NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, October 22, 2009

HEBU TUKIRUHUSU KIZAZI KINACHOMALIZA MUDA WAKE KITUFUNDISHE KABLA HAKIJATOWEKA

Niliiona picha hii katika blogu ya Mjengwa na ikanikumbusha mama yangu mzazi. Ingawa yeye ni mzee sana lakini bado analima kishamba chake kidogo, anakwenda kutafuta kuni, kuchota maji kwenye kindoo chake, kuosha vyombo na kufanya kazi zingine kama kawaida. Ukimwambia akae apumzike basi mtagombana vibaya sana. Kipindi fulani nilijaribu kumleta Dar es salaam eti apumzike lakini haikuwezekana. Nilipomuuliza ni kwa nini alikuwa hataki kukaa mjini ambako kuna kitu jibu lake lilinishangaza. “Maisha gani haya ya kukaa tu bila kufanya kazi?

Jibu hili kidogo lilinishangaza kwani huyu ni mwanamke ambaye tangu nipate ufahamu wa kuelewa mambo sijawahi kumwona amepitisha siku bila kufanya kazi isipokuwa pengine akiwa mgonjwa – tena mgonjwa wa kweli kweli. Nilijaribu kutaka anieleze kulikuwa na ubaya gani kupumzika kidogo Dar es salaam baada ya miaka yote ile ya kufanya kazi. Jibu lake kwa swali hili lilinishangaza zaidi. Alidai kwamba akiacha kufanya kazi basi atakufa na sikujua kama alikuwa anatania ama la!

Tafiti mbalimbali zimeonyesha kwamba kufanya mazoezi mara kwa mara pengine ndiyo jambo la muhimu kuliko yote katika kulinda afya zetu pamoja na kuishi maisha marefu. Magonjwa mengi ya hatari kama vile magonjwa ya moyo, kisukari, shinikizo la damu, aina fulani za saratani na mengineyo yanachangiwa sana na maisha ya deko ambayo hatimaye huishia katika unene usiotakiwa. Nilishangaa kugundua kwamba mwanamke huyu mzee ambaye hakupata “bahati” ya kuingia katika darasa la kizungu na kusoma vitabu alikuwa analifahamu jambo hili vyema. Tulikubaliana na ilibidi “raha za mjini” nilizokuwa najaribu kumpa pale Dar es salaam nimpelekee kule kule kijijini kwake.

Mwaka 2001 alikuja huku Marekani kutembea na nilimpeleka kwa daktari kufanyiwa uchunguzi. Nilishangaa daktari alipowaita wenzake kuja kuona matokeo ya baadhi ya vipimo. Alituambia kwamba alikuwa hajawahi kuona mtu mzee namna ile ambaye alikuwa salama vile. Walipomuuliza alikuwa anakula chakula gani aliwajibu bila kusita “bugali”. Niliwafafanulia ugali ni nini na walishangaa kugundua kwamba ni wanga “carbohydrates” ambazo hapa Marekani kila mtaalamu wa lishe atakwambia usile. Ambacho hawakujua hawa madaktari ni kwamba huyu mwanamke mzee alikuwa anafanya kazi zaidi ya masaa matano kila siku tangu akiwa mtoto mdogo mpaka sasa. Tena chakula anachokula ni cha asili kabisa na hakina aina yo yote ya kemikali! Na kijijini kwetu kuna ajuza wengi ambao ni wazee zaidi kuliko mama na wako salama – hakuna dementia, hakuna Azheimer, hakuna saratani, hakuna kuvunjika mifupa hovyo hovyo, hakuna……

Je, kizazi cha sasa kinachoshinda kikitazama televisheni kitaweza kweli kuishi miaka mingi (bila magonjwa) kama kizazi hiki kinachomaliza muda wake? Kizazi cha sasa kinachokula vyakula vilivyobadilishwa na kujazwa kemikali na homoni za kila aina kitaweza kusafiri safari ndefu ya maisha kama hiki kinachomaliza muda wake? Hebu kizazi kipya na kijifunze yaliyo mema kutoka kizazi hiki kinachoaga kungaliko na muda bado.

5 comments:

 1. Kwa kweli inasikitisha sana kuona wazee wetu wanafanya kazi mpaka siku ya mwisho. Inawezekana ndio sababu wanazeeka kwa haraka zaidi. Ningependa kwa kweli wazee sasa wakae tu na kufaidi maisha yao ya uzeeni.

  ReplyDelete
 2. Yasinta - didn't bother to read the post and just ran to post a comment. Hawa wazee hawakubali kukaa tu bila kifanya kazi. I tried it myself too na kama wanatoka kijijini it is impossible for them to rest. Sasa wewe unasema tena eti wakae tu kufaidi maisha. When they work - inawasaidia kukeep their bodies in shape which is a scientific truth!

  ReplyDelete
 3. Kakangu Masangu.
  Kwanza niombe msamaha kwa kutobandika maoni katika kile niaminicho hapa. Niseme kuwa tumetoka kwenye kublog kwa ajili yetu na sasa twaitambulisha jamii kile kilichomo ndani mwao ambacho hakionekani machoni mwao. Kwa muda sasa nimesoma makala za MUHIMU SAAAANA humu lakini ile pilika uliyoona nimeikumbatia pale ilinikosesha muda kuacha maoni. LAKINI NAELIMIKA KILA UCHAO.
  Nianze kwa kusema kuwa kila aina ya maisha tuishiyo inatufaa sisi na tukiamua kushikilia upande uendanao na maisha yetu sasa, kuna manufaa makubwa. Watu wanazidi kuharibika na kudhoofika nyumbani kwa kuwa wanakimbia lililo jema kwa maisha na mazingira yao na kukimbilia mfumo usioendana nasi na ndio maana twaweza kufanya kama wafanyavyo wenzetu wa magharibi lakini madhara kwetu yakawa makubwa zaidi yao.
  Mfano:::Umesema kuhusu UGALI. Hiki ni chakula chema saana kwetu lakini ni kwa kuwa tunatumia nguvu nyingi inayozalishwa na chakula hicho, kwa hiyo tunafanya kazi bila kuhitaji nguvu ya ziada na mwili haubaki na nguvu ya ziada isiyotakiwa. Tumesha-balance vitu na hakuna kisukari hapo. Lakini tunapoamua sasa kuacha kazi, kuacha kutembea na kuendesha vyombo vya usafiri vitupavyo mazoezi (kama baiskeli) na kung'ang'ania gari kila tuendapo tukidhani ndio ufahari, sukari irundikwayo mwilini inatuua mapema.
  Haya yapo hata kwenye mambo ya uzazi ambako kukataa kuwa tuwavyo na kuendekeza maisha ya USASA ambayo hayaendani saana na mazingira yetu hutufanya tujipoteze. Ni kweli kuwa mtu akisikia kuwa chakula kikuu ni wali na ugali na unakula bila kipimo cha mzani anashangaa inawezekanaje ukawa hai mpaka sasa. Ni kwa kuwa twafanya mazoezi kila wakati (yaani mfumo wetu wa maisha ni mazoezi tosha).
  Na sasa wakati wenzetu wanahimiza mazoezi, wanahimiza kupunguza matumizi ya magari na kuhimiza mazoezi na kuendesha baiskeli kwenda kila uwezapo, sisi tunaendelea kujifaharisha na mwendo wa magari hata tuendapo gengeni.
  Kwa ufupi ni kuwa maisha ya zamani yaliishi kulingana na mazingira lakini cha sasa chataka kutengeneza mazingira yakubaliane nao. Na ndio maana kila wafanyacho sasa wanajitahidi "kuvunja rekodi" ambayo baadae inawavunja wao.
  Asante kwa tafakari nzuri kaka

  ReplyDelete
 4. kwa kweli watanzania wa kizazi kipya na hata watanzania wenye rika mbalimbali inabidi tujifunze kutoka kwa babu zetu na bibi zetu kama huyu hapa katika makala hii,watanzania walio wengi siku hizi kazi yao ni kukaa tu chini ya miti,kwenye mabaa,kandokando ya barabara nk kupanga mipango hewa ya kujipatia utajiri wa haraka pasipo kufanya kazi,kupanga mipango ya wizi,kudhurumu, na hata kuua ili mradi tu wapate pesa kwa njia za mkato..watanzania tufanye kazi na tuachane na mawazo ya utajiri wa haraka kazi ndio msingi wa maendeleo na hili linajulikana hata kwenye vitabu vitakatifu...

  ReplyDelete
 5. Mzee wa changamoto - sawa kwa uchambuzi mzuri. Nakubaliana nawe kabisa. Mitindo ya kimaisha ya Kimagharibi tunayoiiga haitupeleki kuzuri na tayari athari zake tumeshaanza kuziona - mfumuko wa saratani, kisukari na mengineyo.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU