni kujenga ubunifu na ugunduzi ili taifa hili hatimaye liweze kufikia kujitegemea. Nani asiyependa kujitegemea. Mabepari waliipiga rungu hiyo Sera ya elimu ya kujitegemea pamoja na mzazi wake, itikadi ya ujamaa na kujitegemea - na leo hii sio tu kwamba tunajivunia kuwa mabingwa wa dunia wa kuomba misaada, bali pia tunaona ni haki yetu kusaidiwa na tunapanga hata hizo chembe ndogo tulizokuwa tunazipata kutokana na kutumia lugha yetu nazo zitoweke.

Kwa kupendekeza kutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia katika mfumo wote wa elimu ni fikira potofu na ni sawa na kuangalia puani, yaani leo tu na kusahau kesho na kesho kutwa.
Kiswahili kilikuwepo kabla ya mkoloni aliyetuletea Kiingereza, na kiliendelea kuwepo hata baada ya mkoloni kuondoka na kurithiwa na mkoloni mamboleo, na kimeendelea kuwepo hata baada ya ukoloni mamboleo kukabidhi mwenge kwa utandawazi. Kwa mantiki hiyo, hata utandawazi wakati wake utafika na utapisha itikadi nyingine ambayo hatujui kama itakuja na Kiingereza au Kichina.
Lakini ukweli ni kwamba Kiswahili kitaendelea kuwepo. Kitaendelea kuwepo kwa sababu ni lugha ya kienyeji. Na kwa hoja hii, kama tunafanya uamuzi wa busara na unaoangalia mbele katika vizazi vijavyo, Kiswahili ndio lugha inayofaa kufundishia kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu. Na lugha yo yote ya kigeni ambayo inakuwa imeshika hatamu ya zama husika ifundishwe vizuri sana katika ngazi zote za elimu.

Kwa zama za leo Kiingereza ndio kimeshika hatamu na hatuna budi kukifundisha vizuri sana. Tushughulikie sera ya elimu itakayotoa elimu bora na ninaamini kuwa ubunifu na ugunduzi miongoni mwa vijana wetu utabakia ndoto tu kama tutaendelea na huu ung’ang’anizi wa kutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia. Tusikubali utandawazi kutudumaza.

2 comments:

  1. Asante sana kwa makala yako nzuri nimesoma na nimejifunza na pia kugundua siri ya umaskini wa mtanzania ni nini, watunzi wa sera ya elimu wanashindwa kutofautisha kati ya elimu na lugha kipi kitoe tafsiri ya chenzake, lugha ya kiingereza imetufanya kuwa maskini wa fikra na mawazo endelevu. kiswahili kidumu daima

    ReplyDelete
  2. Asante sana kwa mawazo yako mema kuhusu lugha yetu tunayoienzi.Mola akujalie mema.

    ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU