NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, November 5, 2009

KUNUNUA MAUA WARIDI (ROSES) - KIELELEZO CHA MAPENZI AU MATOKEO YA KUSUTWA NA DHAMIRI?


 • Pengine hili ni swali la kipuuzi lakini imebidi niliulize kutokana na kisa kilichonipata jana.
 • Baada ya kutoka kazini nilipita dukani kununua mboga na nikaona maua waridi (roses) mazuri sana. Dazeni moja ilikuwa inauzwa dola 6.99 tena bado freshi kabisa na yamefungwa na kurembwa vizuri. Bei ya kawaida kwa maua kama haya ni dola 13.99 - 29.99.
 • Basi nikanunua dazeni moja ili kumpelekea mama watoto wangu.
 • Nilipotoka nje nikakutana na mwanaume Mmarekani mweusi ambaye alikuwa ameambatana na wanawake wawili.
 • Wale wanawake wakanisifia kwa kusema "Nice roses. She is going to be very happy today"
 • Yule mwanaume yeye akanitupia swali "Bro, what did you do?" Wale wanawake wawili wakaanza kucheka.

Ilinichukua muda kidogo kumwelewa lakini nilipopambazukiwa nilielewa alikuwa anamaanisha nini: mtu unamnunulia maua umpendaye wakati umemkosea na unataka kuomba msamaha. Wakati huo nilikuwa karibu na gari langu na sikupata muda wa kumjibu muuliza swali ambaye tayari alikuwa ameshaingia dukani.


Katika kipindi kimoja cha televisheni niliwahi kusikia wanasaikolojia wakisema kwamba mwanaume anayetembea nje ya ndoa/penzi ana uwezekano mkubwa zaidi wa kumnunulia mke/mpenzi wake "orijino" maua kutokana na kusutwa na dhamiri "sense of guilty". Wanasaikolojia hawa walitoa ushauri kwa wake/wasichana kufanya uchunguzi mara moja kama waume/wapenzi wao wataanza kuwapa zawadi na hata kuwanunulia maua wakati si kawaida yao. Hii inaweza kuwa ni matokeo ya ule msuto wa dhamiri.

Kule usukumani, ilikuwa lazima kumnunulia umpendaye zawadi - ndogo au kubwa - kulingana na uwezo wako. Kanga, hereni, viatu, "chachandu"- kitu cho chote ambacho kingemfanya ajisikie kwamba unampenda na kumjali. Nadhani, mbali na kuhongeresha, maua (waridi) pia yanatimiza lengo lilelile kama hizi zawadi za Kisukuma.

Kwa wanaume: Kwa nini mnanunua maua?

Kwa wanawake: Kama mpenzi/mume hana kawaida ya kukuletea zawadi/maua na mara moja anaanza kufanya hivyo, utajisikiaje? Ni kweli utaingiwa na wasiwasi?

6 comments:

 1. sijawahi mnunulia mtu maua na haitatokea kwani sio utamaduni wangu binafsi japo najitahidi kulima na kuzungushia maua Nymba niishiyo

  na hata nionapoa maua hufarahi lakini kumnunulia mtu maua??? naonaga kwenye TV

  ReplyDelete
 2. Chacha o'WamburaNovember 5, 2009 at 1:30 PM

  Masangu, una bahati hukuoa ukuryani. huku ukimletea nkeo maua utakoma kwani utavurumishwa na kutolewa berenge na hayo maua yako...lol

  ka-pea ka kanga unaweza kuleta bila kujalisha mmekosana ama mko fresh...lol

  ReplyDelete
 3. Kamala, najua maua siyo utamaduni wetu - vipi kuhusu zawadi zinginezo? Wewe hujaingia kwenye mkumbo wa kusherehekea siku ya wapendanao ambayo imekuwa maarufu sana siku za karibuni?

  Chacha - hata kama ningekuwa nimeoa Mkurya maua yangu angeyapokea vizuri sana - tena bila berenge wala nini!

  ReplyDelete
 4. Matondo siku yangu na yule nimpendaye ni kila leo na hamna siku fulani bali ni kila leo sina siku maalumu ya kumpenda bali nampenda kila leo na sassa! here and now!!!

  kwa zawadi nyingine kwakweli kuna vitu huwa naviona na kuona kama vinamfaa yule nimpendaye na hivyo kumnunulia au kumwagiza anunue au namuuliza kama anapenda na kumnunulia, basi na si kwa lengo linginelo.

  kukosana na nimpendaye???? to me life is easy and I always keep it simple and situpid. ni ubinadamu na namchukulia kama alivyo na bahati nzuri yeye pia unichukulia hivyo pia

  ReplyDelete
 5. Binafsi sijaahi kumnunulia wangu maua na sababu kubwa ni kuwa mimi na yeye hakuna anayeona unganisho la maua na penzi la kweli. Ila angekuwa anathamini na kupenda nisingegoma kumnunulia (pale niwezapo)
  Nadhani ni vema kumfariji umpendaye namna apendavyo hasa kama unaweza kumudu, iwe ni maua ama kumuendesha kwenye baiskeli. Haijalishi kama ni kitu ama maombi ama kuwa pembeni yake ama lolote analoweza kuthamini kama zawadi, kama unataka kujitoa kwa ajili yake, basi apendalo na lisilo nje ya mipaka na uwezo wako ni vema kutendeka.
  Ninalomaanisha ni kuwa watu wanafukuzwa na maua kwa kuwa si kila mwanamke anayathamini na kama uliyenaye hayathamini nawe unamlazimisha kuyapokea atakuona "kiazi" kwani ulistahili kumridhisha yeye na si "kufuata mkumbo"
  Baraka kwenu

  ReplyDelete
 6. Asanteni. Kamala na Mzee wa Changamoto nyote mmegonga pointi. Mimi pia naamini kwamba lengo hasa la zawadi yo yote ile kwa umpendaye ni kuonyesha kuwa unamjali, kumthamini na kwamba yupo katika mawazo yako. Namfahamu rafiki yangu mmoja ambaye alikuwa na tabia ya kumnunulia mkewe bazoka (bubble gum) kila mara alipotoka kazini na jambo hili lilikuwa linamfurahisha sana mkewe. Yaani alikuwa na kagudulia kalikokuwa kamejaa bubble gum na kalikuwa kanatunzwa vizuri pengine kuliko vitu vyake vingine vyote. Kwa hivyo ni kweli haijalishi ni zawadi gani. Wapo pia waliowahi kupeleka zawadi za magari mapya wakidhani kwamba kwa kufanya hivyo wataendelea kuchochea moto ule usiozimika lakini baada ya muda wakarudishiwa magari yao na kubakia kushangaa.

  Miaka michache iliyopita "sikukuu ya wapendanao" ilinikuta nyumbani na kila kijana alikuwa katika hekaheka ya kutafuta maua na kadi. Naamini kwamba wengine walikuwa wanafuata mkumbo tu bila hata kujua ni kwa nini wananunua hayo maua na hizo kadi na kama kweli ndicho wakitakacho au kuwaridhisha hao wapenzi wao.

  Mimi nilikuwa natafuta kadi zenye jumbe tofauti tofauti zilizoandikwa kwa Kiswahili ili nije nazo huku lakini sikuzipata. Muuzaji mmoja pale posta mpya akaniambia kwamba walishajaribu kuleta hizo kadi lakini hazikununuliwa kwani maneno ya kimahaba kama "I love You" hayanogi sawasawa yakiandikwa katika Kiswahili. Sikujua kuwa uthamani wa zawadi kwa umpendaye unaweza pia kuathiriwa na lugha iliyotumika katika zawadi hiyo!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU