NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, September 23, 2009

WAMAREKANI NA SERA YAO YA MICHEZO - MFANO KUTOKA CHUO KIKUU CHA FLORIDA

Jumamosi ya wiki jana (tarehe 19/9/2009) kulikuwa na mechi ya "mpira wa miguu" wa Kimarekani kati ya Chuo Kikuu cha Florida na Chuo Kikuu cha Tennessee. Mechi hiyo iliyochezewa hapa Chuo Kikuu cha Florida ilihudhuriwa na watazamaji wapatao laki moja (100,000) hivi. Kwa kawaida kunapokuwa na mechi za mpira wa miguu wa Kimarekani (ambao huchezwa kwa kutumia mikono) familia nzima husafiri hata umbali wa maili 500 kuja kushuhudia mpambano. Hii huambatana na kupika vyakula, kuchoma nyama na kunywa bia. Mwaka huu kuna msisimko wa aina yake kwani Chuo Kikuu cha Florida ndicho kilichukua ubingwa mwaka 2006, mwaka 2008 na mwaka huu timu yake inasemekana ndiyo timu bora kabisa hapa Marekani (gonga hapa). Inawezekanaje mechi ya chuo kikuu ihudhuriwe na watazamaji 100,000?

Wamarekani wana sera nzuri sana ya michezo. Kwao wachezaji huanza kuandaliwa mapema wakiwa katika shule za mwanzo mwanzo kabisa na mtoto anapofika High School tayari kipaji chake kinakuwa kimeshajulikana. Makocha wa vyuo vikuu wanakwenda kusaka wachezaji kutoka katika High School hizi. Makocha wa timu mbalimbali zinazoshiriki ligi za mashirika ya michezo kama National Basketball Association (NBA) na National Football League (NFL) nao huenda kutafuta wachezaji kutoka vyuo vikuu mbalimbali. Ni pale tu mchezaji anapokuwa na kipaji cha pekee (kama Kobe Bryant wa Los Angeles Lakers au Lebron James wa Clevelend Cavaliers) ndiyo anaweza kuruka ngazi ya chuo kikuu na kwenda moja kwa moja katika NBA. Sijui kama kwenye NFL inawezekana kuruka hatua ya kucheza katika chuo kikuu. Kwa hali hiyo wachezaji wao wote wanakuwa angalau wamepita chuo kikuu na wameanza kuandaliwa tangu wakiwa watoto. Hii inawawezesha kucheza michezo yao kisayansi na kuimudu kwa kipeo cha hali ya juu sana.

Hivi karibuni tumekuwa na Hashim Thabeet ambaye amefanikiwa kuingia NBA baada ya kupitia Chuo Kikuu cha Connecticut. Kama vile ambavyo Mzee wa Changamoto alihoji baada ya kukerwa na mapokezi makubwa aliyopatiwa Hashim (ikiwemo kukaribishwa Ikulu), Tanzania ilimfanyia nini ili kukikuza kipaji chake kabla hajaenda Marekani? Ni wazi kwamba tunao akina Thabeet wengi tu lakini je tunawaandaje? Tunasubiri kimiujizaujiza tu wacheze soka la mchangani halafu waibukie Yanga au Simba, wavume kwa miaka miwili mitatu hivi halafu wanafifia na kusahaulika. Wachezaji wa aina hii hata wakienda nje, inawawia vigumu kukubalika katika kiwango cha kimataifa kwani, mbali na matatizo ya tofauti za kitamaduni ikiwemo lugha, bado wanakuwa hawana zile "basics" za mchezo kama taaluma ya kisayansi. Vipaji vyao vinakuwa bado havijanolewa sawasawa. Kumbuka kwamba sisi bado tunategemea "mafundi" na "wazee" wa timu katika michezo.

Naamini kwamba tukiwa na sera nzuri ya michezo tunaweza kuwa na wachezaji wazuri wenye viwango vya kimataifa, wachezaji ambao mbali na kujipatia ajira bora kabisa, wataweza kutusaidia katika kulitangaza jina la nchi yetu na kuwa mfano bora kwa vijana wetu.

No comments:

Post a Comment

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU