NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, December 4, 2009

PADRI KARUGENDO NA UFUNUO WA MAGAZETI YA UDAKU

 • Padri Privatus Karugendo ni mmoja kati ya waandishi, wahakiki na wachambuzi makini sana wa masuala mbalimbali katika jamii yetu. Katika makala haya, anajaribu kuonyesha mchango chanya wa magazeti (yanayoitwa ya) udaku katika jamii na anatoa wito wa kuyaangalia magazeti haya kwa mtazamo mpya. Unakubaliana naye?
**********************
Magazeti ya udaku ama magazeti pendwa kama wenyewe wanavyotaka yaitwe duniani kote, yana sifa mbalimbali, ikiwemo kutangaza uongo na hata umbeya. Pamoja na ukweli kwamba magazeti ya aina hii nchini yanasomwa na wengi, bado tunayadharau na kufikiri kwamba yanasomwa na watu wasiokuwa makini.

Kamusi ya Kiswahili sanifu inaelezea neno udaku kuwa ni tabia ya kutafuta na kutaka kujua habari za watu; kilimilimi na umbea. Kuyabatiza magazeti haya kuwa ya udaku, ni lengo zima la kutoa ujumbe kwamba haya ni magazeti ya umbea na uzushi.

Hoja ninayoijenga katika makala hii si kununuliwa kwa magazeti au kutonunuliwa; bali ni kutaka kumshirikisha msomaji ufunuo nilioupata juu ya magazeti ya udaku. Mimi pia nilikuwa kati ya watu waliokuwa wakiyapiga vita magazeti ya udaku. Nimeandika makala nyingi nikipinga utamaduni wa watu kuacha kusoma vitabu na magazeti makini na kukimbilia magazeti ya udaku. Niliamini kabisa kwamba wale wote wanaoyasoma magazeti ya udaku si watu makini.


Inawezekana kabisa nikawa sijafahamu vizuri sababu inayowasukuma watu kusoma magazeti ya udaku; na inawezekana kwamba pia wale wanaoyaandika magazeti ya udaku wana malengo na nia tofauti na ile niliyofunuliwa. Hata hivyo ukweli unabaki pale pale kwamba magazeti ya udaku yanaandika maswala ya jinsia kuliko magazeti tunayoita ni makini.


Karibu magazeti yote ya udaku kurasa za mbele zinapambwa na masuala ya jinsi. Mifano ya magazeti haya na habari zinazoandikwa ni mingi. Inahusu wanasiasa kushiriki ngono; mafumanizi, ufuska wa kupindukia na nyingine nyingi. Ingawa hapa ninatoa mfano wa habari katika magazeti machache tu, ukweli ni kwamba karibia magazeti yote ya udaku yanaandika mambo ya jinsia na yaliyo tofauti. Kila gazeti linajitahidi kuibua kitu kipya ukitaka kufahamu hali ya jinsia ilivyo katika taifa letu la Tanzania, soma magazeti ya udaku.


Wanaharakati wa kujenga vuguvugu la kumkomboa mwanamke kimapinduzi wanaharakati wa haki za binadamu na wanaharakati wote wanaotetea usawa wa jinsia watakubaliana na mimi kwamba niliyoyataja hapo juu ni masuala ya jinsia. Ni nadra sana kuona magazeti makini yakibeba maswala ya jinsia kwenye kurasa za mbele. Ikitokea wakiwemo ni katikati na yanapewa nafasi ndogo kinyume na yanavyofanya magazeti ya udaku.

Inawezekana kwamba ni habari hizo zinakuwa zimeandikwa na kuchunjwa na wamiliki au na hata serikali. Habari nyingine zinachujwa na viongozi wa dini na zile ambazo ni nyeti zaidi, zinafunikwa na kufichwa kabisa hadi kristo atakaporudi mara ya pili! Nchi nyingi zilizoendelea zimeheshimu na kukumbatia usawa wa kijinsia.


Magazeti tunayoita makini yanaandika habari za siasa za wanasiasa na matukio yanayowahusu wanasiasa hasa katika kurasa zile za mbele. Haina maana kwamba haya nayo si muhimu katika jamii. Ila ni kwamba magazeti yale tunayoyaita makini hayazingatii habari za jinsia.


Pia waandishi wa magazeti haya tofauti na ilivyo kwa magazeti ya udaku, hawajitumi kutafuta habari kwenye vyanzo mbalimbali. Mara nyingi wanajikita kwenye vyanzo vya kiserikali; kusubiri pale maelekezo au kusubiri mikutano ya viongozi wakuu na waandishi wa habari. Pia wamejenga utamaduni wa kutafuta habari za matukio mbalimbali kama vile vifo, kupigwa, kubakwa kutoka kwa makamanda wa polisi wa wilaya na mikoa.

Matokeo yake ni kwamba haya magazeti yetu makini, ukisoma moja, huna haja ya kusoma jingine. Wakati mwingine unakuta karibia magazeti yote yana habari ile ile kwenye kurasa za mbele.


Hata ukisoma kurasa za ndani unakuta habari zinafanana. Kwa wale wanaosikiliza mapitio ya magazeti kwenye runinga watakubaliana na hoja yangu maana anayepitia magazeti akishasoma habari za gazeti linalotangulia, anabaki kusema habari hii imejirudia karibia katika magazeti yote” jambo hili linaeleweka vizuri, maana magazeti haya vyanzo vyao vya habari ni vilevile. Hawatafuti habari, wanasubiri kuletewa habari. Wanasubiri kuambiwa ni lipi la kuandika na lipi la kuacha. Kwa njia hii wanajikuta wanayaweka masuala ya jinsia pembeni.


Magazeti ya udaku hata yote yakitoka siku moja ni vigumu yawe na habari zinazofanana. Waandishi wao wanatafuta habari. Hawategemei kupata habari kutoka maelezo au kusubiria viongozi au watu maarufu katika taifa letu. Wanaingia ndani ya jamii na kutafuta habari zinazogusa maisha ya watu. Wanaibua mambo mengi ya jinsia. Wanaibua ukatili majumbani, wanaibua vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wanayofanyiwa wanawake na watoto, wanaibua matendo ya udanganyifu katika ndoa, wanaibua rushwa ya ngono, kwa kifupi wanaibua mambo yote yanayokwenda kinyume na maadili.


Ni kiasi gani yale yote yanaibuliwa na magazeti ya udaku yanafanyiwa kazi, ni swali la kujiuliza, ni kiasi gani yanayoibuliwa yana ukweli, pia ni swali la kujiuliza. Je, mashirika ya kutetea haki za binadamu, mashirika ya harakati za kujenga vuguvugu la kumkomboa mwanamke kimapinduzi ni kiasi gani wanatumia habari za udaku kuimarisha mapambano yao na mfumodume? Je, na wanaharakati wanayanyanyapaa magazeti ya udaku? Wanayanyanyapaa magazeti yanayoandika na kuibua masuala ya jinsia?


Swali jingine, ambalo nimeligusia mwanzo mwa makala hii ni kiasi gani wamiliki na wahariri wa magazeti ya udaku wanafahamu umuhimu wa habari wanazoziandika? Ni kweli kwamba wanaandika habari hizi kuibua masuala ya kijinsia au imetokea tu bahati mbaya wakati wakiwa kwenye harakati za kutafuta fedha? Au walifanya utafiti na kugundua kwamba vijana wengi wanapenda kusoma habari zinazoelezea mahusiano ya mwanamke na mwanaume? Habari za mapenzi,, habari za ngono na mambo yote yanayofanana na hayo? Vijana ni wengi – hivyo biashara ni kubwa?


Je, wanaandika kuuza magazeti yao? Ili wapate fedha na kuwa matajiri? Kuwa matajiri kuisaidia jamii au kuwa matajiri kwa faida yao na familia zao? Au wanaandika kufundisha jamii? Wanaandika kuibua masuala ya jinsia kwa lengo la kusambaratisha mfumo dume ili kuleta usawa wa kijinsia? Wanaandika kwa vile wao ni wanaharakati au nao pamoja na kuandika kwa vile wao ni wanaharakati? Au nao pamoja na kuandika majumbani kwao wanaendeleza mfumo dume?

Kuna haja ya kuyaangalia magazeti ya udaku kwa mtazamo mpya! Hata kama wanaoyaandaa wana malengo megine, lakini yale wanayoyaibua kuna haja ya kuyafuatilia; kuna haja ya kufanya utafiti zaidi ili kubaini ukweli. Kwa njia hii kuna haja ya kufanya utafiti zaidi ili kubaini ukweli. Kwa njia hii tunaweza mchango mkubwa katika kujenga jamii inayoheshimu haki za binadamu na kuzingatia usawa wa jinsia.


Wakiandika juu ya fumanizi, tukio hili lifuatiliwe. Wakiandika juu ya ukatili majumbani kwa vile wanatoa majina ya watu na wakati mwingine maeneo ya tukio, ni vyema matukio haya yafuatiliwe kwa karibu. Wakiandika juu ya rushwa ya ngono, jambo hili lifuatiliwe.

Wakiandika juu ya wabunge wetu kuwa na nyumba ndogo kule Dodoma kuwasafirisha watoto wadogo hadi Dodoma ili kufanya nao vitendo vya ngono, jambo hili lifuatiliwe ili waheshimiwa wetu wawajibishwe na kusaidiwa kuyabadilisha maisha yao.
Wakiandika juu ya waheshimiwa wabunge kununua dawa za kuongeza nguvu za kiume kwa wingi wakati wa vikao vya Bunge, jambo hili lifuatiliwe. Kwa nini wabunge wetu wahitaji nguvu za kiume kufanya tendo la ngono wakati wako mbali na familia zao? Bungeni wanahitaji nguvu za kufanya kazi? Lolote litakaloandikwa na udaku lifuatiliwe, hasa kama linaibua habari za jinsia.

Chanzo: Global Publishers

4 comments:

 1. hata mimi naona kuna ishu hapa na kuna ya kujifunza na kuna umuhimu wa udaku. kwa mfano niliipenda sana hadith moja ya kibibi kilichowahi kuwa kirafiki cha ngono cha oaoa john paul abla hajawa padre.

  ukiangalia mamabo kama comments ninazopata baada ya kuandika juu ya ndoa au jinsi, utagundua kuwa kuna kitu tunahitaji cha kuzungumzia jinsi! ukikumbuka wewe matondo, hujawahi kufunzwa mafunzo ya maana ya maisha na ngono ila uligraduate na kupewa cheti cha ndoa.

  ReplyDelete
 2. Makala haya yalinifikirisha zaidi, ingawa bado sijakubaliana naye kwa asilimia mia moja.

  ReplyDelete
 3. Padri kasema la maana - lakini nakataa kwamba eti huu ni ufunuo. Amefunuliwa na nani? Mungu? Mungu naye anashughulika na magazeti ya UDAKU? Please!

  ReplyDelete
 4. Dhamira ya padre nimeipata vyema, na cha msingi zaidi hapa ni ushughulikiaji wa yale maswala yanayoandikwa na magezeti ya udaku. kama ni hivyo basi taasisi husika zichukue jukumu la kufuatilia hizo taarifa na kuzifanyia kazi, sioni sababu ya kuuza hizo taarifa kwa jamii, tena kwa kundi jingine ambalo halijakomaa kimawazo, kama watoto na vijana chini ya umri wa miaka 18 ambao pia ni wanunuzi wakubwa wa magazeti hayo. kwa hiyo padre azishawishi taasisi zinazotetea haki za binadamu na ujinsia, na zingine husika hapa, zichukue changamoto hiyo ya upatikanaji wa habari za ovyo katika jamii yetu katika kufanya kazi kwa juhudi zaidi.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU