NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, October 28, 2009

ATI, MWAKA 2012 NDIYO UTAKUWA "MWISHO WA DUNIA"?

Kituo cha runinga cha History Channel cha hapa Marekani kimeanzisha kipindi kipya kiitwacho Nostradamus-effect. Nostradamus alikuwa mtabiri maarufu wa Kifaransa ambaye wataalamu wengi wa mambo ya utabiri wanadai kwamba alitabiri kwa usahihi kabisa, mbali na mambo mengine, kuzuka kwa Alexander the Great, Adolf Hitler, mashambulizi ya Septemba 11 na hata urais wa Obama. Kwa habari zaidi kuhusu kipindi hiki tembelea hapa.

Katika kipindi cha Nostradamus-effect cha wiki jana wataalamu mbalimbali wa Anthropolojia, Fizikia, Historia, Haidrofizikia na taaluma mbalimbali walijadili kwa kina utabiri maarufu wa Nostradamus kwamba dunia itagharikishwa kwa maji na moto ifikapo mwaka 2012. Walitaja kwamba pengine hili si jambo la kushangaza sana ukizingatia kuyeyuka kwa kasi kwa barafu kunakotokea sasa katika pembe ya kaskazini ya dunia. Athari za tukio hili hazifahamiki na binadamu anaonekana hajali. Wengine walisema kwamba mabomu machache tu ya Atomiki yakiripuka (ama kwa makusudi au kwa bahati mbaya) basi dunia nzima inaweza kugharikishwa na mawingu ya miali hatari kabisa ya atomiki.

Jambo la kushangaza ni kwamba hata kalenda ya Wamaya (ambao himaya yao kubwa na yenye nguvu na maendeleo ya juu ya kisayansi na kiteknolojia iliangamia kutokana na sababu ambazo hazijulikani mpaka leo) inatabiri kwamba dunia itafikia mwisho wake mwaka 2012. Inaaminika kwamba Wamaya (Mayans) walikuwa na uwezo mkubwa wa utabiri na kalenda yao imeonyeshwa kwamba iliweza kutabiri kwa usahihi matukio mbalimbali yakiwemo kupatwa kwa jua, miripuko mikubwa ya volkeno, vita n.k. Cha ajabu ni kwamba hawakuweza kutabiri kuangamia kwa dola lao wenyewe.


Sijui kama wasiwasi huu ni wa kweli au ni yale yale ya Y2K (mnakumbuka?). Lakini ukiwasikiliza vizuri wanasayansi hawa, karibu wote wanakubaliana kwamba dunia itakumbwa na misukosuko ya kimazingira ambayo itasababishwa hasa na mabadiliko ya haraka ya hali ya hewa na mambo mengineyo ingawa hawajui misukosuko hii itatokea lini. Kuna haja ya kuwa wasiwasi?

9 comments:

 1. hakuna haja ya kuwa na wasi wasi hizi ni dhana zinazoletwa na wenye taaluma za kimapokeo, hushinda kutwa nzima, wakitafuta njia za kutisha watu HAKUNA AJUE SIKU WALA SAA.

  ReplyDelete
 2. inawezekana kukawa na ukweli kwani hii global warming hakuna anayejua inakotupeleka. Tandasi hiyo hakuna ajuae siku wala saa inafanya katika imani yako. Imani zingine zinaamini differently. Mimi naamini kwamba hakuna mwanzo na hakuna mwisho...Tunazunguka tu yihiiiiiiiiii!!!!!!!!

  ReplyDelete
 3. vitu vingine havituusu sana. tatizo letu ni kutafuta hofu na kuishi nazo. kama hukujua mwanzo wala hukuhusishwa kujua mwanzo sasa mwisho unakuhusu nini?

  ni kawaida ya binadamu na hofu zake hizo. Je wanadai baada ya hapo nini kitatokea? kwa nini wajishughulishe na mwisho na sio mwanzo? hakuna mwisho bwana. sisi jukumu letu ni kuishi kwa ufasaha basi. labda wanatabiri vifo vyao!

  ReplyDelete
 4. "Kwa nini wajishughulishe na mwisho na sio mwanzo?" Hoja nzuri hii. Inavyoonekana mwanzo haujulikani kwani mpaka leo bado ni kitendawili cha kipi kilianza kati ya yai na kuku...Baada ya kushindwa kuuelewa mwanzo pengine wameona afadhali wahangaikie mwisho ingawa kimantiki inaonekana kwamba kama unaufahamu mwanzo vizuri ndiyo unaweza kuufamu mwisho vizuri pia.

  ReplyDelete
 5. yes. hawajkuwahi kukaa mahala na kujadili juu ya mwanzo wa dunia au juu ya ujilio wa dunia, sasa wanakaa na kujadili mwisho!

  mambo ya kiroho ukitumia akili kuyajaddili utachemka tu

  ReplyDelete
 6. Alianza kuku likafuata yai bila shaka. Hakuna mwisho wa dunia ila ni pale kila mtu anapokoma kuwapo duniani kwa muda na wakati wake, kama vile ambavyo kila kitu kilikuja kwa muda tofauti na kingine.

  Nina mashaka na wasiwasi kama ipo siku hii dunia itaangamia na kutoweka kabisa, hayo mawazo ya mwisho wa dunia huwa yatatokea na kuendelea kutokea tangu enzi na enzi. Wapo wajanja kama akina KIBWETERE na wengine wenye lugha za kushawishi na kupumbaza wenzao.

  ReplyDelete
 7. Nadhani haja ya kuwa na wasi wasi ipo. Bila wasi wasi hatutaweza kufikiri namna yoyote ya kuinusu dunia yetu na majanga yanayoisonga kwa siku za usoni.

  Kwa mzunguko wa uasili wa dunia unaotokana na maumbile yake, pasipo msaada wa kinajimu, ni lazima tukubali kwamba kwa mvurugano uliopo wa hali za uasili wa dunia hii, sasa ni wazi kuwa matukio yasiyo ya kawaida yanaweza kuipata dunia yetu kwa siku za usoni.

  Pengine hilo haliwezi kumaanisha mwisho wa dunia, lakini kwa wengine maana ya matukio hayo yaweza kuwa sawa na kitu kama hicho.

  Kuna haja ya kuwa na wasi wasi.

  ReplyDelete
 8. Hiyo kwangu naona kama mganga wa kienyeji tu anatazama kwenye sufuria kile anachohisi akilini ndio anakuambia!! hakuna kitu kama hicho hayo mungu wamuachie mwenyewe,,hawaoni chochote ila wanaropoka tu

  ReplyDelete
 9. Huo mwisho wa dunia labda ulikua wa mamaake

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU