NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, November 13, 2009

JE, WAVUTA SIGARA WANAONEWA?

Mimi sivuti na lengo langu hapa siyo kuwatetea wavuta sigara. Wanasayansi wameshathibitisha kwamba uvutaji wa sigara ni tabia ya hatari inayoua mamilioni ya watu kila mwaka kutokana na saratani ya mapafu na magonjwa mengine yanayoathiri mfumo wa upumuaji. Kutokana na sababu hii uvutaji wa sigara umepigwa marufuku karibu katika kila kona ya dunia. Sehemu zingine zimefikia hatua ya kutunga sheria zinazowabana wavuta sigara kutovuta hata wakiwa majumbani mwao. Mwezi uliopita chuo kikuu cha Florida kilipitisha sheria ambayo inapiga marufuku uvutaji wa sigara katika maeneo yote ya chuo – ndani na nje. Sijui wavuta sigara watafanyeje!

Swali langu ni hili: mbona tumekomalia sana sigara utafikiri kwamba uvutaji ndiyo tabia pekee-angamizi? Mbona tabia zingine za hatari kama unywaji wa bia (ambao pia, mbali na matatizo mengine, umeshathibitishwa kuwa kisababishi kimojawapo kikuu cha aina mbalimbali za saratani na hasa zile za matumbo) hatuzikomalii kama uvutaji sigara? Vipi kuhusu ulaji wa nyama hasa zile “nyekundu” ambao nao pia umeshathibitishwa kwamba ni hatari kwa afya? Wavuta sigara wanaonewa?


Mimi ni mmoja kati ya watu wasiopenda tabia za kinafiki za kujifanya kuchukia tabia moja angamizi na kukumbatia zingine za aina hiyo hiyo. Ndiyo maana huwa sielewi mtu anaponiambia eti ameamua kuacha kula nyama ili kulinda afya yake na wakati huo huo anazitandika bia sawasawa, kuvuta sigara na hata kuwa “kiwembe”.


Ni mawazo yangu tu. Pengine mwanafalsafa Kitururu angeweza kusema ninachojaribu kukisema hapa kwa ufasaha zaidi!


Wasikilize watafiti hapa wakijadili athari za ulaji wa nyama, uvutaji wa sigara na unene wa futufutu (obesity) kwa afya.

5 comments:

 1. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!November 13, 2009 at 9:29 AM

  Kaka Masangu, naomba niwe kimya kwani sivuti sigara, sinywi pombe na soda ya aina yoyote hivo mjadala huu...dah!

  ReplyDelete
 2. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!November 13, 2009 at 9:30 AM

  na wala sili nyama ya aina yoyote :>(

  ReplyDelete
 3. dk leo you made my day. umeyasema ambayo huwa nayafikiria lakini nashindwa mpangilio wa kuyaandika ama kwa kutokuwa mbunifu ama kwa kuogopa.

  mie navuta sigara. 'nimepumzika' sasa miezi sita na ninatamani iwe hivyo moja kwa moja.

  nikiwa navuta sigara huwa sitaki binafsi sigara yangu iwe kero kwa mwingine asiyependa. kama simfahamu huwa namuomba. can i smoke around here? kuna wakati nilikuwa nakaa nyumba ya vinne peke yangu lakini nikijisikia hamu ya tumbaku nilikuwa natoka nje nafunga milango kisha napata kitu roho inapenda. nikiridhika narejea ndani kwa raha zangu.

  siku moja nilipelekwa polisi kisa nimekataa kulipa nauli kwa kuwa dereva alikuwa anavuta sigara. just imagine nakasirikia sigara huku mie ni mvutaji. yaliyotokea polisi hapa sio pahala pake, au vipi?

  hoja ya kwanza na ya pili za namna ya uvutaji wangu (pengine uliokuwa uvutaji wangu kwa kuwa nimeazimia kuacha moja kwa moja) ni jinsi gani nisivyopenda starehe (ama tabu) yangu isiwe kero kwa mtu mwingine. it is a poison of one's choice.

  nilipowahi kutembelea marekani na kuishi kidogo nilifurahishwa na sera za uvutaji sigara huko ( kumbe sasa chuo kikuu cha florida wameendelea zaidi). kwa mfano ili kuzuia watu wasivute maofisini basi kuliwekwa fire alarms ambazo huwaka pinsi zikihisi moto ama moshi. bwenini vivyo hivyo. nilitakiwa kushuka kutoka ghorofani kwenda chini nje kuvuta kidogo.

  falsafa ya uvutaji sigara iko katika biashara yake. binafsi huwa hainiingii akilini kwa nini sigara ni halali na bangi ni haramu. makampuni yanayotengeneza sigara ni makampuni makubwa sana duniani. hata makampuni ya nchi zilizoendelea sasa yameshawekewa ubia na makampuni ya ulaya na marekani. hata kiwanda chetu hapa. cha kushangaza wakati ulaya na marekani uvutaji tumbaku unapigwa vita na kukatishwa tamaa, katika nchi fukara uvutaji sigara unapigiwa baragumu sana na kushabihishwa na maisha bora. tanzania mpaka leo mabango yanayopigia baragumu uvutaji sigara ni jambo halali na usidhani viongozi wamelala. hapana wapo na mwakani tutawachagua usihofu. Unakuta bango la kushawishi kuvuta tumbaku linakuonyesa kinana mtanashati anavuta sigara huku akiwa na redio baab kubwa ya muziki na masofa makubwaa na msichana mrembo. Maandishi yake yanasomeka: ”haya ndio maisha”. Halafu chini kabisa kwa tumaandishi tudooooooogo ”uvutaji sigara ni hatari kwa afya yako”

  biashara ya sigara ina unafiki mkuu.

  Nyama na bia! Mhh....! Nimeanza kuacha tumbaku kwanza. nikifanikiwa kuacha tumbaku labda. nasema labda

  ReplyDelete
 4. yep.

  ni vyema kujadili haya mambo kwamba tunazuia vitu na serikali zinashindwa kuvitokomeza eti kwakuwa vinalipa kodi. naamini hata madawa ya kulevye au bangi vikilipiwa kodi, tutaandikiwa tumaandishi tudogo kuwa ni hatari kwaa.....

  anyway, kuwawekea sheria kali ni kuwanyanyapaa na kuwahumiza watumiaji badala ya kuwa karibu nao na kuwasaidia ili waache salama na kwa amani. pale FAJI, walevi na wavutaji wamewezeshwa kuacha wenyewe bila sheria wala vitisho.

  ReplyDelete
 5. ni kwa sababu uvutaji sigara haumuathiri yule aliyechagua kuvuta tu bali watu wengine watakaofikiwa na huo moshi wanaita secondhand smoke.
  Utaona pia kwenye pombe kampeni ni kuwa do not drink and drive kwani ukiamua kunywa na kuendesha ina madhara si kwa mnywaji tu pia kwa watu wengine

  lakini kama umeamua kunywa au kula nyama wakati unajua ina madhara kwa afya yako hilo ni chaguo lako mwenyewe tatizo ni pale chaguo lako linapoleta madhara kwa watu wasio husika ndio maana wanakataza kuvuta around watu wengine or drink and drive

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU