NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, December 11, 2009

LEO "NIMEADHIRIKA" - HALAFU NIKAKUMBUKA NYUMBANI

 • Tumefunga shule jana kwa wiki tatu hivi. Basi leo, baada ya sherehe ya kumaliza muhula kule idarani, nikapita katika duka moja la kimataifa linalouza sato ambao linadai kwamba wanatoka Ziwa Victoria moja kwa moja (Kamala anasema wana sumu sana siku hizi). Basi hapo nikajipapatua nikanunua wanne. Sato hao wameshasafishwa tayari na nilipofika nyumbani nikawaosha wangu wangu.


 • Sikutaka mapishi yenye "korogesheni" nyingi bali nilitaka kuwapika chukuchuku yaani bila mafuta wala viungo vingi. Ni vitunguu, nyanya, pilipili na mchicha kwa wingi - ni kama supu, ni kama mbogamboga (yaani nusu kwa nusu). Huwa napenda kuwala hawa na kipande cha mkate. Chukuchuku lenyewe ni kama linavyoonekana hapa chini.


 • Ngoma ilikuja nilipotaka kuweka chumvi. Kumbe hakukuwa na chumvi hata kidogo ndani ya nyumba. Nilipiga simu kazini kwa mama kuulizia kama kulikuwa na chumvi sehemu nyingine ambayo siijui (wanawake hupenda kujiwekea akiba ya vitu muhimu). Bahati mbaya naye akawa katika mkutano na hivyo sikumpata. Kutoka hapa nyumbani kwenda madukani kidogo kuna kamwendo - na kusema kweli sikutaka tena kuendesha.
 • Jirani yangu hapa (mzungu tena polisi) alikuwa nje anacheza na watoto wake. Yaani nilitamani kweli nimzukie na kumwomba chumvi lakini nikasita. Japo mahusiano yetu naye si mabaya, kama kawaida maisha ya hapa ni ubinafsi na kila mtu kivyakevyake. Kuna siku ambazo huwa tunasalimiana na hata kuzungumza kidogo, siku zingine tunapungiana mikono tu na siku zingine hatusalimiani kabisa.
 • Basi nilizima jiko, nikamtumia mama ujumbe kumwomba aje na chumvi akirudi kutoka kazini halafu nikajipumzisha huku roho ikiniuma kwa kuchelewa kufaidi chukuchuku langu. Kisa hiki kimenifanya nikumbuke nyumbani Shinyanga ambako kuazimana chumvi (na vitu vingine) bado ni jambo la kawaida sana! Ugenini ni ugenini tu na nyumbani daima kutabakia kuwa nyumbani ati!

7 comments:

 1. African humanity, african unity, african ways of life. tamaduni zetu katika utu, uungwana na umoja wa binadamu hakuna pahala popote duniani. changu chako, nikipata umepata, hufi njaa. kuna mengi ya kujifunza kutoka tamaduni zetu tunazozipiga teke.

  ReplyDelete
 2. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!December 11, 2009 at 11:22 AM

  Hilo nalo neno...lol

  ReplyDelete
 3. Kwanzakabisa nasema umeniumiza roho kweli nilipowaona tu hao samaki. Halafu nimecheka kweli yaani ulishindwa kabisa kuomba chumvi kwa jirani? Ok nakuelewa mimi hapa nimewafundisha kuwa kuombana ni kawaida kwa hiyo nikiishiwa nawaomba na wao sasa wamezoea wakiishiwa wanakuja kwangu kuniomba. Kusema kweli ni vigumu, kwani wana ubinfsi sana. Ila chakula hicho kakangu hata mie nikimezea mate kweli ingekuwa karibu ningekuja tujumuike pamoja. Nakutakia wiki end njema.!!!!

  ReplyDelete
 4. Nimesoma hiki kisa nikacheka sana,mwishoni nikakuonea huruma maskini mi nilifikiri ni huku tu nilipo watu hatuombani chumvi au sukari au hata salam wakati mwingine hakuna,kweli nyumbani ni nyumbani!!

  ReplyDelete
 5. Mwalimu duhh pole sana. Chakula kinaonekana maridadi sana. Yaani mke wako anabahati sana kwani na wewe unapikia chakula familia. Msalimie sana mama Chanja!

  Zakia!

  ReplyDelete
 6. Hicho chakula bila chumvi kilikuwa perfect kwa wagonjwa wa moyo.

  Kaka yangu hii habari wakiisoma kule Bariadi watasema umesharogwa, mwanaume utapikaje? Wasukuma bado tuko nyuma jamani.

  ReplyDelete
 7. Da Mija - ni kweli watu wa kule Bariadi na hasa kijijini wanaweza wakashangaa. Mama alikuja hapa na alishangaa kuona kwamba nilikuwa ninapika na kuosha vyombo. Baadaye nadhani aliielewa hali ilivyo na alizoea. Mpaka leo nikiongea naye huwa namtania kwamba kuna vyombo vya kuosha vinanisubiri, au mboga ya kupika na huwa tunaishia kucheka sana.

  Hili la kujipikia chakula siyo Usukumani pekee bali hata sehemu zingine. Pale Dar es salaam ukianza kujipikia chakula au kuosha vyombo na kufanya kazi zingine za nyumbani wakati una mke basi utasikia unaambiwa eti UMEKALIWA!!!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU