NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, October 20, 2009

MWALIMU NYERERE NA JANGWA LAKE LA KIITIKADI

Makala haya yametoka katika gazeti la Kwanza Jamii la leo - 20/10/2009

Mwalimu Nyerere na Jangwa Lake la Kiitikadi


(Ati, ni Nani Hasa Alikuwa Mfuasi wa Itikadi ya Mwalimu?)


Na Dkt. Masangu Matondo Nzuzullima


Katika diwani ya Karibu Ndani (Euphrase Kezilahabi, DUP, 1988:27) kuna shairi liitwalo “Azimio”. Beti chache za shairi hilo zinasema hivi:


Azimio sasa ni

Mabaki ya chakula

Kwenye sharubu za bepari

Kalamu inayovuja

Katika mfuko wa mwanafunzi

Vumbi zito

Baada ya ng’ombe kupita

Kilichosalia sasa

Ni punje za ulezi

Zilizosambazwa jangwani

Na mpandaji kipofu


Hivi ndivyo Kezilahabi – ajulikanaye pia kama Shaaban Robert wa Pili – alivyoliona Azimio la Arusha mwaka 1988. Nimelikumbuka shairi hili wakati nikitafakari Historia ya nchi yangu Tanzania hasa katika kipindi hiki ambapo nchi hii nzuri inaadhimisha miaka 10 tangu muasisi wake atoweke hapa duniani. Ni kweli Mwalimu alisambaza ulezi wake wa Ujamaa na Kujitegemea jangwani? Kama ni kweli, ina maana Mwalimu hakuwa na mfuasi wa kweli hata mmoja katika genge lake la Makomredi waliokuwa wakiimba ahadi za usawa wa binadamu? Ni nani hasa alikuwa mfuasi wa kweli wa itikadi kombozi za Mwalimu Nyerere? Ni Komredi Kingunge Ngombare Mwiru? Ni Edward Moringe Sokoinne? Ni Dr. Salim Ahmed Salim? Ni Rais Benjamin William Mkapa? Ni Mfaume Rashid Kawawa (Simba wa Vita)? Ni Rais Ali Hassan Mwinyi? Ni Jaji Sinde Warioba? Ni Oscar Kambona? Ni John Samwel Malechela? Ni Bibi Titi Mohamed? Ni Edward Lowasa? Ni Nani?


Msukumo hasa wa kuandika makala hii fupi niliupata kutokana na visa vifananavyo vilivyotokea kwangu mwenyewe na dada Subi Sabato wa nukta77.blogspot.com. Katika kuadhimisha miaka 10 ya kifo cha Mwalimu Nyerere niliweka mkusanyiko wa video 17 za Mwalimu Nyerere katika blogu yangu (matondo.blogspot.com). Subi Sabato pia alifanya hivyo hivyo katika blogu yake. Haukupita muda mrefu nilipata barua kutoka kwa watu waliokuwa wakijiita watumishi wa serikali wakinitaka niziondoe video za Mwalimu Nyerere katika blogu yangu mara moja kwani eti sikuwa na hati miliki na kwa hivyo nilikuwa navunja sheria. Waliendelea kunitisha kwamba nisipofanya hivyo basi sheria kali zingechukuliwa dhidi yangu. Subi Sabato naye alipata vitisho kama hivyo. Jambo hili lilinishangaza sana na nilijiuliza maswali mengi ambayo mpaka leo sijapata majibu na ndiyo maana naandika makala hii. Ina maana kuna mtu anamiliki hotuba za Mwalimu Nyerere? Niliwauliza watishaji wangu wanieleze aliko mmiliki wa hati miliki wa hotuba hizi ili niweze kuwasiliana naye lakini mpaka leo sijapata jibu. Mimi nilikuwa ninadhani kwamba hotuba za Mwalimu ni hazina ya taifa na Watanzania wote tuna haki ya kuzisikiliza bila kutishwa na mtu. Nilichukulia mfano wa hapa Marekani ambapo sheria za hati miliki ni kali sana lakini hotuba nyingi za marais wao ziko mtandaoni na ukienda katika maktaba za maraisi hao utaweza kuzisikiliza bure. Ni hazina ya taifa lao. Ni mali ya wote. Ni kumbukumbu ya historia ya nchi yao. Hotuba hizi hazimilikiwi na mtu! Hata hotuba nyingi za Rais Obama tayari zipo mtandaoni! Kuna tovuti nyingi zenye hotuba hizi na mojawapo nzuri ni hii hapa.


Mpaka nitakapopata ufafanuzi wa kina kuhusu ni nani hasa mmiliki wa hotuba za Mwalimu Nyerere, ninashawishika kuamini kwamba kuna kundi la watu ambao wanakerwa, kutishwa na kukoseshwa amani na hotuba za Mwalimu kwani wamegeuka kuwa wasaliti. Hawa inawezekana walikuwa ni watu wa karibu sana kwa Mwalimu na walijifanya kuwa “ardhi yenye rutuba” kwa mawazo na itikadi zake kumbe kwa ndani walikuwa ni “majangwa” tu yasiyootesha wala kustawisha cho chote. Ni mbwa mwitu waliokuwa wamevaa mavazi bandia ya “ukomredi” huku wakiimba na kudumisha “fikra sahihi za Mwalimu” kikasuku tu huku kimatendo wakiwa wamekakawana jangwani. Na baada ya Mwalimu kuondoka sasa wanajaribu kila wawezalo kufanya mawazo yake kombozi yasiwafikie Watanzania huku wakitumaini kwamba kwa njia hii hatimaye pengine Mwalimu ataweza kusahaulika.


Katika hotuba zake nyingi unaweza kumsikia Mwalimu akikemea rushwa na ufisadi; na utulivu wake wa akili, falsafa komavu na uwezo wa kuona mbali, kuonya na kutabiri mambo unaonekana waziwazi. Anasema waziwazi kabisa kwamba rushwa ikiachwa iendelee itaweza siku moja kuutikisa “msingi” wa nyumba (Tanzania). Mwalimu, pamoja na mapungufu yake yote, alitambua kwamba rushwa na utajiri wa kupindukia wa watu wachache kwa upande mmoja, na umasikini na uhohehahe wa asilimia 100 kwa walio wengi kwa upande mwingine siku moja utaitikisa Tanzania kwani ipo siku hawa wasio na kitu watachoka na kusema “liwalo na liwe”. Na hili likitokea hakuna jeshi litakaloweza kurekebisha mambo. Watu wakiamua wameamua na Historia imejaa mifano tele inayoonyesha kwamba nguvu za umma ni kama sunami. Badala ya kujaribu kurekebisha mambo na kuchukua ushauri wa Mwalimu kama vile mbuni asiye na upeo, kundi hili la “wanajangwa” inaonekana limeamua kuficha kichwa mchangani likiamini kwamba kutokomeza mawazo ya Mwalimu pengine ndiyo njia ya mkato ya kuendeleza “jangwa” lao wanalojaribu sana kuhakikisha kwamba linabakia kuwa jangwa. Kundi hili kwa hakika linajidanganya!


Hali hii inaibua hoja nyingine. Kutokana na “ujangwa” huu ambao sasa unaonekana waziwazi, haishangazi kuona kwamba sera nyingi za Mwalimu zilishindwa na kusema kweli inashangaza kidogo kuona kwamba baadhi ya sera zake zilifanikiwa mf. Elimu.


Historia inatuambia kwamba viongozi wengi waliofanikiwa ni wale ambao walikuwa na wafuasi wa kweli, wafuasi ambao walikuwa tayari hata kupoteza maisha yao ili kulinda na kutetea itikadi na harakati zilizoanzishwa na viongozi wao. Na hapa sizungumzii madikteta waliolazimisha itikadi zao kwa wafuasi wao kwa mkono wa chuma na kumwaga damu. Mara nyingi Historia huwa haina huruma na watu wa aina hii bali kuwatupa katika shimo lake la takataka. Huko ndiko waliko akina Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa Zabanga, Jenerali Bokasa, Jenerali Field Marshal Idd Amin Dada na wengineo wa aina hiyo.


Viongozi ambao hawakupanda mbegu zao katika “jangwa” mara nyingi hawakuwa hata na haja ya kuandika mawazo yao. Wafuasi wao wa kweli walifanya hivyo. Yesu Kristo hakuandika kitabu cho chote lakini wafuasi wake wa kweli walifanya hivyo. Buddha pia hakuandika kitabu cho chote. Wafuasi wake wa kweli walifanya hivyo. Lao-Tzu (mwanzilishi wa Taoism) pia hakuandika kitabu cho chote. Wafuasi wake wa kweli walifanya hivyo. Ferdinand de Saussure – mwanaisimu wa Uswisi ambaye anatambuliwa kama baba wa Isimu ya kisasa hakuandika kitabu cho chote pia wakati wa uhai wake. Wanafunzi wake walikusanya “notisi” na mihadhara yake aliyokuwa akiitoa wakati wa uhai wake na kuandika kitabu ambacho kilibadilisha kabisa mkondo mzima wa taaluma ya Isimu. Historia ina mifano mingi ya watu wa aina hii. Ni vigumu mno kwa kiongozi kufanikiwa kama amezungukwa na “jangwa” kama inavyobainika sasa kwa Mwalimu Nyerere.


Mwalimu Nyerere ataendelea kuenziwa na Watanzania, Waafrika na wapenda amani kokote duniani na juhudi za kundi hili linalojaribu kuzima mawazo yake linapoteza muda wake bure. Pamoja na makosa yake yote na kushindwa kwa sera yake ya msingi ya Ujamaa na Kujitegemea Watanzania wanaendelea kumuenzi na kumheshimu kiongozi huyu kwa msimamo wake na kutotetereka katika kutekeleza kile alichokiamini kwamba kilikuwa na maslahi kwa watu wake. Mwalimu Nyerere alihubiri na kutenda alichokihubiri na karibu kila kitu alichokitenda kilikuwa ni kitu ambacho aliamini kabisa kwamba kilikuwa ni kwa maslahi ya taifa lake changa. Jambo hili linawavutia sana Watanzania hasa wakiangalia maisha yake ya uadilifu aliyoishi – yeye pamoja na familia yake. Ni kwa sababu hii mimi naamini kwamba Nyerere na itikadi yake vitadumu!


Pamoja na “ujangwa” uliopo, wakati sasa umefika wa kumaliza ukiritimba katika hotuba (na vitu vingine ambavyo ni hadhina ya taifa letu). Hotuba za Mwalimu Nyerere siyo mali ya Redio Tanzania, mtu wala shirika au kikundi cha watu bali ni mali yetu sote. Ni wakati sasa wa kuziweka hotuba hizi katika mtandao. Hebu tuwe na tovuti maalumu yenye hotuba zote za viongozi wetu wote kuanzia Mwalimu Nyerere, Rais Mwinyi, Rais Mkapa na rais wetu wa sasa Rais Kikwete. Tovuti hiyo itangazwe na itunzwe vizuri kwani itakuwa mojawapo ya hazina muhimu sana kwetu kama Taifa kwa wakati huu na vizazi vijavyo. Wiki ijayo nitazungumzia kosa kubwa kuliko yote la Mwalimu Nyerere!


Niandikie: profesamatondo@gmail.com

Nisome: matondo.blogspot.com

7 comments:

 1. KAMUA BABA KAMUA....WAMEZIDI WAMEZIDI...WAPE WAPE WAPE!!!

  "Mpaka nitakapopata ufafanuzi wa kina kuhusu ni nani hasa mmiliki wa hotuba za Mwalimu Nyerere, ninashawishika kuamini kwamba kuna kundi la watu ambao wanakerwa, kutishwa na kukoseshwa amani na hotuba za Mwalimu kwani wamegeuka kuwa wasaliti. Hawa inawezekana walikuwa ni watu wa karibu sana kwa Mwalimu na walijifanya kuwa “ardhi yenye rutuba” kwa mawazo na itikadi zake kumbe kwa ndani walikuwa ni “majangwa” tu yasiyootesha wala kustawisha cho chote. Ni mbwa mwitu waliokuwa wamevaa mavazi bandia ya “ukomredi” huku wakiimba na kudumisha “fikra sahihi za Mwalimu” kikasuku tu huku kimatendo wakiwa wamekakawana jangwani. Na baada ya Mwalimu kuondoka sasa wanajaribu kila wawezalo kufanya mawazo yake kombozi yasiwafikie Watanzania huku wakitumaini kwamba kwa njia hii hatimaye pengine Mwalimu ataweza kusahaulika."

  ReplyDelete
 2. UNASIKIKA VIZURI HAPA DR....

  "Viongozi ambao hawakupanda mbegu zao katika “jangwa” mara nyingi hawakuwa hata na haja ya kuandika mawazo yao. Wafuasi wao wa kweli walifanya hivyo. Yesu Kristo hakuandika kitabu cho chote lakini wafuasi wake wa kweli walifanya hivyo. Buddha pia hakuandika kitabu cho chote. Wafuasi wake wa kweli walifanya hivyo. Lao-Tzu (mwanzilishi wa Taoism) pia hakuandika kitabu cho chote. Wafuasi wake wa kweli walifanya hivyo. Ferdinand de Saussure – mwanaisimu wa Uswisi ambaye anatambuliwa kama baba wa Isimu ya kisasa hakuandika kitabu cho chote pia wakati wa uhai wake. Wanafunzi wake walikusanya “notisi” na mihadhara yake aliyokuwa akiitoa wakati wa uhai wake na kuandika kitabu ambacho kilibadilisha kabisa mkondo mzima wa taaluma ya Isimu. Historia ina mifano mingi ya watu wa aina hii. Ni vigumu mno kwa kiongozi kufanikiwa kama amezungukwa na “jangwa” kama inavyobainika sasa kwa Mwalimu Nyerere."

  ReplyDelete
 3. Profesa Matondo, shukrani kwa taarifa hii. Naunga mkono msimamo wako. Napenda pia kusema machache.

  Mwaka 1989 nilienda Kenya kwa mara ya kwanza, kumalizia taratibu za kuniwezesha kufanya utafiti kule. Nina mazoea ya kupitapita sana katika maduka ya vitabu. Nilivyoingia katika maduka ya vitabu ya Nairobi na Mombasa, niliona vitabu vya Mwalimu Nyerere humo. Hii ilinishangaza, kwa sababu vitabu hivi vilikuwa nadra kuviona Tanzania.

  CCM ilikuwa inaagiza mashangingi kwa wingi, na magari ya aina aina ya CCM yalikuwa yakikatiza nchini kama siafu. Vitabu vya Mwalimu Nyerere vilikuwa havionekani. Niliwaeleza waTanzania fulani jambo hilo, niliporejea kutoka Kenya.

  Baada ya Mwalimu kung'atuka, hali ilikuwa hiyo, kwamba CCM iliendelea kupuuzia mwelekeo wake, na Mwalimu alikuwa anaishutumu CCM kwa miaka na miaka, hadi siku zake za mwisho.

  Hotuba za Mwalimu na maandishi yake ya miaka hiyo ya mwisho ni ushahidi na urithi wetu waTanzania. Kwa mfano, kuna hiki kitabu chake kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania. Kinatakiwa kisambazwe na kisomwe na kila Mtanzania. Kwa mfano, katika ukurasa 66 Mwalimu anasema, "Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio ulionifanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi."

  Miaka kama mitatu hivi iliyopita, nilipokuwa Dar es Salaam, niliingia katika duka la vitabu la serikali, nikiwa na lengo la kutafuta vitabu vya Mwalimu Nyerere. Niliangalia kila mahali, na sikukiona hata kitabu kimoja!

  Vitabu vya viongozi (sijui ni viongozi au wababaishaji) wawili watatu vilikuwepo. Lakini kitabu cha Mwalimu Nyerere hakikuwepo hata kimoja. Nilishtuka, nikawauliza wahudumu kama wana vitabu vyovyote vya Mwalimu Nyerere. Waliniambia "jaribu kuja Ijumaa."

  Hawakuwa na uhakika kama hii Ijumaa vitapatikana. Na mimi nilikuwa na haraka ya kuondoka nchini.

  Profesa Matondo, namalizia kwa kukushukuru kwa kile kitabu cha Mwalimu Nyerere ulichoniletea.

  ReplyDelete
 4. Profesa Mbele - hilo la vitabu vya Nyerere nilikuwa sijawahi kulifikiria. Hicho cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania nilikipata kwa bahati bahati na jamaa aliniuzia kwa kujifichaficha utafikiri kwamba ni magendo kumbe ni kitabu tu tena cha kiongozi wa nchi mzalendo. Maandishi ya Nyerere yanaogopwa sana na ndiyo maana ni nadra. Kuweza kuzizima hotuba zake zilizoko mtandaoni itakuwa kazi ngumu kwani vitisho tu havitatosha. Watatokea wataalamu zaidi wa haya mambo wazichomeke katika server ambazo hazifikiki kwa urahisi (kama zile zinazotumiwa na makundi ya uhalifu wa kimataifa/ugaidi/uhafidhina). Sijui watafanya nini. Kazi kwelikweli!

  ReplyDelete
 5. kwa mawazo yangu nadhani hotuba za viongozi wetu ambazo tunatakiwa kuzihifadhi kama hadhina ya taifa ni za mwalimu peke yake, eti tuhifadhi hotuba za kikwete zitusaidie nini? kiongozi wa taifa anashindwa kutatua hata matatizo madogo tu kama vile suala la umeme, kupanua barabara na kuepuka kuzidi kwa foleni hapo dar, watu wanaiba mapesa benki kuu, mikataba hewa,yeye anakaa kimya na kuangalia tu, kazi kufanya ziara zisizo na maana kila siku...na huyu mkapa amelifanyia nini taifa hili zaidi ya kukiuka miiko ya uongozi kwa kujilimbikizia mali? adumu mwalimu !!!

  ReplyDelete
 6. Anony wa mwisho - inabidi tuhifadhi hotuba za viongozi wetu wote. Wote ni viongozi wetu na hata kama wamekuwa wabovu kiasi gani hatuwezi kuwakana. Wote ni sehemu muhimu ya Historia yetu na hatuwezi kuikana Historia yetu. Wakati mwingine kiongozi unayemwona wewe kuwa ni mbaya kabisa wengine wanaweza kuwa na maoni tofauti. Mwamuzi sahihi huwa ni Historia!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU