NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, November 20, 2009

MAREKANI KUNA NJAA!!!

 • Nakumbuka mwaka 2001 mama alipokuja kunitembelea wakati ule nikiwa bado mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha California, Los Angeles (UCLA). Alishangaa sana alipoona utitiri wa wazungu (chokoraa) wasio na makazi wakiomba pesa mabarabarani. Alisema kwa mshangao "kumbe kuna wazungu masikini!"

 • Watu wengi pia wakisikia njaa moja kwa moja wanafikiri kwamba nchi inayozungumziwa ni lazima iwe ya "ulimwengu wa tatu". Kinachowajia akilini ni picha za vile vitoto vya Kiethiopia vilivyokondeana huku viking'ong'wa na mainzi vikiwa tayari kukata roho kwa ajili ya njaa. Kumbe hata hapa Marekani njaa ipo!
 • Ripoti ya Wizara ya Kilimo ya Marekani iliyotolewa juzi imeshawangaza watu wengi. Ripoti hiyo inasema kwamba kuna njaa hapa Marekani na mwaka jana Wamarekani wapatao 49,000,000 waliathirika na njaa au hawakuwa na chakula cha kutosha. Hii ni sawa na kusema kwamba kwa kila Wamarekani sita, kulikuwa na Mmarekani mmoja ambaye hakuwa na chakula (cha kutosha)
 • Kama inavyotegemewa watu wengi wanaoathirika na njaa ni masikini (ambao kutokana na siasa za kitabaka, kibaguzi na kinyonyaji za muda mrefu mimi nadhani wengi wao watakuwa ni Wamarekani Weusi na wahamiaji kutoka Amerika ya Kusini). Inashangaza kidogo kuona kuwa nchi tajiri kuliko nchi nyingine yo yote hapa duniani nayo inakumbwa na tatizo la njaa. Pengine picha hiyo juu itabidi tuifanyie mabadiliko ili kuakisi uhalisia huu mpya: njaa si tatizo la Afrika peke yake!
 • Rais Obama ameahidi kwamba serikali itaongeza misaada zaidi kwa watu masikini. Isome taarifa hiyo fupi hapa.

6 comments:

 1. hakika njaa ni tatizo la ulimwengu na si la nchi za ulimwengu wa tatu tu peke yake. Lakini yashangaza nchi kama marekani kuwa na tatito hili kwa hakika.Hivi nchi ambazo ardhi yake imefunikwa na barafu serikali yao inawezaje kuwalisha watu wao na hata wasife njaa? pengine hii nayo ni changamoto.

  ReplyDelete
 2. Nakubaliana nawe ya kuwa tunahitaji kubadili mtazamo tunapofikiria au kuzungumza matatizo ya watu, sio nchi zinazodaiwa kuwa ni maskini ndio zina matatizo.
  Na nchi nyingi hasa za kiafrika si masikini kwa mantiki ya umaskini, isipokuwa kuna watu wachache wanajinufaisha kwa kudai nchi hizi ni maskini huku wakiendelea kuziibia utajiri wao wa asili, na kuja kuwaopa mikopo yenye masharti magumu huku wao wakiendelea kupata faida kubwa wakiwatumia vibaraka wachache.
  Niomeisoma habari ya huyo mtoto wa dikteta kama nilivyopenda kumuita mimi kutoka Equatorial Guinea ambaye ana mali ambazo hata matajiri wengine waliopo nchi zilizoendelea hawana mali hizo, na nchi yake zaidi ya theluthi 2 ni maskini hohehahe kabisa, cha kushangaza nchi hiyo ni namba 3 katika kuzaklisha mafuta Afrika. Sasa huo umaskini wa watu ni wa kweli au ni wa kupandikiza?
  Tukiamka wote, umaskini wa Afrika hautakuwepo.
  Inasikitisha sana

  ReplyDelete
 3. Du! Waingereza wanatuambia charity starts at home, labda sielewi tafsiri ya usemi vizuri. Majuzi serikali ya marekani ilimwaga mamilioni ya dola za kimarekani kusaidia Tanzania, sasa ni kwanini wasingemwaga kwanza kwa raia wake ambao wamekumbwa na janga la njaa!

  ReplyDelete
 4. Ndiyo njaa ni tatizo la dunia nzima - ingawa pengine makali yake yanatofautiana.

  Bwana Malkiory - hawa jamaa wanapomwaga mamilioni ya dola zao si bure. Kwa kawaida wanajua kwamba mamilioni hayo yatarudi tu kwa njia moja au nyingine. Hakuna mlo wa bure ati! Kwa hivyo ukiona wana moto sana kusaidia nchi yo yote ile - chunguza vizuri utaona. Lazima kutakuwa na kitu ambacho wanakitaka. Itakuwa ni mafuta au madini haba ambayo wanayataka. Tanzania nadhani kuna matumaini ya kupatikana kwa mafuta bila kusahau kwamba Dodoma na mikoa ya kati kuna Uranium ya kutosha. Pia sasa wanahaha kujaribu kupunguza ushawishi wa Wachina ambao kidogo wameshajitandaza sehemu mbalimbali barani Afrika - lakini "ugomvi" uko kwenye nchi zile zenye raslimali wanazozitaka - mafuta, Cobalt, Uranium n.k

  ReplyDelete
 5. Profesa Matondo, hapo umenena. Na hivi sasa migodi ya dhahabu imegunduliwa huko mikoa ya kusini,nadhani Wamarekani wataendelea kumwaga dola za kutosha.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU