NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, December 9, 2009

LEO NI SIKUKUU YA UHURU - TUTAFAKARI SAFARI YETU

 • Mwaka 1954, kiongozi kijana msomi na mwenye bashasha aitwaye Julius Kambarage Nyerere akishirikiana na wazalendo wenzake wachache alianzisha chama cha TANU ili kupigania uhuru wa Mtanganyika.


 • Baada ya kupigania uhuru kwa amani hatimaye usiku wa manane wa kuamkia tarehe 9/12/1961, Union Jack - bendera ya himaya ya Mwingereza - ilishushwa na bendera ya Tanganyika ilipandishwa. Tanganyika ilikuwa nchi huru!

 • Mwalimu Nyerere na viongozi wenzake walikabidhiwa nchi na Gavana wa mwisho wa Kiingereza. Unaweza kuwaona Rashid Mfaume Kawawa (Simba wa Vita) na Oscar Kambona wakiwa tayari kuchapa kazi.

 • Katika kuonyesha matumaini tuliyokuwa nayo, tulimpa Meja Nyirenda mwenge wa uhuru na kumwomba aende kuuwasha na kuusimika katika Mlima Kilimanjaro. Alifanya hivyo!

 • Tulichagua bendera yetu iliyoonyesha historia, utamaduni na utajiri wetu wa kiasili.

 • Ngao yetu ya taifa iliakisi moyo wetu wa umoja, ushirikiano na uchapakazi.

 • Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa kiongozi wa awamu ya kwanza (1961 - 1985). Uongozi wake ulijitahidi kujenga jamii ya watu walio sawa na huru kupitia siasa yake ya Ujamaa na Kujitegemea. Japo siasa yake ilishindwa; na anakiri kwamba serikali yake ilifanya makosa, kiongozi huyu aliishi maisha ya kiadilifu sana na mpaka leo bado anaonwa kama kiongozi bora ambaye alihubiri na kutenda alichokihubiri. Alijali maisha ya Watanzania wa kawaida. Wengi wanamkumbuka!


 • Mwaka 1964 na chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere, Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuunda Tanzania. Muungano huo, japo uko kwenye hatihati, ungalipo mpaka leo hii. Ni moja kati ya vitu ambavyo Mwalimu Nyerere alikuwa anajivunia sana!


 • Baada ya Mwalimu Nyerere, ilikuja awamu ya pili (1985 - 1995) iliyoongozwa na Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi. Hiki kilikuwa ni kipindi cha misukosuko ya kiuchumi duniani na uongozi wake kidogo ulilegalega. Watanzania walimbatiza kiongozi wao Mzee Rukhsa! Sera ya serikali ilibakia kuwa ile ile iliyoanzishwa na Mwalimu Nyerere - Ujamaa na Kujitegemea.


 • Awamu ya tatu (1995 - 2005) ilikuwa chini ya Mheshimiwa Benjamin William Mkapa - mwanafunzi wa Mwalimu Nyerere ambaye pia alisemekana kuwa na uadilifu na uchapakazi wa hali ya juu. Mwalimu Nyerere mwenyewe ilimbidi aende Chimwaga katika Mkutano Mkuu wa CCM kumpigania. Kiongozi huyu alikabidhiwa nchi ambayo haikuwa na nidhamu na maadili mema katika ukusanyaji wa mapato; na rushwa na ufisadi ulikuwa katika kiwango cha juu sana. Alileta nidhamu serikalini, ukusanyaji wa mapato na hakupenda mchezo. Inasemekana kwamba kwa kufanya hivyo alijijengea maadui hasa wale ambao walikuwa wamezoea ulaji katika awamu iliyopita. Kiongozi huyu anaandamwa na kashfa za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka yake. Ngoja tuone Historia itakavyomhukumu.


 • Awamu ya nne (2005 - ) ipo chini ya Mheshimiwa Jakaya Kikwete, kiongozi kijana kuliko wote waliotangulia, mchapakazi na mwenye bashasha. Kauli mbiu yake ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya na kibwagizo cha Maisha Bora kwa Kila Mtanzania vilileta msisimko mpya wa maendeleo kwa wananchi. Pamoja na kujitahidi kutekeleza kauli mbiu hii kwa vitendo, serikali yake imeandamwa na kashfa mbalimbali za ufisadi na mawaziri wake kadhaa walilazimika kujiuzulu nyadhifa zao na wengine bado wana kesi mahakamani. Anategemewa kushinda kipindi cha pili katika uchaguzi mkuu mwaka kesho. Sera rasmi ya serikali bado ni Ujamaa na Kujitegemea na imani na ahadi za MwanaCCM bado ni zile zile.

LEO TUNAPOSHEREHEKEA SIKU YA UHURU TUTAFAKARI:

 • Ati, kuna nchi ya ahadi ambayo tunajaribu kuifikia? Kama jibu ni ndiyo, nchi hiyo ikoje? Tunayo dira sahihi ya kutufikisha huko? Vipi kuhusu viongozi tuliowakabidhi majukumu teule ya kuandaa dira sahihi na kutuongoza kuelekea katika nchi yetu ya ahadi? Ni viongozi makini? Wanajua nchi yetu ya ahadi iliko? Kama wanajua, ni kweli wana lengo la kutufikisha katika nchi hiyo au wanatuzungusha jangwani tu? Tufanye nini?
 • Nyote nawatakieni sikukuu njema ya uhuru wa Tanzania. Mungu Aibariki nchi yetu nzuri yenye amani, upendo na utajiri wa kila aina.

5 comments:

 1. Kama kuna nchi ya ahadi tunayoiendea basi ahadi yake siyo ile tunayoifahamu.

  ReplyDelete
 2. Brief, simple, balanced and seriously mentally challenging. Nice presentation.

  I am not sure if we have a promised land in mind and I doubt it if our leaders know where it is OR WHERE THEY ARE TAKING US TO. Kila Mtanzania afikiri hili kwani siyo tu leaders' responsibilities

  ReplyDelete
 3. najiuliza kama Nyerere alipigania uhuru au ilibidi tu apewe huo uhuru kwani ulifika ule wakati wa kubadilisha kutoka direct to indirect colonialism na hivyo Nyerere akaandaliwa na kupewa! najiuliza tu jamana na labda ndio maana viongozi wengi wa Kiafrika wa enzi za uhuru walikuwa karibu sana na mataifa yaliyowatawala!

  na labda Nyerere anapendwa na wengi kwani vyombo vya habari vyoote huongelea mazuri yake lakini waweza jiuliza maswali wakati mwingine juu ya Nyerere mtakatifu

  na kuhusu Muungano, kwanza sijui nini kiliufnya uwepo na labda ni msukumo wa kutoka nje. Muungano uko kwenye hati hata kwa sababu tu haukuwa chini ya mkoloni mmoja. kama sote tungetawaliwa na mkoloni mmoja, basi yasingekuwepo maswali kwani mkoloni kasema. ila kichekesho ni kwamba wazanzibar wanahitaji muungano huo sasa kuliko wakati wowote kwani inasemekana Climate change itameza visiwa hivyo ndani ya miaka 100 ikiwa na maana kuwa visiwa vinapungua kwa kasi na suruhisho ni jamaa kuhamia bara, muungano sasa utadumu!!

  nashangaa ubora wa mkapa aliounadi Nyerere uko wapi na labda kwa kupitia mkapa tunauona ubora wa Nyerere pianimesikia Kikwete akiongelea mmazuri yake, yaani viongozi wanajiona walivyokuwa wazuri na kufanya mazuri badala ya wananchi. watende wema na kwenda zao wasingojee shukrani maana zikikosa wanaanza kujishukuru wenyewe

  nchi ya ahadi ? siijui, sijui tanzania ni nani na ninani. tunaishi tanzania akilizetu zikiiga kuishi ugaibuni, tunataraji viongozi watufikishe wapi? viongozi au sisi wenyewe?

  ReplyDelete
 4. Nimependa sana huu mtundiko, umeweka katika lugha rahisi na inayoeleweka. Mimi kama Godwin naamini kila mtu ana mapungufu yake. Na kila rais alifanya analotakiwa kufanya katika awamu yake. Ukweli kuna kuzidiana. Mwanzo nilikuwa simuelewi kabisa Mkapa, haswa katika awamu ya kwanza ya Uongozi wake. Ila nikaja kugundua baadae ni katika viongozi wenye upeo na uwezo mkubwa sana. NINAAMINI PAMOJA NA MAZURI ALIYOFANYA,ALIKUWA NA UWEZO WA KUFANYA ZAIDI YA HAYO. Kwa mtazamo wangu mdogo akutumia karama na uwezo wake kwa asilimia mia moja. NI KITU KIMOJA TU MPAKA SASA SIKUBALIANI NAYE. "UBINAFSISHAJI WA MASHIRIKA YA UMMA" wazo la kubinafsisha si baya sana, ila njia zilizotumika ndio mbaya zaidi.Nimefarijika kuwa ata yeye amekiri hilo, ingawaje aisaidii . KWA WASTANI NAWEZA KUSEMA AMEFANYA VIZURI UKILINGANISHA NA WENZAKE. Utabiri wangu, Kikwete ataendelea kumfanya MKAPA aonekane ni bora zaidi kuliko sasa... NATAMANI NINGEKUWA NI MMOJA YA WANA CCM WANAOPIGA KURA KUMPITISHA MGOMBEA WAO WA URAIS. Nisingesita kumwambia muheshimiwa ni muda mwafaka wa kubadilishana vijiti. Tumjaribu Mwana CCM mwingine

  ReplyDelete
 5. Asanteni nyote. Kamala - sikuwahi kufikiria athari za "global warming" kwenye Muungano wetu.

  Naamini pia kwamba hata bila mababa wa mataifa ya Kiafrika - akina Nyerere, Nkrumah, Kaunda, Obote, Kenyatta, Senghor na wengineo uhuru wa mataifa yao ungepatikana tu. Wakati ulikuwa umefika na ukoloni ulikuwa umepitwa na wakati. Ukoloni mpya (ukoloni mamboleo) ulikuwa umewadia na nchi hizi zilipaswa kuwa huru - bila kujali kama kulikuwa na akina Nyerere ama la!

  Nyerere ataendelea kuwa mtu wa muhimu katika historia ya nchi yetu hasa kutokana na mambo aliyoyafanya/aliyojaribu kuyafanya. Japo si Mtakatifu, ni wazi kwamba alikuwa kiongozi mwenye akili sana na mwenye kuona mbali. Ndiyo maana watu wengi sasa wanamjumuisha katika makundi ya wanafalsafa wa karne hii.

  Bwana Godwin - ni kweli. Mkapa pengine ndiye kiongozi aliyepewa nchi ambayo ilikuwa katika wakati mgumu kabisa wa kiuchumi na mparaganyiko wa kiitikadi na kimaadili. Misamaha ya kodi, ufisadi na maovu mengine yalikuwa katika kiwango cha juu sana. Nafikiri alifanya kazi nzuri katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na nidhamu, mapato yanakusanywa na serikali inafanya kazi. Nashangaa mambo haya hayatajwi bali kilichokazaniwa ni yale mabaya ambayo yalitendeka chini ya utawala wake. Ni wazi kwamba ubinafsishaji wa mashirika ya umma haukufanyika kwa uangalifu na uangavu wa kutosha, ununuzi wa ile rada, ndege ya rais na ule mgodi wa Kiwira ni baadhi ya mambo ambayo yataendelea kumwandama. Ningekuwa yeye ningewaomba msamaha Watanzania kwa makosa haya na bila shaka wangenisamehe. Kama nilivyogusia hapo juu - ngoja tuone Historia itakavyomhukumu.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU