NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, October 12, 2009

NAKUMBUKA SIKU NILIYOTUNUKIWA ZAWADI KWA KUWA MWALIMU BORA WA MWAKA!

Katika vyuo vikuu vingi (na hata shule za msingi, sekondari na vyuo vinginevyo) hapa Marekani kuna tuzo linaloitwa "Teacher of the Year Award" Tuzo hili nadra hutolewa kwa mwalimu ambaye ameonyesha uwezo, ubunifu, mafanikio na njia za kipekee katika kufundisha. Mimi nami nililipata tuzo hili hapa Chuo Kikuu cha Florida mwaka wa masomo wa 2004-2005.

Ili kulipata tuzo hili ni utaratibu mrefu na uchaguzi wake hufanywa kwa uangalifu sana. Mbali na kupendekezwa, inabidi wanafunzi wako waandike barua wakieleza kwa kina jinsi ufundishaji wako ulivyowabadilisha na ni kwa nini wanafikiri kwamba unastahili kupata zawadi. Inabidi waseme ni kwa jinsi gani ufundishaji wako uko tofauti (na bora zaidi) na wa walimu wengine ambao wameshawahi kuwafundisha. Pia msimamizi wako (mkuu wa idara/kitengo) pamoja na walimu wenzako ni lazima waandike barua kukuunga mkono (watatembelea madarasa yako ili kujionea wenyewe jinsi unavyofundisha kabla hawajaandika barua zao). Halafu mwenyewe inakulazimu uandike insha ndefu kujieleza jinsi ufundishaji wako ulivyo tofauti na walimu wengine, falsafa inayokuongoza darasani na mtazamo wako mzima kuhusu nafasi ya mwalimu darasani na katika jamii kwa ujumla. Ni lazima pia uambatishe silabasi zote za masomo uliyowahi kufundisha, mifano ya mazoezi na mitihani ya mihula, "handouts" na vikorokocho vingine vingi. Halafu kamati maalumu iliyo chini ya "Dean" inakaa kupitia walimu wote waliopendekezwa na kufanya uteuzi wa mwisho.

Kwa upande wangu wanafunzi wenyewe walijikusanya wakashauriana wakaandika barua, wakawatafuta na wanafunzi wangu wa zamani nao wakaleta barua zao na kisha wakapeleka pendekezo lao katika kamati teuzi. Nilipata bahati ya kusoma baadhi ya barua zao na nilishangazwa na mambo ambayo waliyaeleza. Nilivutiwa na kuguswa mno!

Mbali na kupata bango la kumbukumbu (plaque), mshindi pia unapata cheki ya dola 5,000, unahongereshwa rasmi siku ya mahafali ya wanafunzi (na ukitaka unaweza kutoa hotuba) na unakaribishwa katika dhifa maalumu pamoja na rais wa chuo pamoja na viongozi wengine. Kwa ujumla hii ni siku nzuri ambayo mwalimu unaona kwamba juhudi zako pamoja na kipaji chako cha uelimishaji kweli kinaheshimiwa na kuthaminiwa. Inafurahisha na kutia moyo sana!

Mimi naamini kwamba huu ni utaratibu mzuri sana katika kuwaonyesha walimu wetu kwamba tunawajali na kuuthamini mchango wao na sioni ubaya wo wote kama nasi tukianzisha utaratibu kama huu (tena bila upendeleo wo wote) kwa walimu wetu katika ngazi mbalimbali.

Mwalimu wa binti yangu aliyeko darasa la pili alituambia hivi wazazi tuliokuwa tumekusanyika kumhongeresha (pamoja na kumpelekea zawadi) baada ya kushinda tuzo hili mwaka jana katika shule yake ".....Nitajibidisha zaidi mwaka ujao na wanafunzi wangu wataona mambo mapya na kujifunza kwa urahisi zaidi" Hili ndilo lengo hasa la tuzo hili - kuwapa motisha walimu kwa kuwaonyesha kwamba tunathamini na kuheshimu mchango wao - hasa wale wenye vipaji vya pekee na wanaojitolea sana katika kuelimisha watoto wetu!

Na siku moja natamani kurudi nyumbani na kutumia kipaji changu na mambo ambayo nimejifunza huku katika kuelimisha taifa langu!

13 comments:

 1. Kwanza lazima nikupe pongezi za dhati kwa juhudi zako mpaka kufanikiwa kupata tuzo kubwa kama hiyo.

  Nchi yetu ingekuwa na utaratibu kama huo, nafikiri kwa kiasi fulani tungeweza kuifufua elimu yetu ambayo imeporomoka kwa sasa.

  ReplyDelete
 2. Hongera sana kakangu tena nyingi mno zikufikie na pia kwa familia yako kwani bila wao usingefanikiwa na hilo.

  ReplyDelete
 3. Inatia moyo kwa kweli pale unapoona unachofanya kinakuba
  lika,inaonyesha kipaji cha mhusika pia.Ila inatisha kidogo
  kwa hivyo vigezo?

  ReplyDelete
 4. Mdau kutoka Arusha!October 8, 2009 at 5:04 PM

  Tatizo la Tanzania siyo kwamba eti hatuna wataalamu. Watalamu tunao sana na huu ni mfano mmojawapo. Tatizo ni kwamba watu wenyewe tunaowategemea mmekimbilia nje na sasa mnapewa zawadi na tuzo kwa KUSOMESHA NA KUELIMISHA AMERICANS! Wakati wa Nyerere nyinyi mngekuwa matraitors tu. Mbona mmeikimbia nchi yenu lakini?

  Kama MIMI NINGEKUWA RAISI NINGEMTUMA ISSA MICHUZI NA VIJANA WENGINE WA USALAMA WA TAIFA WAJE WAKUCHUKUE NA KUKURUDISHA TANZANIA. UNGERUDI PALE MLIMANI MARA MOJA AMBAKO HAKUNA WALIMU WA MAANA NA KUANZA KAZI IMMEDIATELY. Hata kama ni nyumba ya kukaa ningearrange.

  Kaa chonjo kwani this is siriazi. Walimu ndiyo hasa chachu ya maendeleo na hatuwezi kuwa na walimu Watanzania eti mnapata tuzo for teaching Americans wakati mmesomeshwa kwa pesa za serikali. JK PLease do something for people like this. Bring them home ASAP!

  ReplyDelete
 5. Kwanza nafurahi kusikia taarifa hii ya mtani wangu kupata tuzo hii. Naifahamu ilivyo adimu katika vyuo vya Marekani. Hongera sana.

  Kuhusu kauli ya Mdau wa Arusha, napenda kusema kuwa dunia ya leo, haijalishi mwalimu yuko wapi "hapa duniani. Tekinolojia ya mawasiliano inamwezesha mwalimu aliyeko Tokyo kuwafundisha wanafunzi walioko Morogoro, Cairo, London, Chicago, na kadhalika. Umbali sio hoja, kwa dunia ya leo ilivyo.

  Jambo la msingi ni wahusika kuwa na nia kweli ya kutafuta elimu. Watanzania wengi hawatafuti elimu, bali vyeti, hata vya kughushi. Wako radhi kununua masuali ya mitihani kuliko kununua vitabu na kuvisoma kwa dhati. Kama wanasoma vitabu, wanatafuta tu vile vilivyoko katika mpangilio wa masomo, si kujisomea vingi, kwa msingi wa kupanua fikra. Wanalenga kwenye mitihani. Hili ni tatizo kubwa. Elimu haina njia ya mkato.

  Mimi ni mwalimu, na wakati huu nafundisha huku Marekani. Lakini nilikuwa mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar kuanzia mwaka 1976 hadi 1991. Nikiwa mwalimu pale, nilikuja kusomea shahada ya udaktari huku Marekani, 1980-86. Nilifanya bidii sana katika masomo yangu, na nikajizatiti kwa kununua shehena kubwa ya vitabu. Nilitumia dola yapata 2000 kununulia vitabu.

  Niliporudi Tanzania, ule mwaka 1986 waTanzania kila mahali waliniuliza kama nimeleta "pick-up."
  Mimi sikuwa nimenunua "pick up," bali hivi vitabu. Watanzania waliniona nimechemsha, kwani hela niliyonunulia vitabu ilitosha kununulia gari kwa wakati ule.

  Lakini waTanzania ndio hao. Wangeniona wa maana iwapo ningekuja na gari. Na hata leo, wanaponiona natembea kwa mguu hapo Dar, au kwa dala dala, wanashindwa kunielewa kama nina akili timamu au la. Kumbe huku Marekani, watu wanajali taaluma. Unaweza kumkuta mkuu wa chuo anatembelea baiskeli hapa Marekani, au anakuja ofisini kwa mguu.

  Hatimaye nilialikwa kuja kufundisha Marekani. Niko hapa. Lakini niko tayari kumfundisha yeyote anayetaka, kutoka sehemu yoyote duniani.

  Vitabu ambavyo nimeandika vinavyotumika hapa Marekani, nimeviweka Tanzania pia, ili wanaotaka waweze kuvinunua na kuvisoma. Vitabu hivi vina yale ambayo nawafundisha wazungu. Sitaki lawama kuwa nimewasahau waTanzania. Lakini waTanzania ni wagumu kununua vitabu, ila ni wepesi kununua bia na kitimoto, wepesi kutoa shutuma kuwa sisi tumewakimbia na tunawafundisha wazungu tu.

  Lawama hizi hazina msingi. Binafsi, ningependa kupata ujumbe kutoka kwa mTanzania ambaye amesoma vitabu vyangu hapa hapa Tanzania, halafu aniandikie kutaka maelezo zaidi. Huyu nitakuwa naye bega kwa bega. Nitamfundisha hata kwa "email," bila gharama kwake.

  Watu wa mataifa mbali mbali nawasaidia kitaaluma kwa njia hiyo. Wameniandikia wakiwa Ulaya, India, Afrika Kusini na sehemu mbali mbali za Marekani. Wanaleta suali, nami nawajibu, au wanaomba mwongozo, nami nawapa. Umbali haujawa tatizo. Nimewahi hata kusaidia kusoma maandishi ya watu wanaohenyea tasnifu za udaktari katika vyuo mbali mbali hapa Marekani. Wanaleta maandishi yao kwa "email," na mimi nasoma na kuwapelekea maoni, mpaka wanamaliza, bila kuonana uso kwa uso.

  Lakini waTanzania wanapenda zaidi kutoa lawama, badala ya kujishughulisha kama hao wengine. Wanapenda kushutumu kuwa sisi tumeikimbia nchi. Mimi nakataa shutuma hiyo. Nataka kumsikia mTanzania aniambie kuwa amesoma vitabu vyangu vilivyoko hapa hapa Tanzania, na kisha alete masuali ili tuendelee kuelimishana. Nikizingatia huu uzoefu wangu kuhusu waTanzania, napenda kusema kuwa sikubali hizi lawama.

  Miaka hii nimechukua hatua mpya: ninaendesha warsha huko huko Tanzania. Mwaka jana nilifanya hivyo Arusha, na mwaka huu nimeendesha warsha Tanga na Dar es Salaam. Kwa namna hii, ninajijengea msingi wa kuwarushia lawama wale ambao wamezoea kutoa lawama.

  ReplyDelete
 6. Sasa wewe Mdau wa Arusha. Ndiyo maana hutakaa uwe President. Unamtuma Issa Michuzi na vijana wa usalama wa taifa waje kumkamata huyu jamaa au? Amefanya kosa gani? Kupata hii tuzo ni kosa mpaka umtumie mashushushu? Ni kweli Issa Michuzi ni shushushu? Mimi nilikuwa sijui but I am not surprised!

  Kama unataka watu warudi please rekebisha mambo - encourage them to come home, jenga mazingira mazuri, wape mishahara mizuri, wapangie nyumba za kuishi wakirudi na trust me wengi wao watarudi bila wasiwasi wo wote. Lakini kama wanarudi na kuwa frustrated na wazee ambao hawataki kustaafu then nothing will change. Kuna mifano mingi ya very intelligent people ambao walijaribu kurudi na sasa wanajuta na wengine even died kama yule jamaa aliyefungua hospitali ya moyo pale Mikocheni. Walimfrustrate akina Anna Makinda mpaka akafa - wewe unafikiri mchezo. Nchi ya watu hii baba na usije ukajidanganya eti na kiPhD chako kuleta mabadiliko hapa. Unaweza UKAKOLIMBWA - sijui kama unaukumbuka msemo huu. Maisha ni popote na mimi siwalaumu hawa jamaa ambao wametimkia nje ingawa kusema kweli kama ningekuwa president NINGEFANYA KILA NIWEZALO ILI WARUDI - HASA KATIKA NYANJA ZA UALIMU, UDAKTARI PAMOJA NA UHANDISI!

  ReplyDelete
 7. hongera sana dk nzuzullima. pengine umechelewa kutujuza mafanikio haya ya mtanzania mwenzetu wewe lakini kama wahenga walivyobainisha hakuna habari iliyozeeka kwa anayeipata sasa. habari mupya hii. hongera sana ndugu yetu. hawa jamaa mpaka wakaona unafaa si haba.

  ReplyDelete
 8. Hongera sana kaka,najivunia kuwa na kaka kama wewe(Mnyantuzu)hakika inapendeza sana na kutia moyo,sisi tu tunafuraha kiasi hiki wewe mwenyewe je na familia yako? sipati picha mungu akupe maisha marefu zaidi uweze kuelimisha wengi.Hiki ni kipaji kikimpata mwenye kujua kukitumia matunda yake ndio haya tunayaona leo.

  ReplyDelete
 9. Wapendwa;
  Asanteni nyote kwa maneno yenu ya kutia moyo. Nimefarijika! Sote tuna talanta tofauti tofauti tulizojaliwa na Muumba wetu. Tuzitumieni vyema.

  Profesa Mbele - nakubaliana nawe. Kutokana na maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia, kwa sasa siyo lazima mtu kuweko mahali ili kuweza kutoa mchango wake si katika ualimu tu bali katika nyanja zote. Lawama hizo za usaliti hata mimi sizikubali na huwa siwaelewi watu wanaokasirika/waliokasirika eti kwa sababu sikurudi nyumbani baada ya masomo yangu. Hata mimi "nimeshasimamia" vijana kadhaa waliokuwa wanaandika tasnifu zao za uzamili na uzamifu pale Mlimani na nafanya hivyo kwa kujitolea kabisa. Mimi sikuwahi kufundisha Mlimani na nikipata nafasi ningependa niende pale au vyuo vingine na kufundisha japo kwa miaka miwili mitatu hivi.

  Huo mkasa wa "pick up" umenifurahisha. Kama hujui hadhi ya mtu na utu wake sasa inapimwa kwa aina ya gari analoendesha. Ndiyo maana kila mtu anakazana kuendesha shangingi ili awe na hadhi hata kama ni kuchukua mkopo ambao utamchukua miaka 30 kuulipa. Tofauti kabisa na wazungu ambao mtu anaweza kuwa anapanda baiskeli yake au kuendesha kimkweche cha gari wakati pesa anazo tena nyingi tu. Pesa hizo hata hivyo zimewekewa malengo mengine muhimu zaidi - hata kama ni ya miaka 30 ijayo! Rafiki yangu mmoja nilimuuliza kwa nini amenunua shangingi jipya (na kulipa Tsh. 120,000,000) wakati angali kijana tu. Nilimwuliza mbona asingenunua Corolla au Rav4 na kutumia hizo milioni nyingine kwa shughuli nyingine muhimu? Nilishangaa aliponiambia kwamba Corolla na Rav4 ni magari ya matineja na watu wanaoanza maisha, na kwamba hilo shangingi lake jipya (Landcruiser V8) limempa hadhi kubwa sana katika jamii na anaweza kumpata mwanamke ye yote amtakaye. Niliishiwa nguvu kwani mimi hata hiyo Corolla sina na nilikuwa nasafiri kwa daladala na taksi. Tangu hapo nilikuwa kila nikiona shangingi likipita nilikuwa natamani nilisimamishe nimwulize mwenye nalo sababu zilizomfanya alinunue. Kazi kwelikweli!

  Kuhusu Watanzania kusoma vitabu hili linajulikana wazi na limeshaongelewa sana. Ndiyo maana sekta ya vitabu Tanzania ni kama vile imekufa. Ndiyo maana kwa sasa vitabu vingi vya Kiswahili vinaandikwa na Wakenya. Pengine tabia ya kujisomea ina unafuu kidogo huko Kenya sijui. Tuendeleeni na hata hizi bogu zetu ni njia mojawapo ya kutolea michango yetu katika uendelezaji wa jamii yetu. Tusichoke!

  ReplyDelete
 10. Mbele na Matondo mmehitimisha vema pamwe na huyo annony.

  Ukishakuwa na self-realization japo kidogo tu hayo masifa hayana nafasi.

  Hongera Masangu. Keep it up

  ReplyDelete
 11. Hili lilikuwa limenipita kidogo kutokana na kuzidiwa na majukumu. Lakini napenda kukupongeza Profesa Matondo kwa kazi iliyotukuka. Endeleza huu moyo ili uwe mfano kwa walimu wengine kwingineko duniani hasa katika bara letu changa la Africa.

  ReplyDelete
 12. Nilikuwa Tanzania juzi baada ya kuondoka kwa takribani miaka kumi.
  Nilisikitishwa saana na muelekeo wa "Taifa la sasa". Vijana wengi hawana muelekeo wa maisha...focus yao kubwa ni Pombe, kuonekana na wanawake...ambayo inafanya wengi wao wawe na fikra za uwizi. Hata kama wana kazi nzuri na wamesoma (1st degree or 2nd degree) targets zao ni "kujilipua"...ikimaanisha kuiba fedha nyingi mno pale watakapopata mwanya.
  Msemo mkubwa ulikuwa "UZA NYUMBA WEKA HESHIMA BAA"

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU