NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, October 5, 2009

KWA NINI WANAUME (WA KISUKUMA) HUFARIKI MAPEMA SANA?

Ni ukweli karibu dunia nzima kwamba wanaume hufa mapema zaidi kuliko wanawake. Katika mataifa yaliyoendelea (ambako umri wa kuishi kwa wastani ni zaidi ya miaka 75) wanawake huishi kati ya miaka 5-10 zaidi ya wanaume. Na katika watu wenye umri wa miaka 100, asilimia 85 ni wanawake. Wanawake wa Japan ndiyo watu ambao huishi miaka mingi zaidi hapa duniani (wastani wa miaka 86.05!)

Nilikuwa nafikiria leo kuhusu jambo hili na nikakumbuka hali ilivyo kule Usukumani. Wanaume wa Kisukuma hufa mapema sana - pengine wakiwa na umri kati ya miaka 50-60 tu. Kijijini kwetu kule Bariadi (kwa Bwana Mapesa na Mzee wa vijisenti), kwa mfano, wazee wa kiume wote wameshafariki na mwanaume ambaye naweza kusema ni mzee kabisa pale kijijini pengine ana miaka 55 hivi au zaidi kidogo. Hali ni hiyo hiyo hata katika vijiji vya jirani ambavyo navifahamu vizuri. Hata watu wanapostaafu wanaogopa kurudi vijijini kwa kuhofia kufa mapema.

Kwa upande mwingine, viajuza ambavyo vimefiwa na waume zao zamani bado vipo vingi sana. Jambo la kusikitisha ni kwamba kwa kiasi fulani jambo hili limehusishwa na imani za kishirikina na watu wanaamini kwamba wanaume wengi pengine huuawa na wake zao watoto waliozaa pamoja wakikua. Matokeo yake ni kwamba viajuza hivi navyo huishia kushukiwa kuwa ni vichawi na hivyo kutengwa na jamii na wakati mwingine huishia kucharangwa mapanga. Mkoa wa Shinyanga ndiyo unaongoza kwa mauaji ya vikongwe kutokana na imani hizi za kishirikina.

Mikoa mingine na hasa vijijini hali ikoje? Kwa nini wanaume (wa Kisukuma) hufa mapema vile? Wanajamii mna maoni gani kuhusu suala hili?

5 comments:

 1. viajuza vya kihaya na kichaga vinaishi miaka mingi vikiwa na afya njema na labda kuliko wajapani na wachina.

  bibi mzaa babu kaishi zaidi ya miaka 120 akiwa na viungo vizuri na akitambua japo alikuwa hatembei.

  moja wapo ya sababu za kuuishi saana ni vyakula. mila za whaya na wachaga zinawazuia akina mama kula nyama, mayai na sumu nyinginezo.

  yawezekana wanaue wanapenda sana ngono pia. eti mila za wasukuma ktk misosi kwa upande wa wanawake zikoje?

  Go Vegeterian!!

  ReplyDelete
 2. Kamala - huyo bibi yako mzaa babu aliyeishi zaidi ya miaka 120 angekuwa Ulaya ungemsikia akitajwa kwenye Guinness Book of World Records.

  Kuna ushahidi wo wowote kwamba kupenda sana ngono kunawafanya wanaume wafe mapema? Isije ikawa wanaume nao wakawa kama nyuki - japo kwa polepole.

  Japo hakuna tofauti kubwa kati ya misosi ya wanaume na wanawake wa Kisukuma nadhani pengine ulaji wa misosi hii unachangia. Kusema kweli wanaume wengi wa Kisukuma (hapa tunazungumzia vijijini) hawafanyi kazi sana hasa wakati wa kiangazi. Kazi yao kubwa ni kwenda vilabuni kunywa pombe na kurudi nyumbani usikuwa wakiwa njwii - tena mara nyingi hata bila kupata lishe ya maana. Kwa upande mwingine wanawake ni lazima wajidamke saa 12 asubuhi kwenda kutafuta maji, warudi wakamue ng'mbe (ingawa kule Mwanza hii ni kazi ya vijana wa kiume), wapike chakula cha asubuhi, wakatafute kuni, waanze kuandaa chakula cha mchana na baadaye cha jioni na shughuli nyinginezo nyingi ndogo ndogo; na kwa kawaida wao hawanywi pombe wala kuvuta sigara - jambo ambalo kwa wanaume ni la kawaida. Pale kijijini kwetu kuna jamaa wachache sana ambao kabisa kabisa hawanywi pombe wala kuvuta tumbaku). Pengine kutokana na mtindo huu wa maisha wanawake hubakia kuwa "fit" zaidi kuliko wanaume ambao kutokana na kunywa pombe sana, kuvuta tumbaku kwa wingi ukijumlisha na ukweli kwamba hawana muda wa kupata lishe ya maana basi inakuwa rahisi zaidi kwao kupata magonjwa tatanishi na kufariki.

  Kuacha kula nyama hapo ni kasheshe. Mimi naamini kwamba nyama siyo mbaya ikiandaliwa vizuri na kuliwa mara chache chache. Tatizo ni kwamba watu wengi hawawezi kupitisha siku bila kula nyama. Eti mboga zinaliwa wakati mtu amechacha! Ni ukweli wa kisayansi kwamba watu wanaokula nyama kwa wingi (hasa "red meat") ndiyo wanaongoza kwa kupata aina mbalimbali za saratani. Utafiti makini uliofanywa kule Harvard ulionyesha kwamba kula nyama iliyoandaliwa vizuri (mf. kutokaangwa katika mafuta au kuunguzwa sana) mara moja moja hakuna madhara yo yote kiafya - na hapa tunaongelea "nyama za Ulaya" ambako ng'ombe, mbuzi, kondoo na kuku wanalishwa madawa wakue haraka na wengine wametokana na upandikizwaji wa bandia. Nyama iliyotokana na ng'ombe aliyezaliwa na kukulia usukumani au Umasaini akila majani ya kawaida sidhani kama ina madhara makubwa kama hizi nyama za huku Ulaya ambazo wakati mwingine mtu unakula wala huwezi kujua unakula nyama ya mnyama gani!

  Mimi pia ni mmojawapo wa watu ambao hawapendi kuzingatia kitu kimoja na kupuuza vitu vingine vyenye madhara yale yale na pengine hatari zaidi. Huwa nashangaa kwa mfano nikimwona mtu ambaye ameamua kuwa vegetarian ili kulinda afya yake na wakati huo huo akawa anavuta sigara, kunywa pombe na hata kuwa "kiwembe".

  ReplyDelete
 3. Prof. Hii ni topic muhimu sana natumaini itafungua macho wengi tukichangia. Sitaongelea wajomba jangu kule Misungwi ila nitaongelea wanaume kwa ujumla.

  Moja:Mie nafikiri kwa ujumla wanaume hawatunzi afya zao kama sisi wanawake. Kuna huu usemi kuwa mwanaume inabidi uwe "mgumu" hapo basi utakuta mwanaume anaumwa haendi hospitali,hamezi dawa,haendi kucheck,hafanyi lolote mpaka amekuwa hajiwezi kabisa,akiambiwa anasema wanawake huwa waoga basi tatizo alilonalo linazidi kukua.Wanaume wengine hata huwa wanasema huu ni ugonjwa wangu hivyo wanatulia tu, kwa maana hii kuwa mgumu au mkakamavu hata kama unaumwa ndio uanaume kitu ambacho ni tofauti na wanawake ambapo wakiumwa wanaenda hospital au kunywa mitishamba kwa kule vijijini au hata kupumzika. Nafikiri hata Pro. utaungana nami ni mara ngapi unaumwa lakini bado unaenda tu kazi wala huombi kupumzika hii nimeona kwa wanaume katika familia yangu,ndugu, jamaa na marafiki.Akina mama tukiumwa tunapumzika na kulalamika huku na kule na hivyokupata msaada.Mwili unahitaji kupumzika wakati fulani ila kwa wanaume wengi hii haipo.Wanawake tunapumzika.Na utashanga wanaume wako radhi kuwapeleka wake zao hospitali lakini sio wao!

  Pili: Stress kwa wanaume zikiwepo wengi wao kupunguza ni ama kwa pombe au sigara lakini kwa wanawake tunatafuta watu tunaowamini na kuongea nao hivyo tunapunguza katika njia inayostahili.
  Tatu: lishe mara nyingi wanaume hawafuatilii lishe yao .

  Nne: sayansi inatueleza kuwa kunyonyesha watoto kuna faida kiafya kwa mama kama kusaidia kupunguza uwezekano wa kupata breast cancer,kuimarisha mifupa na hivyo kupunguza uwezekano wa ugonjwa wa mifupa kama osteoporosis,na faida nyingine kadhaa kama kumfanya mwanamke kuwa mtulizu (calm). Nafikiri hii ni faida ambayo wanawake tunayo kuliko wanaume ila sijui itakuwa inachangia kwa kiasi gani katika kuishi maisha marefu.

  Mwisho:Kwa ujumla wanaume inabidi waanze kuzitunza afya zao zaidi au kama wameoa au wana watoto ina bidi akina mama au hao watoto tuwe mstari wa mbele kuwahimiza kufanya hivyo maana hiyo statistics uliyoitoa hapo juu inatisha.Mada nzuri Pro. asante.

  ReplyDelete
 4. Sophie - Asante kwa maoni yako ya kina. Umesema kweli tupu. Wanaume tunapenda sana kujifanya ngangari na mpaka tukaamue kwenda hospitalini ni lazima tuwe wagonjwa kweli kweli. Umenifanya nikumbuke kwamba hata physical zangu za kila mwaka ni mpaka mama watoto wangu agombe kweli kweli ndiyo niende.

  Kuna makala hapa nimeiona ambayo inaongelea swali hili kwa mtazamo wa jumla wa Kisayansi. Nawahurumia akina ngosha wenzangu kule Usukumani kwani ninapoenda kijijini kwetu na kukuta hakuna wazee huwa ninasikitika na kukereka sana. Inabidi kufanya jambo....

  Makala hiyo inapatikana hapa: http://www.time.com/time/health/article/0,8599,1827162,00.html

  ReplyDelete
 5. Prof. nashukuru kwa hayo makala nimeyapata na kupata maarifa zaidi naona namimi nitaendelea na huo mtindo wa Mama Masangu ili check ups zote zifanyike asante kwa tip!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU