NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, December 11, 2009

KUNA AULIZAYE; "UKO WAPI PROFESA MATONDO?"

 • Swali hili liliulizwa kwa Mjengwa. Japo nililijibu kwa ufupi (tazama maoni), muuliza swali sikumsikia tena. Naliweka hapa ili tuendelee kulijadili.
***************************
  Profesa Matondo, upo wapi?

  nyumba yangu
  nyumba zangu

  ANGALIA HII:

  ng'ombe yangu
  ng'ombe zangu

  AU ni

  ng'ombe wangu
  ng'ombe wangu

  NA HII PIA:

  mama yangu
  mama zangu

  AU ni

  mama wangu
  mama wangu?

2 comments:

 1. Jibu langu:

  Nimechelewa kuiona hii na nitajibu kwa kifupi.

  nyumba yangu
  nyumba zangu

  Hapa ni sawa. Nyumba yangu, nyumba zangu.

  ANGALIA HII:

  ng'ombe yangu
  ng'ombe zangu

  AU ni

  ng'ombe wangu
  ng'ombe wangu

  Sahihi ni ng'ombe wangu (umoja na uwingi). Vitu vyote vyenye uhai, bila kujali ngeli viliyomo (kijana/vijana, rais/marais/, ng'ombe/ng'ombe...) huchukua upatanisho wa kisarufi katika ngeli ya kwanza na ya pili ambayo ndiyo ngeli ya binadamu na vitu vingine vyenye uhai.

  NA HII PIA:

  mama yangu
  mama zangu

  AU ni

  mama wangu
  mama wangu?

  Jibu sahihi ni mama yangu/mama zangu. Japo hii inaonekana kupingana na jumuisho (generalization) la hapo juu kuna sababu za Kihistoria. Katika Kibantu Mama (Proto Bantu), ngeli ya tisa na kumi (n/n) iliundwa hasa na majina ya kifamilia ambayo hayamo katika ngeli ya m/wa (yaani hayaanzi na m/wa). Kwa hivyo mama, baba, dada, kaka, bibi, babu, shangazi...yalichukua upatanisho katika ngeli ya n/n - i/zi. Kwa hivyo tunasema mama i-angu (tunapata mama yangu), mama zi-angu (tunapata mama zangu). Hali hii haijabadilika hadi leo na upatanisho wa majina haya umebakia kama ulivyokuwa katika Kibantu Mama. Kwa vile kila kiumbe hai (animate) kinapaswa kuchukua upatanisho katika ngeli ya m/wa - kiongozi wangu (hatusemi kiongozi changu), viongozi wangu (hatusemi viongozi vyangu), ng'ombe wangu (hatusemi ng'ombe yangu) n.k. majina ya kifamilia (mama, baba, dada, kaka, bibi, babu, shangazi...) kwa sasa yanaonekana kuwa ni vighairi (exeptions) kwa upatanisho wake kubakia katika ngeli ya n/n~i/zi.

  Ughairi ni jambo la kawaida katika kila lugha (tazama jinsi mofimu za wakati uliopita au umoja na uwingi zinavyofanya kazi katika Kiingereza). Si ajabu ulitandikwa viboko na mwalimu uliposema kwamba past tense ya go ni goed badala ya went. Au uliposema kwamba uwingi wa child ni childs badala ya children...

  Nyongeza: ngeli ya tisa na ya kumi (n/n) imejaa mikanganyiko kwa sababu imegeuka kuwa "pipa la takataka" kutokana na ukweli kwamba karibu kila neno la mkopo linalokuja katika Kiswahili linafikia huko (baisikeli, pikipiki, Biblia, hadithi...)

  Kama muuliza swali anataka maelezo ya kina aseme. Nipo!

  ReplyDelete
 2. Mwalimu wa Kiswahili,

  Asante sana kwa uchambuzi wako kuhusu mama yangu au wangu...ng'ombe yangu/wangu, nk, kama ulivyofundisha kwenye blog yako (December 11, 2009 6:08 pm).

  Pamoja na maelezo yako kuhusu hayo ya mama...ng'ombe, wengine huwa wanasema kuwa maneno: mama, baba, dada, kaka, bibi, babu, shangazi... yanawekwa katika ngeli ya n/n~i/zi kwa sababu ni maneno ya kigeni, kama yalivyo maneno ya baisikeli, pikipiki, Biblia, hadithi...nk.

  Leo nina yangu mengine mawili:

  Mosi, miaka ya 1970s Tanzania ilikuwa ikiongoza kwa kisomo cha manufaa katika bara la Afrika - kusini mwa Sahara. Wastani ilipanda hadi kufikia zaidi ya 90%. Lakini leo hii kiwango hicho kimeteremka hadi karibu 55%! Kisoma cha manufaa (functional literacy), kama tulivyokiita, kilidorora kwa sababu, pengine, wanavijiji wetu walikuwa wanajifunza mambo mawili tofauti, inagwa yanashababiana: kusoma, kuandika na kusema, kwa upande mmoja, na kujifunza Kiswahili, kama lugha ya pili kwao (second “foreign “language), kwa upande wa pili. Wengi hawakujua Kiswahili. Lakini, ki-siasa, tulichukulia kuwa kila mmoja alikuwa akifahamu Kiswahili.

  Maswali: Je, wataalamu wa Kiswahili mna ushauri gani kuhusu: Mbinu za kuboresha uelewaji wa Kiswahili kwa watu wetu wa vijijini, ambao kusema kweli hawajui Kiswahili, ili wawe mahiri katika nyanja tatu za lugha hii: kusoma/kuandika (reading), kusikia (audio) na kusema (speaking/conversation) au conceptualisation of learning? Na mbinu za kisasa kuhusu ufundishaji (conceptualisation of teaching).

  Pili, huko kwetu (Mkoa wa Mara) kuna makabila ambayo lugha zake zinakufa polepole: Kikabwa na Kisimbiti. Na kuna hatari ya lugha nyingine nazo kufa polepole: Kizanaki, Kiikizu, Kinata, Kiikoma na Kingurwimi (Kingoreme, kulingana na tahadhari ya Unesco.

  Ka-problem: Ni haja yangu kuchangia katika kufufua (resuscitate) baadhi ya lugha hizi, kama si zote. sababu kubwa ni kupungua kwa watumiaji wa lugha hizi na vifaa vyake. Watumiaji wengine wanakimbilia mijini na kuoana nje ya makabila hayo.

  Katika dhamira hii ya ukombozi wa lugha hizi, ningependa sana kupata ushauri kutoka kwenu wataalamu wa lugha kuhusu theories za kisasa zilizo nzuri katika kile mkiitacho “second language acquisition”.Kwani itabidi baadhi ya watoto wa makabaila hayao wafundishwe lugha za “mama zao”!

  Mimi si mtaalamu wa lugha lakini nilichukua kozi ya ualimu (miaka ya nyuma), ambapo tulikuwa tukifundishwa theories za Behaviourism (Skinner); Cognition (Piaget), Innate (Chomsky) na Symbolic Interactionism katika kuzalisha maana (meaning).

  Nitafurahi sana kama ukipata nafasi ya kutufundisha kuhusu majambo hayo mawili.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU