NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, December 28, 2009

PENGINE SIKU MOJA TUTASAFIRI "UCHI" KWENYE NDEGE

 • Kwa abiria wa ndege mambo yalianza kubadilika baada ya mashambulizi ya kigaidi ya 9/11 nchini Marekani. Sheria kali zaidi ziliwekwa ili kuimarisha usalama na abiria walianza kufanyiwa uchunguzi mkali zaidi kabla ya kupanda ndege ili kuanza safari zao. Kumbe huu ulikuwa ni mwanzo tu.

 • Richard Colvin Reid alipojaribu kuripua ndege kwa kuwasha kifaa kilichokuwa kimefichwa katika viatu vyake baada ya kuchanganya kemikali alizokuwa ameingia nazo kwenye ndege sheria zilibadilika. Abiria wote sasa walitakiwa kuvua viatu vyao ili vichunguzwe vizuri na mitambo ya usalama kabla ya kuruhusiwa kupanda ndege. Vimiminiko vyote pia vilipigwa mafuruku – dawa za mswaki, mafuta ya kujipaka na pafyumu. Vichupa vidogo vidogo pekee ndivyo viliruhusiwa.

 • Baada ya Mnigeria kujaribu kuripua ndege ya shirika la ndege la Northwest juzi, inasemekana baadhi ya mashirika ya ndege yameanza kupiga marufuku abiria kusimama au kuondoka katika viti vyao saa moja kabla ya ndege kutua. Wachambuzi wengi wa masuala ya usalama wa anga wanapendekeza kwamba ili kukata mzizi wa fitina, itakuwa lazima kupiga marufuku abiria kuingia na mzigo wo wote katika ndege. Vitu pekee vitakavyoruhusiwa ni dawa ambazo abiria anazihitaji safarini. Kompyuta za mkononi na vibegi vyote vidogo vidogo itabidi vitiwe katika mabegi yatakayosafirishwa katika sehemu ya mizigo ya ndege – ambako nako mitambo mikali zaidi ya kiusalama itaanza kutumika ili kuchunguza mizigo yote.

 • Isitoshe abiria wote watatakiwa kupita katika mashine mpya ambazo nasikia zinaonyesha sehemu zote za mwili. Mashine hizi zinalalamikiwa sana na watu wa masuala ya haki za binadamu ambao wanadai kwamba kimsingi zinaonyesha kila kitu zikiwemo sehemu za siri na hasa kwa wanaume (tazama video hapa chini).

 • Mtu unaweza kujiuliza, juhudi hizi za kizima moto za Wamarekani zitatufikisha wapi? Inavyoonekana Al Qaida hawalali na kila siku wanakuja na njia mpya za kuweza kutekeleza malengo yao. Baadhi ya watu wanasema kiutani kwamba kama bandika bandua hii itaendelea basi si ajabu siku moja tutatakiwa kusafiri uchi!

 • Kama nilivyogusia hapo juu, juhudi hizi za Wamarekani, japo ni nzuri, ni za kizimamoto tu na hazigusii hasa kiini cha tatizo lenyewe. Wataalamu wengi wanakiri kwamba hakuna silaha ambayo inaweza kumshinda adui ambaye yuko tayari kupoteza maisha yake ili kupigania na kutetea kile anachokiamini. Hivi ni vita vya kifikra/kiitikadi/kimtazamo na suluhisho lake linabidi litafutwe huko. Suluhisho lake kamwe halitapatikana kwa kudondosha mabomu kama Marekani inavyofanya sasa kule Afghanistan na sehemu zingine ambako itikadi kali za kiisilamu zimejitandaza.
 • Kinachotia wasiwasi zaidi ni kuona kwamba itikadi hizi za kihafidhina zinaenea hapa hapa Marekani na kuna visa vingi vinavyotokea ambapo vijana wa Kimarekani wamethibitika kwamba wamekwenda Somalia na Pakistani kujiunga na “kaka” zao wa Kiislamu katika uwanja wa mapambano. Watu wanajiuliza, Marekani itajipiga mabomu yenyewe? Suluhisho la mgogoro huu ni nini?


1 comment:

 1. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!December 29, 2009 at 12:15 PM

  Kama zinaonesha kila kitu itakuwa safi kwa watafiti na washabiki wa masuala ya ukimwi....lol

  si unajua watafiti hao walisema kuwa watu (wanaume) ambao hawajapashwa tohara wana hatari ya kuweza kupata maambukizo?

  sina hakika na hayo kwani kuna wengine wanadai kuwa ambao wamepashwa wako katika hatari zaidi...!

  All in all, wamarekani wanatapatapa tu na wakishagundua tatizo itakuwa too late...lol

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU