NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, November 10, 2009

WANAMUZIKI WA KIZAZI KIPYA - TUMIENI LUGHA ZENU ZA MAMA KAMA ALIVYOFANYA MTOTO WA DANDU!

 • Igeni mfano wa Mtoto wa Dandu, Saida Karoli na Mr Ebbo!

Niliwahi kuandika kwa kifupi juu ya matumizi ya Kisukuma katika nyimbo za Mtoto wa Dandu. Katika maakala hii fupi (ambayo imetoka katika gazeti la Kwanza Jamii la leo 10/11/2009), ninatoa wito kwa wasanii wa kizazi kipya kuiga mfano wa Mtoto wa Dandu, Saida Karoli na Mr Ebbo na kuimba katika lugha zao za mama au hata kutia vionjo vya "kikabila" katika nyimbo zao. Kwa kufanya hivi watakuwa wanatoa mchango wao chanya katika vita vinavyoendelea duniani kote kujaribu kuzitetea lugha za kienyeji ambazo ziko katika hatihati ya kuangamizwa na utandawazi.
*****************************************************************************

Wanamuziki wa Kizazi Kipya – Tumieni Lugha Zenu za Mama kama Alivyofanya Mtoto wa

Dandu (Cool James)

Na Dkt. Masangu Matondo Nzuzullima

James Maligisa Dandu a.k.a Mtoto wa Dandu a.k.a Cool James a.k.a Ng'wanamalia a.k.a CJ Massive a.k.a Ng'wanawapelana a.k.a Nzokaihenge alikuwa na kipaji cha hali ya juu katika muziki. Ndiyo maana muziki wake ungali unapendwa sana miaka saba sasa tangu aage dunia kwa ajali ya gari tarehe 27/8/2002. Sikupata bahati ya kumwona lakini yeye pamoja na Saida Kalori na Mr Ebbo pengine ndiyo waimbaji wa kizazi kipya ambao kwa kiasi kikubwa wameweza kuzitukuza lugha zao za mama katika nyimbo zao - na hivyo kutupilia mbali ile dhana kwamba kizazi kipya hakiwezi kuguswa na nyimbo zenye ladha ya kikabila. Mtoto wa Dandu japo hakuimba katika Kisukuma moja kwa moja kama afanyavyo Saida Karoli, hapa na pale hakuisahau lugha yake ya mama iliyomkuza na kumlea kule Mwanza (Kisukuma). Hapa ni baadhi ya mifano tu ya matumizi ya Kisukuma katika nyimbo za mwanamuziki huyu mashuhuri aliyeondoka akiwa bado mchanga.

Jina lake mara nyingi alipenda kujiita Nzokaihenge yaani nyoka mwenye makengeza (nyoka makengeza). Alikuwa akijiita pia Ng'wanawapelana yaani mtoto mwenye hasira. Ni kawaida ya Wasukuma kujisifu na hapa ndicho alichokuwa akikifanya Mtoto wa Dandu. Ati, umeshawahi kuona nyoka mwenye makengeza maishani mwako? Unadra wa nyoka wa aina hii ndiyo ujumbe aliokuwa akitaka kuuwasilisha. Kipaji chake cha kipekee katika muziki kilikuwa nadra na muziki wake unaonyesha hivyo mpaka leo. Alipenda pia kujiita Ng'wanamalia - mtoto wa Maria. Hii inaonyesha kwamba pengine jina la mama yake ni Maria (Wasukuma hawana sauti " r" na hivyo mara nyingi huitamka kama "l" - kinyume na Wakurya)

Korasi mashuhuri inayosikika katika nyimbo zake nyingi inasema hivi:

Ng'wanamalia Kolobelaga lukumo lwane.
Jaga Ng'wigulya.
Jaga Ubagisha shikamoo abakolobela ng'weli...

Tafsiri

Mtoto wa Maria Umashuhuri wangu acha uenee sehemu zote
Uende juu zaidi

Uende ukiwasalimia shikamoo waliokwishasonga mbele Mashariki.


Kwingineko mara kwa mara anasikika akisema:

Nabiza wa galama.
Nulunagaja gubugeni nadiko gwigashiji gogo mpagi sumbi lya ng’hana

Tafsiri

Nimeshakuwa mtu wa thamani (heshima)
Hata nikienda ugenini siwezi kukalia gogo
Inabidi nipewe kiti kizuri cha kukalia

Inavyoonekana pia alikuwa ni mtu wa kutoa shukrani. Katika baadhi ya nyimbo zake anaonekana akimsifia na kumshukuru Jumanne Kishimba - tajiri mkubwa kule Mwanza na mmiliki wa duka kubwa la Imalaseko Supamaketi jijini Dar es salaam. Anasema hivi:

Jumanne Kishimba
Ulinamoyo gwape giti buluba
Hangi okumuka mpaga Bulaya

Tafsiri

Jumanne Kishimba
Una roho nyeupe mithili ya pamba
Tena umeshajulikana mpaka Ulaya

Akijisifu kidogo kama ilivyo kawaida ya Wasukuma anasema hivi:

Omasala adabunagwa nigo
Natemelwa bugota bonzoka ihenge

Tafsiri

Mtu mwenye akili haelemewi na mzigo (msemo wa Kisukuma)
Nimezindikwa na (madawa ya) nyoka mwenye makengeza

Huyu ndiye Mtoto wa Dandu ambaye hakuusahau utamaduni wake. Huyu ndiye Nyokamakengeza ambaye hakuionea aibu lugha yake ya mama. Huyu ndiye Mtoto wa Maria ambaye hakuuonea aibu Usukuma wake. Huyu ndiye Cool James ambaye alikuwa anatambua kwamba asingeweza kuwa “cool” bila kuwa na utamaduni wake mwenyewe.

Hebu fikiria kama wanamuziki wengi wa kizazi kipya wangeiga mfano wa Saida Karoli, Mr Ebbo na Mtoto wa Dandu, wakaimba nyimbo katika lugha zao za mama (Saida Karoli - Kihaya) au kuingiza vipengele vya lugha zao za mama katika nyimbo zao kama Mtoto wa Dandu (Kisukuma) na Mr Ebbo (Kimasai). Hatua hii ingesaidia sana kukikumbusha kizazi hiki kilichopumbazwa na “usasa” kwamba lugha zao za mama zipo, zina hadhi kama lugha nyingine yo yote na zina manufaa ya kimatumizi hata katika ulimwengu huu wa kisasa. Kwa hivyo dhana ya kwamba lugha hizi ni za kizamani, zimeshapitwa na wakati na hakuna sababu ya kujifunza au kuzizungumza tena haina ukweli wo wote. Ingefurahisha kama nini kama wanamuziki hawa wangetimiza wajibu huu wa kitamaduni na kuziunga mkono lugha zetu za asili katika wakati huu zinapopita katika mikikimikiki ya kudharauliwa na kuonwa kwamba hazifai tena.

Kimsingi huu ni wito wangu kwa waimbaji wa kizazi kipya - tumieni lugha zenu za mama katika nyimbo zenu. Kwa kufanya hivyo mtakuwa mnatoa mchango wenu wa thamani sana katika kuzipa uhai lugha zenu zilizowakuza na kuwalea, lugha ambazo zimo hatarini kufa baada ya vizazi vichache vijavyo kama mtaendelea kuzidharau, kuzionea aibu na kuziona kuwa hazina faida wala nafasi katika ulimwengu wa kisasa.

Mungu aendelee kumpumzisha salama Mtoto wa Dandu a.k.a Cool James a.k.a Ng'wanamalia a.k.a Ng'wanawapelana a.k.a Nzokaihenge a.k.a CJ Massive. Muziki wake kwa hakika utadumu!

Niandikie: profesamatondo@gmail.com
Nisome: matondo.blogspot.com
*****************************************************************************
Je, sasa unaweza kuvisikia vipengele vya Kisukuma nilivyovirejelea hapo juu katika nyimbo hizi za mtoto wa Dandu?8 comments:

 1. Chacha o'WamburaNovember 10, 2009 at 8:00 AM

  Kaka Matondo, wengi wa wanamuziki wetu wanaogopa wataonekana 'waporipori' wakiimba kwa kilugha chao...lol

  Na sasa wanashindana kuimba kwa kuchanganya ung'eng'e ...lol

  ReplyDelete
 2. Chacha Wambura! Hilo ndio tatizo kuogopa kwa nini kuogopa wakati kila mtu yupo huru. Na huu u´ngéngé utamsaidia nani wangéngé wenyewe sasa wanaanza kujifunza lugha zetu za Afrika kama Kiswahili na karibuni wataanza kujifunza lugha zetu za asili kama kisukuma au kingoni.

  ReplyDelete
 3. Nazikubali sana nyimbo za mtoto wa Dandu,nadhani wakati
  sasa umefika kwa wasanii wetu kutumia lugha za asili hata
  kama ni kwa kuchanganya na kiswahili.
  Wenzetu waganda wanathamini sana lugha zao,nyimbo zao
  nyingi ni za kiganda na bado zinakubalika sana hapa Tz
  na Kenya

  ReplyDelete
 4. Waganda hata nyimbo zao nyingi za injili zimeimbwa kwa lugha zao. Hata mwenyewe Camileon pia anafanya hivyo. Huko Kenya pia Wakikuyu, Wakamba na Wajaluo wanaimba nyimbo zao nyingi kwa lugha yao. Mbona sisi tusifanye hivyo? Mada nzuri mkuu

  ReplyDelete
 5. Tatizo letu sisi wabongo tunapenda sana kuiga,na hatupendi kuthamini na kujivunia tulivyona navyo,ni watu wa kuthamini vya wageni/kigeni na kuzarau vya kwetu.
  Kama alivyosema mchangiaji hapo juu,wakiimba kwa lugha zetu za asili wataitwa walugha,lugha(washamba)nakumbuka miaka ya nyuma alipoanza kusikika Saida Karoli, watu wengi walikuwa wanamcheka na kumbeza kwa kusema sawa anasauti nzuri lakini mlugha lugha hajui kabisa kiswahili ndio maana nyimbo zake anaimba Kihaya,Dar ikaenea kila kona eti alikaribishwa nyumbani kwa manager wake Muta/Luta eti hata matumizi ya salamu alikuwa hajui,alikuta watoto wadogo wanacheza akawaamkia shikamoo!!
  Mimi namfagilia sana tena kuna ule wimbo wake wa "KAISIKI... Akatambara ke laki tisa boojo lazima ukajwale"
  niliupenda sana nikatafuta mtu akanifundisha wote mwanzo mpaka mwisho na maana yake.
  Kaka asante sana kwa kuwapa changamoto.

  ReplyDelete
 6. Hebu mtazame Judith Babirye hapa: http://www.youtube.com/watch?v=VOUJsHlnW2w
  http://www.youtube.com/watch?v=aSE_bdT_ya4

  Ni Kiganda but these songs are famous allover the world. Use your mother tongues please

  ReplyDelete
 7. Ninaazikubali lugha zetu sana, na ninaelewa "mguso" mtu anaoupata anaposikia neno fulani likitamkwa katika lugha yake. Ila nina concern moja; vipi kuhusu umoja wa kitaifa? Nakumbuka miaka ile ya ...nilipokua kijana mdogo baba wa Taifa alijitahidi kuwe na lugha moja ambayo itasaidia kutuunganisha-na labda amefaulu. Kuna baadhi ya mataifa kwa sababu ya makabila kumetokea vita kabisa. Wadau naomba mnisaidie hapo...lugha za makabila yetu hazitatugawa????

  ReplyDelete
 8. Kweli itafikia muda lugha zetu zitakuwa adimu, maana watoto wetu wanachokijua ki kiswahili....kwa kupitia nyimbo tutaweza kuhifadhi hii hazina yetu ya lugha zetu.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU