NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, October 9, 2009

ATM NYINGI NCHINI HAZIFAI - WAZIRI

Nchi nyingi za Kiafrika (ikiwemo Tanzania) ni madampo tu ya kutupia bidhaa zisizofaa (na za bandia) kutoka nchi za Kimagharibi na CHINA. Kuanzia vyakula, madawa, vipodozi na sasa ATM. Watu mpaka wanauza dawa za Maralia za bandia! Mpaka kondomu za bandia! Wanaoingiza bidhaa hizi hawajui kwamba ni mbovu? Kama wanajua ni kweli tumekuwa wakatili kiasi kwamba mtu unauza dawa za Malaria au kondomu za bandia huku unajua kabisa kwamba kwa kufanya hivyo unaweza kuwa unahatarisha maisha ya wenzako moja kwa moja? Mamlaka inayohusika na suala hili inafanya kazi gani?
============================================================

ATM NYINGI NCHINI HAZIFAI - WAZIRI

Na Richard MakoreNaibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Jeremiah Sumari.

Serikali imesema mashine nyingi za kutolea fedha benki (ATM), ni mbovu kwa kuwa huingizwa nchini kutoka nje baada ya kuonekana huko hazifai. Imesema hatua hiyo inasababisha kuwepo wimbi la watu kuiba fedha za wenzao kupitia mashine hizo bila wenyewe kujua.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Jeremiah Sumari, alipokuwa akijibu maswali ya wabunge katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi. Sumari alisema kuwepo kwa mashine hizo ni hatari kwa usalama wa fedha za wananchi.

Alifafanua kuwa kuna nchi moja ambayo hakuitaja iliwahi kuhamisha mashine zake zilizokuwa mbovu na kuzipeleka nchi nyingine na kwamba tukio hilo linaonyesha kuwa hata hapa nchini ziliingizwa. Alishazishauri benki kuchukua tahadhari ili kuepusha wimbi la wizi kupitia ATM.

Hivi karibuni, Jeshi la Polisi liliwakamata raia wawili wa Bulgaria kwa tuhuma za kuiba kiasi cha Sh. milioni 70 jijini Dar es Salaam kupitia mashine hizo bila kutumia kadi. Wameufunguliwa mashitaka kortini.

Mbali na matukio ya wizi, baadhi ya ATM zimekuwa zikilalamikiwa na wateja wa benki kutokana na kuharibika mara kwa mara na wakati mwingine kutokuwa na mtandao, hivyo kuwasababishia usumbufu wa kutopata huduma.

Akizungumzia Benki ya Posta Tanzania ambayo serikali inamiliki asilimia 81 ya hisa, alikiri kuwa inahitajika sheria itakayoibadilisha kuwa kampuni ili iweze kufanya kazi kwa kushindana. Sumari alikuwa akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliokuwa wakijadili utendaji wa benki hiyo.

Uongozi wa benki hiyo uliwaeleza wabunge kuwa unakabiliwa tatizo la mtaji mdogo, jambo ambalo linawafanya washindwe kufikia malengo waliyojiwekea. Wakichangia katika kikao hicho baadhi ya wabunge walisema bila sheria kufanyiwa marekebisho itakuwa vigumu benki hiyo kuweza kufanikisha malengo yake.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Abdallah Kigoda, alishauri mabadiliko hayo yafanyike haraka na serikali iache kutumia neno "ipo kwenye mchakato" kwani hali hiyo inakatisha tamaa.

Alisema neno mchakato halina mwisho na halisemi ni lini kazi husika au itaanza kufanyika, kauli ambayo iliungwa mkono na wabunge wengi. Kwa upande wake mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed, alisema wananchi wamechoshwa na neno "mchakato" ambalo serikali inapenda kulitumia kwa kuwa halionyeshi ni lini itafanya kile inachokusudia kukifanya.

Aliishauri serikali kuuza hisa zake zote za Benki ya Posta na kujitoa katika biashara. Aidha, aliutaka uongozi wa Benki ya Posta kuacha kulalamika badala yake ufanye kazi kwa kushindana na watu wengine. Vikao vya kamati hiyo vinaendelea leo katika ofisi ndogo ya Bunge, jijini Dar es Salaam.

CHANZO: NIPASHE

3 comments:

 1. Nanukuu..."Serikali imesema mashine nyingi za kutolea fedha benki (ATM), ni mbovu kwa kuwa huingizwa nchini kutoka nje baada ya kuonekana huko hazifai"

  I love my government with ALL my heart!!! God Bless Tanzania.

  ReplyDelete
 2. Huu ni wendawazimu!! Sasa mtu unajua mashine zinazoingizwa nchini ni mbovu unaishia kusema wenye benki wawe waangalifu! Badala ya kuweka sheria kali ya kuingiza ATM ambayo itakuwa imeonekana inakidhi viwango vilivyowekwa. Jamani tuna mtindio wa .... au....

  ReplyDelete
 3. Mi nadhani pengine sisi Waafrika sijui tumerogwa? Mbona kila kitu chetu hovyo? Sasa hapa serikali tena bila aibu kabisa inasema eti ATM zinazoletwa ni zile zilizoharibika na kukataliwa huko zinakotoka. Sasa wananchi wafanye nini? Watengeneze za kwao au? Jamani, jamani, jamani mbona hivi lakini? Hata ATM - mamashine makubwa kabisa hatuwezi kujua kwamba hili ni zima au limeharibika???? Nakubaliana na Chib. Sisi ni WENDAWAZIMU au tuna mtindio wa...

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU