NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, November 26, 2009

UZEMBE WA WATU KUSOMA MAKALA ZA UCHAMBUZI NA KUELIMISHA - TUFANYEJE?

Hii ndiyo ilikuwa timu ya kwanza ya gazeti ya Kwanza Jamii - Muuguzi na Mchambuzi wa masuala ya kiafya dada Subi Sabato, Profesa Joseph Mbele, Profesa Charles Bwenge, Dkt. Masangu Matondo Nzuzullima, Mchambuzi wa masuala ya kisheria Eliamini Laltaika, Padri Privatus Karugendo, Mwanamuziki, Mtunzi na Mchambuzi Freddy Macha na Mhakiki na Mchambuzi Born Again Pagan.
 • Makala hizi hata hivyo zimesomwa na watu wachache sana na hakuna aliyejaribu kutoa maoni. Katikati ya hizo kulikuwa na moja yenye kichwa cha habari kisemacho "Ulimwengu Wa Mahaba (Mada endelevu): Hiki Ndicho Kinachomsisimua Mwanamke". Makala hii ilikuwa imesomwa mara 352 ukilinganisha na mara 40 kwa makala ya Profesa Mbele, mara 23 kwa makala ya Profesa Bwenge na mara 29 kwa makala ya Joseph Mihangwa.
 • Nilipoangalia upande wa maoni mapya, maoni yote yalikuwa ni juu ya makala yenye kichwa kisemacho "Wanaume wana haraka ya kufanya sex". Hivi ni kwa nini hasa watu hawapendi kusoma makala muhimu zinazochambua na kuhoji mambo ya msingi katika jamii?

 • Gazeti la Kwanza Jamii limejibidisha sana kuandika makala za wachambuzi makini mbalimbali (akiwemo Kamala Lutatinisibwa Omwami Ta Jasson Lutabwasibwa) lakini taarifa nilizokuwa nazo miezi michache tu iliyopita ni kwamba gazeti hilo lilikuwa halifanyi vizuri sana kutokana na ukweli kwamba watu hawapendi kusoma makala ndefu za kichambuzi. Watu wanapenda kusoma makala fupi fupi zenye vichwa na mada za kusisimua kama vile yanavyofanya magazeti ya udaku ambayo ndiyo yanatamba sana. Pengine ni kwa sababu hii ndiyo maana nimeona gazeti hili limeanza pia kupenyezapenyeza makala za kimahaba ili kuvutia wasomaji.
 • Japo jambo hili linakatisha tamaa, kama isemavyo kauli mbiu ya Mzee wa Changamoto "Better to write for yourself and have no public, than to write for the public and have no self." inabidi tuendelee kujibidisha kuelimisha umma japo ni kwa mwendo wa kobe. Wanablogu wenye blogu za kiuchambuzi inabidi tusikate tamaa kwa blogu zetu kutosomwa na watu wengi kama blogu zinazoandika mambo ya "macelebrity, umodo, udaku na mavazi". Mimi naamini kwamba kazi yetu si bure ati!

9 comments:

 1. kwanza labda nimwombe pia kijana wa Changamoto naye aje na changamoto zake kwenye gazeti hilo.

  mwanzoni mwa mwezi huu nilikuwa na mkutana na mwenyekiti wa jarida hili na tukafanya mikakati ya kuliboresha. kwa ufupi mimi niko bize saana kuandika. ila katokea mwanautambuzi mwingine anayeandika makala kibao mle japo hazijatoka mtandaoni. Mwenyekiti aliniambia ni kwa kiasi gani wasomaji walilifagilia gazeti hili na kuliona ni la kwao zaidi.

  unajua watanzania wamechoshwa na habari zile zile za richmondi nk, sasa wanataka vitu tofauti na hasa vile kuhusu wao (kujitambua). kupenda vitu vya ngono inaweza kuwa ni sababu ya changamoto kubwa zilizopo katika jamii zetu kwani kama ndoa haina ngono njema, basi ujue itaathiri utendaji wa wanandoa, familia na hivyo taifa kwa ujumla na kwa hiyo inahitajika chuo katika hilo.

  uchambuzi mwingine, mimi nafakgilia makala za karugendo, Mihangwa na prof mbele, ni za utofauti sana na sio zile zile.

  ndo yangu kwa sasa

  ReplyDelete
 2. Swala hili linasikitisha!

  Lakini linajibu ni kwanini watu wengi hutupa vitabu wakimaliza shule.

  Lakini hakuna cha kukata tamaa kwa kuwa tupo tupendao kusoma makala za kichambuzi.

  Na taratibu tutafika tu!

  ReplyDelete
 3. Mtakatifu Simon;
  Unaonaje ukianzisha "Kona ya Kutafakari/Tafakuri/Falsafa" katika gazeti hilo na kuanza kupeleka baadhi ya post zako huko. Kwa vile post hizo tayari unazo katika blogu yako hutakuwa na shida ya kuziandika. Hii itakuwa changamoto mpya kwa gazeti hilo na hakuna gazeti ambalo limeshawahi kufanya hivyo. Ukiweza fanya hivyo. Wasiliana na Maggid Mjengwa (mjengwamaggid@gmail.com)

  ReplyDelete
 4. Heshima kwenu.
  Kwanza niseme kuwa mara baada ya Da Koero kuandika ileee makala ya BINTI YASINTA ambayo wengi tuliamini kuwa inastahili kuwa gazetini, nilimuandikia Majjid Mjengwa email kumuomba kuwe na kipengele cha "kutoka bloguni" na nilimsihi awatumie wana-blog makini alionao kuchagua makala ambazo wanaamini ni za kijamii zaidi na kisha kuzitumia. Sikuamini kama kuna mwana-blog ambaye angeweza kukataa maandishi yake kutumiwa gazetini.
  Lakini kama nilivyozoea niwaandikiapo wanablogu wakonwe, SIKUJIBIWA.
  Kwa hiyo binafsi sikuwa na la ziada. Naamini ujumbe niliufikisha japo yawezekana haukufika.

  Kuhusu kutopenda kusoma ni kuwa yaonesha TUNAFUATA wanachotaka wale wanaotupa sifa. Na (NASEMA HILI KWA LENGO ZURI) wanaopenda kusifia ni wale wasiojua wanalosifia. Na ndio maana wanaosifiwa wanalazimika kuacha njia sahihi ili kufuata sifa.
  Nimewahi kusema kuwa licha ya heshima niliyonayo kwa baadhi ya blogger maarufu, bado nasikitishwa na namna wanavyoendekeza "hits" za wasomaji kwa kuweka mambo yanayowafanya jamii waendelee kuwa katika mawazo finyu ya kimaendeleo. Wanaendekeza mambo ambayo jamii isiyofikiria maendeleo inataka badala ya kujaribu kuungana na wenzao kupita kipindi kigumu cha kuibadilisha jamii
  Wanapenda mteremko, wanapenda kuonekana wana wasomaji wengi lakini wanawasomesha upuuzi na ujinga zaidi ya mambo mema. Wanajali idadi ya posts na visitors kuliko kile kisemwacho ama kufanywa na posts hizo. Na sasa naweza kusimama kidete na kusema BLOGU ZIIFAAZO JAMII NI ZILE ZENYE MAONI MACHACHE AMA BILA MAONI AT ALL.
  Hakuna anayetaka kuwaweka watu MAWAZONI wakawaza kilicho nyuma ya pazia. Wanafikiri kila kitu ni cha kuitafunia jamii nayo isifikirie hata kidogo. Na hili ni kuanzia vyombo binafsi mpaka vile vya serikali. Taani TBC ndio uozo kwa kwenda mbele kwani licha ya kuwa na uwezo wa kuwashirikisha wataalamu kuwafikirisha wananchi wanabakia kuripoti tuuu (kama nilivyoandika hapa http://changamotoyetu.blogspot.com/2009/09/tanzania-yangu-yenye-vyombo-vingi-vya.html ). SHAME ON THEM
  Na ninapoona wenye uwezo na mvuto kwa jamii, wale tuwaonao kama kioo cha jamii ndio wanaisokomeza jamii mtaroni kwa uchu wa sifa binafsi
  TUNAKIUA KIZAZI CHETU SISI WENYEWE HUKU WATUPUMBAZAO WAKIKAA PEMBENI WAKITUCHEKA TUUU. Kama alivyosema Lucky Dube kuwa "Bob Marley said how long shall they kill our prophets while we stand aside and look. Little did he know that eventually the enemy will stand aside and look while we slash and kill our own brothers"
  Ndilo linalotokea, wakati tunajitahidi kupambana na uharibifu wa utandawazi wa nje, wengine walio ndani na wanaoaminiwa wanazidi kuharibu
  TUTAFIKA TUU

  ReplyDelete
 5. Matondo,nadhani ni vema kuwa na mtu moja anayetembelea au kutoa mchango kwenye blog yako, kulikoni kuwa na watu arobaini ambao huchangia na kubakia kutoa pumba. Nimeshuhudia hili kwenye zile blog zinazoitwa mashuri/popular.

  Hili la watu kutochangia au kutotembelea blog zinazoandika mambo ya msingi pengine linasikitisha,pengine linatokana na wadau kujikatia tamaa kwasababu ya mifumo migumu ya maisha,kisiasa na kiuchumi. Mwishowe watu hubakia kutembelea mambo ya burudani ila kupunguza msukumo wa damu (pressure) itokanayo na magumu hayo.Kikubwa hapa ni kwamba wanablog tujitahidi kuandika habari zitakazolenga kujenga na kuleta au kuharakisha maendeleo kwa jamii.

  ReplyDelete
 6. @ Profesa Masangu Matondo Nzuzullima : Nafanya hilo ulilonishahuri .Na samahani nitakutafuta pembeni pia kuhusu jingine lakini lihusianalo na Lugha.

  ReplyDelete
 7. Nashukuru kwa maoni yaliyotolewa hadi sasa. Labda niongezee tu kuwa labda tatizo hili liko mijini ambako ndiko kwenye hayo magazeti. Vijijini, ambako magazeti hayo hayapatikani sana, huenda hawangekuwa na tatizo la kusoma hizi makala za kuelimisha, iwapo magazeti yangepatikana.

  Hivi karibuni, tuliona taarifa katika KWANZA JAMII, kutoka kwa katibu kata fulani huko mikoani akishangilia kupatikana kwa gazeti la KWANZA JAMII kwenye kata yake. Huu ni mfano hai.

  Nilipoanza kuandika makala kwenye KWANZA JAMII, nililetewa taarifa na mdogo wangu aliyeko kijijini Umatengo (Mbinga) kwamba wanakijiji wamefurahi kusoma makala yangu kwenye KWANZA JAMII, na kwamba wanataka niendelee kuandika. Taarifa hii niliiweka kwenye blogu ya Mjengwa.

  Kwa hivi, nahisi kuwa tatizo la watu kupenda kusoma magazeti ya udaku liko, lakini nadhani tukumbuke kuwa magazeti hayo yanapatikana mijini, kama ilivyo kwa magazeti kwa ujumla. Magazeti ya udaku yamejaa mijini pamoja na magazeti mengine.

  Vijijini kuna ukame wa magazeti. Tujaribu kufanya mikakati ili makala zetu ziende vijijini, ambako wana kiu ya kuyaona magazeti.

  Vile vile, napendekeza kuwa tufanye mkakati wa kupeleka magazeti mashuleni. Kuna shule za sekondari na msingi kila mahali nchini. Tukilenga huko, tutaweza kupambana vizuri na hayo magazeti ya udaku yanayotamba mijini.

  ReplyDelete
 8. Baada ya kusoma makala ya Padri Karugendo kutoka Global Pulbishers (ambayo pia nimeitundika katika blogu hii) nina maoni tofauti kidogo kuhusu suala hili. Ninaandika makala na nitaituma kwa wenyewe wafalme wa udaku Tanzania Global Publishers; pia nitaitundika hapa ili tuendelee kujadiliana. Asanteni nyote!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU