NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, October 12, 2009

ATI, MAFISADI NAO NI BINADAMU?

Niliulizwa swali hili na mwanafunzi anayesomea shahada ya uzamifu (Ph.D) katika Anthropolojia. Mwanafunzi huyu anafanya utafiti wake katika Jamhuru ya Kidemokrasia ya Kongo na alipokuwa huko wakati wa kiangazi mwaka jana alipata bahati ya kutembelea Gbadolite – yaliyokuwa makao makuu na makazi ya aliyekuwa raisi wa Zaire marehemu Mobutu Sésé Seko Nkuku Ngbendu wa Za Banga (Tafsiri - The all-powerful warrior who, because of his endurance and inflexible will to win, will go from conquest to conquest, leaving fire in his wake).

Mwanafunzi huyu hakuelewa inawezekanaje mtu anatumia mamilioni ya dola za umma kujijengea makao makuu ya kifahari kama yale wakati watu wengi katika nchi yake hawana huduma za msingi kabisa kama chakula, maji, matibabu, elimu na usafiri? Aliendelea kudai kwamba watu kama Mobutu kimsingi siyo binadamu kwani, kwa maoni yake, hakuna binadamu ambaye anaweza kufanya yale aliyoyaona kule Kongo na akabakia kuitwa binadamu.

Alipoondoka nilibaki nikifiriki hasa sisi binadamu ni nani na nini hasa kinachotufanya tuitwe binadamu. Ati, wana hisia na utu gani akina “Mobutu” wetu (ambao ni wengi sana barani Afrika) ambao hawana ubinadamu na wanachojali ni kunenepesha matumbo yao – wakiwaibia watu masikini na kuwasikinisha kabisa bila kujali cho chote? Ni kweli watu hawa wana furaha, hisia za ridhiko, mafanikio na utu? Huwa wanafikiri nini wakiona watoto wanasomea chini tena katika majengo mabovu wakati pesa za kununulia madawati na kujengea majengo ya shule wamezificha katika akaunti zao za siri? Huwa wanajisikiaje watoto mamilioni wanapokufa na malaria wakati pesa za kununulia vyandarua na dawa za malaria wamezitumia kujengea majumba ya kifahari? Huwa wanajisikiaje wakiwaona akina mama wakitembea maili sita kwenda kutafuta maji wakati pesa zilizotengwa kwa shughuli hiyo wamezitumia kujinunulia maghari ya gharama kubwa na kupeleka watoto wao nje kusoma? Wanajisikiaje? Mafisadi wana ubinadamu wowote? Ati, mafisadi ni binadamu?

Kwa habari kuhusu Gbadolite soma hapa. Hata Mtume Onesmo N. Ndegi wa Living Water Center Makuti Kawe Dar es salaam haelewi kabisa!

1 comment:

  1. Hawa jamaa si binadamu hawa. Hawa ni wanyama na kama ni mimi wote natandika risasi. UFISADI UKOME JAMAA!!!!!!

    ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU